Jibu ni ndio kwasababu biblia inasema pasipo kumwagika damu hakuna ondoleo, ukisoma waebrania 9:22 "Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. "
Hii ndio njia pekee ambayo Mungu aliichagua tangu awali kwamba, ili tendo lolote la rohoni lifanyike na kufanikiwa ni lazima damu ihusishwe, na ndio maana tunaona katika agano la kale ilikuwa kwamba ili mtu apate kibali mbele za Mungu ni lazima aende na sadaka ya damu ambapo mnyama alisiyekuwa na mawaa anachinjwa ili kufanya upatanisho, na mambo yote yanaliyohusishwa na dhambi yalikuwa yanatakaswa kwa damu, hiyo ilikuwa ni kanuni.
Kwahiyo tunaona damu ina mahusiano makubwa kuwa kama kiunganishi kati ya ulimwengu wa mwilini na wa rohoni, na ndio maana hata shetani kwa kulijua hilo anapenda kutumia damu ili kufanikisha mambo yake maovu katika ulimwengu huu, kwamfano mara nyingi wachawi wanawaambia watu wapeleke damu za mnyama fulani ili kufanikisha mambo yao ya kishirikina pamoja na haja za hao watu, na ukitazama kwa makini utaona kuwa wanapendelea zaidi damu za wanadamu kuliko za wanyama kwasababu wanajua hizo zina mlango mkubwa zaidi wa kuunganisha mambo ya rohoni na ya mwilini kiurahisi. Na ndio maana hao wanaotoa damu za watu utakuta matokeo yao ya kiroho(kichawi) yanakuwa ni makubwa zaidi kuliko wale wanaotoa damu za wanyama.
Kuna kitu kikubwa sana ndani ya DAMU ambacho mkristo akikitambua hakuna chochote kitakachomsumbua na hakika ataweza kufanya mambo yote, ataweza kufanya yote ya mwilini na ya rohoni, na kama tunavyojua hiyo damu ili iwe na nguvu ni lazima iwe ya mwanadamu na sio mnyama, tena inatakiwa ipatikane ya mwanadamu asiyekuwa na hila wala mawaa, hakika ikipatikana hiyo ni zaidi ya tambiko lolote ambalo lilishawahi kufanyika duniani!!!
Kumbuka mambo yote yanatoka rohoni, ni ngumu kushindana na watumishi wa shetani ambao wamepata nguvu nyingi za kumkaribia shetani kwa sadaka zao za damu za watu wasio na hatia,halafu na wewe unataka kwenda kushindana nao pasipo damu yoyote, hapo ni lazima ushindwe tu! ni lazima ujue mbinu za kumshinda adui yako, mambo ya rohoni yana kanuni zake.
Lakini habari njema ni kwamba hii damu yenye nguvu ipitayo damu zote isiyoharibika ambayo inaweza ikashinda mambo yote ipo na inajulikana,na hii DAMU si nyingine zaidi ya DAMU YA YESU ambayo haikuwa na hila wala mawaa yoyote. lakini wengi wanashindwa kuielewa matumizi yake, na ndio maana shetani anaendelea kupata nguvu juu yao,
Jambo shetani analotaka ni waifahamu tu lakini wasiielewe matumizi yake, kila mtu anaifahamu damu ya YESU lakini ni wachache wanayoielewa, siku utakapoielewa kisawasawa utamshinda shetani kwa kila nyanja.
ukisoma;
Ufunuo 12:9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
10 Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.
11 NAO WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. "
Unaona hapo? ni Damu tu ya mwana-kondoo inayoweza kumshinda yule joka ( shetani ) na hakuna kingine chochote. Lakini wengi wanadhani utamshinda kwa kutamka tu "nakukemea kwa damu ya Yesu"..."na kukemea kwa damu ya Yesu"...akidhani hapo amempata shetani, kumbe hajui hapo hajafanya lolote kama hajaingia ndani ya hilo Agano kwanza. Ni lazima uingie kwanza.
JINSI YA KUINGIA KATIKA HILI AGANO LA DAMU YA YESU.
Kumbuka katika agano la kale kuhani mkuu alipokuwa akienda kila mwaka kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa njia ya damu za wanyama, hakuwa anafanya kwa watu wote wa ulimwengu mzima bali tu kwa wale waliokuwa katika hilo agano yaani wana wa Israeli pekee. Na ndio waliokuwa wanafunikwa dhambi zao na kushiriki baraka zote za rohoni na sio watu wa ulimwengu mzima.
Vivyo hivyo katika Agano jipya ili maombi yako yasikiwe, ili sadaka zako zikubaliwe, ili dhambi zako zisamehewe, ili uweze kumshinda shetani na magonjwa yake yote na laana ni lazima uingie katika hili Agano jipya la DAMU YA YESU KRISTO. na hauingiii kwa kuzaliwa katika familia ya kikristo, wala hauingii kwa kujiunga na dhehebu fulani, wala hauingii kwa njia nyingine yoyote isipokuwa KWA KUTUBU kwanza, NA KUMWAMINI YESU KRISTO, NA KUBATIZWA KWA JINA LA YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kisha upokee ROHO MTAKATIFU hapo ndipo umezaliwa mara ya pili na umeingia katika hili AGANO KUU la DAMU YA YESU KRISTO.
Sasa kuanzia hapo na kuendelea ile damu inaanza kunena kwa ajili yako mbele za Mungu, shetani hana la kukushinda kwa lolote, wala la kukushitaki, kwasababu damu isiyoharibika tayari ipo kunena kwa ajili yako, hauhitaji kupigana na wachawi, wala waganga, wala kuogopa magonjwa au shida, ipo hiyo damu tayari inafanya kazi kuliko tambiko lolote lililowahi kufanyika tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu. Kumbuka shetani anapotaka kuleta laana juu yako jambo la kwanza analoangalia ni je! upo chini ya damu? shetani hawezi kulaani kilichobarikiwa kama vile Balaamu alivyoshindwa kuwalaani wana wa Israeli.
Kwahiyo ndugu hakuna njia nyingine yoyote katika hii dunia unaweza ukamshinda shetani isipokuwa kwanza kutubu, na kumruhusu Yesu Kristo ayasafishe maisha yako kwa damu yake, uchukua uamuzi wa kubatizwa leo kwa ubatizo ulio sahihi wa kuzamishwa na sio wa kunyunyuziwa na iwe ni kwa jina la YESU KRISTO kulingana na maandiko ( matendo 2:38.), kisha Bwana atakupa Roho Mtakatifu hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili na kuingia katika lile AGANO KUU LA DAMU YA YESU, kwa uhakika wa maisha yako ya sasa na ya baadae, kumbuka hakuna ubatizo wa watoto wachanga, kama ulifanyiwa hivyo hapo hujabatizwa unapaswa ukabatizwe tena.
Nakukumbusha tena ndugu yangu hauwezi ukamshinda shetani kwa njia nyingine yoyote ile, sio kwa matendo, wala kwa juhudi yako bali kwa damu ya mwana-kondoo pekee.
Ufunuo 12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. ". tubu, kabatizwe na upokee Roho Mtakatifu.Mungu akubariki!
No comments:
Post a Comment