Wengi tunafahamu habari za Yusufu, tunajua alikuwa ni mmoja wa watoto wa Yakobo aliyependwa sana na baba yake, Lakini baada ya kuota zile ndoto tu, ndugu zake walianza kumwonea wivu, na mwisho wa siku wakaamua kumuuza kama mtumwa kwa watu wa mataifa (Wamisri). Na kama tunavyoisoma habari alipokuwa kule Misri Mungu alikuwa pamoja naye akamfanikisha katika mambo yote, akawa wa pili baada ya Farao mfalme wa Misri, kiasi cha kwamba hakuna mtu yoyote aliyeweza kufika kwa Farao bila kupitia kwanza kwake, Mali na vitu vyote vya Misri Farao alivikabidhisha kwa Yusufu,[Kumbuka Misri ndiyo iliyokuwa ngome yenye nguvu kuliko zote duniani kwa wakati ule], tunaweza kusema mfano leo hii taifa la Marekani lilivyo.
Lakini habari hii ya maisha ya Yusufu na yote aliyoyapitia imebeba siri na ujumbe mzito katika roho kwa kanisa,. Yusufu anafananishwa na Bwana wetu Yesu Kristo, na Farao anafananishwa na Baba yetu wa mbinguni. Wale wana 11 wa Yakobo wanafananishwa na wayahudi [yaani waisraeli], na Taifa la Misri Yusufu alipokimbilia linafananishwa na Kanisa la mataifa [wakristo], na Yule mke wa Yusufu (Asenathi) ambaye alimpata katikati ya wa-Misri kutoka katika jumba la kifalme la Farao, anafananishwa na BIBI-ARUSI safi wa Kristo.
Kama vile Yusufu alivyoonewa wivu na ndugu zake na kukataliwa, kisha kwenda kuuzwa utumwani, vivyo hivyo Bwana Yesu alipokuja duniani kwa ndugu zake wayahudi kama masihi wao waliyekuwa wanamtazamia kwa siku nyingi, walimwonea wivu, alipojishuhudia kuwa yeye ndiye mwana wa Mungu, wakamdharau hivyo wakamfanyia hila, wakamkataa kabisa na kumtia mikononi mwa warumi na kumuua [Huko ndiko kumuuza kwa watu wa Mataifa].
Na ndio maana ukisoma biblia utaona mtume Paulo anawaambia hivi wayahudi;
Matendo 13:46 “ Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza [wayahudi]; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa.47 Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.48 Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.49 Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote".
Unaona hapo walimkataa Kristo, ambaye alikuja kwa ajili yao..Bwana hakuwahi kujidhihirisha kwa mataifa hapo kabla, ile neema ilikuwa ni kwa wayahudi tu ndugu zake waliokuwa wakimtazamia kwa muda mrefu, Na ndio maana alisema katika Mathayo 15:24 ".... Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” lakini kwa kuwa wao walimwonea wivu kama vile wale watoto wengine wa Yakobo walivyomwonea wivu ndugu yao Yusufu, basi ile neema ikaondoka kwao na kuja kwetu sisi watu wa mataifa [ambao katika habari hii tunaweza kusema wamisri],
Lakini jambo lingine pia la kuliangalia ambalo limejificha katika maisha ya Yusufu alipokuwa Misri, ni kwamba utaona watu wengi wa Misri hawakuwa na imani sana na Yusufu, kama alivyokuwa nayo Farao kwa Yusufu. Na ndio maana utaona, wakati wa kile kipindi cha miaka 7 ya neema, ni Yusufu peke yake aliyekuwa akifanya bidii kutimiza yale maono aliyoyaona juu ya njaa itakayokuja kuikumba karibia dunia nzima. Kama wale watu wa Misri wangekwenda sambamba na Yusufu baadaye utaona baada ya njaa kuanza kuipiga dunia wasingekuwa nao pia wanatangatanga kwenda kuomba na kununua chakula kwa Yusufu, kwa kuwa ni raia wa nchi yao, Yusufu asingewauzia chakula, wala kubadilishana nao chakula kwa mali na mashamba yao..angewapa bure, au kuwauzia kwa gharama ambayo isingelazimu mpaka kutoa mali zao na vitu vyao.
Inaonyesha wazi kabisa wale watu, hawakuyasadiki maono ya Yusufu kwa kiwango kikubwa pindi alipowaambia wakusanye hazina kwa wakati wa ukame unaokuja huko mbeleni. Ni mfano dhahiri wa wingi wa wakristo waliopo leo ambao ni kweli walimpokea Masihi (yaani Kristo) kama Mwokozi wao, lakini wameyapuuzia yale aliyowaambia yatakayokuja kuipata dunia huko mbeleni pindi itakapopitia miaka ya njaa na ukame wa rohoni na wa mwilini ( yaani wakati wa ile dhiki kuu).
Mtu pekee ambaye hakuathirika na ile dhiki ya njaa ilipokuja duniani kote ni MKE WA YUSUFU tu peke yake kwasababu yeye alikuwa katika JUMBA LA KIFALME..Akizipeleleza zile siri za ndani kabisa zilizokuwa katika moyo wa Yusufu..na kama ukichunguza vizuri utaona yule mke Yusufu hakumtwaa ovyo ovyo tu mahali popote hapana, bali alipewa na Farao mwenyewe.. Ni mfano halisi wa BIBI-ARUSI wa KRISTO, wateule wa Mungu, ambao ni Mungu pekee yake ndio anayempa KRISTO.
Kumbuka ndugu, katikati ya wanaojiita wakristo yapo makundi mawili, yupo BIBI-ARUSI wa Kristo yaani MKE wa Bwana Yesu, na wapo Masuria, hawa wanafananishwa na wanawali werevu na wanawali wapumbavu.(Mathayo 25). Katika siku za mwisho makundi yote mawili yatakuwepo, na litakalokwenda kwenye unyakuo ni lile tu la wanawali werevu yaani BIBI-ARUSI wa Kristo.
Sasa kama vile Yusufu alivyokuwa ni mkuu wa Wamisri wote (yaani watu wa mataifa), waliomwendea na kumwomba chakula wakati wa dhiki, ambapo kwa wakati huo mke wa Yusufu alikuwa anakula raha katika jumba la kifalme.
kadhalika na katika siku za taabu za ile dhiki kuu ya mwisho, wapo wakristo vuguvugu ambao wao wasingepaswa kupitia dhiki, lakini wataipitia kwa upumbavu wao, wakati wenzao (wale BIBI-ARUSI wa Kristo) wapo mbinguni kwa Baba kwenye enzi ya kifalme katika karamu ya mwana-kondoo.
Na kama vile dalili ya kipindi cha dhiki kuanza ni kuona ndugu zake Yusufu wanaanza kwenda kutafuta chakula Misri pamoja na wamisri wenyewe kuanza kutangatanga huku na kule kutafuta chakula, Vivyo hivyo Na katika kipindi hichi tunachoishi sasa, Njaa ya kulisikia Neno la kweli inaongezeka.
Wayahudi kwa miaka mingi wamekuwa wakimtazamia masihi wao aje kuwakomboa, lakini hawaoni chochote kwa kipindi chote hicho, lakini nyakati hizi kidogo kidogo, tunaona wanaanza kujua makosa yao, kwamba hakuna Masia mwingine atakayekuja, wanaanza kutambua kuwa kuna chakula Misri yaani kwa Wakristo, wanaanza kuona mbona Yule waliyemkataa ndiye amekuwa TEGEMEO LA DUNIA NZIMA?.
Ndugu yangu siku ile watakapotubu tu!, basi ujue kile kipindi cha DHIKI KUU kimeshaanza, na neema haitakuwepo tena kwa watu wa mataifa, kama ndugu zake Yusufu walivyomlilia ndivyo itakavyokuwa kwa wayahudi kwa wakati huo, waisraeli watafumbuliwa macho kikabisa kabisa na kumtambua Yesu Kristo, biblia inasema watamwombolezea yeye waliyemchoma…
Zekaria 12: 10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao WATAMTAZAMA YEYE AMBAYE WALIMCHOMA; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido"
Sasa baada ya hapo itakuwa imebaki miaka michache tu mpaka ile miaka 7 ya mwisho iishe, na baada ya hiyo dunia itakuwa imeisha, wakati huo duniani kutakuwa na dhiki isiyokuwa ya kawaida, huo ndio wakati watu wote watakapojua kuwa YESU KRISTO NDIYE JIWE KUU LA PEMBENI LILE LILILOKATALIWA NA WAASHI, Watu wa ulimwengu wote watajua kuwa ufalme na mamlaka yote ya mbinguni na duniani amekabidhiwa YESU KRISTO, na Hakuna WOKOVU NA UZIMA nje ya yeye. Kama vile watu wa kipindi cha Yusufu walivyofahamu kuwa malmlaka yote na ufalme amekabidhiwa Yusufu.
Unaweza ukaona ni wakati gani tunaishi, Taifa la Israeli linazidi kunyanyuka, hivi karibuni waisraeli watafumbuliwa macho yao na kumtambua Yesu Kristo, je! Wewe ni miongoni mwa Bibi-arusi atakayeenda kwenye unyakuo siku ile kabla ya DHIKI KUU KUANZA? Unamchukulia Bwana Yesu Kristo kwako kama nani?, je! Unamchukulia kama ni mtu wa kawaida tu, au mfalme?, kumbuka Yusufu alivyokuwa gerezani sio sawa na alivyofanywa mfalme, na vivyo hivyo Bwana Yesu Kristo, alivyokuwa pale msalabani kalvari sio sawa na alivyo sasa, Biblia inasema ameketi katika NURU ISIYOWEZA KUKARIBIWA, na maneno yake ni kweli na uzima..
Hivyo kama hujaingizwa katika ile familia ya kifalme, hautaweza kuikwepa dhiki, kama hujazaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho, hautaweza kuuingia katika karamu ya mwana kondoo kule mbinguni, kwanini ukose hayo yote?? Jitahidi kufanya hivyo sasa kabla mlango haujafungwa. Tubu leo mgeukie Bwana azioshe dhambi zako, naye atakupa neema ya kuwa miongoni mwa Bibi-arusi wake. UNYAKUO NI SIKU YOYOTE.
Ubarikiwe!
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.
Kwa mpangilio mzuri wa masomo haya tembelea website yetu hii >>> www.wingulamashahidi.org