"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, April 26, 2019

KWANINI NABII ISAYA ALIAGIZWA KUHUBIRI UCHI.?

Habari hiyo tunaipata katika kitabu cha Isaya 20: 1-6
 
1 Katika mwaka ule jemadari Yule alipofika Ashdodi,alipotumwa na Sargoni mfalme wa Ashuru;naye alipigana na Ashdodi akautwaa.
2 wakati huo Bwana alinena kwa kinywa cha Isaya,mwana wa Amozi, akisema, Haya, uvue nguo ya magunia viunoni mwako, na viatu vyako miguuni mwako.
3 Naye akafanya hivyo akaenda UCHI, miguu yake haina viatu. Bwana akasema, Kama vile mtumishi wangu Isaya anavyokwenda UCHI, hana viatu, awe ishara na ajabu kwa muda wa miaka mitatu juu ya Misri na juu ya Kushi;
4 vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi waliohamishwa, watoto kwa wazee, hawana viatu, MATAKO YAO WAZI, Misri iaibishwe.
5 Nao watafadhaika, na kuona haya kwa ajili ya Kushi, matumaini yao, na Misri, utukufu wao.
6 Na mwenyeji wa nchi ya pwani atasema katika siku hiyo, Angalia, haya ndiyo yaliyowapata watu wale tuliowatumaini, ambao tuliwakimbilia watuokoe na mfalme wa Ashuru; na sisi je! Twawezaje kupona?”.

Misri wakati huo wa kipindi cha nabii Isaya ilikuwa ni moja ya mataifa matatu makuu yenye nguvu duniani, ikitanguliwa na Ashuru pamoja na Babeli, lakini kutokana na majivuno yake kuzidi na maovu yake kuwa mengi kwa sanamu zake, Mungu alikusudia kuuangamiza, tena sio kwa maangamizi ya kawaida tu bali ya aibu, pamoja na nchi ya kando yake iliyoitwa kushi (ambayo ni nchi ya Ethiopia kwa sasa) lakini kabla ya Mungu kufanya hivyo alimtuma kwanza nabii Isaya awatolee unabii na kuwaonya , ndio hapo tunaona Isaya anaambiwa avue nguo zake na viatu vyake atembee uchi katika hiyo miji awahubirie kuwa wasipotubu, basi mfalme wa Ashuru atakuja kuwafanya hivyo watu wote wa Misri na Kushi, yaani ataipiga miji yao na kisha hataishia hapo tu atawachukua watu mateka wao wakiwa uchi wa mnyama, kutoka Misri mpaka Ashuru.

Tunafahamu kabisa kitendo cha kutembea uchi ni kitendo cha aibu kubwa sana, kwanza utaanzaje anzaje kutembea barabarani uchi,.Nakumbuka wakati Fulani nyuma kabla sijampa Bwana maisha yangu niliota ndoto ambayo siwezi kuisahau nilipoamka nilimshukuru Mungu haikuwa kweli. Niliota nimejikuta ghafla nipo katikati ya mji, nikiwa uchi wa mnyama,sasa kwa kupaniki nikaanza kutafuta nguo au kitu chochote cha kujifunika lakini nilikosa, nikaanza kutumia mikono kujisitiri, huku nikijibanza kwenye vikona kona vya kuta ili watu wasinione, ikawa nikiona watu wamepungua kidogo ninatokea pale na kwenda kukimbilia kujificha sehemu nyingine, mpaka ikafanikiwa kuwa usiku, ndipo nikakimbia moja kwa moja nyumbani, nikapata unafuu kidogo,.

