Mtu ambaye ni mwepesi kuudhiwa, au mwepesi kulia, au mwepesi kukasirishwa basi mtu huyo mara nyingi anakuwa pia ni mwepesi kusahau makosa, au mwepesi kufurahi au mwepesi kucheka..Lakini mtu ambaye ni mzito kuudhika pale anapoudhiwa, au kukasirika au kulia au kuwaka hasira, basi mtu huyo vile vile mpaka afikie hatua ya kukasirishwa na baadhi ya mambo basi ujue kuwa itachukua muda sana kuituliza ghadhabu yake au hasira yake.
Tuchukulie tu mfano mtoto mdogo, kama ukimtazama kwa siku anaweza kulia hata mara tano au sita, utakuta kinachomliza ni vitu vidogo vidogo tu visivyo na maana, lakini mtu huyo huyo dakika chake mbeleni utakuta ameshasahau anacheza na wewe kana kwamba hujawahi kumuudhi kabisa..Lakini tuje kwa mtu mzima, anaweza asidondoshe chozi kwa hata kwa mamiaka, lakini siku ukimkuta analia basi ujue kuna jambo zito, tena zito sana tena sio jepesi hata kidogo, pengine utakuta ni msiba au kaumizwa sana,au kajeruhiwa sana, na hivyo mpaka hali hiyo imtokea ndani yake, basi haiwezi kuwa ni kitendo cha dakika chache kuondoka, pengine itamgharimu miezi au miaka ndipo iishe kabisa.
Hali kadhalika biblia imetuweka wazi kabisa, kuhusu hali ya Mungu wetu wa mbinguni tunaye mwabudu siku zote, yeye ni Mungu mvumilivu sana, ni mwingi wa rehema, ni mnyenyekevu, ni mwenye neema, ni mwingi wa huruma, haoni hasira haraka,..Na ni kweli ndivyo alivyo hata sisi wenyewe tunalishuhudia leo hilo pale tunapoona watu tunaona wanatembea barabarani uchi, watu wanamtukana Mungu hadharani lakini hasemi chochote, watu wanawachinja wenzao kama wanyama bila huruma na Mungu hafanyi lolote, watu wanawakata viungo watoto wadogo wasio na hatia wakiwa hai, na kuchukua viungo vya maalbino, wengine wanawachuna ngozi ili kwenda kuuza kwa waganga, mpaka tunajiuliza hivi Mungu hayaoni haya yote? Mbona hachukui hatua yoyote kali..Ingekuwa ni wewe au mimi ni Mungu ni wazi kuwa hakuna hata mmoja angesalia tungeshawateketeza wote.Lakini kwa Mungu haipo hivyo yeye alisema “..
Bwana si mwepesi wa hasira, (Nahumu 3:1)…Ni mpole wa Hasira, mwingi wa rehema (Hesabu 14:8)
Pia Kutoka 34: 6 "…., Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; 7 mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi;.."
Na pia Daudi anashuhudia hilo na kusema “Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, Zaburi 145:8” Na ukisoma pia Yona 4:2 na Nehemia 9:17..utathibitisha jambo hilo hilo.
Unaona hiyo ndio sifa yake kuu.. Lakini yeye kuonyesha rehema zake hata kwa waovu sio kwamba anapenda kuendelea kuwaona wanafanya mambo yao maovu, bali kinyume chake anataka wote wafikie toba, na ndio maana kila siku anawahubiria watubu, Lakini wasipotaka kutubu, kama tulivyoona kuwa mtu Yule ambaye si mwepesi kuudhika,ikifika siku ameudhika basi jua kuwa ghadhabu yake haiishi leo wala kesho, ndivyo ilivyo kwa Mungu ukali wa hasira yake hakuna atakayeweza kuuzima, si kwa toba wala kwa kulia siku ile itakapofika..
Watu wa kipindi cha Nuhu walipuuzia sana uvumilivu wa Mungu kwao, walihuburiwa injili kwa miaka mingi, lakini waliona mbona hakuna dalili yoyote ya kuadhibiwa, kama vile Mungu hayupo, Mungu hawezi kuangamiza dunia yote na watoto ndani yake,ndivyo walivyokuwa wanajifariji, Nuhu alionekana kama kichaa anacheza lakini siku ile walipoingia kwenye safina, ndipo waovu walipojua kweli hasira ya Mungu ni kali…watu 8 tu kati ya mabilioni ya watu waliokuwa wanaishi duniani ndio waliopona…Vivyo hivyo ilikuwa katika siku za Lutu, na ndivyo itakavyokuwa katika SIKU ILE YA HASIRA YA BWANA kama Bwana alivyoifananisha siku ile na hizo, ambayo hiyo ipo karibuni sana kutokea. Kutakuwa na kulia lakini Mungu hatasikia, kutakuwa na maombolezo lakini Mungu hataokoa, utasema ni wapi tena jambo hilo lilishawahi kutokea kwenye Maandiko,? Wakati wana wa Israeli walipoonywa kwa mamia ya miaka waache maovu na wamgeukie Mungu, lakini hawakutaka, Bwana aliwaonya waache maovu wasije wakapelekwa utumwani hawakusikia, wakatenda maovu mpaka ikafikia hatua ya Mungu kutokusamehe tena..kikombe cha ghadhabu ya Mungu kilikuwa kimejaa juu yao, ulinzi wa kiMungu ukaondoka juu yao, Nebukadneza akaja akawachinja watu mbele ya macho kama kuku, na waliosalia akawapeleka utumwani Babeli.. Tunasoma hayo katika.
2 Nyakati 36: 11 “Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja, alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja;
12 akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, Mungu wake; wala hakujinyenyekesha mbele ya Yeremia nabii aliponena kwa kinywa cha Bwana.13 Tena akamwasi mfalme Nebukadreza, aliyemwapisha kwa Mungu; lakini akajifanyia shingo ngumu, akajitia moyo nguvu asimgeukie Bwana, Mungu wa Israeli.14 Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu.15 Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;16 lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.17 Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake”.
Soma tena mstari wa 15 na wa 16…inasema.. “Bwana aliwatumia wajumbe wake, kwasababu aliwahurumia lakini wakawacheka na kuwadhihaki, hata ilipozidi ghadhabu HATA KUSIWE NA KUPONYA”..Unaona kuna hatua inafika kutakawa HAKUNA KUPONYWA TENA!! Yaliyotokea yametokea, hayawezi kubadilika tena wala kubadilishwa.
Ndugu usidhani ukiachwa sasa kwenye UNYAKUO utakuwa na nafasi ya pili mbele za Mungu, kwamba utatubu na Mungu atakuhurumia, Fahamu nafasi ni moja tu nayo ni kwa Njia ya YESU KRISTO peke yake na sio kwa njia yako, ingekuwepo ipo nafasi nyingine, Yesu asingesema mtu haji kwa Baba isipokuwa kwa njia yangu mimi, badala yake angesema mtu haji kwa Baba isipokuwa kwa njia yangu au yako..Hautafika mbinguni ndugu kama chujio la UNYAKUO litakupita.. Na wote watakaobaki hakuta kuwa na lingine lililosalia kwao isipokuwa kukutana na ghadhabu ya hasira ya Mungu, na hiyo haina lengo lingine zaidi ya kuwaharibu watu wote waovu ambao, walikataa neema, walikataa kuishi maisha ambayo Mungu alikusudia kila mwanadamu ayaishi, ni mapigo ambayo hata mtu aombolezeje hawezi kusikiwa.
Kumbuka hiyo ni tofauti na dhiki ya mpinga-kristo, siku ya Bwana ni tofauti kabisa, ni wakati Mungu aliojitengea kujilipizia kisasi cha hasira yake. Usitamani uwepo huo wakati ukadhani kuwa utastahimili, au utaokoka..
Yoeli 2: kwa kuwa siku ya Bwana ni kuu, yenye kitisho sana; naye ni nani awezaye KUISTAHIMILI.
Bwana anasema tena Siku hiyo watu duniani wataadimika kuliko DHAHABU, kumbuka sio kama dhahabu, hapana! bali kuliko dhahabu…Tafakari hilo neno tunajua dhahabu ni jamii ya mawe, lakini upatikanaji wake sio wa kwenda tu nje na kuikota kama kokoto, ndivyo itakavyokuwa siku hiyo watu watakuwa wachache sana kama vile dhahabu ilivyoadimu, si ajabu hili taifa lote la Tanzania watasalia watu 2 au 3 tu au asisalie mtu kabisa…wakati wa gharika watu waliadimika kama dhahabu, alisalia Nuhu tu wanawe watatu na wake zao.
Isaya 13: 6 “Pigeni kelele za hofu; maana siku ya Bwana i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu.7 Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka.8 Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto.9 Tazama, siku ya Bwana inakuja, SIKU KALI, YA HASIRA NA GHADHABU KUU, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.11 Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;12 NITAFANYA WANADAMU KUADIMIKA KULIKO DHAHABU SAFI, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri.13 Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali.
Adhabu hiyo itakuwa ndani ya yale mapigo ya vitasa 7. (Yohana16 :1-21). Embu tazama kwa ufupi yatakayo tokea.
Ufunuo 16:1 “Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi.
2 Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake.
3 Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa.
4 Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu.
5 Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi;
6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili.
7 Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.
8 Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.
9 Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu yamapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu.1
10 Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu,
11 wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao.
12 Na huyo wa sita akakimimina kitasa chake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua.
13 Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.
14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.
15 (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)
16 Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni.1
17 Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa.
18 Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo.
19 Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake.
20 Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena.
21 Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno.
(Ikiwa utahitaji kufahamu kwa urefu juu ya vitasa 7 nitumie ujumbe inbox, nitukutumie uchambuzi wake wote.)…Sasa baada ya hayo mapigo kuisha kitakachofuata ni Hukumu kisha ziwa la moto.
Lakini hayo ni machache kati ya mengi yatakaowakuta wale wote ambao watakosa UNYAKUO sasa ambapo dalili zote zinaonyesha kuwa kizazi chetu hichi ndio kile Yesu alichokizungumzia kuwa hayo yote yatatimia..Ni saa gani hii tunaishi?..Kwanini huyathamini maisha yako ya milele?..Kwanini unaipuuzia hiyo neema iliyo juu yako? Unazini lakini Mungu hakusemeshi chochote, unatazama pornography kwa siri, lakini Mungu hakuadhibu kwa lolote, unafanya mambo machafu lakini Mungu kama vile hakuoni..sio kwamba anapendezwa na wewe au kwamba wewe ni mtu pekee sana kwake, na ndio maana hayakukuti mabaya sasa..
Lakini fahamu si mwepesi wa hasira ni Mwingi wa hasira..uvumilivu wake ndio unaokuvuta utubu..
2Petro 3:8 “Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, BALI HUVUMILIA KWENU, MAANA HAPENDI MTU YE YOTE APOTEE, BALI WOTE WAFIKILIE TOBA.10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa,”
Usipotubu leo upo wakati mbaya unakusubiria mbeleni usiokuwa na msamaha. Leo hii ukiwa tayari kuyakabidhi maisha yako kwa Bwana kwa kumaanisha kabisa, na sio nusu nusu, mguu mmoja huku na mwingine kule atakusamehe kabisa na kuyafuta makosa yako yote, kwasababu hicho ndicho anachokitafuta kwako.
Na ndio maana anasema:
Sefania 2: 3 “Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; HUENDA MTAFICHWA KATIKA SIKU YA HASIRA YA BWANA”.
Uamuzi ni wako, lakini maombi yangu ni leo utubu ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.Kisha baada ya hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili, kwa Roho Mtakatifu atakayeingia ndani yako”