"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, February 27, 2019

MKUU WA GIZA.


Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, libarikiwe sana. Karibu tujifunze Biblia, leo kwa Neema za Bwana tutajifuza juu ya Namna ya kutoka katika uvuguvugu wa kidunia.

Katika kitabu cha ufunuo sura ya pili na ya tatu tunasoma juu ya ufunuo wa yale makanisa saba, na kama tunavyojua makanisa yale yalikuwa ni makanisa halisi kabisa, yaliyozaliwa kutokana na Injili za Mitume hususani mtume Paulo aliyokuwa anaihubiri nyakati hizo, hata hivyo yalikuwa ni zaidi ya saba, lakini Roho aliyachagua hayo saba kwa kusudi maalum kuyafundisha makanisa ya siku za mwisho ambayo tunayoishi, utaona kulikuwa na makanisa mengine yaliyokuwa Korintho,Galatia, thesalonike,filipi nk lakini hayajatokea katika kitabu cha ufunuo isipokuwa yale saba tu..

Hivyo kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa vipindi vya kanisa utakuwa unajua kuwa, tayari kuna vipindi sita vimeshapita vya kanisa tangu Bwana Yesu Kristo aondoke, na sasa tupo katika kipindi cha kanisa la saba, na kanisa tulilopo ndilo la saba na la mwisho linalojulikana kama LAODIKIA. Kama hujafahamu kabisa jambo hili au ndio mara ya kwanza unalisikia basi katafute kujua kwasababu ni jambo linalojulikana na wasomaji wengi wa biblia, au nitumie ujumbe inbox nikutumie uchambuzi wa nyakati hizi saba za kanisa na wajumbe wake.
Sasa tabia ya hili kanisa la LAODIKIA ni kanisa vuguvugu, kama tunavyosoma katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana mlango wa tatu.

Ufunuo 3: 14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu UNA UVUGUVUGU, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja name”.
Kanisa hili la Laodikia lilianza mwaka 1906, na litaisha siku unyakuo utakapofika, sasa hili kanisa ndilo lililoonyesha tabia ya hatari kuliko makanisa mengine yote ya nyuma, kwasababu mbele za Bwana limepimwa na kuonekana kuwa ni vuguvugu, nusu Mungu, nusu shetani, ni kanisa Nafki, na ndio inayopelekea kuonekana kuwa ni kanisa lililoharibika kuliko makanisa yote.

Sasa huu uvuguvugu unatoka wapi?..Huu uvuguvugu ni Pepo maalumu lililotoka kuzimu, na kutumwa duniani ili kufanya kazi maalumu ya ushawishi, na hili pepo halijatumwa kwa mtu mmoja hapana bali limetumwa kwa kizazi…Ni pepo lenye nguvu mara saba zaidi ya mapepo mengine yote..Ni pepo linalotenda kazi katika viwango vya juu kabisa vya utendaji kazi wa shetani, ambalo kazi yake hasaa ni kuwakosesha wanadamu wa kizazi cha siku za mwisho wamkosee Mungu wao, ili Mungu awakatae kabisa kabisa na kuwakana.

Sasa tujifunze kwa ufupi hili pepo linatendaje kazi, kabla ya kuja kuona madhara atakayoyapata mtu yule endapo hatalishinda..
Biblia inasema katika Waefeso 6: 11 
“Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, JUU YA WAKUU WA GIZA hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”.
Sasa Hawa wakuu wa giza wanaozungumziwa hapa wapo SABA, katika kila kanisa kulikuwa na mkuu mmoja, na katika hili kanisa la Laodikia yupo mmoja na ndiye mwenye nguvu kuliko wote. Na kama jina lake lilivyo “mkuu wa giza” anahakikisha kunakuwa na giza katika ulimwengu wa roho, anahakikisha hakuna nuru, na anahakikisha Nuru ya haki haiwazukii watu.

Na kauli mbiu yake aliyoipokea kutoka kwa shetani mkuu wake ni “KUHAKIKISHA WATU WOTE WANAKUWA VUGUVUGU DUNIANI”…kwahiyo anayo mapepo chini yake anayofanya nayo kazi kuhakikisha anatimiza lengo hilo. Kumbuka huyu mkuu wa anga, hatumshindi kwa kumkemea, hapana! Tutakuja kuona mbeleni namna ya kulishinda hili pepo.

Sasa anachokifanya ni kutumia nguvu za giza, na mapepo yake kuwafanya watu wawe vuguvugu, sio wanakuwa baridi wala moto! Hapana bali wanakuwa vuguvugu, hilo ndio lengo lake kubwa…Anahakikisha watu wamfahamu Mungu kidogo, na waufahamu uovu kidogo!..hataki kabisa mtu awe baridi hilo halitaki, anataka mtu awe hapo katikati..kwasababu anajua Mungu anamchukia mtu vuguvugu kuliko hata mtu yule aliye baridi..yaani kwa Mungu ni heri mtu awe mlevi na mwasherati moja kwa moja, kuliko mtu ambaye ni mwasherati kwa siri na bado anaenda kanisani au bado anasali..Huyo kwa Mungu anafananishwa na MATAPISHI!! Ni Bwana mwenyewe ndio alisema hivyo “ni heri ungekuwa moto au baridi kuliko kuwa vuguvugu”. Hivyo kule kuzimu katika vikao vyao ndio wameona wakifanikiwa kumfanya tu mtu awe vuguvugu, basi watakuwa wamemlaza kwa kila kitu.