Nikadhani imeishia hapo hakuna mtu aliyejua, lakini baada ya muda kidogo rafiki yangu mmoja wa kike akaja kunifuata, akaniambia mbona tumeona picha zako za uchi zimezagaa mtandaoni kila mahali? Yule ni wewe kweli au ni mwingine?..Niliposikia vile nilitamani nife palepale ili aibu ile inipotee!, maana picha ikishaingia mitandaoni haitakaa ifutike milele, vizazi na vizazi wataona..na hapo hapo likaja neno la kiingereza mbele yangu ambalo nilikuwa sijawahi kulisikia sehemu yoyote likisema “NUDE”. Halafu saa hiyo hiyo nikashutuka usingizini..Nikaenda moja kwa moja kutazama kwenye dictionary ya kingereza lile neno lina maana gani..nikakuta linamaanisha UCHI wa mnyama.. Hapo ndipo nikajua nilikuwa uchi katika roho.

Nimetoa mfano huo kuonyesha ni hali mbaya kiasi gani mtu kujikuta upo uchi halafu isitoshe mbele za watu wengi, Kulikuwa kuna sababu kubwa kabisa Mungu kumruhusu Nabii Isaya atembee vile kwa miaka 3 ili watu wa Misri na Kushi waogope kwa mambo yatakayowakuta miaka michache mbeleni.

Kwahiyo ni kawaida ya Mungu, kuzungumza na mtu au watu wake kupitia ishara fulani, tunamsoma pia Nabii Ezekieli, Bwana Mungu alimwambia ale kinyesi, kuwaonyesha wana wa Israeli kuwa wasipotubu, watapelekwa utumwani na watakula chakula kilichotiwa unajisi kwa kinyesi kwa namna hiyo. Na kwasababu wana wa Israeli hawakutaka kusikia jambo hilo lilikuja kutimia kama lilivyo siku walipokuja kuchukuliwa mateka kupelekwa utumwani.

Vivyo hivyo tunamsoma nabii mwingine, ambaye ndiye NABII MKUU , naye Mungu aliruhusu atoe ujumbe wake katika hali kama hiyo hiyo ya kuwa tupu ili watu wake wajiulize ni nini maana ya mambo hayo, watu waogope, watubu, lakini wasipotaka kutubu hali kama hiyo hiyo itakuta huko mbeleni, na huyu si mwingine zaidi ya BWANA wetu YESU KRISTO. Yeye alitundikwa uchi pale msalabani, mataifa yote yalikuja kuitazama aibu yake, mpaka watu wakasema amelaaniwa huyu..japo kuwa vile hakukuwa kwa ajili yake bali kwa ajili yetu sisi lakini Mungu aliruhusu aenende vile kama ishara ya yatakayowakuta watu wasipotubu huko mbeleni..Wakati ule wanawake walikuwa wanamlilia Bwana, lakini yeye aliwaambia msinililie mimi, hii ni ishara kwa ajili yenu, jililieni ninyi na nafsi zenu, na watoto wenu. (Luka 23:28), Na kwasababu hawakutubu kama Bwana alivyowaonya na kuwaambia ..“ni mara ngapi amejaribu kuwakusanya pamoja kama kuku akusanyavyo vifaranga vyake lakini mlikataa” hivyo nyumba yao imeachiwa hali ya ukiwa…Mnamo mwaka AD 70, Jeshi la kirumi chini ya Jenerali Titus liliizunguka Yerusalemu, na kuliteketeza hekalu na kuwaua watu kwa kuwachicha kama kuku..

Kulingana na mwanahistoria JOSEPHUS, aliyeandika historia nyingi katika usahihi za kuhusiana na matukio ya nyakati za kale za biblia, anaeleza kuwa, wakati Jeshi la Rumi limeuzunguka mji wa Yerusalemu, walikuwa wanakamata wayahudi kila siku na kuwasulibisha uchi kama walivyomsulibisha Bwana Yesu, anasema ilifika mpaka idadi ya watu 500 kwa siku waliokuwa wanasulibiwa nje ya ukuta wa Yerusalemu, na wote walikuwa wanasulibiwa uchi wa mnyama, anasema ilikuwa ni idadi kubwa mpaka kufikia MTI ya kusulibishia watu maeneo yale ikawa inakosekana …Jeshi la Rumi lilifanya vile kuwahimiza Wayahudi (Waisraeli) wasalimu amri, na wanawake na watoto wauawa kikatili sana.

