1Wafalme 19: 9 Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama Neno la BWANA likamjia, naye akamwambia, UNAFANYA NINI HAPA ELIYA?.10 Akasema nimeona wivu mwingi kwa ajili ya BWANA Mungu wa majeshi ; Kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe.11 Akasema, toka, usimame mlimani mbele za BWANA. Na tazama BWANA akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunjavunja miamba mbele za BWANA; Lakini BWANA hakuwamo katika upepo ule; Na baada ya upepo tetemeko la nchi; lakini BWANA hakuwamo katika lile tetemeko la nchi;12 Na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; Lakini BWANA hakuwamo katika moto ule; Na baada ya moto sauti ndogo ya utulivu.13 Ikawa Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama sauti ikamjia, Kusema, UNAFANYA NINI HAPA, ELIYA ?.
Tukirudi nyuma kidogo katika habari hii, tunasoma kabla ya Eliya kukimbilia mlima Horebu alienda kuwaua wale manabii wa Baali , baada ya kuona Israeli yote imekengeuka kwa kuigeukia miungu migeni, lakini pamoja na kuwaua hao, akapata taarifa nyingine kuwa malkia, [mke wa mfalme Ahabu aliyeitwa Yezebeli] anataka kumwangamiza yeye naye kama alivyowaua manabii wa baali, Kumbuka Yezebeli alikuwa ni mkatili sana alifanikiwa kuwaangamiza manabii wengi wa Mungu waliokuwa Israeli kwa wakati ule, na baadhi yao waliosalia walikuwa wanaishi kwa kujifichaficha mapangoni siku zote za maisha yao.
Hivyo njia pekee Eliya aliyoiona ya kupata suluhisho la mambo yote ni kukimbilia katika mlima wa Mungu uliokuwa mbali sana na Israeli, [Ni ule ule mlima ambao Mungu alisema na wana wa Israeli hapo kwanza] akae huko ajitete mbele za Mungu. Na ndio ule ule Mlima Mungu aliomwitia Nabii Musa ampe yale maagizo na sheria kwa wana wa Israeli kwamba wayashike siku zote za maisha yao, Sasa mlima huo ulikuwa ukijulikana kama mlima mtakatifu wa Mungu kwa wakati ule, ndio unaoitwa mlima Sinai au mlima Horebu.
Hivyo Eliya kwa kufikiria kwake aliona ni vema amwendee Mungu, kama Musa alivyomwendea, kwa kufuata kanuni zile zile,..Na ndio maana tunaona Eliya alifunga siku 40 usiku na mchana bila kula wala kunywa chochote, jambo ambalo Musa alilifanya. Akijua kuwa kule Mungu atazungumza naye kama alivyozungumza na Musa, pengine ataitikisa dunia tena na kuikomboa Israeli kwa Ishara na mapigo makubwa kutoka kwa ile miungu ya kipagani [ma-baali] aliyoacha Israeli kama kipindi kile Bwana alivyofanya kule Misri..Alifika mpaka kilele cha mlima Sinai na kukaa kule, katika pango mojawapo, akingoja Bwana azungumze naye. Na ni kweli tunasoma Bwana alishuka na kuzungumza naye kama alivyozungumza na Musa.
Ndipo sauti ya Mungu isiyoambatana na chochote ikasema naye na kumuuliza, ELIYA UNAFANYA NINI HAPA?. Lakini Eliya hakuielewa kwasababu matarajio yake hayakuwa hayo!!, yeye alitazamia Mungu atazungumza naye kwa moto, na tufani na upepo wa kisulisuli kama alivyofanya kwa Musa mtumishi wake na kwa wana wa Israeli zamani zile kwenye mlima huo huo.. Lakini baada ya kitambo kidogo Bwana akamwambia Eliya toka usimame nje! Utazame uone,…
Ndipo Mungu akapita kwa UPEPO mwingi sana uliopasua miamba, na MATETEMEKO, na MOTO kama Eliya alivyotazamia, kwa mfano ule ule aliojidhihirisha kwa wana wa Israeli na kwa Musa..Lakini pamoja na ishara zote hizo na maajabu yote yale Eliya alipata ufahamu na kugundua kuwa kuna kitu hakipo sawa kwenye hizo ishara zote kadhalika na kwenye ule mlima …
Na ndipo Mungu akazungumza naye tena kwa mara ya pili kwa sauti ya utulivu na kumuuliza.. ELIYA UNAFANYA NINI HAPA?, Hapo ndipo alipogundua ile ilikuwa ni sauti ya Mungu inayosema naye, hivyo kwa aibu na kwa hofu akijifunika uso wake jambo ambalo hapo mwanzo hakufanya iliposema naye kwa maneno hayo hayo!!.. Alipogundua kuwa Mungu hayupo katika mlima Sinai uwakao moto, Mungu hayupo katika matetemeko, Mungu hayupo katika upepo wa kisulisuli na tufani, Mungu hayupo katika nguzo ya moto, Mungu hayupo katika Wingu, Mungu hayupo katikati ya kijiti kinachowaka moto, Mungu hayupo katika mvua ya mawe..Alitambua kuwa Mungu yupo katika SAUTI NDOGO YA UTULIVU, Kwamba hata ishara zile wana wa Israeli Mungu alizokuwa anawaonyesha kule jangwani hazikuwa uthibitisho wa kuwa Mungu alikuwa katikati yao, Mungu alizutumia zile kama ishara tu, ili wamwamini atakapotaka kuzungumza nao wamsikie.. Eliya aliligundua hilo. Zile SHERIA Mungu alizompa Musa ndio iliyokuwa SAUTI NDOGO YA UTULIVU iliyokuwa inasema mioyoni mwao, > usiabudu miungu mingine, waheshimu baba yako na mama yako, usiue, usiibe, n.k..
Hivyo mtu yeyote ambaye angezitii zile sheria hata asingeona ishara yoyote ile, Mungu angekuwa katikati yake, angekuwa ameisikia sauti ndogo ya Mungu ya utulivu..Lakini wengi wao waliona upepo, na matetemeko, na moto, na bahari kugawanyika, na miamba kutoa maji, lakini hawakuitambua sauti ya Mungu iliyokuwa inazungumza nao katikati yao, walidhani kuwa ile zile ishara ndio utimilifu wa wote wa Mungu, mwisho wa siku wengi wakaangamia jangwani.
Kadhalika na katika wakati wetu huu wa agano jipya Kanisa lilipoanza tunasoma katika ile siku ya Pentekoste [Ambao ndio mlima Sinai wetu], Mungu alishusha vipawa na ishara nyingi katikati ya wateule wake, Bwana alishuka na UPEPO wa KISULISULI kama ulivyowashukia wana wa Israeli kule jangwani na Eliya, Soma;
Matendo 2: 1 Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. 2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa UPEPO wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. 3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama NDIMI ZA MOTO uliowakalia kila mmoja wao. 4. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.
Unaona hapo? siku ile ya Pentekoste, Moto ulishuka kama ndimi za moto ukakaa juu ya watu, karama tofauti tofauti zikaanza kujionyesha katikati ya watu, wakaanza kunena kwa Lugha mpya, watu wakaanza kutabiri, miujiza na ishara zisizokuwa za kawaida zikafanyika katikati ya watakatifu, nchi ikatikiswa kwa matetemeko ya nguvu za Roho wa Mungu (Soma Matendo 4:23-31)…Lakini Mungu hakuwepo katikati ya hivyo vitu vyote, Mungu aliviruhusu viwepo kama ishara tu ya watu kuwa tayari kumsikia ni kati gani anataka kusema katikati yao.
Hivyo lile kundi dogo lililokuwa limekusudiwa kumwona Mungu baada ya zile ishara, na maajabu liliisikia ile sauti ndogo ya utulivu na ndio maana tunaona katika ile siku tu ya kwanza ya Pentekoste watu walipokuwa wanazistaajabia zile ishara kuona watu wanashukiwa na ndimi za moto, na kuzungumza katika lugha nyingine mbali mbali ndipo wale watu wakamwambia Petro na mitume wengine, sasa tutendeje ndugu zetu?...Ndipo Petro akawajibu,
Matendo 2: 37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, tutendeje, ndugu zetu? 38 Petro akawaambia TUBUNI, MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.
Unaona hapo, wale watu hawakumwambia Petro moto huu ni wa ajabu, upepo huu ni wa kipekee,Hakika Mungu kaonekana, Mungu kajifunua, Mungu ni mwema, leo katutembelea haleluya hapana.! Bali wao moja kwa moja walimuuliza Petro na mitume wenzake, TUTENDEJE NDUGU ZETU?.. Na ndipo ile sauti ndogo ya Mungu ya utulivu ikawaambia “TUBUNI” maana yake ni Geukeni mwache njia zenu mbaya .. Kama tu vile ile sauti ndogo ya utulivu ilivyomwambia Eliya kule mlima, UNAFANYA NINI HAPA ELIYA? “RUDI” KATIKA NJIA YA JANGWA, [maana ya kurudi ni kugeuka urudi ulikotoka].
Lakini katika hichi kipindi cha siku za mwisho, kile ambacho Bwana Yesu alisema katika Mathayo 7:22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?. 23 Ndipo nitawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” …Kimeshindwa kuisikia sauti ya Mungu inayonena katika utulivu badala yake kimeng’ang’ana na yale madhihirisho ya Roho kwamba ndio uthibitisho kuwa Mungu yupo katikati yao.
Ndugu yangu, ikiwa leo hii utadhani Mungu yupo katika karama yoyote uliyonayo, ukidhani kuwa kunena kwa lugha ndio uthibitisho kwamba umepokea kweli ubatizo wa Roho Mtakatifu, au kufanya miujiza, au kutoa pepo, ndio uthibitisho kwamba Mungu yupo na wewe, huku umeiweka kando ile sauti ya Mungu inayozungumza na wewe kwa utulivu na upole inayokuambia UACHE DHAMBI, NA UTUBU, UKABATIZWE KATIKA UBATIZO SAHIHI, wa jina la YESU KRISTO, Hutaki kuisikia, basi fahamu kuwa utakuwa umepotea bila hata wewe mwenyewe kujijua.
Kama Leo hii hutaki kusikia Neno la Mungu, habari za TOBA na UTAKATIFU kwako hazina maana sana, wewe unachokifuata kanisani ni Upepo wa kisulisuli, na matetemeko na hisia za kiroho pamoja na moto wa Roho Mtakatifu na miujiza na uponyaji, ni kweli hivyo vinapaswa viwepo kanisani, na ni lazima kanisa liambatane navyo, lakini ile sauti ya Mungu iliyosema na Eliya hapo mwanzo bado itaendelea kusema na wewe ndani yako siku zote, UNAFANYA NINI HAPA? UNAFANYA NINI KATIKA DHAMBI??
Ni kitu gani unachokwenda kukitafuta katika nyumba ya Mungu, ni miujiza tu,? ni ishara? Ni uponyaji? Ni kufunguliwa biashara yako?, ni kuombewa upate mtoto?, ni Kufunguliwa upate mume/mke?, ni kuombewa tu ufaulu shuleni?. Ndugu kama ni mojawapo ya hayo ndio yanayokupeleka huko ukidhani kuwa Mungu kukufanikisha katika hivyo ndio uthibitisho kwamba yupo na wewe, basi hujaisikia bado sauti ya Mungu, yeye alisema wazi kabisa,“mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuuona ufalme wa mbinguni Yohana 3:3” na kuzaliwa mara ya pili ni KUTUBU (KUGEUKA) kwa kumaanisha kuacha maisha uliyokuwa unaishi ya kale, ya ulevi, uasherati, usengenyaji, ushirikina, kutokusamehe, ya chuki, ya wivu, ya ugomvi, ya utukanaji,maisha ya anasa, maisha ya uvaaji vimini, na suruali, maisha ya upakaji wanja na lipstiki na uvaaji mawigi na hereni, maisha ya ibada za sanamu na uvuguvugu.
Na baada ya kugeuka, hatua inayofuata ni kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa Jina la Yesu Kristo, ili hatia ya dhambi zako iondolewe mbele za Mungu na kisha Bwana mwenyewe atakupa uwezo wa kushinda dhambi kwa kupitia Roho wake Mtakatifu katika wakati uliobakia wa maisha yako.
Ndugu sauti ndogo leo ya utulivu inazungumza nawe kupitia maandiko kwamba hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa na huo UTAKATIFU, (waebrania 12:14.). Isikie sauti ya Mungu sasa inayosema katika kanisa lake na sio ishara, miujiza, maono, ndoto, uponyaji, n.k…Ukivifuata hivyo kanisani, bado ile sauti itakuuliza FULANI UNAFANYA NINI HAPA?..mimi sipo huko, nipo katika sauti ndogo ya utulivu..
Na kama ni ya utulivu basi ni rahisi kuidharau. Ni maombi yangu ndugu yangu sisi sote tusiiache itupite, Bwana atupe masikio ya kuisikia inaposema nasi katika Neno lake na sio katika miujiza. Hizi ni siku za mwisho tuwe macho.
Mungu akubariki.
Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu.
Kwa mpangilio mzuri wa masomo haya tembelea website yetu hii >>> www.wingulamashahidi.org
No comments:
Post a Comment