"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, January 31, 2018

NJIA MUNGU ALIYOIWEKA KWA KILA JAMBO:

Kuna NJIA za kufikia kila jambo, ambayo Mungu tayari alishaziweka tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, kwa mfano ili mwanadamu amfikie Mungu, tayari njia ilishaandaliwa, nayo ni YESU KRISTO, (Yohana 14:6" Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi". ), watu wengi wanapotea wakidhani au wakijifariji kuwa zipo njia nyingi mbalimbali za kumfikia Mungu na zote zinaishia sehemu moja, kwamba unaweza ukawa muhindu, au m-muhamedi au m-budha n.k. na bado ukafika kwa Mungu. Huo ni uongo NJIA ni moja tu (nayo ni YESU KRISTO) na Mungu alishaitengeneza na hakuna mikato. Hivyo kama unataka kumfikia Mungu ni sharti upitie hiyo, nyingine zote zinapotosha.


Vivyo hivyo pia katika kufikia BARAKA fulani za MAISHA, Kuna njia ambazo Mungu alishaziweka zifuatwe hapa duniani, kwamfano ili kupata afya, ili kupata maisha marefu, ili kupata mafanikio, ili kupata cheo, ili kupata amani,n.k. ni lazima uzingatie njia hizo ambazo Mungu alishaziweka vinginevyo utajikuta unakosa shabaha na kuona kama Mungu hana msaada wowote kwako kwasababu tu ulikosa kujua njia sahihi ya kupita ili kufikia malengo yako ni ipi.


Kwa mfano Njia ambayo Mungu aliiweka kwa mtu apate kuishi maisha marefu na ya kheri biblia inasema katika Mithali 10:27 "Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa. Na pia ukisoma.." Waefeso 6:2-3 inasema " Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia."

Kwahiyo kama ungependa uwe na maisha marefu hapa duniani kwanza ni UMCHE BWANA, na lingine ni kuwaheshimu wazazi, lakini njia nyingine zinazoonekana kuwa ni sawa kama vile kuzingatia MLO KAMILI, kuzingatia MAZOEZI, au Kupata muda mrefu wa kupumzika, au kuzingatia vyakula vya asili, vyote hivyo ni sawa lakini Havikuongezei maisha marefu na ya Kheri duniani. Kumbuka kosa la kwanza lilofanya maisha ya wanadamu kupunguzwa kutoka miaka 1000 mpaka miaka 120 ilikuwa sio kutokuzingatia mlo kamili bali ni kwasababu ya kutokushika maagizo ya Mungu. Hivyo kama unalegalega na njia zako hazimpendezi Mungu badilika sasa ishi maisha ya kumpendeza Mungu kama Mkristo na zingatia pia kuwaheshimu wazazi Mungu aliokupa hapa duniani. Kwa kufanya hivyo Mungu atakuongezea maisha marefu na sio tu marefu bali pia na ya Kheri.


Vivyo hivyo ili kupata afya, ni vizuri ukafahamu njia ya Mungu ni ipi aliyoiweka yeye, Mithali 3:7 Usiwe mwenye hekima machoni pako; MCHE Bwana, ukajiepushe na uovu. Itakuwa AFYA MWILINI PAKO, Na mafuta mifupani mwako. " Ukisoma pia. Kutoka 15:26 "akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye. ".


Mara nyingi tunajiuliza kwanini kila kukicha magonjwa yanatuandama, nimezunguka kutoka kwa mtumishi huyu hadi mtumishi huyu, nimeombewa na kila mtu lakini hali inazidi kuwa mbaya unaona kama vile Mungu hayupo pamoja nawe, Lakini hujui kuwa wewe ndio umemwacha Mungu na shetani ndipo anapopata nafasi ya kukutesa kwasababu umeiacha njia ambayo Mungu aliiweka tangu mwanzo tuiendee na kuwa na afya zetu, huwezi ukawa mwasherati, mlevi, mvutaji sigara, msengenyaji, fisadi, mwizi, au mtukanaji n.k halafu hayo yote yasikupate. Kumbuka biblia inasema KUMCHA BWANA ni KUCHUKIA UOVU (Mithali 8:13). Jifungue mwenyewe kwanza katika hivyo vifungo vya uovu kwa kuacha kutenda dhambi, kumpoke Yesu Kristo, ndipo Bwana akulinde na maradhi kwasababu yeye anasema "ndiye Bwana akuponyaye", Kwahiyo hauhitaji nguvu nyingi kujinyima kula vyakula vya aina fulani, au kuzunguka kwenda kuombewa na watumishi wakati wewe mwenyewe unaweza kujifungua..KUMCHA BWANA ndio msingi wa kila kitu!!

Vivyo hivyo ili kupata mafanikio ya kimwili ipo njia ambayo Mungu alishaiweka ukiikosa hiyo utaona kama vile Mungu kakuacha kwasababu Mungu siku zote anatembea katika kanuni zake na si katika kanuni zetu sisi tunazotaka yeye azitembelee. Tumekuwa tukimkumbusha Mungu kila siku tukisema "Mungu umesema; Utatubariki mijini, utatubariki mashambani, utatubariki tuingiapo utatubariki tutokapo, utatubariki kapu letu, na vyombo vyetu vya kukandia unga, atatufanya kuwa vichwa wala si mikia, atatubariki mifugo yetu na uzao wa matumbo yetu n.k."


Ni wimbo ambao tumekuwa tukiuimba pengine pasipo kuona matokeo yoyote, na kufanya watu waishie kuzunguka kutoka kwa nabii huyu hadi nabii huyu,.Nataka nikuambie tu ndugu yangu mtu anayekutamkia kwamba "pokea baraka mwaka huu", ki-uhalisia ni kwamba huyo mtu hajakubariki bali "AMEKUTAKIA TU KHERI"..kama vile tu mtu anavyokutakia Kheri ya mwaka mpya, au kheri ya maisha marefu.


BARAKA HALISI INATOKA WAPI?

Tumesahau Neno moja katika hiyo mistari ambalo ni la muhimu sana nalo ni "IKIWA".."IKIWA UTAKAPOSIKIA SAUTI YA BWANA MUNGU WAKO"

Kumbukumbu 28:1 inasema; ITAKUWA UTAKAPOSIKIA SAUTI YA BWANA, MUNGU WAKO, KWA BIDII, KUTUNZA KUYAFANYA MAAGIZO YAKE YOTE NIKUAGIZAYO LEO, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;
2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.
3 Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.
4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.
5 Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.
6 Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo...."

Kwahiyo unaona hapo NJIA Mungu aliyoiweka ili kupokea hizo baraka, ni KWA KUYATUNZA NA KUYAFANYA MAAGIZO YOTE YA MUNGU, ambayo ki uhalisia ni wachache wanafanya hivyo, utakuta mtu ni fisadi au mla rushwa bado anakwenda mbele za Mungu na kumwomba baraka, utakuta mtu anaishi maisha ya anasa halafu anamfuata mtumishi amwombee abarikiwe, utakuta mtu hata hana mpango na Mungu na yeye pia anakimbilia kwenda kununua mafuta ya upako, hiyo ni sawa na uganga wa kienyeji tu, ni vyema ukaacha na kutubu. Njia pekee Mungu aliyoiweka ni KUMCHA yeye na kuyashika aliyokuagiza, kwa kuzingatia hivyo hautahitaji kwenda kwa mtumishi yoyote akuombee, au kukesha kuomba, au kutumia mafuta au chumvi vinavyoitwa vya upako, ili kufanya mambo yabadilike, Mungu mwenyewe atakutengenezea njia, kwa wakati wake, kwasababu anasema yeye mwenyewe anajua kuwa tunahaja na hayo yote.


Na ndio maana biblia inasema..Mathayo 6:32-33 "...kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa." Usihangaike huku na huko, hakutakusaidia chochote MCHE MUNGU.

Vivyo hivyo ukitaka CHEO (ukubwa mahali popote), njia ipo nayo ni "kuwa mdogo kuliko wote" jinyenyekeze kwa maana ajishushaye atakwezwa na ajikwezaye atashushwa,usitumie njia za kujipendekeza kwa watu ili upate kibali wewe jishushe kuwa mnyenyekevu hakuna mtu yeyote asiyependa mtu mnyenyekevu..hizo ndio NJIA zilizowekwa na Mungu, ukitaka kupokea vitu kutoka kwa watu, Bwana Yesu alisema.. katika Luka 6:38 "Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. " Hata siku zote ili bomba litoe maji ya kujaza vyombo vingi ni sharti lifunguliwe, lakini likifungwa litabakia na maji yake ya ndani tu..vivyo hivyo ukitaka upokee "favour" inakupasa utoe kwa wengine na kwa Mungu.

Ukitaka furaha, amani na watu, mche Bwana kwa kuzishika amri zake,Mithali 16:7 " Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye."

Sulemani mtu aliyekuwa na mafanikio na mwenye utajiri mwingi kuliko watu wote waliomtangalia na waliokuja baada yake, japo katika ufahari wake wote alihitimisha na kusema..Mhubiri 12:13-14" Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; MCHE MUNGU, NAWE UZISHIKE AMRI ZAKE, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya. "

Sisi ni akina nani tusimche Bwana?.

Ubarikiwe sana na Bwana wetu YESU KRISTO.

No comments:

Post a Comment