"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, November 7, 2017

MASWALI YANAYOULIZWA MARA KWA MARA NA WASIO-WAKRISTO: Part 2



 
SWALI: JE! UKRISTO NI DINI?  Ni wapi kwenye biblia imetaja kama ukristo ni dini?

JIBU: Ili kujibu hili swali ni vizuri kuelewa nini maana ya DINI. Dini ni neno lilitoka kwenye lugha ya kilatini "religio" likiwa na maana kuwa ni mfumo fulani au utamaduni fulani wa kuabudu unaotokana na imani fulani. Kwa lugha iliyo nyepesi dini ni matunda ya imani ya mtu. Kwamfano kitendo cha kufanya ibada, kufunga, kuswali, kuomba dua, kutoa zaka, kuvaa mavazi ya kujisitiri, kuvaa kanzu, kuvaa misalaba, kuchoma ubani, kusujudu,tohara, kuabudu, kutawadha, n.k. haya yote ni matunda ya imani ambayo ndiyo sasa yanayoitwa DINI.
 
Kwa utangulizi huu sasa tunaweza kurudi kwenye swali letu linalouliza je! ukristo ni Dini??.

Jibu ni HAPANA ukristo sio dini na ni swali linaloulizwa mara kwa mara na watu wengi je! ni wapi kwenye biblia imetaja kuwa ukristo ni dini? ni kweli kabisa hakuna sehemu yoyote kwenye biblia inayosema ukristo ni dini kwasababu UKRISTO sio dini.

Hivyo kama sio dini ukristo ni nini basi?

Jibu lake fupi ni hili: "UKRISTO ni IMANI" , Hivyo basi ili uwe mkristo lazima uwe WA-KRISTO (yaani wa YESU KRISTO), Ikiwa na maana kuwa mtu anapomwamini YESU KRISTO ndipo anapokuwa mkristo na sio anapojiunga na shirika lolote la kidini linalojiita la kikristo ndipo awe mkristo kama dini nyingine zinavyofanya.

Na ndio maana kila mahali kwenye biblia YESU alikuwa anasisitiza Neno hili; " yeye aniaminiye mimi"..."yeye aniaminiye mimi".. :Hakusema yeye aaminiye dini ya kikristo au shirika fulani la kikristo ana uzima wa milele, bali "yeye aniaminiye mimi anao uzima wa milele"...Kumbuka YESU sio DINI wala hahitaji dini yako (yaani kutoa sadaka, kuvaa misalaba, kuvaa kanzu, n.k.) ili uwe mfuasi wake, anahitaji IMANI yako kwake kwanza ili uwe mfuasi wake, Na ndio sasa baada ya kumwamini yeye ndipo DINI yako ifuate. Kwahiyo mtu yeyote anayejivunia dini uelewa wake juu ya masuala ya imani bado ni hafifu sana, kwasababu dini isipokuwa na chanzo sahihi cha imani ni kazi bure.

Biblia imetoa tafsiri ya DINI kama ifuatavyo soma Yakobo 1:26
"Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa. "

Unaona hapo biblia inaelezea maana ya dini ya kweli, nayo ni hii; kujizuia ulimi wako, kwenda kuwatazama mayatima, kujilinda na dunia pasipo mawaa akiwa na maana ya kutokuiba, kutokuwa mzinzi, kujisitiri, kuwa safi n.k. Lakini swali linakuja pale pale je! unadhani kwa kuwa na DINI SAFI KAMA HII inatosha kukufanya wewe kuwa mkristo??. HAPANA unapaswa uwe MKRISTO kwa kumwamini YESU KRISTO ndipo DINI yako ifuate kwasababu matendo hayo yote hata wasio wakristo wanaweza kuyaiga, wahindu wanaweza kuyaiga, wabudha wanaweza kuyaiga, hata wapagani wanaweza wakaiga n.k, lakini bado wakawa mbali na UKRISTO.

Hivyo usijivunie DINI bali IMANI yako kwani hata huyo umdhaniaye kuwa adui yako anaweza akawa na DINI safi kuliko hata ya kwako.

Ushauri wangu kwako ndugu  muislamu au dini nyingine mwamini YESU KRISTO leo akupe uzima wa milele, hakuna njia nyingine ya kumfikia Mungu zaidi ya hiyo. Dini haikufikishi kwa Mungu badilisha mtazamo wako.

Yohana 14:6"Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. "

Ubarikiwe.

1 comment:

  1. Bado haujatoa maana ya KRISTO yaani uhusiano wa yesu na kirsto, kwanini tusimwite yesu wa mariam au wa Mungu?

    ReplyDelete