Wakolosai 3:1 “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, YATAFUTENI YALIYO JUU KRISTO ALIKO, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. 2 YAFIKIRINI YALIYO JUU, SIYO YALIYO KATIKA NCHI.”
Kama wasafiri hapa duniani, kila siku shabaha yetu inapasa iwe ni kufika mbinguni kwa gharama yoyote ile, Biblia imetuambia “tuyatafute” na “kuyatafakari” yaliyo juu, ikiwa na maana kuwa kwa bidii zote na nguvu zetu zote, tutafute kanuni za kutufanya sisi kuingia mbinguni, tumeambiwa tuutafute kama vile tunavyotafuta fedha au kama hazina iliyositirika (Mithali 2:4),
> Mambo ya ulimwengu huu yasiwe kikwazo cha wewe kuikosa mbingu, unapaswa utumie hekima popote ulipo usiwe na kisingizio kwamba kitu fulani kimekusonga usimtafute Mungu, kumbuka wapo katika dunia hii hii matajiri wakubwa kuliko wewe na bado wanayafikiria yaliyo juu, na maisha yao ni kama wasafiri tu hapa duniani, kama mfano wa akina Sulemani katika biblia, japo alikuwa ni tajiri lakini aliyatafakari sana yaliyo juu ,
> Wapo wenye vyeo vikubwa kuliko wewe katika kizazi hiki hiki unachoishi lakini fikra zao na mawazo yao yapo mbinguni, usiku na mchana wanamwomba Bwana ufalme wake uje!, mfano ni kama Danieli alivyokuwa katika biblia,japo alikuwa mwenye cheo kikubwa lakini kutwa mara tatu alikuwa akimwomba Mungu kuhusu hatma yake na watu wake.
> Vivyo hivyo wapo maskini kuliko wewe, hawana chakula wala nguo wala mahitaji yoyote lakini mawazo yao na fikra zao si katika mambo ya ulimwengu huu bali mbinguni, japo wanapitia magumu, wanaishi kama wasafiri tu hapa duniani…Wanaishi kama Lazaro wa kwenye biblia, ingawa alikuwa anakula makombo lakini hakutupa wokovu wake chini.
> Wapo wenye shida nyingi kuliko zako; wagonjwa, walemavu, hawana watoto, mayatima, lakini kwao hayo yote si kitu, mawazo yao na fikra zao zimeelekea juu mbinguni, siku kwa siku wakijihakiki maisha yao wasianguke, wakijiepusha na maovu wasije wakaikosa mbingu.
Na wewe je! UNAYATAFUTA YALIYO JUU! Au FIKRA ZAKO ZIMEELEKEA JUU MBINGUNI? Katika hali yoyote uliyopo?..Kumbuka vya duniani vinapita, hivyo visiwe sababu ya wewe kukusonga na kuikosa mbingu. Anza sasa kutamani kwenda mbinguni.
Tunaishi katika muda wa nyongeza Bwana Yesu anakaribia kurudi.
Ubarikiwe.
No comments:
Post a Comment