"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, September 11, 2017

UWEZA WA MUNGU UNAONEKANA WAPI?



Neno la Mungu linasema pale tulipo dhaifu ndipo tulipo na nguvu, ikiwa na maana pale tunapokuwa si kitu ndipo tunapoonekana kuwa kitu mbele za Mungu, Bwana Yesu alisema yeye ajishushaye atakwezwa na ajikwezaye atashushwa, pale tunapokataa akili zetu kututawala na kumwachia Mungu azitawale ndipo tutakapofungua mlango na wigo mpana wa kuuona UWEZA wa Mungu zaidi katika maisha yetu.

Na ndio maana mtume Paulo alisema 2wakoritho 12:9-10" Naye akaniambia neema yangu yakutosha; maana UWEZA WANGU HUTIMILIKA KATIKA UDHAIFU. Basi najisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili UWEZA WA KRISTO ukae juu yangu.Kwahiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida kwa ajili ya Kristo. MAANA NIWAPO DHAIFU NDIPO NILIPO NA NGUVU."
 
 

Mungu hawezi akawa ni mponyaji kwetu kama hatujawa na madhaifu (mwenye afya haitaji tabibu),mafarisayo na masadukayo YESU alikuwa hana maana kwao kwasababu wao walijiona kuwa wana afya hivyo hawakufaidiwa chochote na uweza wa Mungu katika Yesu Kristo. Kwa kawaida huwa tunashukuru pale tunapotendewa mahitaji yetu, huwezi ukashukuru au ukaomba kama unayo mahitaji yako yote. Na pia hauwezi kutegemea kama unao uwezo wa kujitegemea. vivyo hivyo na kwa Mungu wetu ili tuweze kuuona UWEZA WAKE, yatupasa tuwe dhaifu mbele zake kwa namna zote, kiasi cha kwamba tujione pasipo yeye sisi hatuwezi lolote. Kwa jinsi tutakavyojiachia kwake kwa kila kitu ndipo tutakapofungua wigo wa yeye kutuhudumia sisi na kuuona uweza wake,

Watoto wa Mungu wamefananishwa na kondoo na sio mbuzi kwasababu kondoo hawezi akajiongoza mwenyewe huwa anamtegemea mchungaji wake kwa kila kitu tofauti na mbuzi wao wana uwezo wa kwenda kujichunga wenyewe hivyo hawahitaji msaada mkubwa sana kutoka kwa mchungaji. Vivyo hivyo Na mtoto mdogo anahudumiwa kwa kila kitu na wazazi wake ikiwemo malazi, chakula, afya, n.k. kwasababu anaonekana dhaifu kwa wazazi wake pasipo wao hawezi kufanya lolote hivyo uweza mkubwa wa wazazi wake unaonekana juu yake, kwa jinsi hiyo hiyo na sisi pia tunapaswa tuwe hivyo kwa Baba yetu wa mbinguni, sisi ni watoto kwake tunapaswa tujinyenyekeze kama vitoto vichanga ili tuone uweza wake katika maisha yetu, kumbuka yule mtoto anapojifanya amekua na kutaka kujiamulia mambo yake mwenyewe ndipo kidogo kidogo anapojiachilia kutoka katika mikono ya wazazi wake na uweza wao unavyozidi kupungua juu yake, mpaka inafikia wakati mzazi hana sehemu yoyote kwa mtoto.

Biblia inasema "Mkaribieni Mungu naye atawakaribia"(Yakobo 4:8). hii ikiwa na maana kwa kiwango kile kile tutakachompa Mungu katika maisha yetu, ndicho atakachokitumia kufanya kazi katika maisha yetu. Kama unampa Mungu Jumapili kwa jumapili na yeye atajifunua kwako hiyo hiyo jumapili kwa jumapili, kama ni mwezi kwa mwezi na ndivyo hivyo atakavyojifunua kwako mwezi kwa mwezi, lakini kama ni siku kwa siku ndivyo utakavyomwona siku kwa siku, kwa kiwango kile kile utakachopima ndicho utakachopimiwa biblia imesema.

Kama umempa Mungu asilimia 20 ya maisha yako ayatawale ataonekana kwako katika hiyo asilimia 20 usitegemee zaidi ya hapo, kama umempa 70% ataonekana katika hiyo 70, kama umempa 100% ataonekana katika hiyo 100% kama Bwana YESU alivyompa Baba yake. Maana uweza wa Mungu unatimilika katika udhaifu na udhaifu huu ni pale unapokataa kuzitegemea akili zako na kuwa kama mtoto mchanga mbele zake.
 
