"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, December 28, 2018

MOYO ULIOELEKEA KWA MUNGU.


2Nyakati 16: 9 “Kwa maana macho ya Bwana hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake”. 

Tukisoma habari za wafalme katika biblia tunakuja kukutana na mfalme mmoja aliyeitwa ASA. Huyu biblia inasema aliiendea njia ya ukamilifu, alifanikiwa kuwaondoa  watu wote waliokuwa mahanithi (Mashoga) katika nchi ya Yuda, akaondoa maashera yote pamoja na sanamu zote zilizokuwa zimewekwa na baba zake kabla yake. Kwa  ujumbla ni mfalme aliyemtumainia sana Mungu kwa kila jambo na hivyo Mungu akamfanikisha sana(1Wafalme 15:9-15). Ilifikia hatua ambayo baada ya kugundua mama yake mzazi amesimamisha sanamu na kuziabudu, alimwondoa katika kiti chake cha umalkia bila kujali kuwa ni mama yake mzazi yupo hapo. Kwani kipindi kile cha wafalme, ilikuwa ni desturi mahali mfalme anapoketi ni lazima na mama yake awekewe kiti cha enzi kidogo pembeni yake.

 Lakini Mfalme Asa mara baada ya kugundua kuwa mama yake Mzazi anaabudu miungu mingine, bila kujali hisia yoyote ya mtu alimwondoa asionekane tena katika jumba la kifalme daima. Jambo ambalo halikuwahi  kufanywa na mfalme yeyote wa Israeli kabla yake… eti! Kumtoa mama yake aliyekuzaa katika cheo cha umalkia kisa tu kaisujudia miungu mingine?, Hakuna mfalme yeyote aliyedhubutu kufanya kitendo hicho cha kishujaa cha kumvunjia mamaye heshima na kumfanya kuwa kama mtu wa kawaida ili tu ailinde heshima ya Mungu wake japo wengi wao walikuwa wanawaona mama zao wakiwakosesha lakini walikaa kimya kulinda heshma za wazazi wao. Lakini kwa mfalme Asa ilikuwa tofauti, leo hii je! na sisi tunaweza kuyaweka mashauri  ya wazazi wetu chini yale yanayopingana na Mungu na kuyaruhusu yale tu ya Mungu yasimame?. Mungu atusaidie katika hilo na sisi.

Mfalme Asa alisimamia kweli hakubakisha sanamu yoyote katika Yuda na Benjamini, aliingia maagano na Mungu kuwa yeye na watu wote wa Yuda watamtafuta Mungu kwa mioyo yao yote, kwa akili zao zote na kwa nguvu zao zote, akapiga mbiu katika nchi yote ya  Yuda kwamba watu wote wamtufute Mungu muumba wa mbingu na nchi. Na wakakubaliana wote kuwa mtu yeyote ambaye hatamtafuta Mungu wa Mbinguni atauawa bila huruma, si mdogo, si mkubwa, si mwanamke, si mwanaume yeyote yule atauawa.. 
  
Hivyo Mungu akapendezwa sana na Mfalme Asa na hivyo akampa Amani na maadui zake wote waliokuwa wanamzunguka kwa muda mrefu tofauti na wafalme wengine waliosalia, na pindi maadui zake walipokuja kupigana naye Mungu aliwapa ushindi mnono, na nyara nyingi hivyo akaongezeka utajiri, na hofu kubwa ikawaangukia maadui zake wote waliokuwa wanamzunguka. Mungu akamjalia kuijenga Yuda kwa maboma, na minara na malango na makomeo makubwa, Na Hivyo mji ukathibitika na kuimarika kwa miaka mingi katika ufalme wake.

Lakini Bwana alimwambia Asa kwa kinywa cha Nabii Odedi ajitie nguvu wala mikono yake isilegee kwasababu kazi yake itakuwa ina malipo baadaye, haitakuwa bure aendelee hivyo hivyo kuulekeza moyo wake kwa Mungu, aondoe machukizo yote katika nyumba yake na katika Israeli aendelee hivyo hivyo kumtumaini Bwana wala asiwayategemee mataifa.  Tunakuja kusoma ni  kweli Mfalme ASA aliendelea kumsimamia Mungu kwa muda mrefu lakini ilifika wakati akapoa kidogo pindi maadui zake walipokuja kutaka kumzuia asitoke ndani ya mji wake, ndipo badala akimbilie kwa Mungu ambaye amekuwa akimtumainia na kumshindania  kwa muda mrefu, Mungu ambaye amekuwa akimpigania vita vikubwa kwa muda mrefu, na kumfanikisha katika mambo yote siku zote za utawala wake, Mungu ambaye amekuwa akimpa amani pande zote, lakini badala yake akakimbilia kwa mfalme wa Shamu ili amsaidie kufanya vita na maadui zake, hivyo akampelekea na zawadi nyingi kutoka katika hazina ya nyumba ya Mungu, na kweli mfalme wa Shamu alimsaidia kupigana na maadui zake, na wale maadui zake wakaacha kuujengwa uzio wa kuwazuia, Hivyo nchi ikastarehe tena kwa muda mfupi.

Lakini jambo hilo halikumpendeza sana Mungu, kwasababu Mungu alimwona  ASA kama ni mtu ambaye moyo wake ulimwelekea sana zaidi ya wengi waliotangulia, ni mtu ambaye Mungu angeweza kuonyesha uweza na nguvu zake zote kwa mataifa mengine kupitia yeye kama vile alivyoonyesha kwa Daudi na Sulemani, lakini sasa amefanya kitendo cha aibu, moyo wake kuwaelekea wanadamu na sio Mungu wake tena, kwenda kuwaomba wafalme wengine wa kipagani wamsaidie kupigana vita. Na ndio hapo tunakuja kusoma Mungu akimtumia nabii wake na kumwambia maneno haya.

2Nyakati 16: 7 “Wakati ule Hanani mwonaji akamwendea Asa mfalme wa Yuda, akamwambia, Kwa kuwa umemtegemea mfalme wa Shamu, wala hukumtegemea Bwana, Mungu wako, kwa hiyo limeokoka jeshi la mfalme wa Shamu mkononi mwako.
8 Je! Hao Wakushi na Walubi hawakuwa jeshi kubwa mno, wenye magari na wapanda farasi wengi sana? LAKINI, KWA KUWA ULIMTEGEMEA BWANA, ALIWATIA MKONONI MWAKO.
9 KWA MAANA MACHO YA BWANA HUKIMBIA-KIMBIA DUNIANI MWOTE, ILI AJIONYESHE MWENYE NGUVU KWA AJILI YA HAO, WALIOKAMILIKA MOYO KUELEKEA KWAKE. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita”.

Angalia hapo maneno hayo yalimjia mfalme Asa, hakujua kuwa macho ya Mungu yalishazunguka duniani kote kutafuta mtu aliyekamilika moyo ulioelekea kwake, ili Mungu ajionyeshe kuwa mwenye nguvu kwake, na akamwona ASA peke yake, lakini yeye hakulijua hilo, alidhani Mungu hakuwa anauthamini uthabiti wa moyo wake, alidhani Mungu hakumaanisha kumwambia yale maneno kuwa taabu yake kwake itakuwa na malipo (2Nyakati 15:7), yeye alichukulia juu juu tu, mpaka hapo alipoutoa moyo wake kwa Bwana na kuulekeza kwa wanadamu. Ndipo Mungu alipokasirika na kumwambia umefanya upumbavu…Mungu hapendi upumbavu kwa watu wanaomtumainia. Lakini pamoja na hayo yote Mfalme Asa alifanya mema machoni pa Mungu mpaka siku ya kufa kwake, na Bwana hakumwacha kabisa.

Leo hii ndugu yangu biblia inatufundisha na sisi tuwe ni mioyo iliyomwelekea Mungu. Kwasababu macho ya Mungu yanakimbia-kimbia duniani kote,  ikiwa na maana Mungu anaangalia anarudi tena anaangalia, anarudi tena anaangalia aone mtu atakayekuwa na moyo mkamilifu utakaomwelekea yeye kwa kila kitu ili azionyeshe nguvu zake. Kama ilivyokuwa kwa mfalme Asa. Tuweke tegemeo letu lote kwa Mungu, tumtwike yeye fadhaa zetu zote, tusiwe wepesi kuwakimbilia wanadamu, bali mioyo yetu siku zote tuielekeze kwa Mungu muumba wa mbingu na nchi, kwasababu yeye anawaangalia watu kama hao waliokamilika mioyo aonyeshe nguvu zake zote. Tuvumilie na kumtegemea Mungu hatari inapojitokeza mbele yetu..Tusiwapendelee wanadamu hata kama ni ndugu zetu, bali sisi tuangalie tu kile Mungu anachosema basi, tusifanye ibada za sanamu, ambazo biblia inazitaja kama uasherati, na tama mbaya, bali tuvivunje vunje vikae mbali nasi, ndipo hapo Mungu atakapotuona na kazi yetu ikawa na faida kubwa. Na Mungu atatuimarisha.

Ikiwa haujampa Bwana maisha yako, mlango wa neema bado upo kwa ajili yako, damu ya thamani ya Yesu Kristo bado inafanya kazi hata sasa hivi, imebaki kipindi kifupi sana isimame kufanya kazi yake. Usisubiri kipindi Fulani kifike , hicho hakitafika ndugu yangu, hiyo ni injili ya shetani anayokuhubiria moyoni mwako.. muda wa wokovu ni sasa biblia inasema hivyo. Chukua uamuzi sasa wa kuyakabidhi maisha yako kwa Bwana Yesu kikamilifu, na utakapofanya hivyo kwa kudhamiria kabisa kutoka ndani ya moyo wako, kutubu kwa kuacha dhambi na maisha yako ya kale, basi yeye mwenye atakupa uwezo wa kuzishinda dhambi. Na haraka mara baada ya kuamini kwako unapaswa ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwa jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako. Kisha Roho wa Mungu ataachiliwa juu yako kukulinda na kukuongoza katika kweli yote. Na baada ya hapo utakavyozidi kuuelekeza moyo wako kwa Mungu na kumtegemea yeye siku zote ndivyo utakavyouona mkono wake katika maisha yako, Na Mungu atakutumia wewe kuonyesha nguvu zake kwa wengine.

Ni matumaini yangu utafanya hivyo. Na Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment