Zekaria 14: 6 “Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba nuru yake haitakuwa na mwangaza na kiwi;7 lakini itakuwa siku moja, iliyojulikana na Bwana; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, ya kwamba wakati wa jioni kutakuwako nuru”.
Jaribu kutengeneza picha mfano Inatokea siku moja, wakati wa jioni labda tuseme saa moja hivi muda ambao umezoea kila siku kuona jua likizama ghafla unashangaa kuona mwanga ni ule ule haufifii, tena inafikia saa mbili jioni jambo ni lile lile, kunamulika mwangaza kama wa saa 11 jioni hivi, ni wazi kuwa kwa namna ya kawaida utashangaa sana hiyo siku kimetokea nini?, mbona giza haliingii maana muda wa usiku umeshaanza na sasa ni saa 2 usiku lakini kunaonekana kama saa 11, kwa namna ya kawaida mtu yeyote atakayeliona jambo hilo atashtuka sana.
Kadhalika na katika roho pia Bwana alitabiri itakuja siku moja inayofanana na hiyo, kwamba wakati wa jioni kutakuwa na NURU. Lakini kwa hekima hatuna budi tufahamu huo wakati ni wakati gani, je! Umeshatimia au bado?. Hivyo ili kufahamu ni lazima pia tujue Nuru ni nini na giza ni nini? Na huo wakati wa jioni ni upi?.
Kama tunavyojua nuru ya dunia inaletwa na jua, na hili jua huwa linaangaza katika majira matatu yaani asubuhi, mchana na jioni,..Kadhalika na katika roho Bwana Yesu alisema:
Yohana 8: 12 “…, MIMI NDIMI NURU YA ULIMWENGU, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima”.
Unaona hapo yeye katika roho ndio jua letu lililoanza kuangaza asubuhi, na likaja kuangaza mchana, kadhalika na litaangaza jioni. Kazi yake ni kutia nuru ulimwengu, alianza kutia nuru asubuhi (yaani kanisa la kwanza lilioanza na mitume), akaendelea kutia nuru mchana(yaani katika wakati way ale makanisa 5 yaliyofuata), na akamaliza kuangaza Nuru yake wakati wa jioni (katika kanisa lile mwisho la 7 linaloitwa Laodikia ambalo ndilo hili tunaloishi sasa ). Ufunuo 2 & 3
Na kanisa hili la Laodikia ni wazi kabisa na inajulikana na watu wote kwamba lilianza katika karne ya ishirini, yaani kuanzia mwaka 1906 na kuendelea.. Hivyo sisi wote tuliopo leo tunaishi katika ile NURU ya BWANA ya jioni, kumbuka hakutakuwa na kanisa lingine zaidi ya hili, ni kanisa ambalo litashuhudia kuja kwa pili kwa Kristo. Ilijulikana Katikati ya wakristo wote kuanzia huo wakati wa mwanzoni mwa karne ya karne ya 20 kwamba wao ni WANA WA JIONI, kwasababu walikuwa wanafahamu kabisa ni kweli wanaishi wakati wa jioni kabisa wa nuru ya Kristo kumalizikia.
Sasa katikati mwa karne ya ishirini yaani kipindi cha miaka ya 1940-1980, wakristo wote kutokana na matukio yaliyokuwa yanayaona yakitokea duniani, wakilinganisha na unabii wa kibiblia, walifahamu kuwa karne ile haitaisha bila Kristo kurudi mara ya pili, na ni kweli walikuwa sahihi, ukizingatia kwamba asilimia kubwa wa yale Bwana Yesu aliyoyazungumza katika Mathayo 24 yalitimia katika huo wakati, kwamfano, Bwana alisema.
Kutakuwa na matetemeko ya nchi mahali na mahali, kwa wakati ule yalikuwa ni mengi mno duniani, alisema pia kutakuwa na vita na matetesi ya vita, taifa litaondoka kwenda kupigana na taifa lingine…Jambo ambalo lilionekana wazi katikati ya ile karne ya 20, vita viwili vikubwa vya dunia vilitokea kwa mpigo, jambo ambalo halikuwahi kuonekana hapo kabla katika historia ya dunia, mamilioni ya watu kufa, magonjwa ya ajabu ndio yalianzia kuzuka katika hicho kipindi, kansa, ukimwi, kisukari, Malaria n.k. mambo ambayo Bwana aliyatabiri yatatokea katika siku za mwisho, na kikubwa zaidi kilichowafanya watakatifu wa karne ya ishirini kunyanyua vichwa vyao juu, kama Bwana alivyowaambia katika
Luka 21:28 “Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia”
Ni kutokea kwa kitendo cha kihistoria katika nchi takatifu Israeli, pale waliposhuhudia taifa la Israeli likichipuka tena baada ya ma-karne ya miaka kupita bila kuwa taifa huru, walishuhudia kuona Israeli kupata uhuru wao tena mwaka 1948 na kuwaona wayahudi wakitoka katikati ya mataifa yote ulimwenguni na kurudi katika nchi yao tena.
Ezekieli 36: 24 “Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. “
Huko ndiko kuchipuka kwa mtini Bwana Yesu alikokuzungumzia,Maana Taifa la Israeli linafananishwa na MTINI kadhalika pia watakatifu walipokuwa wanaona na miti mingine ikichipuka (yaani mataifa mengine tofauti na Israeli kupata uhuru wao yaani mataifa ya Afrika, Asia na Marekani ya kusini),ambayo hayo yote yalianza kupata uhuru wao mara baada tu ya Israeli kutangazwa kuwa taifa huru, wakilinganisha na maandiko Bwana Yesu aliyoyasema katika..
Luka 21:29 “Akawaambia mfano; Utazameni MTINI na MITI MINGINE YOTE.30 Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu.31 Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu.32 Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. ”
Hivyo walivyokuwa wanayaona hayo yote yanatimia, walitambua kabisa kwamba karne ya 21 haitafika (yaani miaka ya 2000 haitakuwepo), na walikuwa wapo sahihi kabisa, Sasa kilichotokea na cha kustaajabisha, ni kuona mpaka karne ya 21 inaanza na mwisho bado haujafika…
Na ndio hapo tunarudi kwenye lile andiko letu la msingi..
Zekaria 14: 6 “Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba nuru yake haitakuwa na mwangaza na kiwi;
7 LAKINI ITAKUWA SIKU MOJA, ILIYOJULIKANA NA BWANA; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, YA KWAMBA WAKATI WA JIONI KUTAKUWA NURU”.
Huo wakati ambao Bwana alisema JIONI KUTAKUWA NA NURU, ndio huu tunaoishi sasa (wakati huu wa karne ya 21), Mambo yote yalipaswa yaishe tokea karne ya 20, lakini kwa jinsi Mungu alivyokuwa wa rehema na neema, hataki mtu yeyote apotee bali wote waifikilie toba, akalazimika kuisimamisha NURU ya ulimwengu isizame ( yaani Neema ya Yesu Kristo isiishe) katika hichi kipindi cha wakati wa jioni wa kumalizia..
Ndugu yangu mwisho ungepaswa uwe umeshafika siku nyingi, moja ya hizi siku mambo yote yatabadilika ghafla, kama vile jua linavyokaribia kuzama kidogo kidogo giza linaingia..ndivyo walivyoweza kutambua watu wa karne ya 20, lakini sisi tunaoishi katika Hii NURU ya nyiongeza (watu wa karne ya 21), tupo katika hatari kubwa sana kwasababu Nuru hii haitadumu kwa kipindi kirefu, kadhalika na haitabiriki, siku ya kuondoka kwake haitakuwa taratibu taratibu tena kama mwanzo, hapana, bali itaondoka kwa ghafla, na saa hiyo hiyo giza nene sana litaikumbuka dunia (huo ndio uharibifu wake)…
Ndio lile neno litatimia 1Wathesalonike 5: 1 “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.
2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 WAKATI WASEMAPO, KUNA AMANI, NA SALAMA, NDIPO UHARIBIFU UWAJIAPO KWA GHAFULA, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. “
Watu wengi wametokea badala ya kumkaribia Mungu awape neema ndio kwanza wanaanza kudhihaki, wakisema hakuna kitu kama hicho kurudi kwa Yesu, Yesu harudi leo wala kesho, miaka na miaka mambo yapo vilevile hawajui kwamba wanaishi katika muda wa nyiongeza wa ILE NURU YA JIONI.. ili watubu..
1Petro 3: 1 “Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha,
2 mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu.
3 Mkijua kwanza neno hili ya kwamba KATIKA SIKU ZA MWISHO WATAKUJA NA DHIHAKA ZAO WATU WENYE KUDHIHAKI, WAFUATAO TAMAA ZAO WENYEWE,
4 na kusema, IKO WAPI AHADI ILE YA KUJA KWAKE? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.
5 Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;
6 kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.
7 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.
8 Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.
9 BWANA HAKAWII KUITIMIZA AHADI YAKE, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, MAANA HAPENDI MTU YE YOTE APOTEE, BALI WOTE WAFIKILIE TOBA.
10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.
11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa,
12 mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? "
Unaona ndugu,..tunaishi wakati wa muda wa nyongeza muda wa ile siku iliyojulikana na Bwana, wakati wa jioni, wakati wa NURU YA NEEMA. Je! Bado unaishi katika dhambi? Bado hujazaliwa mara ya pili? Utajitetea vipi siku ile pamoja na huu muda wa nyongeza uliopewa katika hili giza lililopo duniani, utatoa udhuru gani mbele ya hukumu. Kumbuka baada ya hii nuru kuondoka, (ambayo itaisha na UNYAKUO), kutakuwa kumebakia miaka saba tu mpaka dunia kuisha, huko ndiko ile dhiki kuu ya mpinga-kristo pamoja yale mapigo yote yaliyoandikwa katika kitabu cha ufunuo 8 & 16 yatatimia, kisha baada ya hapo itakuja hukumu na kisha ziwa la moto.
Kama hujatubu kwa kumaanisha kuziacha dhambi zako, fanya hivyo leo, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji tele na kwa jina la YESU KRISTO upate ondoleo la dhambi zako (kulingana na Matendo 2:38), na Bwana atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu..
Bwana akubariki sana.
Tafadhali “share ” ujumbe huu kwa wengine na Bwana atakubariki.
Kwa mpangilio mzuri wa masomo haya, tembelea >>> wingulamashahidi.org
No comments:
Post a Comment