Sasa hili pepo lenye nguvu mara saba kuliko mengine ndio lengo lake kubwa hilo!... wengi wanajua kuwa shetani mwanzoni alikuwa ni malaika mbinguni, lakini hawajui kuwa baada ya kulaaniwa hakunyanganywa nguvu zake na akili zake bali aliendelea kuwa nazo..Hivyo ni muhimu kujua kuwa yeye naye anatenda kazi kwa akili sana kiasi kwamba pasipo Roho wa Mungu, ni rahisi kuwadanganya hata yamkini walio wateule. Atahikikisha anatumia ushawishi mkubwa kumfanya mtu ajione yupo sawa na Mungu wakati bado ni mwasherati, mlevi, mla rushwa, anaishi na mwanamume au mwanamke ambaye hawajafunga ndoa, na bado mtu huyo ajione yupo sawa na Mungu n.k.

Huwa inauma sana unapokutana na mtu na unamwuliza umempa Bwana maisha yako na anakujibu NDIO, na unaendelea kumwuliza je! Bwana akija leo una uhakika wa kwenda naye mawinguni anakujibu NDIO nina uhakika kabisa, lakini ukija kumwangalia maisha yake utahuzunika kiasi cha kufa..

Kwamfano kuna mtu mmoja alinitumia ujumbe akaniambia mtumishi naomba uniombee kwasababu ni miaka mingi sasa sijapandishwa kazi, mimi ni kibarua tu,kazi yangu ni ya udereva, na bado ninafamilia, kwakweli alivyokuwa anaeleza alitilisha huruma sana huyu ndugu, nikamwuliza umempa Bwana maisha yako? akanijibu NDIO, nikazidi kumwuliza je! unauhakika Bwana leo akija utakwenda naye? Akajibu Ndio ninauhakika..Nikazidi kumwuliza tena je! una uhakika uovu wote haupo ndani ya maisha yako?.. namaanisha sio mlevi, sio mwasherati, hauna mwanamke unayetembea naye ambaye hamjaoana, sio mtukanaji, sio mla rushwa, sio mtazamaji wa pornography, sio mfanyaji masturbation n.k. akaniambia ndio hafanyi hayo yote!...na zaidi ya yote ameoa na ana mtoto, sasa lengo la kumwuliza vile sio kumweka kwenye mtego hapana! Bali kujua chanzo cha tatizo lake ili nijue namna ya kumsaidia kulingana na maandiko.

Baada ya kuniambia vile basi nikamwambia huna haja ya kuwa na hofu, wala usiogope! Maadamu upo katika mstari wa Bwana, Bwana hawezi kukutupa, Zidi kudumu katika haki subiri wakati wa Bwana, Bwana atakupatia kazi nzuri tu! mwamini yeye, akajibu amina!..Najua alitegemea nimwombee lakini sikufanya vile..

Baada ya siku kadhaa, nikaingia kwenye mitandao, nikakutana na post yake mahali.. “nguvu ziliniishia”…mambo anayo ya-post hata wasiomjua Mungu kabisa wanaona aibu kushiriki na wengine post hizo, ni picha chafu zisizoelezeka!!..Nilijihisi vibaya sana.

Nimekutana na watu wengi sana wa namna hiyo..wanahitaji Bwana awafanyie kitu fulani katika maisha yao, wanatamani wafanikiwe katika maisha, wawe matajiri, lakini hawajijui kuwa wao ni maskini wa roho, wanajiona kuwa ni matajiri wa roho kumbe ni maskini, wanajiona wapo sawa na Mungu kumbe hawamjui Mungu kabisa, ni lile lile pepo la Laodikia ndio lipo juu yao na ndilo linalowapusha wengi macho! Wasitambue ni hali gani mbaya ya kiroho waliyopo.

Nikakutana na dada mwingine nikamwuliza umempa Bwana maisha yako, akajibu ndio nampenda sana, nikamwuliza unamfahamu mtu fulani (nilimtaja tu mhubiri fulani maarufu wa zamani)..akajibu ndio namjua, nikamwuliza ulimsikia wapi..akanitajia nilimsoma kwenye agano la kale!..nikamwambia mbona huyo hayupo kwenye agano la kale,..akaniambiaa aah samahani nilimsoma kwenye agano jipya! Nikwambia hayupo hata kwenye agano jipya, akaniambia yupo wapi?, nikamwambi ni muhubiri tu aliyewahi kutokea miaka hamsini iliyopita nyuma..Huyu pia sikumwuliza kwa nia ya kumtega bali nilikuwa nataka nimfundishe kitu,…lakini tayari yeye alikuwa anajiona anajua kila kitu hana haja ya kitu kingine, baada ya muda mfupi nilijaribu kumpeleka kwenye maandiko nimfundishe, akakwazika akaondoka.

Nikakutana na mwingine tena, …nikamwuliza dada umempa Bwana Yesu maisha yako akanijibu ndio nimempa, ndio mwokozi wangu na ninampenda sana, nikamwambia akija leo una uhakika wa kwenda naye, akanijibu kabisa asilimia 100, nikamwuliza unamjua aliyeandika kitabu cha mhubiri? Akasema hamjui, nikamwuliza aliyendika kitabu cha wimbo uliobora je! akasema pia simjui, nikamwambia kama kweli unampenda Bwana ingekupasa kuyajua haya yote na zaidi ya haya, ila sikulaumu!..nikataka kujaribu kumfundisha msingi wa imani ya kikristo kwanza ndipo tuendelee mbele..hakutaka kuendelea kuongea akakatisha mazungumzo na kuondoka.

Hilo ndio tatizo la watu wengi katika kizazi chetu hichi cha Laodikia, Tunamwomba Mungu utajiri, na wakati ndani ya mioyo yetu ni Adui yetu, tangu lini mtu akaenda kumwomba adui yake gari, au mali au fedha?? Je! Atampa? Sharti apatane naye kwanza ndipo hayo yote apewe…Wengi leo wanapenda kwenda kumwomba Mungu mali wakati ndani ya mioyo yao wamekorofishana naye, ni matapishi mbele za Mungu, wapo mbali naye, ndani ya mioyo yao kuna kila aina ya uchafu..uasherati, ulevi, rushwa, anasa, mizaha, usengenyaji, pornography, punyeto n.k Biblia inasema ..” 
Mathayo 23:25 Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. 26 Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.”
Ni lile lile pepo la LAODIKIA linalotenda tenda kazi katika siku hizi za mwisho, kuwafanya watu wajione kuwa wana kila kitu katika roho, wakati ni maskini wa roho..
Bwana Yesu anasema maneno haya… “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi”.

Ndugu unayesoma ujumbe huu, kamwe usiruhusu hii roho ya uvuguvugu, kila siku yachunguze maisha yako, shetani yupo kazini, kuhakikisha kuwa unakuwa hapo katikati, si moto wala si baridi…Na kama maandiko yalivyotangulia kusema, Ni heri uwe baridi kabisa…ni heri ukawe mwasherati na useme hujaokoka, ni heri uwe mvaaji vimini na mpakaji lipstick na wanja na useme hujaokoka, ni heri uwe unaenda disco kila siku au unaishi na mwanamke/mwanamume ambaye hamjaoana na useme sijaokoka na wala simjui Mungu, wewe adhabu yako siku ile haitakuwa kubwa, kuliko useme mimi nimeokoka na unampenda Bwana wakati bado unavaa vimini, tena bila aibu unauonyesha maungo yako wazi kwenye mitandao, bado unapaka wanja mfano wa Yezebeli na lipstick kiasi kwamba tofauti yako na mwanamziki maarufu wa kidunia hapa nchi hakuna. Unamdhihaki Mungu. Wewe mbele za Mbele za Mungu ni matapishi na kinyaa.

Ni heri ukatubu sasa, na kukusudia kuacha hayo mambo, usiruhusu fikra zako zipotoshwe na mkuu wa ulimwengu huu(shetani) kwa kupitia wakuu wake wa anga..
Waefeso 2: 1 “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;
2 ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, NA KWA KUMFUATA MFALME WA UWEZO WA ANGA, ROHO YULE ATENDAYE KAZI SASA KATIKA WANA WA KUASI;
3 ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.
4 Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda;”
Unaona? Bwana anaweza kukugeuza ukikusudia kumfuata kweli kweli, unachopaswa kufanya ni kutubu kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi, na kufanya maamuzi ya kutokuwa vuguvugu tena!! Hiyo ndio njia pekee ya kulishinda hili PEPO (MKUU WA ANGA) wa Laodikia…Ni kufanya maamuzi thabiti kwamba kuanzia leo mimi na dhambi basiii….lipstick basi, vimini basi, ulevi basi, uasherati basi, rushwa basi, anasa basi, marafiki wabaya basi, pornography basi,..Huo ndio ushauri wa Bwana alioutoa kwa kanisa la Laodikia…anasimama mlangoni na kubisha, hataingia mpaka wewe umefungua mlango, hatavunja mlango wa moyo wako na kuingia kwa nguvu, anasubiri wewe ufanye maamuzi ya kuacha dhambi, ndipo aingie. Na baada ya hapo fanya hima ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo. Usishirikiane kabisa na MKUU WA GIZA HILI, na Bwana mwenyewe atachukua nafasi ya kuhakikisha haujikwai.

Mungu akubariki. Tafadhali "share" ujumbe kwa wengine.

No comments:

Post a Comment