Ni rahisi KUANGUKA au KUPOA katika Imani kama hautajiwekea utaratibu wa Kujikumbusha matendo yote mema Mungu aliyokutendea nyuma katika maisha yako. Jambo lililowafanya Wana wa Israeli kule jangwani washindwe kusonga mbele na kukwazwa na mabaya, lilikuwa si lingine zaidi ya KUSAHAU fadhili za Mungu walizotendewa nyuma, kwamfano walipotoka Misri, na kukutana na kikwazo cha bahari, walianza kunung’unika wakasahau siku chache tu nyuma Mungu aliwapigania kwa mkono hodari dhidi ya maadui zao wamisri,
vivyo hivyo mara baada tu ya kufanyiwa muujiza mwingine wa bahari kupasuka walimshangilia Mungu kwa furaha na kumwimbia nyimbo za shangwe lakini baada ya siku tatu mbeleni, manung’uniko yakaanza tena pale walipokosa maji ya kunywa, tatizo lilikuwa ni moja tu! Walisahau wema wa Mungu waliotendewa siku chache nyuma, laiti wangetilia maanani mema yale na kukumbuka fadhili zote zile, wasingeshindwa kustahimili majaribu waliyokutana nayo. Na ndivyo ilivyoendelea kuwa katika safari yao yote, manung’uniko kila walipokutana na changamoto.
Na ndio sababu Mungu aliwakataza Israeli wote wasile WANYAMA WASIO CHEUA, kwa mfano nguruwe au farasi nk. Unajua ni kwa sababu gani??, kwasababu katika roho wanafunua kitu Fulani. Mnyama anayecheua ni mnyama ambaye akila chakula anao uwezo wa kukirudisha tena kinywani mwake na kukitafuna kisha akimeze tena, kwa mfano ng’ombe analo tumbo la akiba, akila baadaye anarudisha na kukitafuna tena. Hivyo wanyama wa namna hiyo hawakuwa najisi, kwa tabia hiyo tu. Ikifunua katika roho kuwa watu wote wasiokuwa na uwezo wa kuzikumbuka na kuzitafakari fadhili na sheria za Mungu ni NAJISI mbele zake. Watu wote wa Mungu wanapaswa wawe na uwezo wa kucheua, baada ya kusikia au kufanyiwa miujiza, sasa kinachofuata ni kuyarudisha tena katika akili na kuyatafakari hayo kila mara.
Yakobo 1: 22-25 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.23 Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.24 Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.25 Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, ASIWE MSIKIAJI MSAHAULIFU, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.”
Kadhalika na kwa wakati tuliopo sasa, ili tusonge mbele au tuweze kusimama katika IMANI na kushinda wakati wa majaribu inatupasa tujiwekee utaratibu wa kutafakari na kujikumbusha kila siku mambo mema ambayo Mungu amewahi kututendea katika maisha yetu ya nyuma, Kwa mfano ulipowahi kupatwa na ugonjwa Fulani ambao ulikutesa sana na Bwana akakuponya, ni vizuri kujikumbushia jambo hilo kila siku, au ulimwomba Mungu jambo Fulani akakupa na kukufanikisha katika mambo yako na ukafahamu kabisa huyo ni Mungu aliyekutendea hivyo, unapaswa kulifikiria hilo kila siku usije ukasahau pale tatizo litakapokuja ili uweze kukabiliana nalo.
Kumbuka tena mahali Mungu alipokushindania ambapo unajua kabisa pasipo yeye usingeweza kufanikiwa, uwe unalitafakari hilo kila siku litakusaidia huko mbeleni ili umsimnung’unikie Mungu..Kuna hatari kubwa sana ya kuanguka kama hautajijingea huo utaratibu wa kukumbuka mambo uliyotendewa..Sisi wanadamu tuna tabia ya kusahau hivyo ili usisahau ni vizuri uwe unaandika chini kila wema Mungu anaokufanyia kila siku.Kwa kufanya hivyo ndivyo utakavyoweza kudumu katika IMANI siku zote. Na pia unaposoma Neno la Mungu jenga tabia ya kujikumbusha kila wakati ili usisahau mapenzi ya Mungu katika maisha yako.
Wakati mwingine unajikuta unadondoka katika dhambi za usengenyaji, kwasababu unasahau Neno la Mungu, linakuwa halijakaa kwa wingi ndani yako, unajikuta unashindwa kusamehe kwasababu huna tabia ya kutafakari kila siku NENO LA MUNGU, Unajikuta wewe ni mkristo lakini unazungumza maneno ya mizaha, kwasababu mistari inayohusiana na mambo kama hayo imefutika ndani ya moyo wako, huna jambo la kukukumbusha kila wakati.
Ni maombi yangu utaanza kujenga utaratibu kuanzia leo wa kurekodi mambo yote mazuri Mungu anayokutendea ili yawe akiba kwa wakati wa shida au majaribu mbeleni. Na pia utaanza kutafakari NENO la Mungu kila siku. Sulemani kwa hekima ya Roho alituandikia sisi tulio watoto wa Imani na kusema;
Mithali 7:2 “Mwanangu, yashike maneno yangu, Na kuziweka amri zangu akiba kwako.2 Uzishike amri zangu ukaishi, NA SHERIA YANGU KAMA MBONI YA JICHO LAKO.3 ZIFUNGE KATIKA VIDOLE VYAKO; ZIANDIKE JUU YA KIBAO CHA MOYO WAKO.”
Na Daudi alisema;
Zaburi 119: 97 “Sheria yako naipenda mno ajabu, NDIYO KUTAFAKARI KWANGU MCHANA KUTWA.98 Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, KWA MAANA NINAYO SIKU ZOTE.99 Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo NIZIFIKIRIZO.100 Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.”
Ubarikiwe na BWANA YESU.
No comments:
Post a Comment