MFALME wa WAFALME YESU KRISTO Bwana wetu, atukuzwe daima.
Karibu kwa neema za Mungu tujifunze kitabu cha Esta leo tukianza na ile sura ya 1 na ya 2.Ni vizuri ukiwa na biblia yako pembeni uipitie habari hii kwanza ndipo tuende pamoja. Kama tunavyofahamu Agano la Kale ni kivuli cha Agano jipya hivyo kila habari inayozungumzwa katika agano la kale, inafunua jambo fulani linaloendelea katika roho kwa wakati tunaoishi sasa.
Kitabu hiki kwa ufupi kinaelezea habari ya Mfalme Ahasuero wa Ufalme wa Umedi & Uajemi aliyekuwa tajiri sana na mwenye nguvu ni mfalme aliyetawala mataifa 127, biblia inasema kuanzia India mpaka taifa la Kushi (Ethiopia), kote huku alimiliki na kwa wakati ule alikuwa ni kama Mfalme wa dunia. Kwasababu Umedi na Uajemi ndio zilikuwa zinatawala dunia kwa wakati huo.
Hivyo ilifika wakati mfalme aliandaa sherehe kubwa sana kwa wakuu wake wote, pamoja na watu wote waliokuwapo katika mji wake (huko Shushani ngomeni), wakubwa kwa wadogo walihudhuria, watu walikula na kunywa jinsi wapendavyo, na kwa fahari yake aliamua kumwasilisha malkia aitwaye VASHTI, mbele za wakuu wote wauone uzuri wake, maana biblia inasema Vashti alikuwa ni mzuri sana wa uso, kwasababu hata tafsiri ya jina Vashti linamaanisha “mwanamke mzuri”.
Lakini mambo hayakuwa kama yalivyotarajiwa, Badala ya Vashti kumtii mume wake, na zaidi ya yote alikuwa ni MFALME, alikaidi amri ile kwa KIBURI cha Uzuri wake na kuamua kutokwenda, Jambo hili lilionekana kuwa ni aibu kubwa kwa Uajemi yote, kwasababu hakukuwa na desturi ya mwanamke kumvunjia heshima mfalme, Na tunasoma Vashti alikuja kuvuliwa umalkia wake na kutafutwa mwengine “ALIYE MWEMA KULIKO YEYE”.
Esta 1:19 “Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye.”
Hivyo moja kwa moja, ikaanza kupangwa mipango ya kumtafuta malkia mwingine mahali pa Vashti, mbiu zikapigwa katika mataifa yote duniani (127) aliyokuwa anayamiliki, walikuja MABIKIRA vijana wengi na ESTA alikuwa mmoja wapo. Kumbuka wote hawa walitokea katika machimbuko tofauti tofauti, wengine katika familia za kitajiri, wengine katika koo za kifalme, wengine walikuwa mabinti za maakida, wengine familia za kisomi, wengine familia za mabinti warembo n.k. Kwahiyo walikusanyika wengi sana pengine mabinti 30,000 au zaidi.
Lakini tukiendelea kusoma habari tunaona kwamba kila mmoja alipewa uhuru wa kujipamba kwa jinsi atakavyo, apewe chakula atakacho, au lolote atakalolitaka apewe ili tu siku atakapopelekwa mbele ya mfalme isionekane kasoro yoyote kama walivyofanyiwa wakina Danieli, Shedraka, Meshaki na Abednego mbele ya mfalme Nebukadreza. Hivyo mabikira wote na Esta akiwa miongoni mwao waliwekwa chini ya msimamizi mmoja wa nyumba ya mfalme aliyeitwa “HEGAI”.
Kazi ya huyu HEGAI ilikuwa ni kuhakikisha kuwa anawahudumia na kuwapa mahitaji yao kwa jinsi watakavyo. Tukisoma;
Esta 2:1-4 “ 1 Baada ya hayo, hasira yake mfalme Ahasuero ilipotulia, alimkumbuka Vashti, na vile alivyotenda, na yale yaliyoamriwa juu yake.
2 Basi watumishi wa mfalme waliomhudumu walimwambia, Mfalme na atafutiwe mabikira vijana wazuri;
3 naye mfalme aweke wasimamizi katika majimbo yote ya ufalme wake, ili wakusanye pamoja mabikira vijana wazuri wote waende Shushani ngomeni, kwenye nyumba ya wanawake mikononi mwa HEGAI, MSIMAMIZI-WA-NYUMBA WA MFALME, mwenye kuwalinda wanawake; tena wapewe VIFAA VYA UTAKASO.
4 Naye yule msichana atakayempendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti. Neno hilo likampendeza mfalme, naye akafanya hivyo.”
LAKINI NI SIRI IPI ILIYOMFANYA ESTA AKUBALIKE KULIKO MABIKIRA WENGINE?.
Biblia haimtaji Esta kama alikuwa ni mwanamke mzuri kuliko wote waliohudhuria, hapana biblia inasema alikuwa na Uso mwema tu, wala hakutokea katika familia ya kitajiri kama wenzake, wala hakuwa na elimu kama wale wengine pengine ingekuwa chachu ya kumfanya mfalme avutiwe naye lakini vyote hivyo hakuwa navyo. Bali kuna jambo lingine liliomfanya mfalme avutiwe naye. Na hili tunalipata kwa HEGAI, YULE MSIMAMIZI WA NYUMBA YA MFALME na MORDEKAI mjomba yake.
Wakati wengine wakimwendea Hagai na kumlazimisha awape vitu wanavyotaka wao ili wamwendee mfalme, Esta hakuwa hivyo, bali alijinyenyekeza kwa Hegai, Huku akishikilia maagizo aliyopewa na mjomba wake Mordekai kuwa ASIJIONYESHE KABILA LAKE HUKO AENDAKO, hivyo kwa jambo hilo tu ilimpelekea Hegai avutiwe naye sana kwasababu hakupeleka sifa yoyote imuhusuyo yeye mbele zake, na kwa kuwa Hegai alikuwa ni msimamizi wa nyumba ya mfalme, kwa uzoefu wa miaka mingi aliokuwa nao kule alitambua mfalme huwa anapenda msichana wa tabia gani au huwa hapendi msichana wa tabia gani, kwasababu yeye ndiye aliyekuwa msimamizi wa Vashti kabla hajawa malkia. Kwahiyo alitambua tabia ya mfalme kuwa anapenda mwanamke katika mwonekano upi, na katika tabia ipi. Na siri hiyo HEGAI alimfunulia Esta peke yake.Akamtenga Esta na wale wengine na kumpa matunzo ya kipekee kwa msaada wa vijakazi wengine saba.
Esta 2:8-9 “Basi ikawa, wakati iliposikiwa amri ya mfalme na mbiu yake, wasichana wengi wakakusanyika huko Shushani ngomeni mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake.
9 Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; naye akampa upesi vifaa vya utakaso, pamoja na posho zake, na vijakazi saba walio haki yake, wa nyumbani mwa mfalme. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake.
10 Walakini Esta hakudhihirisha kabila yake wala jamaa yake, kwa maana ndivyo alivyomwagiza Mordekai asiwadhihirishe.”
Kwahiyo baada ya ule muda wa utakaso kuisha ambao ulikuwa ni miezi 12 tu, Esta na wenzake waliingizwa mbele za mfalme kila mmoja akijionyesha ujuzi wake na uzuri wake, na utashi wake, kila mmoja kwa namna yake, pengine wengine walionyesha familia za kitajiri walizotokea, wengine tamaduni zao za kujua kucheza vizuri na urembo wao, wengine pamoja na uzuri wao juu ya hilo walionyesha elimu zao kubwa mbele ya mfalme, pengine wengine walionyesha kuwa wametoka kabila moja na mfalme, hivyo wangestahili, na mambo kadha wa kadha.
Lakini tukirudi kwa Esta yeye hakuonyesha chochote, isipokuwa vile tu alivyopewa na Hegai aende navyo mbele za mfalme. Na badala yake hakuonekana aliyekuwa mfano wa Esta mbele ya mfalme.
JE! BIBI-ARUSI WA KRISTO ANAPATIKANAJE?
Tunaposoma habari hii tunajifunza kwa Bwana Yesu jinsi alivyoanza kumtafuta BIBI-ARUSI wake bikira safi tangu vizazi vya kale hadi sasa, Kwahiyo mambo haya tafsiri yake kwa kanisa ni;
>Mfalme Ahasuero anamwakilisha BWANA YESU,
>malkia VASHTI ambaye baadaye alikuja kutolewa katika Umalkia wake anawakilisha taifa la ISRAELI,
>ESTA anamwakilisha BIBI-ARUSI wa kweli aliyekubaliwa na Kristo,
> Wale mabikira wengine ; Wanawakilisha MADHEHEBU.
>Hegai na Mordekai wanawakilisha NENO LA MUNGU na Roho Mtakatifu.
Israeli kama taifa teule la Mungu, lilifananishwa na mke wa Mungu(Yeremia 3:14), na ndivyo lilivyokuwa kwa miaka yote, Lakini Mfalme wake (YESU KRISTO) alipokuja ili afanye nao karamu, walimkataa kwa kiburi na zaidi ya yote wakamzalilisha pale kalvari mbele ya dunia yote ni mfano tu wa Vashti alivyomwaibisha mfalme Ahasuero mbele ya dunia yote. Japo Bwana Yesu alikuja kwa upole kwa mke wake Israeli wao walimkataa na kumpinga, Na ndio maana tunaona Bwana Yesu aliwaambia Ee Yerusalemu, Yerusalem “Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!”
Mathayo 23:38 “Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa.
39 Kwa maana nawaambia, Hamtaniona kamwe tangu sasa, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.”
Unaona hapo baada ya wayahudi kumkataa aliye mfalme wao na mume wao, walikuja kukatwa(Warumi 11) na kutolewa katika nafasi yao ya umalkia, na ndipo Mungu akaanza kutafuta malkia mwingine mahali pake, Ndipo NEEMA ikatugeukia sisi mataifa, akitafuta BIBI-ARUSI safi atakayekaa mahali pa Israeli.
Na kama vile tunavyoona walijihudhurisha mabinti wengi mbele za mfalme kutoka maeneo mbali mbali duniani kote. Hawa mabinti si wengine zaidi ya madhehebu mbalimbali na kila moja linajiona kuwa limestahili kuwa bibi-arusi wa BWANA YESU zaidi ya lenzake. Huoni leo hii Kanisa Katoliki linajiona kanisa pekee mama ambalo Mungu amelipokea?, walutheri nao vivyo hivyo, Waanglikana wanajiona wao ndio wapo sawa, wasabato nao vivyo hivyo wao ndio kanisa litakalokwenda kumlaki Bwana mawinguni, mashahidi wa Yehova nao vivyo hivyo, wapentekoste nao wanajiona kuwa wamestahili kuwa bibi-arusi wa KRISTO, na madhehebu mengine yote yanafanya ivyo hivyo..kumbuka leo hii duniani kuna madhehebu ya kikristo zaidi ya 40,000 na yote wanadai kuwa yapo sahihi zaidi ya mengine?. Lakini tujiulize je! Wote hawa watakuwa bibi-arusi wa Kristo??.
Jibu ni hapana bibi-arusi ni mmoja tu na ni ESTA basi. Yule tu atakayekidhi vigezo vya mfalme ndiye atakayekuwa malkia.
JE! ESTA NI MFANO WA DHEHEBU GANI SASA HIVI?
Tabia ya kwanza ya Esta aliyoonywa na Mordekai mjomba yake(aliye mfano wa Roho Mtakatifu) ni “KUTOKUFUNUA KABILA YAKE” mahali aendapo . Hiyo ni sifa iliyomfanya Esta apate kibali kwanza kwa HEGAI na kisha kwa Mfalme. Ukitaka kufahamu kwamba jambo la kujisifia, au kueleza chimbuko lako lilikuwa ni harufu mbaya mbele za mfalme, utaona kuwa japo Esta alikuwa ni malkia kwa muda mrefu mfalme alioishi naye hakuwahi hata siku moja kumuuliza Esta yeye ni kabila gani au jamaa zake ni nani?, au watu wake ni watu na namna gani!!, mpaka baadaye sana matatizo yalipotokea, hii ilionyesha kuwa mfalme alikuwa havutiwi na chimbuko la mtu unapokuja mbele zake, Yeye alimtaka Esta kama Esta tu katika unyenyekevu wake wote yeye kama alivyo, bila kujihesabia haki mbele zake. Na ndivyo Kristo anavyotaka watu wamwendee mbele zake.
Na jambo lingine lililomfanya Esta akubalike mbele za mfalme ni kumsikiliza HEGAI, ambaye ni Mfano wa mitume na manabii (yaani NENO LA MUNGU), Esta alipata ujuzi wa taratibu za kumwendea mfalme tofauti na wale mabinti wengine kwa kudumu katika maagizo ya HEGAI.
Na sasa hivi maana ya “KUFUNUA KABILA NI NINI?”. Pale unapomwendea Kristo na desturi za kimadhehebu; Ukatoliki, ulutheri, usabato, uanglikana, u-JW,n.k. pale unapoulizwa je! Wewe Ni MKRISTO? unasema mimi ni mlutheri, au mimi ni mbranhamite au mimi ni mpentekoste n.k...mpaka hapo hizo ni hatua za awali za wewe kutokidhi vigezo vya wewe kutokuwa bibi-arusi wa Kristo. Kwasababu pale utakapokwenda kukutana na HEGAI wako(yaani NENO LA MUNGU), na kuambiwa vitu visivyoendana na dhehebu lako.. utaishia kupinga na kujikuta unamfuata Bwana Yesu kwa desturi zako mwenyewe na sio desturi zilizopo katika NENO LAKE.
Hivyo ndugu ili uwe bibi-arusi aliyekubaliwa jambo la kwanza ondoa udhehebu ndani ya fikra zako, toka kwenye kamba za kidini na za kimadhehebu, halafu mfuate yeye kama ulivyo, unaona mafarisayo walimfuata Yesu na madhehebu yao wakaishia kukatwa, vivyo hivyo ukishilia dhehebu na kumfuata YESU utakatwa kama wao. Mgeukie HEGAI wako yaani INJILI YA MITUME NA MANABII.. BIBLIA TAKATIFU.. mfuate MFALME YESU KWA NJIA HIYO ndipo utakapomwona.
Biblia inasema Tokeni kwake enyi watu wangu..kumbuka udhehebu ni chapa ya mnyama, alama hii ukiikumbatia itakusabibishia usimuone Bwana siku ile ya unyakuo itakapofika..bibi-arusi wa kweli wa Kristo ni mnyenyekevu aliyekaa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu peke yake na kudumu katika kile NENO LINACHOSEMA na SIO KILE KANISA LINACHOSEMA.
Neno la Mungu linaposema “mwanamke avae mavazi ya kujisitiri(1Timotheo 2:9)” na wewe unasema haijalishi dhehebu letu halihimizi hivyo, ni sawa na kukataa maagizo ya Hegai na bado unataka uwe bibi-arusi hiyo haiwezekani..pia NENO linaposema “usijifanyie sanamu za kuchonga na kuziabudu (kutoka 20)” na wewe anaenda kuchukua sanamu ya mtakatifu Fulani na kuiabudu na kusema dhehebu letu linatufundisha hivyo..Na bado unasubiri siku ile uchaguliwe na Bwana uende mbinguni…Nataka nikuambie ndugu yangu siku ile utaikosa licha ya juhudi zako zote za kujionyesha kukubaliwa siku ile utalia na kuomboleza kama wale wanawali wapumbavu wa kwenye Mathayo 25 walivyokuwa. Kwasababu tu ya kuyadharau maagizo ya HEGAI (NENO LA MUNGU).
Hivyo maombi ni Bwana akupe kuliona hilo, na kuwa Bibi-arusi safi aliyestahili kwenda katika KARAMU YA MWANA-KONDOO. Mfuate Bwana kama ulivyo bila kuwa na utambulisho wowote unaokufuata hapo nyuma.
Mungu akubariki. Usikose mwendelezo huu wa Kitabu cha Esta sura zinazofuata.