Kwahiyo Bwana kuangikwa msalabani akiwa tupu (licha ya kuwa msalaba unabeba ufunuo mwingi na tofauti tofauti wa kinabii) lakini pia ile ilikuwa ni ishara kwa Wana wa Israeli kwamba wasipotubu mambo hayo hayo na zaidi ya hayo yatawakuta mbeleni…Bwana alifanyika ishara kama Isaya alivyofanyika Ishara.

Kumbuka Pia Bwana wetu huyo huyo alisema maneno haya katika Ufunuo 16:15 (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na KUYATUNZA MAVAZI YAKE, ASIENDE UCHI HATA WATU WAKAIONE AIBU YAKE.)..

Unaona hapo kwa bahati mbaya siku Bwana atakapokuja atakuta kuna watu ambao wapo UCHI rohoni, (YAANI HAWAJASITIRIWA DHAMBI ZAO)..Hao ndio wale siku ile ya hukumu watasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu na ndipo jambo lao moja baada ya lingine liwe la siri lisiwe la siri, lilifanyika gizani, litachambuliwa mbele ya mataifa yote, na mbele ya malaika wote wa Mbinguni..hatua baada ya hatua, tukio baada ya tukio, ulizini kwa siri, ulitazama pornography kwa siri, ulitoa mimba siri, uliua kwa siri, ulitukana kwa siri, ulikula rushwa kwa siri, yote yatawekwa wazi pale, ndipo hapo mtu atakumbana na aibu isiyoelekeza ambayo hajawahi kuiona katika maisha yake yote, na moja kwa moja atatupwa katika lile ziwa la moto..Lakini kwa mtu Yule ambaye sasa maisha yake yamefichwa na Kristo, siku ile vivyo hivyo dhambi zake zitafichwa na hivyo hatapita hukumuni bali atavuka na kwenda moja kwa moja uzimani.
Warumi 4: 6 “Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,
7 Heri waliosamehewa makosa yao, NA WALIOSITIRIWA DHAMBI ZAO.
8 Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi”.
Hilo ndilo vazi ndugu..Hiyo DAMU YA YESU…Lakini kwa bahati mbaya kanisa tunaloishi sisi, ambalo ndio kanisa la mwisho kati ya yale saba, limetabiriwa kuwa kanisa baya kuliko yote, na katikati ya ujumbe wetu tuliopewa, tumeonekana kuwa tu UCHI, tofauti na makanisa mengine ya nyuma yaliyopita..Hiyo ni kuonyesha kuwa tupo katika hali mbaya sana.
Tusome.

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na UCHI.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, NA MAVAZI MEUPE UPATE KUVAA, AIBU YA UCHI WAKO ISIONEKANE, na dawa ya macho ya kujipakamacho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
22Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”.
 
 

Unaona hapo?. Huu ni wakati wa kugeuka na kumaanisha kabisa kumfuata Bwana, tuhakikishe uhusiano wetu na Mungu upo sawa kila siku ili siku ile tuwe na ujasiri wa kusimama mbele zake. Ndugu Kudumu katika dhambi hakuna manufaa yoyote, zaidi ni kila siku kuishi katika maisha ya mashaka na hofu, usiikatae neema ya Kristo maishani mwako hiyo ni kwa faida yako mwenyewe. Tubu sasa umaanishe kumfuata Kristo naye atakupokea, naye atakupa VAZI, lililochovywa katika damu yake liwezalo kusitiri aibu yako yote ya rohoni.Na siku ile hutakuwa uchi mbele zake, bali utaweza kuvuka kutoka mautini kwenda uzimani…

Damu ya Bwana wetu YESU KRISTO itukuzwe milele.Amina
 
Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.

No comments:

Post a Comment