"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, November 7, 2017

MASWALI YANAYOULIZWA MARA KWA MARA NA WASIO-WAKRISTO: Part 1




SWALI: Napenda kuuliza kama Yesu alikufa kwa ajili ya watu pale msalabani, kwanini basi alisema 
kila mtu abebe msalaba wake?.

JIBU: Tusome hilo andiko Bwana Yesu alivyosema ili tupate nuru zaidi ya kulifafanua..

Luka 14:25" Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,
26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
27 Mtu ye yote ASIYECHUKUA MSALABA WAKE na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?
29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,
30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.
31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?
32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.
33 Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. "

Tunaona hapo kama tukisoma kwa umakini,Yesu alikuwa anazungumzia juu ya "gharama ya kuwa mwanafunzi wake". Kwamba mtu yoyote akitaka kuwa mwanafunzi wake anapaswa kujitoa na awe tayari kukabili kila hali atakayokutana nayo, tuchukulie tu kwamfano mtu yeyote anayetaka kujiunga na jeshi, haendi hivi hivi tu na kuwa mwanajeshi hapohapo ni lazima aingie gharama fulani, na gharama zenyewe ndio hizi; awe tayari kuishi kambini mbali na ndugu zake,awe tayari kuacha vitu vyote, awe tayari kufanya mazoezi magumu, awe tayari kutii kanuni zote za jeshi atakazoamriwa pasipo kuhoji, awe tayari hata kufa kwa ajili ya taifa lake, n.k..

Vivyo hivyo na kwa Bwana Yesu pia alisema mtu yoyote akitaka kuwa mtumishi/mwanafunzi wake, ni lazima akubali kupitia mambo yote hata mabaya kama kuchukiwa na ndugu, kutengwa na wazazi au jamii, akubali kujitenga na mambo ya kidunia, akubali kudharauliwa kwa ajili ya Kristo, kutukanwa, kuuliwa kwa ajili ya Kristo, kuvumilia mabaya n.k. huko ndiko kuuchukua msalaba alikokuzungumzia ambako hakuepukiki.

Lakini YESU hakumaanisha kwamba kila mtu akafe msalabani kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe. Hapana, mwenyewe alishakufa kwa ajili ya dhambi zetu. Jambo linalotokea ni kwamba pale mtu anapoamua kumfuata KRISTO lazima vita viwepo vinavyoletwa na shetani ili tu aiache ile imani. kwamfano mtu anapotaka kumpa KRISTO maisha yake, lakini inatokea wazazi wake na ndugu zake wanakataa au kumtenga na pengine hata kumtishia kifo, sasa hapo anapaswa aingie gharama kwa kukataa mashauri ya ndugu zake na kufuata mashauri ya Mungu, Na hiyo gharama atakayoingia ndio MSALABA wenyewe Kristo aliokuwa anauzungumzia.

Ndugu muislamu hii neema ya thamani iliyo katika YESU KRISTO shetani anaionea wivu na kuiwinda, unapomaanisha kumfuata KRISTO ni lazima kukutana na majaribu ya adui, hivyo kuingia gharama kwa namna moja au nyingine ni lazima (kuubeba msalaba). Lakini fahamu tu! BWANA ameahidi kutokukuacha na atakuwa pamoja na wewe mpaka mwisho. Hivyo mgeukie mpe leo maisha yako naye atakuongoza hata uzima wa milele.

Mungu akubariki.

Unaweza pia ukauliza swali lolote linalokutatiza kuhusu biblia kwa neema za Mungu tutalijibu, lakini iwe ni kwa nia njema ya kujifunza na wala sio mashindano.

No comments:

Post a Comment