Mathayo 24:32-35 " 32 Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;
33 nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.
34 Amin, nawaambia, KIZAZI HIKI HAKITAPITA, hata hayo yote yatakapotimia.
35 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Mambo haya Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake walipokuawa wameketi katika mlima wa Mizeituni, akiwaonya mambo yatakayokuja kutokea siku za mwisho kabla ya kurudi kwake, yakaandikwa kwaajili yetu sisi tusiwe gizani ili wakati huo ukifika mambo hayo yasitujie kama mwivi. Yapo mambo mengi Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake kama tunavyoyaona katika vitabu vya injili na vitabu vingine kuhusu siku za mwisho zitakavyokuja kuwa.
Lakini katika kitabu cha mathayo 24 Bwana Yesu alisema katika siku za mwisho kutatokea vita na matetesi ya vita (mathayo 24:6), Hii ni sahihi hivi vita tumekuwa tukiviona vikipiganwa kwa karne na karne kati ya mataifa na mataifa, lakini vita vingi na vikubwa vimekuja kukithiri zaidi katika karne ya 20 na 21,tunaona mfano wa vita vya kwanza (1914-1918) na vya pili vya dunia (1939-1945) ambavyo vimesababisha mauaji ya mamilioni ya watu ulimwenguni kote, kitu ambacho hata hakijawahi kuonekana katika historia ya vizazi vyote vya nyuma., lakini Bwana alieleza wazi yatakapoanza kutokea haya msitishwe ule mwisho bado,alisema kuwa huo ndio mwanzo wa utungu.
Bwana Yesu alisema pia siku za mwisho kutakuwa na njaa (mwilini na rohoni), matetemeko ya nchi, kutakuwa na magonjwa mengi, mambo ambayo tumekuwa tukiyaona kila kukicha matetemeko kila mahali, magonjwa mapya yanazuka kila siku((kama cancer, kisukari,presha,zika,ukimwi,ebola,sars,kimeta, n.k) ambayo hayakuwepo katika vizazi vya zamani, lakini haya yote Bwana Yesu pia alisema ni mwanzo wa utungu, kwamba ule mwisho unakaribia lakini bado haujafika.
Jambo lingine Bwana Yesu alilolisema ni kuwa manabii na makristo wengi wa uwongo watatokea na kuwadanganya wengi, Kila mtu anafahamu kama tunavyowaona leo mafundisho mengi ya uwongo yamezagaa kila mahali, alisema pia upendo wa wengi utapoa, ni dhahiri kabisa upendo(shauku) ya watu kumpenda Mungu na kupendana wao kwa wao imetoweka,na tamaa mbaya za ulimwengu huu zimewasonga watu na kumsahau Muumba wao, alisema pia watu watakuwa wakijipenda wenyewe, wakisalitiana na kuchukiana.
Aliwaambia wanafanzi wake pia,
luka 21:20-24 " Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia.Hili jambo lilitimia kama lilivyo mwaka 70AD pale majeshi ya Rumi yalipouzunguka mji wa Yerusalemu na kuharibu mji na hekalu kuliteketeza kwa moto, na wayahudi wote waliokuwa wamesalia Yerusalemu walitawanywa katika mataifa yote duniani hivyo basi Izraeli wakawa wageni katika mataifa mengine, mpaka Mungu alipowarejesha tena nchini kwao mwaka 1948 kuwa kama taifa huru tena linalojitegemea.
21 Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.
22 Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.
23 Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.
24 Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia.".
Mwisho Bwana Yesu alisema habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.
Lakini hapa kuna jambo kuu na la muhimu sana tunatakiwa tulione,
Tukisoma katika mathayo 24:32-35 na Luka 21:29-33 inasema "29 Akawaambia mfano; Utazameni mtini na miti mingine yote.
30 Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu.
31 Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu.
32 Amin, nawaambieni, KIZAZI HIKI HAKITAPITA, HATA HAYO YOTE YATIMIE.
33 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Alisema kwa mtini jifunzeni, "Mtini" siku zote kwenye biblia unawakilisha Taifa la Izraeli,(soma yeremia 24), na aliposema utazameni mtini na miti mingine,hii miti mingine ni mataifa mengine, sasa aliposema mtini utakapoanza kuchipua alikuwa na maana Taifa la Israel kuzaliwa tena upya baada ya kukaa katika mataifa mbalimbali kwa muda mrefu. Tunaona jambo hili lilitimia mwaka 1948 pale Izraeli waliporejea katika nchi yao wenyewe kama ilivyotabiriwa na Bwana, hiyo ndiyo maana ya kuchipuka kwa Izraeli. Hivyo basi kuanzia huo mwaka wa 1948 mpaka sasa tunaona mataifa mengi yalianza kupata uhuru wao ikiwemo mataifa karibu yote ya Afrika, baadhi ya Asia na Marekani ya kusini hii inatimiza ule unabii Yesu aliosema mjifunze pia kwa miti mingine (miti mingine ni sisi mataifa mengine mbali na Izraeli).
Taifa la Izraeli likisherekea siku ya uhuru wao 1948 |
Sasa baada ya mtini kuchipuka(Izraeli) hapo ndipo Bwana aliposema "Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe."
Hichi kizazi kinachozungumziwa hapa sio kile kizazi cha Yesu alichokuwa anazungumza nacho, bali ni kile kizazi kilichoshuhudia Izraeli ikichipuka yaani Izraeli kuwa Taifa huru tena kama ilivyokuwa hapo mwanzo zaidi ya miaka 2500 iliyopita.
Na kizazi kilichoshuhudia hayo ni kuanzia watu waliozaliwa mwaka 1948 na kuendelea hadi sasa, kwahiyo tumeshafahamu kuwa kizazi cha wale waliozaliwa mwaka 1948 Bwana Yesu ndicho alichosema hakitapita. Na tunajua kizazi mpaka kitoweke kabisa katika dunia ni miaka 100,kwa dunia ya sasa, tukiangalia tangu mwaka 1948 hadi leo ni miaka 69 imeshapita, na hapa Bwana Yesu alisema kizazi hiki hakitapita hakusema kitatimia ndio mwisho uje bali alisema hakitapita, kwahiyo hii ina maanisha hapa hapa katikati kabla ya kufikia hicho kipindi cha kizazi kutoweka Bwana Yesu Kristo atakuwa ameshakuja, ni wazi kabisa wengi waliozaliwa chini ya mwaka 1948 ni asilimia 7% tu inayoishi duniani sasa (kwa mujibu wa takwimu za dunia), kwahiyo hili rika la hawa watu linakaribia kupotea, lakini Bwana Yesu Kristo aliapa kuwa hili rika halitapita,
aliweka msisitizo kabisa akasema Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe."..
Na baada ya hapo ndipo Bwana Yesu aliposema mtakapoona hayo yanaanza kutokea tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu, kwa hiyo ndugu tambua hilo wewe unayesema bado sana Yesu kurudi, wewe ambaye unasitasita kwenye mawazo mawili, maneno haya yanaonyesha wazi kabisa kuwa kuja kwa Bwana kuko mlangoni, Baada ya hayo maneno Bwana Yesu Kristo alimalizia kwa kusema
" Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
35 kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima.
36 Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu."
Bwana Yesu Kristo hakutoa muda wala saa ya kuja kwake lakini alitupa majira kwamba yatakapokuja yasitujie kama mwivi au kama mtego unasavyo, je! wewe ambaye unatambua kabisa tunaishi katika kizazi ambacho tutashuhudia kuja kwa Yesu Kristo mara ya pili, umejiwekaje tayari, umebatizwa kweli kwa Roho Mtakatifu?? umeufanya imara kweli uteule wako na wito wako? Bwana Yesu akija leo una uhakika wa kwenda naye??.
Huu ni wakati wa wale wanawali werevu kutengeneza taa zao kwenda kumlaki Bwana Yesu, je! na wewe una uhakika kuwa taa yako iko sawa?? Tambua ya kuwa Bwana akija leo na taa yako haipo sawa utabaki hapa na kuingia katika ile dhiki kuu? Kumbuka ujumbe huu unakuhusu wewe mkristo unayesema umeokoka, kumbuka wale walikuwa wote ni wanawali na wote walikuwa wanamsubiria Bwana wao isipokuwa watano walikuwa werevu na watano walikuwa wapumbavu (mathayo 25) kwahiyo hao wanawali 10 wote ni wakristo na sio watu wasioamini, fahamu tu uchungu utakuwa kwa wale ambao walidhani wangeenda katika unyakuo lakini wakabaki, na sio wale wasioamini, hivyo ndivyo itakavyowakuta wakristo wote ambao ni vuguvugu sasa wanachofahamu tu ni madhehebu yao lakini hawataki kumjua Kristo katika neno lake, hawataki kujazwa Roho Mtakatifu ili awaongoze katika kweli yote uteule wao uwe wa uhakika, Roho Mtakatifu ndio muhuri wa Mungu (waefeso 4:30) pasipo Roho Mtakatifu hakuna unyakuo. je! wewe ni mmoja wa wanawali mwerevu au mpumbavu? wanawali wote werevu wanajivunia kuwa wakristo wa NENO na sio wakristo wa madhehebu, wanawali wapumbavu wanaona aibu kuitwa wakristo, wanajivunia madhehebu ukimwuliza yeye ni nani atakwambia mimi ni mlutheri,mkatoliki,msabato,mbranhamite,m-eagt,morovian., hawafahamu jambo lingine lolote nje ya madhehebu yao, ukiwaambia biblia inasema hivi wanasema dhehebu letu halifundishi hilo,
Lakini BWANA YESU KRISTO leo anatuita tuwe WANAWALI WEREVU(SAFI).....na ujumbe tulionao sasa kwa wakati wetu ni ufunuo 18:4 "4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake. Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake." Jihadhari na mafundisho ya uongo.
Ndugu tubu, mgeukie Bwana muda ndio huu, usidanganyike na mafundisho yanayosema kuwa Kristo bado sana kurudi.
Mungu akubariki!
No comments:
Post a Comment