"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, August 22, 2018

TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO.

Mambo ya asili yanafunua mambo ya rohoni, Bwana Yesu alituambia “wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru. (Luka 16:8)”..Neno hili linatuhusu sisi tulio wakristo, Embu tujifunze mojawapo ya busara walionayo wana wa ulimwengu huu, Mtume Paulo alisema katika "1Wakorintho 9: 24 Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate…"

Kama tunavyosoma katika andiko hilo tunaona jinsi Mtume Paulo alivyoweza kuwatazama wakimbiaji wa kidunia akapata hekima, kadhalika na sisi tujifunze ili tupate hekima mbele za Mungu wetu aliye mbinguni. Kama ulishawatazama wakimbiaji wanaoshiriki katika michezo ya mbio ndefu au fupi, utafahamu kuwa wao huwa hawashiriki tu watu wote ovyo ovyo, yaani tukiwa na maana kuwachanganya watoto, na wazee pamoja na wanawake na wanaume humo humo katika riadha moja, hapana, waligundua wakifanya hivyo basi kutakuwa hakuna usawa wowote na mwisho wa siku katika ugawaji wa tuzo, litapatikana kundi moja la kipekee litakalokomba tuzo hizo zote,(hivyo michezo haitakuwa na maana yoyote) Lakini ili kuweka mambo yote sawa, walifanikiwa kutenganisha mbio hizo kulingana na uwezo wa watu, umri wa watu, pamoja na jinsia za watu.

Kwamfano kama ukitazama wanaoshiriki katika mbio zile fupi tuseme labda zile za mita 100, utakuta zimetengwa mbio za wanaume kivyao na wanaweka kivyao, hawachanganywi kwasababu uwezo unatofautiana kulingana na jinsia, kwamfano kama wanawake watakaoshiriki wapo 10, na wanaume 10, tuseme wakimbie pamoja basi utakuta nafasi zote 10 za kwanza zitachukuliwa na wanaume wote, na kuanzia nafasi ya 11 ndipo mwanamke wa kwanza ataanza kutokea..Hivyo mwisho wa siku inatokea kuwa hatapatikana mwanamke atakaye pokea tuzo yoyote pamoja na taabu zake zote..

Sasa kwa kwa kulitatua hilo, wakatofautisha makundi mawili, wanaume kwa wanaume, na wanawake kwa wanawake,.. Mwanaume atakayemaliza wa mwisho, kwa sekunde tuseme 11, na mwanamke aliyeingia wa kwanza kwa sekunde 12..Yule mwanamke wa kwanza aliyeshinda katikati ya wanawake wenzake, unakuta anapokea tuzo sawa na yule mwanaume aliyeingia wa kwanza kule akiwa na sekunde 8 katika mashindano ya wanaume wenzake. Wote watapokea medali moja (labda tuseme ya dhahabu), kadhalika na wa pili na wa tatu hivyo hivyo kwa pande zote medali zao zitafanana..Ingawa kiuhalisia inaweza kuonekana kuwa wale wanaume wengine waliokosa medali wangestahili kupewa zile tuzo za wale wanawake , kwasababu wao walikimbia ndani ya muda mchache kuliko wao, lakini haiko hivyo katika utoaji wa medali (tuzo). Utoaji unategemea na kundi unaloshiriki. Kadhalika mbio za walemavu, na watoto haziwezi zikawa sana na mbio za watu wazima, lakini medali ya atakayeshinda katikati ya walemavu itakuwa na thamani sawa na medali za wale wazima.

Kadhalika na katika mbio za kikristo, wote tunashiriki mchezo mmoja, wote tunashindana katika mbio, lakini Mungu aliziweka hizo mbio katika makundi tofauti tofauti. Watoto kivyao, wanaume kivyao pamoja na wanawake kivyao. Lakini kwa kila kundi thamani ya tuzo kwa watakaoshinda hazitofautiani.. Lakini Bwana alisema kwetu sisi wana wa Nuru hatuna hekima katika mashindano yetu haya duniani..Wote tunataka tujichanganye tukimbie katika kundi moja wote, wanaume hukohuko, wanawake huko huko, watoto huko huko n.k. Ndugu kwa Mungu hakupo hivyo, Mungu alitoa majukumu katika kanisa, Majukumu ya wanaume na majukumu ya wanawake, na majukumu yanayopaswa yafanywe na wote.

Biblia inaposema katika 1Timotheo 2: 8 “Basi, nataka WANAUME WASALISHE KILA MAHALI, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano”, Haikukosea, Kama inavyotupa mwongozo, mahali popote panapohusiana na kuongoza ibada ikiwemo uongozaji wa maombi, kusalisha, kuelekeza, vyote hivyo vinapaswa katika kanisa vifanywe na wanaume tu. Kwasababu jukumu hili limewekwa katika upande wa mbio za wanaume.

Kadhalika biblia ilisema pia..1Timotheo 2: 11 “MWANAMKE NA AJIFUNZE KATIKA UTULIVU, , akitii kwa kila namna.
12 SIMPI MWANAMKE RUHUSA YA KUFUNDISHA, WALA KUMTAWALA MWANAMUME, bali awe katika utulivu.
13 Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye”.

Unaona? Hili ni agizo la pili la Bwana kwa kanisa, kwamba kazi ya kufundisha, mfano uchungaji, ualimu, uaskofu na ushemasi, haupaswi ufanywe na mwanamke. Na Mungu alishatoa sababu ya kufanya hivyo hapo juu, Hivyo ikiwa mwanamke ataona kama hapewi haki yake na kutaka kwenda kuwa mchungaji au mwalimu ni sawasawa na ameingia katika mbio ambazo sio za jinsia yake, Hivyo matokeo yake mtu kama huyo, ataonyesha kweli nguvu nyingi na jitihada nyingi, lakini hatapokea tuzo yoyote katika siku ile,..Siku ile atasema Bwana mimi nilikuwa mchungaji wa kimataifa kanisani, nilifanya hivi nilifanya vile, lakini Bwana siku ile atamwambia hukupiga mbio mahali panapokupasa. Unaona hapo angepaswa akawe mchungaji, au mwalimu kwa wanawake wenzake, akawe muhubiri kwa wanawake wenzake, lakini sio kanisani penye mchanganyiko wa wanaume na wanawake.

1Wakoritho 14: 34 “Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo.
35 Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa.
36 Au je! Neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu?
37 Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana.
38 Lakini mtu akiwa mjinga, na awe mjinga”.

LAKINI MBIO ZA WANAWAKE NI ZIPI?

Biblia ilisema tena pale pale kwenye..
 1Timotheo 2: 9; “Vivyo hivyo wanawake na WAJIPAMBE KWA MAVAZI YA KUJISITIRI, PAMOJA na ADABU NZURI, na MOYO WA KIASI; SI KWA KUSUKA NYWELE, wala KWA DHAHABU na LULU, wala KWA NGUO ZA THAMANI;
10 bali kwa MATENDO MEMA , kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.
11 Mwanamke na AJIFUNZE KATIKA UTULIVU, akitii kwa kila namna.”
Mwanamke akidumu katika hali ya utulivu, pamoja na adabu, pamoja na kiasi,(Ikiwa na maana awe mwenye nidhamu pia hasengenyi watu,) pamoja na kujisitiri mwili wake kwa kutokuvaa mavazi yanayoonyesha maungo yake, kwa kutokuvaa suruali kama wanaume, kutokuvaa vimini, haweki wigi, wala lipstick midomoni mwake, wala hereni, anadumu katika utakatifu wote, basi Huyo atakuwa katika mashindano miongoni mwa wanawake wenzake (akina Sara, Rebeka, Hana, n.k.) , na siku ile atapokea tuzo yenye thamani kubwa kuliko hata mwanaume ambaye ni mchungaji au muhubiri au mwalimu ambaye hajatumika katika uaminifu wote katika nafasi yake..Atakwenda kuketi pamoja na Kristo katika kiti chake cha Enzi katika siku ile.

Kuna muhubiri mmoja maarufu wa kimarekani anaitwa Rick Jonyer, anaeleza: siku moja alichukuliwa katika maono na Bwana Yesu juu mbinguni katika ulimwengu wa Roho, alipofika kule alianza kutembezwa katikati ya viti vya enzi, na alipokuwa anapita katikati ya baadhi ya hivyo viti vya enzi aligundua kitu, kwamba mbona viti vingi vinakaliwa na wanawake pamoja na watoto? Ndipo akamwambia Bwana inaelekea huku wanawake na watoto ndio wamechukua nafasi kubwa..Anasema alishangazwa sana kuona wale aliokuwa anadhani wangekuwa wana nafasi kubwa kule, kuona ni wadogo sana.

Unaona hapo Dada katika Kristo?, unaweza ukadhani ukidumu katika nafasi yako kama mwanamke hautapata chochote, hapana! Kinyume chake utapata vyote, Thawabu za Bwana zinapimwa kulingana na umri, jinsia na maumbile…talanta uliyopewa kulingana na jinsia yako itumie hiyo vizuri bila kuingilia mbio za jinsia nyingine, tumia talanta ulizopewa katika uaminifu wote ni mfano tu wa mwalimu aliyetoa jaribio kwa wanafunzi wake wawili, mmoja akampa mtihani wa maswali 10 marefu, mwingine akampa mtihani wa maswali 100 mafupi, Yule aliyepewa maswali kumi akapata 9 kati ya yale kumi na kukosa moja, hivyo akahesabiwa kuwa kapata asilimia 90 kati ya mia (yaani 90%). Lakini Yule aliyepewa maswali mia mafupi akapata hapo maswali 50 na maswali mengine 50 yaliyosalia akakosa hivyo akahesabika kapata asilimia 50 kati ya mia (yaani 50% ).

Hivyo mwalimu wakati wa kugawa tuzo akampa tuzo(zawadi) kubwa Yule wa kwanza aliyefanya maswali kumi na kupata hapo tisa,(asilimia 90% ) kuliko Yule pili aliyefanya maswali 100 mengi na kupata hapo asilimia 50% tu. Na ndivyo Baba wa mbinguni atakavyotoa Tuzo siku ile. Mwanamke Yule ambaye atajitunza katika utulivu wote, na kiasi na kujisitiri, na upole na uvumilivu, na utakatifu, na adabu atafananishwa na Yule mwanafunzi aliyepewa maswali 10 nakupata hapo 9, kuliko mwanaume aliyepewa maswali mia na kupata hapo 50.

Dada kabla ya kujifunza kwa Musa, hebu jifunze kwanza kwa Miriamu dada yake Musa alivyokuwa, kabla hujajifunza kwa Eliya nenda kwanza kajifunze kwa Yezebeli Yule mwanamke aliyempinga Eliya, kabla hujajifunza kwa Petro hebu kajifunze kwanza kwa Miriamu na Martha na Mariam Magdalena, na Susana (luka 8:1-3), wanawake walioshuhudiwa kumuhudimia Kristo kwa kila hali, kabla ya kujifunza kwa Paulo hebu kajifunze kwanza kwa Tabitha na mwanamke Lidia aliyewakaribisha wakina Paulo walipokosa mahali pa kukaa (Matendo 16:13-15).
 
Hivyo nakupa moyo dada, ambaye umeanza safari yako hii ya kumtii Kristo, na kubaki katika nafasi yako Mungu aliyokuweka, zidi kuwa mtakatifu na kujisitiri na kuwa kielelezo kwa wanawake wengine kwasababu kiti cha enzi mbinguni kinakuongojea.

Hivyo yapo pia majukumu tulikabidhiwa wote, nayo ni kuwa “mashahidi wa Kristo”. Kila mmoja wetu [awe mwanamke au mwanaume] anapaswa popote pale alipo awe kielelezo cha kuwavuta watu wengine katika ufalme wa mbinguni (kwa mienendo na matendo)..Biblia inasema katika 1Petro 3: 15 Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.
16 Nanyi mwe na dhamiri njema,…

Ubarikiwe.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu.

Kwa mpangilio mzuri wa masomo haya tembelea  website yetu >>> www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment