"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, January 30, 2018

FUVU LA KICHWA.


Luka 23:32 "Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye.
33 Na walipofika mahali paitwapo FUVU LA KICHWA, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. "

Zamani zile tunafahamu utawala wa kikatili wa kirumi, uliua watu wengi kwa kuwatundika katika miti na misalaba, ni utawala uliokuwa umesambaa karibia ulimwenguni kote, na Israeli pia, Lakini tunaona wakati wa kumsulibisha Bwana wetu Yesu Kristo walimchukua na kumpeleka mahali panapoitwa FUVU LA KICHWA, Lakini swali la kujiuliza ni kwanini asipelekwe mahali pengine kama vile bethania, au Emau, badala yake walimpeleka mahali panapoitwa FUVU LA KICHWA.? Ipo sababu.

Vitu hivi vinafunua mambo ya rohoni, kama vile tu biblia inasema wana wa Israeli ule mwamba waliounywea maji kule jangwani, haukuwa tu ni mwamba wa kawaida, bali katika roho ulikuwa unamfunua Kristo, (1Wakorintho 10:4) Kadhalika na katika tukio hili.

Ni kiashirio cha wazi  kuwa kabla Kristo hajapandishwa msalabani tayari walikuwa wameshamsulibisha katika VICHWA vyao wenyewe, Kitendo cha kumpandisha msalabani ni matokeo tu ya kitu kilichokuwa kimeshatendeka  ndani , walishamkataa tangu siku nyingi na ndio maana biblia inasema Yohana 3:19 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. " unaona hapo NURU ilikuja lakini waliipinga tangu mwanzo. Bwana alikataliwa tangu kuzaliwa kwake kama tunavyosoma katika maandiko habari hizo zilimfadhahisha Herode pamoja na Israeli yote. Alipingwa na viongozi wa dini pamoja na jamaa zake wakaribu,wengine walimsaliti, wengine walikuwa wanamjaribu kwa maneno ili wapate jambo la kumshitaki, sasa huko ndiko kumsulibisha Kristo katika vichwa vyao.

Isaya 53:3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.

Ni rahisi kusema mimi ningekuwepo  kipindi kile cha Bwana Yesu kamwe nisingeshirikiana nao kumsulibisha Bwana, Lakini ukweli ni kwamba Kristo anasulibishwa mpaka leo, na jambo hili linaanzia katika VICHWA VYA WATU.

huwezi kusema moja kwa moja unamsulibisha Kristo lakini ulishamsulibisha Katika KICHWA CHAKO, kwa kulikataa Neno La Mungu lilipokuwa linalia ndani ya moyo wako kwa mara ya kwanza na ukakataa kutubu, Ulipenda Giza kuliko Nuru.
Unakuwa ni mtu wa kutoa  maneno ya kijeli na mizaha juu ya jina la Bwana( maneno kama " eti unakuja umekuwa Yesu?), ni kumsulibisha Kristo, unapoambiwa ukweli na moyoni mwako unajua kabisa ni kweli lakini unapinga kama walivyofanya wale mafarisayo na masadukayo ni sawa na kumsulibisha Kristo huna tofauti na watu wa kipindi kile, n.k.

Huu ni wakati wa kufungua moyo wako, Kristo ayafanye maisha yako kuwa mapya, badilisha fikra zilizo ndani ya fuvu la kichwa chako, kwa kulitii NENO la Mungu uokolewe, ukabatizwe katika ubatizo sahihi utakaokuwezesha kuwa na uhakika wa kuondolewa dhambi zake, nao si mwingine zaidi ya kuzamishwa kwenye maji tele katika Jina la YESU KRISTO, na kuanzia hapo uishie maisha ya yakumpendeza yeye, ili jambo lile lisikutokee kama lilivyowatokea wale watu wa wakati ule.
 

Wanaomsulibisha Kristo mara ya pili, biblia inasema ni vigumu kufanywa upya tena, kwasababu WANAMFEDHEHI Bwana kwa DHAMIRA ZAO, (Waebrania 6:5)..Hivyo tukiyajua hayo tumwombe Mungu tusifike huko, tuwe tayari kugeuka, kwa kumaanisha kutubu dhambi zetu,  ili Bwana atuponye.

Ubarikiwe

No comments:

Post a Comment