Jina KUU la Bwana wetu YESU KRISTO libarikiwe.
Ndugu mpenzi karibu tujifunze Neno la Mungu na leo tukiwa katika mwendelezo wa kitabu cha Danieli, kama Biblia inavyosema, katika 2 Timotheo 3:16" Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa MAFUNDISHO, na kwa kuwaonya watu makosa yao, NA KWA KUWAONGOZA, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema."
Hivyo kila habari tunayoisoma katika biblia kwa namna moja au nyingine ina mafunzo tosha ya kutufanya sisi tuenende kiukamilifu katika safari yetu hapa duniani pasipo kukwazwa na majaribu ya aina yoyote ya shetani, na ndio maana maandiko yanasema " Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. (1Wakoritho 10:11) ". Kwahiyo mambo yote waliyoyapitia watakatifu wa kale ni kwa ajili ya kutuonyesha sisi njia ya kupita tunapokumbwa na majaribu kama ya kwao.
Katika sura hii ya sita Danieli licha ya kwenda katika ukamilifu wake wote lakini bado tunaona akiingizwa katika majaribu mazito, kama tunavyoweza kusoma habari hii:
Danieli 6:1-18"1 Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote;2 na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara.3 Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote.4 Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.5 Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, TUSIPOIPATA KATIKA MAMBO YA SHERIA YA MUNGU WAKE.6 Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele.7 Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.8 Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.9 Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.10 Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.11 Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.12 Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.13 Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.14 Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa.15 Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme.16 Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.17 Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli.18 Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa.
Kama tukifuatilia habari hii tunaona Danieli alitumika kikamilifu katika kazi zote za uliwali pasipo dosari yoyote, alikuwa mwaminifu, hakuruhusu jambo lolote ovu limkoseshe katika kazi zake za uliwali siku zote za maisha yake, hakuwa anakula rushwa, wala kuwa na matumizi mabaya ya fedha za ufalme katika mamlaka aliyopewa, na ndio maana mfalme ilibidi atafute watu watatu waaminifu ambao wataweza kuzisimamia hizo hazina kubwa za fedha ili mfalme asipate hasara katika mahesabu yake na mmojawao alikuwa ni Danieli.
Lakini haikuwa hivyo kwa wale wakuu wenzake waliokuwa na Danieli, wao walikuwa wanatafuta faida zao wenyewe, mambo kama ufisadi, rushwa, na ubadhilifu wa fedha vilikuwa ni sehemu ya maisha yao, Hivyo mtu kama Danieli alikuwa ni kikwazo kikubwa kwao. Pengine walipojaribu kuhujumu fedha za nchi Danieli aliwakemea na kuwashitaki kuwa wanachokifanya sio sawa, Hivyo ikawapelekea kumchukia Danieli sana na kuanza kumuundia visa, kwasababu nuru na giza haviwezi kuchangamana.
Kumbuka huo ulikuwa ni mpango wa shetani ndani ya watu, alipoona kuwa Danieli ni mkamilifu na hawezi kuuacha ukamilifu wake, akaamua kubadilisha kinyago chake na kuja na mbinu mpya, isipokuwa hii ni katika IMANI YAKE. Na hapo ndipo vita vinapokuwa vikali, pale unapolazimika kuchukua maamuzi ya NDIO AU HAPANA juu ya IMANI yako.
Na ndio maana ukisoma pale kwenye ule mstari wa 5 "Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, TUSIPOIPATA KATIKA MAMBO YA SHERIA YA MUNGU WAKE".
Kwahiyo wale wakuu tunaona waliunda SHERIA moja madhubuti ihusuyo IMANI katika DUNIA YOTE ili tu kumnasa mtu mmoja wapate kumuangamiza. Lakini Danieli alipoona kuwa ile amri imeshapitishwa hakuacha msimamo wake zaidi ya yote alifungua madirisha yake kuelekea YERUSALEMU na kuendelea kusali kutwa mara tatu kama ilivyokuwa desturi yake, alichukua uamuzi wa kukubali kufa kwa ajili ya imani yake, na walipomwona bado anashikilia uamuzi wake wakamtupa katika Tundu la Simba, lakini tunaona Bwana ni mwaminifu alikuja kumwokoa.
Vivyo hivyo mambo hayo waliyoyakuta akina Danieli na sisi pia yatatukuta kwa namna moja au nyingine, Kama hao walikuwa ni watoto wa Mungu waliopendwa wameyapitia hayo vivyo na sisi pia tutayapitia kama hayo. Kumbuka ikiwa wewe ni mkristo na unajiona umesimama katika imani yako, fahamu kuwa shetani anakuchunguza maisha yako kila siku, ni kweli unaweza ukawa hauli rushwa kazini kwako, au haufanyi uasherati, au haunywi pombe, au hauvai mavazi ya kikahaba au hauabudu sanamu au haukosi kwenda ibadani au kusali n.k. Hivyo vyote shetani anaviangalia na atakapokujaribu kwa ushawishi wa muda mrefu ili uache msimamo wako na kuona unazidi tu kuvishinda, atatafuta njia mbadala ambayo moja kwa moja itaathiri UHUSIANO wako wewe na Mungu, aidha ukiache uishi au uendelee nacho uangukie MATATIZO MAKUBWA.
Kwamfano umekuwa mwaminifu kwa bosi wako kazini kwa muda mrefu na anafahamu kuwa wewe ni mkristo, lakini hapa ghafla anakuletea ripoti ya kukulazimisha usaini mapatano ya rushwa, kumbuka yule ni bosi wako na ukimkatalia utafukuzwa kazi,mkumbuke Danieli,
Au wewe wewe desturi yako ni kujisitiri lakini ghafla sheria mpya inakuja ofisini ni lazima kuvaa suruali au vimini, na usipofanya hivyo ni kuhatarisha kazi yako, sasa hilo ni jaribu shetani anakuletea la kutumia nguvu ili umtendee Mungu wako dhambi kwamaana ameona kwa utaratibu huwezi, hivyo anakuja kwa nguvu.
Au pengine kiongozi/mwalimu wako anakulazimisha ufanye naye uasherati usipokubali anakufelisha mitihani, au anakuzushia mabaya yatakayokupelekea hata pengine kufungwa. Katika mazingira kama hayo mkumbuke Yusufu, Kimbia! ni heri upoteze kila kitu kuliko kuipoteza nafsi yako.
Au wewe ni mwombaji mzuri, unasoma Neno, unafunga lakini unashangaa ghafla mzazi anatoa sheria nyumbani hakuna kuomba muda mrefu tena, hakuna kufunga, au hakuna kusoma NENO, unalazimishwa kurudia ibada za sanamu ambazo hapo mwanzo ulishaziacha, na ukijaribu kukataa tu, unatengwa na wazazi au unafukuzwa nyumbani. Usiogope kufukuzwa wala kutengwa hayo ni mapito ya muda tu! Bwana anakuwazia yaliyo mema.
Fahamu tu yatakapokutokea hayo yote usione kama Mungu amekuacha, wewe mkumbuke Danieli, mkumbuke Yusufu, mkumbuke Shedraka, Meshaki na Abednego, mkumbuke na Ayubu, mkumbuke Mordekai, hawa wote baada ya kuonekana wamesimama katika imani yao, shetani aliwaletea SHERIA ZA MASHARTI YA NGUVU. aidha ukubali kuabudu sanamu au ufe, aidha ukubali kuzini au uende gerezani, aidha ukuendelee kumtumikia Mungu wako kwa dua na sala au uishie kwenye matundu ya simba na moto. Lakini kumbuka mwisho wao hawa wote ulikuwa ni wa faraja, badala ya kuangamia kabisa walinyanyuliwa mara dufu. Hivyo usiogope yatakapokupata.
Na mambo hayo hayatamkuta kila mtu isipokuwa ni wale tu watoto wa Mungu waliosimama imara katika Imani ya YESU KRISTO, haya hayana budi kuja na ndio maana Bwana Yesu mwenyewe alisema.
Yohana 16:1-4 ” Maneno hayo nimewaambia, MSIJE MKACHUKIZWA.2 Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.3 Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi.4 Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi.
Unaona hapo, shetani hatoweza kuvumulia kumuona mtoto wa Mungu anadumu katika utakatifu wakati wote hivyo ni lazima ameletee majaribu yatakayohusu imani yake na wakati mwingine Mungu anaruhusu kama vile Ayubu kwasababu biblia inasema. Wafilipi1:29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; “
Na pia inasema kwenye 2 Timotheo 3:12 "Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa."
Kumbuka pia jambo kama hili hili litajitokeza tena wakati wa kipindi cha dhiki kuu pale mpinga-kristo atakaponyanyuka na kuunda SHERIA MOJA YA SHARTI inayohusu IMANI, na shabaha yake itakuwa sio kila mtu aliye duniani bali ni kwa wale waliobaki (wasiokwenda kwenye unyakuo) wakristo vuguvugu wanawali-wapumbavu ambao watajaribu kutoshirikiana naye hao ndio watakaopitia dhiki kuu kwa kuteswa kwa mateso ambayo hayajawahi kuwako tangu ulimwengu kuumbwa. Na sheria itakuwa ni moja tu aidha uisujudie sanamu yake na kupokea chapa yake, ili uendelee kuisha au ukatae kuisujudia na kuteswa na kuuawa kikatili.
Kumbuka lile neno : Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. (1Wakoritho 10:11) ". Mambo ya kale ni kivuli cha mambo yanayokuja.
Hivyo ndugu kuna wakati unakuja mbeleni ulio mgumu sana, wa ulimwengu mzima kujaribiwa na yule mwovu shetani( katika dhiki kuu), Na huu ndio wakati wa kuziweka taa zetu sawa kwa kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu ili Bwana atuepushe na hiyo saa itakapofika (kwa kutunyakua). Kwasababu muda umeisha na wakati wowote Bwana anakuja kulichukua kanisa lake. NI WATAKATIFU TU! NDIO WATAKAOEPUKA HIYO DHIKI KAMA BWANA ALIVYOSEMA..
Ufunuo 3:10-11" Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, UTOKE KATIKA SAA YA KUHARIBIWA ILIYO TAYARI KUUJILIA ULIMWENGU WOTE, KUWAJARIBU WAKAAO JUU YA NCHI. Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako."
Kama bado haujatubu ndugu, ni vema ukafanya hivyo leo angali muda upo.
Ubarikiwe.
Amina Ubarkiwe sana ndugu katka KRISTO YESU.
ReplyDeleteAmen ndugu yangu..
Delete