Huu ni wakati wa kuwa makini sana juu ya hatma ya maisha yetu ya rohoni, kwasababu tusipokuwa makini katika nyakati hizi na kwa jinsi siku zinavyozidi kwenda tunaweza tukajikuta tunaangukia katika vifungo vya shetani pasipo hata kujijua.
Kumbuka shetani sasa hivi anatenda kazi ndani ya KANISA la Mungu, hawezi kutilia mkazo sana kwa watu wa nje walio waovu kwasababu hao ameshawapata siku nyingi..anakutafuta wewe unayejiita mkristo unayejiona umesimama. Na unadhani atakupatia wapi zaidi ya kanisani.? Huko ndiko kiti chake cha enzi alipokiamishia.
Bwana Yesu alizungumza hivi;
Mathayo 13:24-3024 Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?28 Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?29 Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo.30 Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.
Kumbuka magugu na ngano ni vitu vinavyofanana sana, kwa kuviangalia huwezi ukavitofautisha mpaka vitakapokuwa vikubwa na kutoa mazao, Katika mfano huo tunafahamu kuwa aliyepanda hizo mbegu njema ni BWANA YESU na shamba lake ni KANISA. Tunaweza tukaona jinsi kanisa la kwanza lilivyokuwa safi, takatifu lisilojichanganya na mafundisho yoyote ya uongo au mapokeo yeyote ya kibinadamu, ni kanisa lililokuwa halina dosari,
Lakini baada ya shetani kuona hilo alianza kuja na mbinu za kuliharibu, hivyo aliiga njia ile ile ya kupanda mbegu kama vile Bwana alivyofanya. Ndipo akaanza kwanza kwa kupenyeza mafundisho ya uongo katikati ya kanisa la Mungu, kisha ile mbegu ya uongo ilipomea baadaye ikageuka na kuwa dini, na kukaa katikati ya kanisa la Mungu. Kuanzia hapo hizi mbegu mbili zikawa zipo pamoja zikishindana katika kanisani la Kristo.(Magugu na Ngano)
Mungu kwa kulifahamu hilo aliruhusu vyote vimee kwa pamoja mpaka wakati wa mavuno utakapowadia kwasababu kama tulivyoona magugu yakiwa machanga ni ngumu kuyatofautisha na ngano, yanafanana sana kwa tabia zao. Na Mungu aliposema yaache yakue pamoja ni kiashiria kuwa yote yapate mvua kutoka kwa Mungu.(Mathayo 5:45). Ikiwa na maana kuwa Mungu aliyaruhusu yafanikiwe katika njia zao kama vile tu zile mbegu njema zifanikiwavyo mpaka wakati wa mavuno utakapowadia. Yote yananyeshewa mvua, kumbuka hata manabii wa uongo wanatabiri kwa jina la Bwana na inatokea, wanaponya na kutoa pepo kwa jina la Yesu na yanawatii, lakini siku ile Bwana atawaambia siwajui nyinyi mtendao maovu. Kwasababu hawa walinyeshewa mvua moja na ngano halisi lakini ndani yao walikuwa ni magugu.
Hivyo Kanisa katoliki lilianza kujitokeza katika kanisa la Mungu kama GUGU la kwanza, enzi zile za kanisa la kwanza, lilianza na mafundisho tu (MBEGU), baadaye likaota mizizi na kujiundia dini inayofanana na ukristo katika kanisa, likazidi kusambaa katika shamba la Mungu na kusonga zile mbegu halisi za Mungu na ndio maana tunaona hili kanisa lilianza kuharibu mafundisho ya NENO LA MUNGU na kupachika mafundisho ya uongo na kama tunavyofahamu tabia halisi ya gugu ni kuharibu kile kilicho halisi, na ndio maana baadaye tunavyosoma katika historia liliuawa watakatifu wa Mungu zaidi ya milioni 68 waliojaribu kwenda kinyume na mafundisho yake ya uongo.
Na lilipofikia kilele likazaa na magugu mengine mengi yanayofanana ni hilo, yakifanya kazi moja, kuiharibu mbegu halisi ya Mungu. Lakini biblia inasema wakati wa mwisho ambao ndio tuliopo sasa, yale magugu na ngano vitatenganishwa, yale magugu yataanza kwanza kwa kufungwa matita matita kwasababu yapo mengi,
JE! HAYA MATITA MATITA NI NINI?..Haya si mengine zaidi ya MADHEHEBU, na watakaoyafunga ni akina nani? Hawa Si wengine zaidi ya wanaojiita viongozi wa dini lakini ndani ni mitume wa uongo (2Wakoritho 11:13).
Mhubiri yoyote anayekupeleka kwenye dini yake zaidi ya kukupeleka kwa Kristo huyo ni mvunaji anayekufunga katika mojawapo ya tita la magugu. Kiongozi anayekufundisha mafundisho yasiyotokana na utakatifu, anakuambia tu! Mungu ni wa rehema, huku hana habari na mambo ya toba au kuhubiri utakatifu yeye anakazania mambo ya ulimwengu huu tu, ujue huyo ni mvunaji anayetaka kukufunga katika mojawapo ya tita la magugu lililoandaliwa kwa ajili ya kuchomwa moto.
Mhubiri anayekuhubira kutwa kuchwa mafanikio tu! Agusii hata siku moja hatma ya maisha yako ya rohoni, anayekuhubiria Kristo harudi leo wala kesho..mkimbie huyo ni mvunaji wa siku za mwisho kazi yake ni kuwafunga watu wa namna hiyo wasiotaka kujihusisha na mambo ya Mungu bali wajihusishao na mambo ya ulimwengu huu tu.
Ukiona kanisa linakuambia hakuna kuzimu na mateso yake, au halitaki kudumu katika NENO LA MUNGU peke yake,linakuongoza katika ibada za sanamu ambazo Mungu amezipinga vikali, kimbia haraka sana hilo ni TITA la kukusanya watu wa dizaini hiyo wasiotaka kudumu kutenda mapenzi ya Mungu..
2Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; KWA SABABU HAWAKUKUBALI KUIPENDA ILE KWELI, WAPATE KUKOLEWA.
11 Kwa hiyo Mungu awaletea NGUVU YA UPOTEVU, WAUAMINI UONGO;
12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.”
Na Kumbuka kila siku hawa wavunaji(Manabii wa uongo) na haya matita ya magugu yanazidi kuongezeka kuonyesha kuwa huu ni wakati wa mavuno wa siku za mwisho.
LAKINI NGANO HALISI NI IPI?
Ukisoma mfano huo kwa makini utaona kuwa NGANO HALISI haijakusanywa katika matita matita mengi kama magugu yalivyofanywa, bali Ngano imekusanywa pamoja mara moja tu na kupelekwa ghalani. Kuonyesha kuwa bibi-arusi wa Kristo hatakuwepo kati ya mojawapo ya hivyo vikundi, Bibi-arusi hana utambulisho wa kimadhehebu. Baada ya kukusanywa maramoja atapelekwa ghalani (mbinguni). Ndugu tunaishi katika wakati wa bibi-arusi wa Kristo kukusanywa kwa ajili ya unyakuo. Na anakusanyikia wapi?.
Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake katika Mathayo 24: 23 “Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.
24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.
25 Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.
26 Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki.”
Hii Ikiwa na maana kuwa katika siku za mwisho watatokea mitume na manabii wengi wa uongo, na zitatokea dini nyingi na madhehebu mengi ya uongo, na kila moja likidai kuwa lenyewe lina Kristo, ili tu yapate kuwakufunga watu kwenye matita yao..lakini Bwana alisema yatakapowafuata na kuwaambia hivyo msisadiki?. Na ndipo wanafunzi wake wakamuuliza..kama hatutawasidiki hao basi tukusanyike wapi sasa? Jibu lake lilikuwa ni hili.
Luka 17: 37 “Wakajibu, wakamwuliza, WAPI, BWANA? Akawaambia, ULIPO MZOGA, NDIPO WATAKAPOKUTANIKA TAI.”
Mzoga ni NENO LA MUNGU, na TAI ni BIBI-ARUSI, Hivyo katika siku hizi za mwisho bibi-arusi safi wa Kristo hatakusanyika katika madhehebu na dini bali atakusanyika katika NENO LA MUNGU tu..yeye hatafungwa na dini bali atafungwa, ‘’na nini NENO linasema’’ Hicho tu. Hii ndio ndio nguvu Mungu aliyoiachia sasa hivi kwa bibi-arusi wake, kurudi katika imani ya Mitume, Biblia.
Hivyo ndugu jitathimini je! na wewe umefungwa kama magugu kwenye matita tayari kwa kuchomwa au unakusanywa ghalani mwa Mungu kwa NENO lake?. Kama umefungwa huko toka, sio kwa miguu bali kwa kugeuzwa moyo wako na kuligeukia NENO linachosema na sio mapokeo ya dhehebu. Kwasababu biblia inatuambia 1Petro 1:23 “Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; KWA NENO LA MUNGU LENYE UZIMA, lidumulo hata milele.”
Hivyo Umeona hapo? Bibi-arusi amezaliwa kwa mbegu isiyoharibika KWA NENO LA MUNGU tu, na sio kitu kingine.
Ni maombi yangu kuwa utazaliwa mara ya pili kwa NENO LA MUNGU na kumtazama Kristo peke yake aliyekufia msalabani ili ufanyike kuwa ngano na sio gugu.
Ubarikiwe.
No comments:
Post a Comment