"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, May 1, 2019

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1


Shalom!..Karibu tujifunze Maneno ya Mungu ya uzima, leo tunajifunza kwa uchache juu ya vitabu vya Biblia, jinsi vilivyoandikwa na maudhui yake, kwa neema za Mungu.
 
Zamani mwanzoni wakati nampa Bwana maisha yangu, nilikuwa siielewi biblia vizuri, vitabu nilivyokuwa navielewa vilikuwa ni vile vya injili tu! Yaani Mathayo,Marko, Luka na Yohana…na katika agano la kale kitabu cha Mwanzo kidogo na Kutoka ndio nilikuwa nikivisoma navielewa, na cha Esta pamoja na Ruthu…kwasababu mtiririko wa hadithi zake umejipangilia vizuri… Lakini vitabu vingine kama Zaburi, Mithali,Ezekieli, Yeremia, Isaya, Danieli, Habakuki, Malaki n.k nilikuwa sivielewi kabisa.. Kwasababu nilikuwa sijui viliandikwa kwa sababu gani..Na mwandishi alikuwa anaviandika katika mazingira gani…kwaufupi vilikuwa vinanichanganya sana.

Kwahiyo niliishia kuhisi tu kuwa kitabu kama cha Isaya, kiliandikwa na Nabii Isaya pengine ndani ya siku moja au mbili, au ndani ya wiki moja, nilikuwa nadhani alikuwa anajifungia ndani na kisha maneno ya Mungu yanamshukia na anayaandika kwenye kitabu aya baada ya aya, hivyo pengine ilimchukua muda kama wa wiki moja hivi kumaliza kuandika sura zote 66…Na vitabu vingine nilijua ndio hivyo hivyo. Lakini kumbe ulikuwa ni uchanga tu wa kiroho.

Hakuna kitabu kizuri na kilichopangiliwa vizuri kama BibliaTakatifu, ni kitabu pekee kilichoandikwa kwa utaratibu mzuri na mpangilio endapo ukikielewa. Leo kwa ufupi tutaanza kujifunza mpangilio huu jinsi ulivyokaa na tutaanza na vitabu vichache..
 
 

1) Kitabu cha MWANZO: 
 
Kiliandikwa na Nabii Musa, wakati akiwa jangwani baada ya kuwatoa tu wana wa Israeli Misri, Bwana alimpa ufunuo wa kilichotokea Edeni na hata kabla ya Edeni. Alimpa ufunuo pia wa jinsi dunia ilivyoumbwa katika siku zile 6, na akaambiwa aandike vile ilivyoandikwa, kumbuka Musa ndiye Nabii pekee aliyekuwa anazungumza na Mungu uso kwa uso. Lakini pia kitabu cha Mwanzo hakijabeba tu historia ya Adamu na Hawa, Bali pia kimebeba historia ya dunia kuangamizwa kwa gharika, habari za Nuhu na safina, habari hizo pia ziliandikwa na Nabii Musa, ingawa kabla ya Musa pia habari hizo zilikuwa zinafahamika na baadhi ya watu, pia historia ya Wana wa Israeli, kuanzia Ibrahimu mpaka Yusufu na mpaka walipoingia Misri wapo watu wachache walikuwa na rekodi ya chimbuko lako. Kwahiyo Musa wakati yupo jangwani na wana wa Israeli aliagizwa na Mungu aandike mambo hayo, na akayaandika kwenye kitabu na hicho kitabu ndio kinaitwa mwanzo.

2) Kitabu kinachofuata ni kitabu cha KUTOKA
 
Nacho kiliandikwa na huyo huyo Musa, akiwa jangwani pamoja na wana wa Israeli…Kilikuwa ni kitabu kirahisi kwasababu hakikuhitaji ufunuo wowote wa Roho kukiandika, ilikuwa ni kuandika tu mambo waliyokuwa wanayapitia siku baada ya siku,na waliyokuwa wanayaona..tangu Musa alipotumwa na Mungu kwenda kwa Farao, mpaka mapigo Farao aliyopigwa, mpaka kuvushwa bahari ya Shamu, mpaka walivyolishwa mana jangwani, mpaka wakati wa kukabidhiwa amri kumi na kupewa maagizo ya kutengeneza Maskani ya Bwana,...Kwahiyo hakikuwa kitabu kigumu kuandika kwasababu ni maisha waliyokuwa wanayaishi, na mambo waliyokuwa wanayaona..kulikuwa hakuna haja ya mtu kuwaadithia au kungojea ufunuo kutoka kwa Mungu ya jinsi ya maneno ya kuandika kama ilivyo kwenye kitabu cha UFUNUO.

3) Kitabu kinachofuata ni MAMBO YA WALAWI.
 
 Kitabu hichi kiliandikwa na huyo huyo Musa wakati wana wa Israeli bado wapo jangwani katika safari yao ya kuelekea Kaanani. Baada ya Mungu kuwapa sheria alimwagiza Musa awatenge wana wote wa Lawi, ambalo ndio kabila lake Musa, alifanye kuwa kabila la kikuhani..Na hivyo kama limeteuliwa kuwa kabila la ukuhani, hivyo ni lazima kutakuwepo na majukumu machache machache yanayowahusu hao makuhani walawi (yaani Kabila la Musa).

Kwahiyo Mungu akamwagiza Musa aandike kitabu kitakachowahusu hao walawi na majukumu yao katika utumishi wa kikuhani. Kama ukisoma kitabu cha mambo ya walawi utaona kulikuwa na majukumu mengi sana, ambayo yaliwahusu maana hao ndio waliochaguliwa na Mungu kuwa kama wawakilishi wake duniani, wajukumu yote ya namna ya kuwahudumia wana wa Israeli kuhusu masuala ya kiibada waliyabeba wao, kwahiyo ilipasa kiwepo kitabu pekee cha namna ya kuendesha ibada ndani ya hema ya kukutania, ndio maana utaona ndani ya kitabu hicho kimejaa maagizo kwa wana wa Lawi ya namna ya kumtolea Mungu sadaka, utaona wana wa HARUNI (Ambao ndio wana wa Lawi) wanaagizwa nini cha kuvaa wakati wakitumika kwenye hema, namna ya kuiandaa sadaka pindi inapoletwa na wahusika namna ya kuikata kata na kuiweka juu ya madhabau, na wanafundishwa pia jinsi ya kutumika madhabahuni utaratibu na zamu,wanafundishwa namna ya kuvukiza uvumba, wanafundishwa jinsi ya kufanya upatanisho kwa dhambi za wana wa Israeli, wanafundishwa pia namna ya kumfanyia mtu utakaso pindi anapokuwa najisi, au anapotenda dhambi, wanafundishwa pia sheria za kuwafundisha watu na hukumu zake, ikiwa imetokea mtu amefanya kosa atendewe nini n.k

Kwahiyo kwa ufupi ni kitabu kinachohusu MAJUKUMU YA WANA WA LAWI ndio maana kinaitwa MAMBO YA WALAWI..Musa pamoja na Haruni ndugu yake walikuwa WALAWI. Kwahiyo kabila lao liliteuliwa na Mungu kuwa Kabila la KIKUHANI. Walikuwa hawana jukumu linguine zaidi ya hilo. Kitabu hichi pia kimeelezea maagizo na aina za sadaka wana wa Israeli wanazopaswa kumtolea Mungu..Na jinsi wanavyopaswa wazipeleke kwa makuhani WALAWI.

4) Kitabu cha cha Nne ni HESABU: 
 
Kitabu hichi kiliandikwa na Nabii Musa huyo huyo, wakati bado wakiwa katika safari yao jangwani. Kipindi wana wa Israeli wanatoka Misri walitoka kama jeshi la mtu mmoja..walikuwa ni wadhaifu kwa hiyo Mungu aliwapigania dhidi ya maadui zao kwa asilimia zote, hawakutumia hata upanga wao au visu vyao kushindania wokovu wao…Ulikuwa ni mkono wa Mungu mwanzo mwisho, hawakunyanyua hata kisu kushindana na maadui zao, utaona Farao adhabu alizokuwa anapata ni Mungu mwenyewe ndio aliyekuwa anahusika mwanzo mwisho, hakuna hata jiwe la mwisraeli mmoja lililohusika, mpaka wanatoka Misri ndio ilikuwa hivyo..Lakini mbeleni utakuja kuona wana wa Israeli wanabadilika tabia, wanaanza kuukataa uongozi wa Mungu na kutaka kujiongoza wenyewe…Na ni kawaida Mungu anapowaonya watu na wanapokataa maonyo huwa anawaacha na kuwapa haja ya mioyo yao kama wanavyotaka..

Utaona walitaka kula nyama, wakati ambao haukuwa wakati wa kula nyama, lakini kwasababu walililia Mungu aliwapa nyama kama wanavyotaka, kadhalika utaona hata walipoingia nchi ya ahadi walijitakia Mfalme, jambo ambalo halikuwa mapenzi ya Mungu wao wawe na mfalme wa kibinadamu, lakini utaona Mungu aliwapa Mfalme kama walivyotaka.

Na kadhalika wakati wakiwa jangwani, baada ya kupewa zile amri 10 na Mungu..mioyoni mwao walikuwa tayari wameshaanza kuukataa uongozi na wokovu wa Mungu, wakaanza kutamani kupambana wao na maadui zao, jambo ambalo halikuwa ni mapenzi ya Mungu wana wa Israeli washike upanga kuuwa maadui zao, lakini kwasababu tayari mioyo yao ilishakuwa migumu, Bwana akawaacha watumie silaha zao kwa wokovu wao…Lakini hakuwaacha kabisa, akaendelea kuwa nao hata kwa njia hiyo..lakini haikuwa mpango kamili wa Mungu, wokovu upatikane kwa njia ya upanga…Kusudi la Mungu ilikuwa ni kuwapa hiyo nchi ya Ahadi kwa mkono wake mkuu na matendo yake makuu kama alivyofanya kwa wa Misri, kusudi lake lilikuwa ni kuwatoa wakaanani kwa matendo ya kimiujiza pengine kama kwa mapigo yale ya Misri, pasipo hata wana wa Israeli kutumia upanga, Lakini wana wa Israeli waliuharibu mpango kutaka kujipigania..

Kwasababu hiyo basi, Mungu aliruhusu wana wa Israeli, wapange majeshi… WAHESABIWA KULINGANA NA IDADI YAO, wahesabiwe wanaume tu walio na miaka 20 na zaidi, WALIO NA UWEZO WA KWENDA VITANI, waandikwe majina yao na makabila yao, kwasababu ya vita wanavyokwenda kukutana navyo mbeleni. Ndio maana ukisoma pale mwanzo wa kitabu cha HESABU utaona:
Hesabu 1: 1 “Bwana akanena na Musa katika bara ya Sinai, hemani mwa kukutania, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, katika mwaka wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri, akamwambia,
2 Fanyeni HESABU ya mkutano wote wa wana wa Israeli, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina ilivyo, kila mtu mume kichwa kwa kichwa;
3 tangu mwenye miaka ishirini umri wake, na zaidi, WOTE WAWEZAO KUTOKA KWENENDA VITANI KATIKA ISRAELI; wewe na Haruni mtawahesabu kwa kuandama majeshi yao”.
Kwahiyo hiyo ndio sababu ya kuandikwa kitabu cha HESABU, Ni Kitabu cha orodha ya mashujaa watakaosimama vitani kulipigania Taifa la Israeli, na kuliingiza katika nchi ya Ahadi, kuanzia huo wakati Mungu akaanza kuwaokoa na kuwapigania wana wa Israeli kwa kutumia majeshi yao wenyewe, huo ndio ulikuwa mwanzo wa wana wa Israeli kupigana vita…wokovu ukawa unapatikana kwa upanga!..Ndio mashujaa kama wakina Yoshua wakatokea huko, kwa kutiwa nguvu za kiMungu ndani yao kama simba, waliyaangusha mataifa saba makubwa ya Kaanani kwa Upanga…

Kwahiyo kama ukikisoma kitabu hichi vizuri utaona mwanzo wa majeshi ya Israeli kwa Idadi yao na makabila yao, utaona jinsi yalivyojipanga kuizunguka hema, wakati wametulia na wakati wanasafiri..Na pamoja na hayo kitabu hichi pia ni ufupisho wa hatua moja moja waliyopitia wana wa Israeli tangu walipotoka Misri mpaka walipoikaribia Kaanani. Na pia Hesabu hiyo hiyo ya majeshi ya Israeli ndio iliyokuja kutumika katika kuigawa hiyo nchi ya Kaanani waliyokuwa wanaiendea, kwamba Kabila lenye watu wengi ndio waliopewa urithi mkubwa zaidi ya kabila lenye watu wachache.

Bwana akubariki sana…

Tutaendelea na vitabu vinavyofuata, Bwana akitupa Neema kwahiyo usikose mwendelezo huu.

No comments:

Post a Comment