"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, August 27, 2018

UMETEKWA NA UPENDO WA KRISTO?

Ni rahisi kudhania kuwa mtu akizaliwa mara ya pili, basi anakuwa anampenda sana Mungu kiasi kwamba kukitokea kitu mfano shida, au tabu,au magonjwa, au dhiki na kadhalika anakuwa yupo tayari kupambana nacho ili asimwache Mungu wake au asimkane Kristo,..yaani kwa jinsi anavyompenda Bwana hataweza kuruhusu tabu zimtenge na yeye kama tunavyosoma ilivyoandikwa katika maandiko haya;

Warumi 8: 31 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?
32 Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?
33 Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.
34 Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.
35 NI NANI ATAKAYETUTENGA NA UPENDO WA KRISTO? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?
36 Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa.
37 Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.
38 Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,
39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote HAKITAWEZA KUTUTENGA NA UPENDO WA MUNGU ULIO KATIKA KRISTO YESU BWANA WETU.”

Je! Ni kweli hiyo ndiyo maana halisi ya hiyo mistari hapo juu kwamba sisi tunao uwezo wa kupambana na dhiki, tabu, na mateso kwasababu ya upendo wetu mwingi kwa Kristo?. Jibu ni hapana, hakuna mwanadamu yeyote mwenye upendo wa kiwango hicho, ni muhimu kufahamu maana ya huo mstari hapo juu, Biblia inasema JE! NI NANI ATAKAYETUTENGA NA UPENDO WA KRISTO?..Unaona hapo, inasema ni UPENDO WA KRISTO na sio UPENDO WETU SISI KWA KRISTO.

Kuna tofuati kati ya upendo wetu sisi kwa Kristo, na upendo wa Kristo kwetu sisi.

Mtu anapozaliwa mara ya pili kweli kweli [Tutakuja kuona huko mbeleni mtu anazaliwaje mara ya pili], Kuanzia huo wakati na kuendelea ule Upendo wa Kristo unaingia ndani yake, huo sio upendo wake[huyo mtu] kwa Kristo, hapana! bali Upendo wa Kristo kwake. Hivyo Bwana Yesu ndiye anayekuwa anachukua jukumu lote la kuhakikisha ule upendo wake kwako unadumu milele haupotei kwa namna yoyote ile.

Hivyo kuanzia huo wakati linapotokea jambo lolote juu yako mfano iwe ni dhiki, shida, njaa, hatari, adha, upanga n.k. Ni Yesu Kristo ndiye anayehakikisha wewe haujitengi na yeye, na sio wewe utakayehakikisha kwamba hujitengi na yeye. Watu wanaojaribu kufanya hivyo, kwa kujizuia kwa akili zao kutokujitenga na Kristo hawafiki mbali, wanajikuta wanaanguka na watu wa namna hiyo huwa bado hajazaliwa mara ya pili.

Mtume Paulo anasema, … 38 Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,
39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote HAKITAWEZA KUTUTENGA NA UPENDO WA MUNGU ULIO KATIKA KRISTO YESU BWANA WETU.”

Hii ni faida kubwa sana kwa mtu aliyezaliwa kweli kweli mara ya pili, Unakuwa UMETEKWA na UPENDO WA YESU KRISTO mwenyewe, ndio hapo unakuta dhiki inapomjia mtu wa namna hiyo kwamfano, shetani anapomjaribu kwa misiba, badala ya yeye kufarijiwa yeye ndio anawafariji wengine, anapokuwa katika magonjwa ya kufisha, badala amkufuru Mungu yeye ndiye anaonekana mwenye tumaini kushinda hata mtu aliye na mzima, kama vile Ayubu, utashangaa mtu wa namna hiyo anapita katika hali ya kupungukiwa kupita kiasi na njaa lakini bado anafuraha na kumshukuru Mungu, mpaka watu wa nje wanamshangaa ni mtu wa namna gani, yupo katika hali kama hizi lakini bado anashikamana na Mungu wake,

Kadhalika utakuta mtu mwingine [tunawazungumzia waliozaliwa kweli kweli mara ya pili] ni tajiri, lakini hauangalii na kuutumainia utajiri wake kama ni kitu cha thamani sana katika maisha yake, mpaka watu wengine wa nje wanamshangaa wanasema tungekuwa na mali kama za kwako dunia nzima ingetujua, tungetembelea magari ya thamani, tungetia heshima, lakini mtu kama Ayubu pamoja na utajiri wake alisema maneno haya,

Ayubu 31: 25 “Kama nilifurahi kwa kuwa mali yangu yalikuwa mengi, Na kwa sababu mkono wangu umepata vitu vingi; ….28 Hilo nalo lingekuwa uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; Kwani ningemwambia uongo Mungu aliye juu. “

Unaona sasa uwezo wa namna hiyo, wa kuweza kuendana nayo na kushinda mambo yote hayo pasipo kumwacha Mungu, sio kwa jitihada za mtu binafsi kupambana na hizo hali, hilo haliwezekani kwa mtu yeyote Yule, hiyo ni YESU KRISTO mwenyewe ndio anafanya ndani ya mtu ili kuhakikisha kwamba hakupotezi wewe kipenzi chake, haungamii, hivyo tatizo linapokuja, kabla ya kukufikia wewe, linawasili kwanza kwake, kisha analipatia utatuzi, ndipo litakaposhuka kwako, na litakaposhuka linakuja na dawa madhubuti ya kulishinda, Uwezo wa kipekee unatoka kwa Mungu, na nguvu ya kushinda majaribu na mitikisiko yote..

Ndio hapo watu wa nje watakushangaa unawezaje kushinda hayo yote?, unawezaje kukaa katikati ya jamii ya wazinzi na wewe sio mmojawao?, unawezaje kuwa katika hali ya kutokuwa na pesa lakini bado unamtumikia Mungu, na unayo amani?, Unawezaje kuwa mgonjwa lakini unawaombea wengine, na hauna hofu ya kufa? Unawezaje kuwa na mali na usitamani anasa za ulimwengu huu, wala kiburi, unawezaje kuwa mzuri na bado huvai mavazi yasiyo na heshima n.k…Hawajui kwamba hayo yote hayatokani na upendo wako wewe kwa Mungu..hapana bali yanatokana na UPENDO wa KRISTO kwako .. Yeye ndiye anayefanya juu chini, wewe usipotee katika hizo njia mbovu na majaribu..kama biblia inavyosema:

Zaburi 125: 1 “Wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, Ambao hautatikisika, wakaa milele.
2 Kama milima inavyouzunguka Yerusalemu, NDIVYO BWANA ANAVYOWAZUNGUKA WATU WAKE , TANGU SASA NA HATA MILELE. “

Sasa karama hii ya UPENDO WA MUNGU KWA MTU, haiji kwa watu wote wa ulimwenguni hapana! Bali inakujua kwa wale tu waliomtumainia yeye {yaani wale tu WALIOZALIWA MARA YA PILI}, wengine ambao hawajazaliwa mara ya pili hawataweza kushinda majaribu na misukosuko, yatakapotokea mawimbi wataanguka tu, zitakapotokea dhiki watakufuru, ikitokea misiba watalaani, hawana raha usiku na mchana, watajitahidi kwa nguvu zao kushinda dhambi na ulimwengu lakini hawataweza, hata wakipata utajiri utawaangamiza, hata wakiwa wagonjwa na maskini watataka kujaribu kuishikilia imani lakini watamkana Kristo, kwasababu hawajazaliwa mara ya pili.

Sasa Kuzaliwa mara ya pili kunakuja kwanza baada ya mtu kutubu dhambi zake, [kumbuka maana ya kutubu ni KUGEUKA], sio kuongozwa sala ya toba, unageuka kwa kudhamiria na kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako, kuyaacha ya kale na kuanza maisha mapya kwa Kristo, na baada ya kutubu, bila kukawia hatua inayofuata ni kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele, na kwa JINA LA YESU KRISTO, (kulingana na Matendo 2:38), upate ondoleo la dhambi zako, na hatua ya tatu na ya mwisho ni Roho wa Kristo kuingia ndani yako, sasa hapo ndio lile PENDO LA KRISTO linamiminwa ndani yako. Mtu yeyote akiruka hatua yoyote kati ya hizo, bado hajazaliwa mara ya pili..Kumbuka ndugu hii sio dini wala dhehebu ni maagizo ya Bwana Yesu mwenyewe ambayo yapo kwenye biblia.

Biblia inasema wazi kabisa, katika Yohana 3: 5 “Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.”

Sasa kumbuka kuzaliwa kwa maji kunakozungumziwa hapo ndio UBATIZO WA MAJI, na kuzaliwa kwa Roho ndio UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU. Hapo ndipo unakuwa umeshazaliwa mara ya pili. Lakini Wapo wengine wanataka kubatizwa lakini hawajadhamiria kuacha maisha yao ya kale ya dhambi, hao hata wakienda kubatizwa wanafanya kazi bure, hakuna chochote kitakachotokea katika maisha yao.. Kadhalika wapo wengine, wametubu lakini hawataki kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wanasema ubatizo wa maji hauna maana sana hawa nao pia hawataona mabadiliko yoyote katika maisha yao.. Maagizo yote aliyoyatoa Bwana Yesu hakuna hata moja lisilokuwa na maana, alisema aaminiye na kubatizwa atakoka, na sio aaminiye tu peke yake. Hapana bali vyote viwili vinakwenda pamoja.

Hivyo mtu akizingatia hizo hatua zote za yeye kuzaliwa mara ya pili utapokea UWEZO, wa kutokutenganishwa na chochote kile, iwe shida, dhiki, uzima, mauti, raha, malaika, mamlaka, utajiri, kupungukiwa, upanga, misiba, n.k. kwasababu lile PENDO LA YESU KRISTO tayari litakuwa limeshamiminwa ndani yake. Hivyo ANASHINDA siku zote na ZAIDI YA KUSHINDA.

Ubarikiwe.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki.

Kwa mpangilio mzuri wa masomo haya tembelea website yetu >>> www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment