"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, November 21, 2017

JE! DAMU INA UMUHIMU WOWOTE KATIKA MAISHA??


Jibu ni ndio kwasababu biblia inasema pasipo kumwagika damu hakuna ondoleo, ukisoma waebrania 9:22 "Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. "


Hii ndio njia pekee ambayo Mungu aliichagua tangu awali kwamba, ili tendo lolote la rohoni lifanyike na kufanikiwa ni lazima damu ihusishwe, na ndio maana tunaona katika agano la kale ilikuwa kwamba ili mtu apate kibali mbele za Mungu ni lazima aende na sadaka ya damu ambapo mnyama alisiyekuwa na mawaa anachinjwa ili kufanya upatanisho, na mambo yote yanaliyohusishwa na dhambi yalikuwa yanatakaswa kwa damu, hiyo ilikuwa ni kanuni.Kwahiyo tunaona damu ina mahusiano makubwa kuwa  kama kiunganishi kati ya ulimwengu wa mwilini na wa rohoni, na ndio maana hata shetani kwa kulijua hilo anapenda kutumia damu ili kufanikisha mambo yake maovu katika ulimwengu huu, kwamfano mara nyingi wachawi wanawaambia watu wapeleke damu za mnyama fulani ili kufanikisha mambo yao ya kishirikina pamoja na  haja za hao watu, na ukitazama kwa makini utaona kuwa wanapendelea zaidi damu za wanadamu kuliko za wanyama kwasababu wanajua hizo zina mlango mkubwa zaidi wa kuunganisha mambo ya rohoni na ya mwilini kiurahisi. Na ndio maana hao wanaotoa damu za watu utakuta matokeo yao ya kiroho(kichawi) yanakuwa ni makubwa zaidi kuliko wale wanaotoa damu za wanyama.


Kuna kitu kikubwa sana ndani ya DAMU ambacho mkristo akikitambua hakuna chochote kitakachomsumbua na hakika ataweza kufanya mambo yote, ataweza kufanya yote ya mwilini na ya rohoni, na kama tunavyojua  hiyo damu ili iwe na nguvu ni lazima iwe ya mwanadamu na sio mnyama, tena inatakiwa ipatikane ya mwanadamu asiyekuwa na hila wala mawaa, hakika ikipatikana hiyo ni zaidi ya tambiko lolote ambalo lilishawahi kufanyika duniani!!!

Kumbuka mambo yote yanatoka rohoni, ni ngumu kushindana na watumishi wa shetani ambao wamepata nguvu nyingi za kumkaribia shetani kwa sadaka zao za damu za watu wasio na hatia,halafu  na wewe unataka kwenda kushindana nao pasipo damu yoyote, hapo ni lazima ushindwe tu! ni lazima ujue mbinu za kumshinda adui yako, mambo ya rohoni yana kanuni zake.


Lakini habari njema ni kwamba hii damu yenye nguvu ipitayo damu zote isiyoharibika ambayo inaweza ikashinda mambo yote ipo na inajulikana,na hii DAMU si nyingine zaidi ya DAMU YA YESU ambayo haikuwa na hila wala mawaa yoyote. lakini wengi wanashindwa kuielewa matumizi yake, na ndio maana shetani anaendelea kupata nguvu juu yao, Jambo shetani analotaka ni waifahamu tu lakini wasiielewe matumizi yake, kila mtu anaifahamu damu ya YESU lakini ni wachache wanayoielewa, siku utakapoielewa kisawasawa utamshinda shetani kwa kila nyanja. ukisoma;Ufunuo 12:9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
10 Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.
11 NAO WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. "

Unaona hapo? ni Damu tu ya mwana-kondoo inayoweza kumshinda yule joka ( shetani ) na hakuna kingine chochote. Lakini wengi wanadhani utamshinda kwa  kutamka tu  "nakukemea kwa damu ya Yesu"..."na kukemea kwa damu ya Yesu"...akidhani hapo amempata shetani, kumbe hajui hapo hajafanya lolote kama hajaingia ndani ya hilo Agano kwanza. Ni lazima uingie kwanza.


JINSI YA KUINGIA KATIKA HILI AGANO LA DAMU YA YESU.


Kumbuka katika agano la kale kuhani mkuu alipokuwa akienda kila mwaka kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa njia ya damu za wanyama, hakuwa anafanya kwa watu wote wa ulimwengu mzima bali tu kwa wale waliokuwa katika hilo agano yaani wana wa Israeli pekee. Na ndio waliokuwa wanafunikwa dhambi zao na kushiriki baraka zote za rohoni na sio watu  wa ulimwengu mzima.

Vivyo hivyo katika Agano jipya ili maombi yako yasikiwe, ili sadaka zako zikubaliwe, ili dhambi zako zisamehewe, ili uweze kumshinda shetani na magonjwa yake yote na laana ni lazima uingie katika hili Agano jipya la DAMU YA YESU KRISTO. na hauingiii kwa kuzaliwa katika familia ya kikristo, wala hauingii kwa kujiunga na dhehebu fulani, wala hauingii kwa njia nyingine yoyote isipokuwa KWA KUTUBU kwanza, NA KUMWAMINI YESU KRISTO, NA KUBATIZWA KWA JINA LA YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kisha upokee ROHO MTAKATIFU hapo ndipo umezaliwa mara ya pili na umeingia katika hili AGANO KUU la DAMU YA YESU KRISTO.


Sasa kuanzia hapo na kuendelea ile damu inaanza kunena kwa ajili yako mbele za Mungu, shetani hana la kukushinda kwa lolote, wala la kukushitaki, kwasababu damu isiyoharibika tayari ipo kunena kwa ajili yako, hauhitaji kupigana na wachawi, wala waganga, wala kuogopa magonjwa au shida, ipo hiyo damu tayari inafanya kazi kuliko tambiko lolote lililowahi kufanyika tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu. Kumbuka shetani anapotaka kuleta laana juu yako jambo la kwanza analoangalia ni je! upo chini ya damu? shetani hawezi kulaani kilichobarikiwa kama vile Balaamu alivyoshindwa kuwalaani wana wa Israeli.

Kwahiyo ndugu hakuna njia nyingine yoyote katika hii dunia unaweza ukamshinda shetani isipokuwa kwanza kutubu, na kumruhusu Yesu Kristo ayasafishe maisha yako kwa damu yake, uchukua uamuzi wa kubatizwa leo kwa ubatizo ulio sahihi wa kuzamishwa na sio wa kunyunyuziwa na iwe ni  kwa jina la YESU KRISTO kulingana na maandiko ( matendo 2:38.), kisha Bwana atakupa Roho Mtakatifu hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili na kuingia katika lile AGANO KUU LA DAMU YA YESU, kwa uhakika wa maisha yako ya sasa na ya baadae, kumbuka hakuna ubatizo wa watoto wachanga, kama ulifanyiwa hivyo hapo hujabatizwa unapaswa ukabatizwe tena.


Nakukumbusha tena ndugu yangu hauwezi ukamshinda shetani kwa njia nyingine yoyote ile, sio kwa matendo, wala kwa juhudi yako bali kwa damu ya mwana-kondoo pekee. Ufunuo 12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. ". tubu, kabatizwe na upokee Roho Mtakatifu.
Mungu akubariki!

Tuesday, November 7, 2017

MASWALI YANAYOULIZWA MARA KWA MARA NA WASIO-WAKRISTO: Part 2 
SWALI: JE! UKRISTO NI DINI?  Ni wapi kwenye biblia imetaja kama ukristo ni dini?

JIBU: Ili kujibu hili swali ni vizuri kuelewa nini maana ya DINI. Dini ni neno lilitoka kwenye lugha ya kilatini "religio" likiwa na maana kuwa ni mfumo fulani au utamaduni fulani wa kuabudu unaotokana na imani fulani. Kwa lugha iliyo nyepesi dini ni matunda ya imani ya mtu. Kwamfano kitendo cha kufanya ibada, kufunga, kuswali, kuomba dua, kutoa zaka, kuvaa mavazi ya kujisitiri, kuvaa kanzu, kuvaa misalaba, kuchoma ubani, kusujudu,tohara, kuabudu, kutawadha, n.k. haya yote ni matunda ya imani ambayo ndiyo sasa yanayoitwa DINI.
 
Kwa utangulizi huu sasa tunaweza kurudi kwenye swali letu linalouliza je! ukristo ni Dini??.

Jibu ni HAPANA ukristo sio dini na ni swali linaloulizwa mara kwa mara na watu wengi je! ni wapi kwenye biblia imetaja kuwa ukristo ni dini? ni kweli kabisa hakuna sehemu yoyote kwenye biblia inayosema ukristo ni dini kwasababu UKRISTO sio dini.

Hivyo kama sio dini ukristo ni nini basi?

Jibu lake fupi ni hili: "UKRISTO ni IMANI" , Hivyo basi ili uwe mkristo lazima uwe WA-KRISTO (yaani wa YESU KRISTO), Ikiwa na maana kuwa mtu anapomwamini YESU KRISTO ndipo anapokuwa mkristo na sio anapojiunga na shirika lolote la kidini linalojiita la kikristo ndipo awe mkristo kama dini nyingine zinavyofanya.

Na ndio maana kila mahali kwenye biblia YESU alikuwa anasisitiza Neno hili; " yeye aniaminiye mimi"..."yeye aniaminiye mimi".. :Hakusema yeye aaminiye dini ya kikristo au shirika fulani la kikristo ana uzima wa milele, bali "yeye aniaminiye mimi anao uzima wa milele"...Kumbuka YESU sio DINI wala hahitaji dini yako (yaani kutoa sadaka, kuvaa misalaba, kuvaa kanzu, n.k.) ili uwe mfuasi wake, anahitaji IMANI yako kwake kwanza ili uwe mfuasi wake, Na ndio sasa baada ya kumwamini yeye ndipo DINI yako ifuate. Kwahiyo mtu yeyote anayejivunia dini uelewa wake juu ya masuala ya imani bado ni hafifu sana, kwasababu dini isipokuwa na chanzo sahihi cha imani ni kazi bure.

Biblia imetoa tafsiri ya DINI kama ifuatavyo soma Yakobo 1:26
"Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa. "

Unaona hapo biblia inaelezea maana ya dini ya kweli, nayo ni hii; kujizuia ulimi wako, kwenda kuwatazama mayatima, kujilinda na dunia pasipo mawaa akiwa na maana ya kutokuiba, kutokuwa mzinzi, kujisitiri, kuwa safi n.k. Lakini swali linakuja pale pale je! unadhani kwa kuwa na DINI SAFI KAMA HII inatosha kukufanya wewe kuwa mkristo??. HAPANA unapaswa uwe MKRISTO kwa kumwamini YESU KRISTO ndipo DINI yako ifuate kwasababu matendo hayo yote hata wasio wakristo wanaweza kuyaiga, wahindu wanaweza kuyaiga, wabudha wanaweza kuyaiga, hata wapagani wanaweza wakaiga n.k, lakini bado wakawa mbali na UKRISTO.

Hivyo usijivunie DINI bali IMANI yako kwani hata huyo umdhaniaye kuwa adui yako anaweza akawa na DINI safi kuliko hata ya kwako.

Ushauri wangu kwako ndugu  muislamu au dini nyingine mwamini YESU KRISTO leo akupe uzima wa milele, hakuna njia nyingine ya kumfikia Mungu zaidi ya hiyo. Dini haikufikishi kwa Mungu badilisha mtazamo wako.

Yohana 14:6"Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. "

Ubarikiwe.

MASWALI YANAYOULIZWA MARA KWA MARA NA WASIO-WAKRISTO: Part 1
SWALI: Napenda kuuliza kama Yesu alikufa kwa ajili ya watu pale msalabani, kwanini basi alisema 
kila mtu abebe msalaba wake?.

JIBU: Tusome hilo andiko Bwana Yesu alivyosema ili tupate nuru zaidi ya kulifafanua..

Luka 14:25" Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,
26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
27 Mtu ye yote ASIYECHUKUA MSALABA WAKE na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?
29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,
30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.
31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?
32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.
33 Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. "

Tunaona hapo kama tukisoma kwa umakini,Yesu alikuwa anazungumzia juu ya "gharama ya kuwa mwanafunzi wake". Kwamba mtu yoyote akitaka kuwa mwanafunzi wake anapaswa kujitoa na awe tayari kukabili kila hali atakayokutana nayo, tuchukulie tu kwamfano mtu yeyote anayetaka kujiunga na jeshi, haendi hivi hivi tu na kuwa mwanajeshi hapohapo ni lazima aingie gharama fulani, na gharama zenyewe ndio hizi; awe tayari kuishi kambini mbali na ndugu zake,awe tayari kuacha vitu vyote, awe tayari kufanya mazoezi magumu, awe tayari kutii kanuni zote za jeshi atakazoamriwa pasipo kuhoji, awe tayari hata kufa kwa ajili ya taifa lake, n.k..

Vivyo hivyo na kwa Bwana Yesu pia alisema mtu yoyote akitaka kuwa mtumishi/mwanafunzi wake, ni lazima akubali kupitia mambo yote hata mabaya kama kuchukiwa na ndugu, kutengwa na wazazi au jamii, akubali kujitenga na mambo ya kidunia, akubali kudharauliwa kwa ajili ya Kristo, kutukanwa, kuuliwa kwa ajili ya Kristo, kuvumilia mabaya n.k. huko ndiko kuuchukua msalaba alikokuzungumzia ambako hakuepukiki.

Lakini YESU hakumaanisha kwamba kila mtu akafe msalabani kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe. Hapana, mwenyewe alishakufa kwa ajili ya dhambi zetu. Jambo linalotokea ni kwamba pale mtu anapoamua kumfuata KRISTO lazima vita viwepo vinavyoletwa na shetani ili tu aiache ile imani. kwamfano mtu anapotaka kumpa KRISTO maisha yake, lakini inatokea wazazi wake na ndugu zake wanakataa au kumtenga na pengine hata kumtishia kifo, sasa hapo anapaswa aingie gharama kwa kukataa mashauri ya ndugu zake na kufuata mashauri ya Mungu, Na hiyo gharama atakayoingia ndio MSALABA wenyewe Kristo aliokuwa anauzungumzia.

Ndugu muislamu hii neema ya thamani iliyo katika YESU KRISTO shetani anaionea wivu na kuiwinda, unapomaanisha kumfuata KRISTO ni lazima kukutana na majaribu ya adui, hivyo kuingia gharama kwa namna moja au nyingine ni lazima (kuubeba msalaba). Lakini fahamu tu! BWANA ameahidi kutokukuacha na atakuwa pamoja na wewe mpaka mwisho. Hivyo mgeukie mpe leo maisha yako naye atakuongoza hata uzima wa milele.

Mungu akubariki.

Unaweza pia ukauliza swali lolote linalokutatiza kuhusu biblia kwa neema za Mungu tutalijibu, lakini iwe ni kwa nia njema ya kujifunza na wala sio mashindano.

Sunday, November 5, 2017

WA KUABUDIWA NA KUPEWA UTUKUFU NI YESU KRISTO PEKEE.


Kuna hatari kubwa sana, kumlinganisha Bwana wetu YESU KRISTO na mtu yeyote, ambaye kwetu sisi ni Bwana na ni Mungu. Tangu zamani Mungu amekuwa akiwatumia watumishi wake kutenda kazi zake akithibitisha kwa ishara na miujiza mingi iliyofuatana nao kiasi cha kwamba baadhi ya watu wasiokuwa na ufahamu kutaka kuwaabudu wao kama Mungu. 


Jambo kama hili tunaweza tukaiona likijitokeza katika enzi za mitume, tukisoma 


[matendo 14:8-15 inasema;
 " Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa.
9 Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa
10 akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.
11 Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu.
12 Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji.
13 Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng'ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano.
14 Walakini mitume Barnaba na Paulo, walikpopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele,
15 wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha].

Kama tunavyoona hapo mitume waliwaambia makutano kuwa wao sio miungu, na anayepaswa kuabudiwa ni mmoja tu!. Vivyo hivyo katika kizazi chetu hichi cha kanisa la mwisho la LAODIKIA,  Mungu alimtumia mtumishi wake mwaminifu ndugu. William Marrion Branham kama mjumbe na nabii wa kanisa hili la mwisho, BWANA  akilithibitisha Neno lake kwa ishara nyingi na miujiza isiyokuwa ya kawaidia iliyofuatana naye, kwa mfano ile nguzo ya moto iliyotokea juu ya kichwa chake wakati anahubiri, utambuzi wa siri za mioyo, sauti kusema naye kutoka mbinguni n.k. Na zaidi ya yote aliwafundisha watu wamgeukie KRISTO na kumwabudu yeye pekee.


Lakini cha kusikitisha ni kwamba yule ibilisi wa zamani ameingia na kunyanyua watumishi wake kumwabudu William Branham kama vile tu dini ya katoliki inavyomwabudu mariamu na kusujudia picha zake, hizi ni ibada za sanamu za hali ya juu.


Hivi karibuni mchungaji mmoja huko nchini Congo ambaye amekuwa akiabudu picha za William Branham kwa muda mrefu, alidiriki kutoa maneno ya makufuru dhidi ya Bwana Yesu Kristo. Siku moja katika mahubiri yake alisimama na kusema YESU ni nyoka, ni shetani na sio Mungu bali william branham ndiye Mungu, aliendelea kusema kama huyo YESU ni Mungu basi aniue sasa hivi. Lakini kabla hata hajamaliza kusema hayo maneno alidondoka saa ile ile na kufa, kwa hofu watu walikimbia na baada ya dakika kama kumi waliporudi walimkuta ameshaoza kaliwa na CHANGO na kuzikwa hapo hapo, kama tu vile Herode alipotaka kujifananisha na Mungu akaliwa na CHANGO(matendo 12:23). tazama video ya tukio hili chini...
Ndugu Mungu sio wa kudhihakiwa wala utukufu wake hagawani na mtu mwingine yeyote, ikiwa wewe unamwabudu bikira Mariamu, ikiwa unaabudu picha za William Branham, ikiwa unawaabudu watakatifu wa aina yoyote, ikiwa unamwabudu Buddha, n.k. Tubu  umgeukie Mungu jiepushe na uzinzi wa kiroho.


BWANA alitoa amri na kusema katika Kutoka 20:3-6" Usiwe na miungu mingine ila mimi.
4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.
5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,
6 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. "

Mungu akubariki.