"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, March 28, 2018

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU

Naomba usome ushuhuda huu mfupi utakujenga,
 
 "Mimi na ndugu yangu tumekuwa na desturi ya muda mrefu kukaa pamoja na kushirikishana NENO LA MUNGU mara nyingi ili kuepuka usumbufu wa watu tumekuwa tukiondoka na kwenda mbali na makazi ya watu, sehemu zenye utulivu na kutumia muda mwingi kulitafakari NENO LA MUNGU, pamoja na kutiana moyo katika safari yetu ya Ukristo. Siku moja wakati tunatembea muda wa mchana kama saa 7 huku tunazungumza habari za Mungu na kutafakari ghafla mbele yetu njiani umbali si mrefu sana, tulioana punda watatu wamefungwa NIRA wanafuata njia, wakikokota kigari cha mzigo wa majani na nyuma kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akiwaendesha hao punda, lakini jambo moja lilitushangaza kidogo ni kuona punda 3 wamefungwa nira huku wakikivuta kile kigari wakati mara nyingi inakuwa ni punda wawili tu!.

Hivyo tulipokaribia kuwasogelea ili tuone vizuri, Yule punda aliyekuwa katikakati yao alitoweka wakabaki punda wawili kama kawaida. Wakati tunalishangaa hilo tukio lilitokea wale punda walifika mahali wakakuta na mtaro, uliokuwa mgumu kidogo kuvuka kutokana na ule mzigo waliokuwa wanauvuta, hivyo Yule Bwana wao aliokuwa anawaongoza alipoona wamesimama aliwachapa kwa fimbo yake aliyokuwa nayo, lakini japo ule mzigo ulikuwa ni mkubwa kwa wao kuuvukisha katika ule mtaro mwishoni walifanikiwa kupandisha na kuendelea na safari.
Tulibaki tunajiuliza maswali ni kitu gani tumeona? Ni mazingaumbwe au nini?. Ndipo Mungu akutupa ufahamu saa ile ile ni kwamba Mungu alitufumbua macho tuone jambo linaloendelea katika roho kuhusu sisi,"


Biblia inasema Mathayo 18:20 “ Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”

Tafsiri ya lile ono ni kuwa wale punda wawili wanatuwakilisha sisi wawili mimi na ndugu yangu, Yule punda wa tatu aliyekuwa katikati na kisha baadaye akaja kutoweka alimwakilisha Bwana YESU.

Na ule mzigo wale punda waliokuwa wameubeba ni SHERIA ZAKE, hivyo tunapokuwa wawili au zaidi Mungu anatufunga Nira yake mwenyewe sisi kwa sisi, na yeye akiwa katikati yetu kutusaidia mzigo wake(sheria zake), hivyo sheria zake zinakuwa nyepesi kuzishika.

Bwana Yesu pia alitupeleka kwenye hili andiko Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 JITIENI NIRA YANGU, MJIFUNZE KWANGU; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 KWA MAANA NIRA YANGU NI LAINI, NA MZIGO WANGU NI MWEPESI.

Bwana alituonyesha kuwa anayo NIRA yake na MZIGO wake kwa watu wake, japo watu wa nje watauona kama ni mzigo mzito lakini Bwana akiwa katikati yetu unakuwa mwepesi kwasababu yeye anatusaidia, anakuwa anafanyika kama punda wa tatu katikati yetu.

> Kuishi maisha ya kuukataa ulimwengu huo ni mzigo wa Kristo aliokutwisha, na ndio maana wengine watakushangaa unawezaje kuishi maisha ya kutokufanya uasherati.

> Kufanya kazi yoyote ya Mungu ni mzigo wa Kristo, lakini yeye anakupa wepesi hususani mnapokuwa wawili au zaidi na ndio maana kila mahali Bwana alikuwa akiwatuma wawili wawili kazini kuhubiri injili.

Hivyo ndugu, kuna umuhimu mkubwa kuwa na mwenzako au wenzako mnaofanana imani, kwasababu mnapokuwa wawili au watatu au zaidi kwa jina lake lile NENO lazima litimie, ATAKUWA KATIKATI YENU. Mnakuwa mmefungwa NIRA na Kristo pamoja, hivyo mtajikuta kiurahisi mnazitimiza sheria za Bwana bila ugumu wowote tofauti na unapokuwa mwenyewe.

Umuhimu wa kuwa na mwenzako au kukusanyika na wenzako ni uwepo wa kipekee unashuka mahali mlipo, vitu kama faraja, kutiana moyo, kulindana, kushirikishana, mafunuo n,k. vinatoka huko kiasi kwamba hata shetani inamuwia ugumu kupata nafasi ya kukujaribu kwasababu yupo ndugu yako pembeni anayekuchunga.

Ndio maana biblia inasema katika Mhubiri 4:9-12 “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.
10 Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua!
11 Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?
12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.”

Unaona hapo, kuna umuhimu wa kuwa karibu na ndugu anayeenda na wewe imani, Sisi baada ya Bwana kutufundisha hayo, tumekuwa tukikaa pamoja muda mrefu wakati mwingine kuanzia asubuhi mpaka jioni na tumekuwa tukimwona Mungu kwa namna ya kipekee isiyokuwa ya kawaida tofauti na pale mwanzo kila mtu alipokuwa kivyake.

Unawakumbuka wale watu wawili waliokuwa wanatoka Yerusalemu na kuelekea Emau, Njiani wakati wanazungumza habari za kufufuka kwake Yesu, Bwana mwenyewe aliwatokea na kuungana nao pasipo wao kujijua, baadaye kabisa mwishoni ndipo walipofunguliwa macho na kufahamu kuwa Yule alikuwa ni BWANA YESU mwenyewe(Luka 24).

Vivyo hivyo na wewe utakapojumuika na mwenzako au wenzako na kuanza kumzungumzia Bwana Lile Neno lake la ahadi lazima litimie. Na safari yako ya ukristo haitahitaji nguvu nyingi.
Natumai ushuhuda huu utakufanya uchukue uamuzi wa kujumuika na ndugu aliye  moja na wewe.

Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment