"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, August 29, 2018

JE! NYWELE ZAKO ZINAOTA AU ZIMESIMAMA?

Mambo yote yaliyoandikwa katika agano la kale ni kivuli cha mambo yanayoendelea katika roho katika agano jipya tulilopo sasa. Kwamfano kama vile tunavyoweza kusoma Mungu alivyowaita wana wa Israeli kutoka Misri, kuelekea Kaanani kupitia jangwani, ndio hivyo hivyo Mungu anavyowaita watoto wake leo kutoka katika utumwa wa dhambi [Misri], kisha anawavusha katika bahari ya shamu [ambao ndio ubatizo 1Wakorintho 10], na baada ya hapo safari ya jangwani inaanza ambayo hiyo ni lazima kila mkristo aipitie, mahali ambapo atafundishwa kumcha Mungu, na kumtegemea yeye kwa kila kitu, mahali ambapo Mungu ataruhusu ajaribiwe kwa kila kitu lakini hataachwa. Na hatua ya mwisho ni Kuingia Kaanani, Ambayo nayo inaanzia hapa hapa duniani kisha kumalizikia kwenye nchi mpya na mbingu mpya..

Kadhalika tunajifunza pia jambo lingine katika habari ya Samsoni, ambayo nayo ni kivuli cha mambo yanayoendelea sasa hivi katika roho. Tunasoma Samsoni Mungu alimtia mafuta tangu alipokuwa tumboni mwa mama yake, akifananishwa na kanisa la Kristo jinsi lilivyoanza pale Pentekoste lilikuwa takatifu na safi lisilokuwa na waa lolote, Tunasoma pia Samsoni aliamuriwa na Mungu asikate nywele zake bali azifunge katika vishungi saba, Picha halisi ya kanisa la Kristo ambalo tunaona katika kitabu cha Ufunuo sura ya 2 &3 Bwana Yesu akitoa ujumbe kwa yale makanisa 7, Kumbuka kanisa la Kristo limekuwa likipita katika vipindi 7 tofauti tofauti vinavyojulikana kama NYAKATI 7 ZA KANISA kwa muda wa miaka 2000 sasa, na katika majira tunayoishi ni majira ya kanisa la mwisho la 7 linaloitwa LAODIKIA.

Kama vile Samsoni nguvu zake zilivyokuwa katika zile nywele, hivyo kanisa nalo katika nyakati zote saba limekuwa likitegemea nguvu zake katika NENO LA MUNGU ili likae. Lakini kwa habari mbaya tunasoma Samsoni alionyesha tabia za uasherati za kwenda kuzini na wanawake makahaba na wanawake wasio wa uzao wa Ibrahimu, na ndio hao baadaye waliokuja kujua siri ya nguvu zake, biblia inasema katika Mithali 31: 3 “Usiwape wanawake nguvu zako;”

Lakini Samsoni yeye hakufanya hivyo, badala yake alikubali kulaghaiwa na wale wanawake wasiomjua hata Mungu wa Israeli, wanawake wa kidunia, matokeo yake akaangukia katika mikono ya maadui zake wafilisti kwa muda mrefu, tunasoma;

Waamuzi 16: 15 “Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi.
16 Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa.
17 Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.
18 Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.
19 Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.
20 Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha.
21 Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.

Unaona hapo?. Ndio jambo hilo hilo lililikuta kanisa la Kristo mara baada ya mitume kuondoka, Paulo aliandika hivi…Matendo 20: 29 “Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi;
30 tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.”


Hivyo katika agano jipya Delila anafananishwa na kanisa kahaba na hili kanisa si lingine zaidi ya kanisa Katoliki, ambalo lilianza kwa kuanza kupenyesha mafundisho potofu ya uongo ndani ya kanisa la Mungu, na hatimaye kufanikiwa kutengeneza dini kabisa, mnamo mwaka 325 WK katika Baraza la Nikea, lilifanikiwa kuyachanganya mafundisho ya kikristo na ibada za kipagani za kirumi, huko ndiko kulikozuka ibada za miungu mingi, ibada za sanamu, kusali rozari, kuomba kwa watakatifu waliokufa kale, mafundisho ya kwenda toharani, kanisa kuongozwa na vyeo vya kibinadamu badala ya karama za Mungu, mambo ambayo hayapo katika maandiko wala hayakuonekana katika kanisa la kwanza.

Na kanisa hili lilipozidi kupata nguvu kwa kuwashawishi watu na kuwadanganya kidogo kidogo nguvu za Roho Mtakatifu zikaanza kupungua katika Kanisa, na hatimaye kupoa kabisa isipokuwa kwa kikundi kidogo sana cha wateule, na kupelekea kanisa kupitia katika kipindi kirefu cha giza kwa zaidi ya miaka 1000, ni kipindi kinachojulikana katika historia kama KIPINDI CHA GIZA.

Katika siku ile kwenye hilo baraza la Nikea ndio siku hiyo huyu mwanamke kahaba [Kanisa Katoliki] anayefananishwa na Delila alifanikiwa kuzinyoa nywele za kanisa la Mungu kabisa, hivyo nguvu za kanisa zilipoa kwa muda mrefu sana, kukawa hakuna tena karama za rohoni, biblia ikazuiliwa kusomwa kwa washirika, zile nguvu za watu kumwamini Kristo zilizoanza pale Pentekoste zikafa, watu waliojaribu kushikilia mafundisho ya mitume waliuliwa, mafundisho ya watu kuhesabiwa haki kwa Imani katika Yesu Kristo yakafa badala yake watu wakawa wanafundishwa kuhesabiwa haki kwa kuwa mshirika wa kanisa Katoliki, utozwaji wa pesa wa vitu vinavyoitwa vya ki-Mungu ukaanza, kwamfano mtu akitaka kuombewa ni lazima atoe kiwango Fulani cha fedha kwa kasisi ili ahudumiwe, mtu akitaka kuwekewa wakfu mtoto wake au mali zake mbele za Mungu, sharti kwanza atoe kitu Fulani, na asipofanya hivyo basi hatapata huduma yoyote, mambo ambayo hayakuwepo katika kanisa la kwanza..n.k.

Lakini kama tunavyosoma baada ya Samsoni kutumika muda mrefu kusaga ngano katika magereza ya Wafilisti tunaona nywele zake zilianza kuota tena pasipo wao kujua. Na zilipomalizika kuota, madhara aliyoyaleta mwisho yalikuwa ni makubwa kuliko yale aliyoyafanya kule mwanzoni kama tunavyosoma..
Waamuzi 16: 22 “Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake.
23 Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, Mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu.
24 Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, Mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.
25 Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili.
26 Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea.
27 Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza.
28 Samsoni akamwita Bwana, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili.
29 Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto.
30 Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. BASI WALE WATU ALIOWAUA WAKATI WA KUFA KWAKE WALIKUWA WENGI KULIKO WALE ALIOWAUA WAKATI WA UHAI WAKE”.

Kadhalika na katika kanisa jambo ni lile lile ulipofika wakati nywele za Kanisa kuanza kuota tena, [na kuota kwenyewe ni kurudi kwenye NENO kwenye mafundisho ya mitume]..Ndipo hapo Bwana akaanza kuwanyanyua watu wa kulitengeneza kanisa akawanyanyua wakina Martin Luther, mjumbe wa kanisa la tano, katika karne ya 16 akifundisha mafundisho ya kuhesabiwa haki kwa Imani katika Kristo Yesu, na sio katika dini ya kikatoliki, Bwana akawanyanyua wakina John Wesley na wenzake, katika karne ya 18 wakifundisha utakaso wa damu ya Yesu, kwamba Kristo amekuja ili umfanye mtu kuwa mtakatifu kwamba pasipo huo hakuna mtu atakayemwona Mungu, (Waebrania 12:14) na sio kwamba pasipo ushirika wa kanisa watu hawatamwona Mungu…

Vile vile katika kipindi cha kanisa la mwisho la Laodikia ambalo lilianza mwanzoni mwa karne ya 20 mpaka sasa, Bwana aliwanyanyua wakina William Seymor na wengine katika uamsho wa mtaa wa Azusa kule Marekani pamoja na William Branham ambaye ni mjumbe wa kanisa la mwisho la LAODIKIA, na mafundisho ya Ubatizo wa Roho Mtakatifu, ya kwamba Roho Mtakatifu ndio MUHURI WA MUNGU (Waefeso 4:30). Na wote wasiokuwa na Roho wa Mungu hao sio wake (Warumi 8:9), Na ndio maana inajulikana kuwa tunaishi katika nyakati ya KI-Pentekoste kama ilivyokuwa kule mwanzo, na ndio maana katika nyakati hii zile karama zilizokuwa zimeuliwa na Kanisa Katoliki Bwana alianza kuzirejesha tena kuanzia mwanzoni mwa karne ya 20..(Yaani kuanzia mwaka 1900 na kuendelea)
Lakini haya yote ni kwa ajili ya kumwandaa BIBI-ARUSI wa kweli wa KRISTO kwa ajili ya unyakuo uliokuwa karibu kutokea. Zile nywele zimeshafikia ukomo, ni jambo moja tu linasubiriwa, Uamsho wa mwisho wa BIBI-ARUSI kupitia ufunuo wa zile ngurumo 7 kama tunavyosoma katika ufunuo 10:14, Ambazo hizo zitampa Bibi-arusi imani timilifu (Luka 18:8) ya kwenda katika unyakuo, ni uamsho wa kipekee, nao utakuwa ni wa muda mfupi sana utakaokuwa wa nguvu na wa ajabu kuliko hata ule uamsho wa kwanza uliotokea kule Pentekoste kama vile Samsoni baada ya nywele zake kukua tena, maangamizi aliyoyaletea mwishoni yalikuwa ni makubwa kuliko hata yale ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa Bibi-arusi wa Kristo katika hichi kipindi cha kukaribia na unyakuo.

Na wewe je! Ni miongoni mwa watu ambao nywele zao zimekuwa?? Au bado tu unatumikia katika dini na madhehebu? Kumbuka kuota nywele maana yake ni kurudi katika Neno, nguvu za mkristo yoyote Yule hazipo nje ya Neno la Mungu..Biblia inasema usiabudu sanamu, wala usijifanyie sanamu ya kuchonga, lakini kanisa lako linasema ni sawa kufanya hivyo..hapo unapaswa ufuate kile Neno linasema na uweke chini kile kanisa linasema.


Biblia inasema aaminiye na kubatizwa ataokoka, [na maana ya kubatizwa ni kuzamishwa kwenye maji mengi], lakini kanisa linasema haijalishi, linasema ubatizo wa kunyunyiziwa ni sawa..Hapo unapaswa uweke chini mapokeo ya kanisa na kuchukue kile mitume walichokifanya kwenye biblia…

Matendo 2: 37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.”


Hivyo ndugu hizi ni siku za mwisho, huu ni wakati wa kuhakikisha nywele zako zinakuwa, tafuta uhusiano wako binafsi na Mungu, Rudi kwenye Neno la Mungu, dini na madhehebu hayatakufikisha popote, kumbuka watakaokwenda kwenye unyakuo ni wachache biblia inasema hivyo..Je! umezaliwa mara ya pili? Kwa kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu.?

Mungu akubariki.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu.

Kwa mpangilio mzuri wa masomo haya tembelea website yetu >>> www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment