"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, January 16, 2017

MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA.

Mwanzo 2:8-9 "Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.
9 Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya".
Tukisoma katika mistari hii hapa juu, tunaona kabisa mwanzoni Mungu alipopanda bustani mashariki mwa Edeni Mungu aliiweka miti ya aina tatu bustanini nayo ni:
 • Kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa.
 • Mti wa uzima katikati ya bustani,
 • Na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
Hapa usichanganye hii ni miti aina tatu tofauti yenye tabia tatu tofauti tofauti, tukianzana na mti wa kwanza, 


 1. Kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa
Sasa mti wa aina hii unaozungumziwa hapa biblia inasema Mungu alichepusha katika ardhi ''KILA'' mti unaofaa kwa chakula, tunaona hili neno "KILA" linamaanisha ni miti mingi na sio mti mmoja, mfano wa miti hii ni  mapeasi, matofaa, maembe,mananasi, ndizi, mapasheni,mapapai n.k. hii ni miti aina ya kwanza ya mti ambayo Mungu aliichepusha katika ardhi kwa ajili ya chakula cha mwanadamu kumfaa kwa ajili ya mwili wake na mahitaji yake akiwa bustanini, yeye pamoja na wanyama wake wote Bwana aliompa. Adamu hakupewa masharti juu ya miti hii alikuwa na uhuru wa kula jinsi apendavyo na jinsi atakavyo kama biblia inavyosema. 

      2. Mti wa uzima katikati ya bustani.

Huu ni mti aina ya pili ambao Bwana aliuweka bustanini, tunaona kuwa mti wa pili na watatu imebeba tabia, na hii miti miwili ya mwisho ipo mmoja, mmoja tu. sio mingi kama ile aina ya kwanza ya mti, sasa huu mti wa uzima. Huu mti ulikuwa hauonekani kwa macho, kama miti mingine, na ulikuwa ni mti ambao ukila matunda yake (sio kula kwa mdomo) unapata uzima ambao umebeba ule uzima wa milele. Kwahiyo huu mti Mungu aliuweka kama hazina kwa Adamu endapo ikitokea wameupoteza ule uzima, waende kula matunda yake wapate uzima tena, Mungu kwa kujua kuwa mwanadamu baadaye atapoteza uzima aliuumba huu mti kuwa kama akiba ya tiba baadaye. Na huu mti Adamu hakuwa na matumizi nao kwasababu tayari alikuwa na uzima wa milele ndani yake.

Lakini tunaona baadaye Adamu alipodondoka kwenye dhambi na kupoteza uzima ndani yake alitamani kwenda kula matunda ya mti wa uzima lakini njia yake ilikuwa imeshafungwa ikilindwa mpaka wakati ulioamuriwa wa hiyo njia kufunguliwa ufike.kwahiyo ilipasa mwanadamu aijue hiyo njia ni ipi. soma mwanzo 3:24.  kuanzia hapo wanadamu ndipo walipoanza kufa na kuanza kutafuta suluhisho la kuishi milele tena, na ndipo hapo wanadamu walipoanza kuliitia jina la BWANA, mwanzo 4:26

  Lakini sasa sisi tunaoishi wakati huu wa neema tunajua NJIA ni ipi?... na huo MTI WA UZIMA  ni nani?... na MATUNDA yake ni nini?..na tunajua sio mwingine zaidi ya BWANA wetu YESU KRISTO mwokozi wetu Haleluya!! .Kwa ufafanuzi mfupi wa jambo hili tusome maandiko yafuatayo...

  Yohana 14:6" Yesu akamwambia, Mimi ndimi NJIA, na KWELI, na UZIMA; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi." Unaona hapo!?? hakuna njia yoyote sisi tunaweza kumfikia Baba kama ilivyokuwa hapo mwanzo kabla ya Adamu kuasi isipokuwa kwa njia ya YESU tu!    na pia tena ukisoma
 Yohana 6:47-51" Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna UZIMA WA MILELE.
48 Mimi ndimi chakula cha uzima.
49 Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa.
50 Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife.
51 Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ATAISHI MILELE. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu."

  Maandiko hayo hapo juu  yanaonyesha wazi kabisa kuwa hakuna uzima wa milele mahali pengine popote nje ya BWANA YESU KRISTO, matunda ya porini siku zote hayajawahi kumpa mtu uzima wa milele, kwahiyo mtazamo wa kuwa matunda ya mti wa uzima ni matunda yafananayo na ya mwituni sio sahihi,(ni kukosa tu Roho ya mafunuo) kwasababu matunda ya kawaida hayawezi kutupa sisi uzima wa milele, biblia inasema hakuna wokovu wowote nje ya Yesu Kristo, Hivyo basi maana ya kula matunda ya mti wa uzima ni kulitafakari na kuliamini NENO la Bwana Yesu tu, na kusafishwa kwa damu yake ambaye yeye ndiye huo mti wa uzima. Na hili NENO la Mungu ndilo liletalo Utii,Upendo,Amani,Uvumilivu,Fadhili,Kiasi,Utakatifu,Utu wema,Hekima,Haki n.k. 

Wagalitia 5:22" Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria".


   3.Mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
Kama tulivyouona mti wa pili, haukuwa mti wa kawaida kama ule wa kwanza, ndivyo ulivyo na huu pia, mti huu nao upo mmoja na umebeba tabia ya kipekee kwamba ukila matunda yake, utapata maarifa ya ujuzi wa mema na mabaya na ndio mti pekee Mungu aliomkataza mwanadamu asiule, alimwambia kabisa siku atakapokula tu matunda ya mti ule atakufa hakika. Lakini mwanadamu alikaidi  akala na ikapelekea hata sisi wote tukaingia katika hali ya laana ambayo tunayo mpaka sasa, lakini ashukuriwe Mungu njia ya mti wa uzima (YESU KRISTO) imeshafunguliwa tunao ukombozi wetu.

Huu mti asili yake ni mauti, na mauti inaletwa na shetani, kama vile uzima unavyoletwa na Yesu Kristo vivyo hivyo mauti inaletwa na shetani. Kwahiyo huu mti alikuwa ni "shetani" mwenyewe, na matunda yake ni "kwenda kinyume na NENO la Mungu" ndio huko unazaliwa uongo,uasherati,uuaji,ulevi,wizi,ulafi,sanamu,ufisadi,wivu, usengenyaji, n.k. ambayo mwisho wake ni mauti.

sasa kilichotendeka Edeni. shetani ambaye ndio ule mti wa ujuzi wa mema na mabaya, alimwingia nyoka. na nyoka akaenda kumdanganya Hawa kwa mafundisho yake ya uongo aliyoyatoa kwa baba yake shetani. kumbuka Mungu alimwonya mwanadamu adumu katika maagizo yake, asitafute maarifa mengine nje na Neno lake, lakini kwa kuwa shetani alijua mwanadamu anapenda maarifa ambayo Mungu alimkataza mwanadamu asiyatafute, na shetani siku zote ni mpingamizi wa Mungu hivyo alimjaribu katika hayo hayo, ndipo alipomwingia nyoka, na kumshawishi Hawa kutokumtii Mungu. na njia shetani aliyotumia ni ushawishi wa kufanya uasherati, kwa maana nyoka alimwambia ukila matunda haya utafanana na Mungu ukijua mema na mabaya. kumbuka kuwa nyoka hakuwa mnyama "reptilia" kama tunavyomwona leo, bali alikuwa ni mnyama anayekaribiana sana na mwanadamu, alikuwa na uwezo wa kuongea, kutafakari, alikuwa anatembea kwa miguu miwili, kwa ufupi alikuwa kama mtumwa wa mwanadamu.Baada ya kulaaniwa ndipo alipotembea kwa matumbo, na kula mavumbi.


nyoka alikuwa mnyama aliyekuwa anakaribiana sana na mwanadamu, mbali na wanyama wengine, katika wanyama wanaokaribiana na mwanadamu, alikuwa akitoka nyani anafuata nyoka kisha mwanadamu. tazama picha juu.


Kwahiyo baada ya nyoka kuingiwa na shetani na kwenda kufanya uzinzi na Hawa, Hawa naye akaenda kumpa tunda (kuzini) na mumewe, ikapelekea Hawa kubeba mimba ya mapacha wawili wasiofanana, akamzaa Habili na Kaini kila mmoja akiwa na baba yake. Baba yake Habili alikuwa ni Adamu na baba yake Kaini alikuwa ni nyoka. kumbuka nyoka hakuwa kama nyoka tunayemwona leo.(kwa ufafanuzi mrefu fuatilia somo langu liitwalo UZAO WA NYOKA.)

Tujue kuwa kitendo cha kula matunda ya porini kama peasi, embe au papai, hakuwezi kumfanya mtu ajione kuwa uchi, na kama walikula matunda yale kwa midomo hiyo midomo ndiyo ingetakiwa ilaaniwe na sio viungo vya uzazi, tunaona kabisa baada ya kula tunda (kuzini) walikimbilia kwenda kujifunika sehemu zao za siri, kiashirio kuwa hizo sehemu zao ndizo zilizohusika katika tendo lile.
Ni dhahiri kabisa kuwa mwanadamu ni vigumu kushawishika kwa matunda ya porini, kwa sababu alikuwa na matunda mengine mengi kwanini sasa aende kula lile la katikati ya bustani ya Edeni? Jibu ni dhahiri kuwa ni dhambi ile ile ya asili ambayo shetani alifahamu atampata nayo mwanadamu kirahisi na ndiyo hiyo hiyo anayowapata nayo wanadamu hata leo na hii sio nyingine bali ni dhambi ya uasherati.

Mungu ni yeye yule jana, na leo na hata milele, alichokichukia Edeni ndio hicho hicho anakichukia hata leo. Kama ilikuwa kula tunda kama tunda la kawaida ni makosa angeendelea kukichukia na kukikemea hicho kitu mpaka leo. lakini ni dhambi ya uasherati Mungu anayoichukia hata leo na ndiyo inayowaangusha watu wengi, kwa wanaojiita wakristo na wasio wakristo. kwahiyo hili tunda la kutokuliamini neno la Mungu (ambalo kwa mara ya kwanza shetani alilitangaza kwa kivuli cha uzinzi) hadi leo watu wanalila hili tunda. kama vile tu watu wa Mungu wanavyoendelea kula matunda ya mti wa uzima (kama tulivyosema ni kuliamini na kuliishi Neno la Mungu)  ili wapate uzima wa milele vivyo hivyo hadi leo watu wanaendelea kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya kama uasherati, n.k. kwa ajili ya mauti yao wenyewe. Akipandacho mtu ndicho atakachovuna.

Kwahiyo ndugu jambo lile lile lililotendeka Edeni linaendelea kutendeka hadi leo, je! unakula matunda ya ule mti wa ujuzi wa mema na mabaya huku ukijua kabisa Mungu amekataza usiyale ambayo tunayajua matunda yake ndiyo haya, uasherati, na mengine ni uongo, ulevi,ufisadi, usengenyaji, ushoga, ulafi, anasa, kuupenda ulimwengu, wizi, rushwa, tamaa mbaya, chuki, wivu, n.k. unafahamu kabisa mwisho wa haya ni mauti kama Mungu alivyosema pale Edeni, siku utakapokula matunda hayo utakufa hakika. Apple haliwezi likakufanya ufe! na biblia inasema mshahara wa dhambi ni mauti. Kimbilia kwa Yesu sasa ukale matunda ya Mti wa uzima, upate uzima wa milele, Bwana Yesu alisema itakufaidia nini uupate ulimwengu mzima na kupata hasara ya nafsi yako au utatoa nini badala ya nafsi yako. Kuzimu ipo, tazama miti miwili ipo mbele yako, chagua moja MTI WA UZIMA au MTI WA MAUTI. 

warumi 6:16 Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.

 Chaguo lipo kwako. Wakati umekwenda sana na mlango wa neema unakaribia kufungwa, je! umejiweka tayari.?? Umejazwa Roho Mtakatifu,??

Neema ya Mungu iwe pamoja nawe.

3 comments:

 1. Kwanza Mwenyezi Mungu alipowaumba alisema wazae,waongezeke wakaijaze dunia.Walitakiwa waijaze vipi dunia bila kujamiiana?Pili kama kweli kula tunda la ujuzi wa mema na mabaya ni kuzini kwa Hawa na nyoka basi Adam hakuwa na kosa kwa sababu alikuwa anajamiiana na mkewe na siyo kuzini

  ReplyDelete
 2. Hakuwa bado ameruhusu ilo tendo litendeke

  ReplyDelete
 3. Kwani ujuzi wa mema na mabaya Ni tabia ya Mungu au shetani? Hapa naona kufeli kwa SoMo kwa kiwango Cha juu Sana.

  ReplyDelete