Ushuhuda:

Nakumbuka kuna wakati tulikuwa tumepanga chumba sehemu fulani na kila mwisho wa mwezi tulikuwa na desturi ya kulipia bill ya umeme lakini ilifika wakati fulani hatukupata pesa ya kulipia na hatukuwa na chochote mfukoni lakini tulimwamini Mungu na kumwachia yote, tukasema kama Mungu wetu yupo atatupigania, maana hao wadai pesa za umeme ni watu wakorofi ukipitisha tu siku moja haujalipia ni balaa umelianzisha, lakini ulipofika mwisho wa mwezi hatukuwa na chochote mfukoni, cha ajabu wale wadai-umeme hawakuja siku hiyo kudai pesa ya umeme na sio desturi yao, vyumba vingine vyote walienda kulipa kilikuwa kimebaki chumba chetu tu! lakini ni kama walipigwa upofu hivi hawakuja, ukaingia mwezi mwingine, tarehe 1,2,3......mpaka tarehe 24 tulikuwa bado hatujalipa deni la mwezi uliopita na kweli hela hatukuwa nayo na umeme tunaendelea kutumia lakini tulimwachia Mungu yote tulisema liwalo na liwe hatutamkopa mtu,

nakumbuka siku hiyo hiyo gesi ya kupikia iliisha kwahiyo matatizo yakaongezeka, lakini ilipofika tarehe 25 mida ya jioni huku tukiwa na mawazo tulifungua simu tukakuta sh.48,000 kwenye mpesa hatukujua imetoka wapi, haijatumwa na mtu yoyote, wala hakuna jina wala message ya kuonyesha mtu katuma pesa, ni kama vile iliongezeka katika account ya m-pesa. tukaenda kuitoa jioni ile ile cha ajabu saa hiyo hiyo baada ya kuitoa hiyo pesa wale wadai-umeme wakafika na ghadhabu wanataka pesa yao ya umeme ya mwezi uliopita, tukawapa saa ile ile, sh.15,000 kiasi kilichobaki tulinunua gesi na matumizi mengine. Hivyo ndivyo Bwana alivyotuokoa na aibu. na sio hili tu Bwana amekuwa
akituonekania kwa namna hii mara nyingi tu na kwa njia nyingi

.
Lakini tungesema tujiongeze tukakope pesa hakika uweza wa Mungu tusingeuona maana yeye anasema zaburi 46:1" Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, MSAADA UTAKAOONEKANA TELE WAKATI WA MATESO." pale tutapokuwa dhaifu na kumwachia yeye ndipo tutakapouona uweza wa Mungu, wana waisraeli wasiongeweza kuona bahari inagawanyika kama wasingekutana na kizuizi cha bahari, wasingekula mana kama wasingepita jangwani, wasingepasuliwa maji miambani kama wasingekuwa na kiu, Hivyo pale unapomkabidhi Mungu mambo yote atawale katika misukosuko pasipo kutafuta njia mbadala ya akili zako, ndipo uweza wa Mungu utakapoonekana.

Vivyo hivyo unapopitia shida fulani, au unapoumwa, au tatizo fulani haraka haraka usikimbilie kutafuta njia mbadala, usianze kutangatanga jua hiyo ndio fursa ya wewe kuuona uweza wa Mungu na ndio yeye anataka iwe hivyo, ndio ni vizuri kwenda hospitali na sio dhambi kwenda hospitali lakini sio kila ugonjwa kukimbilia hospitali ukifanya hivyo uweza wa Mungu utauonaje?, naweza nikakupa mfano ulifikia wakati nilikuwa nikipata ugonjwa kidogo nakimbilia dawa lakini ilifika wakati nikasema nataka nimuone Mungu katika maisha yangu, yeye aniponye pasipo kumtegemea mwanadamu wala dawa, nikasema sitameza kidonge cha aina yoyote wala kwenda hospitali, tangu niseme hivyo hadi sasa ni miaka mitatu sijawahi kumeza kidonge wala kwenda hospitali, kila ninaposikia hali ya udhaifu ndani yangu, nasema Bwana ndiye daktari wangu ataniponya na kweli ile hali haidumu baada ya muda mfupi narudia hali yangu ya kawaida, kwa kufanya hivyo uweza wa Mungu nauona ndani ya maisha yangu kila siku.

Na kwako wewe ndugu unaweza ukasema mbona sijawahi kumwona Mungu akinifanyia miujiza katika maisha yangu? ni kwasababu wewe mwenyewe hujaruhusu atende kazi ndani yako. haujataka kuwa dhaifu mbele zake kwa kujishusha kuwa kama mtoto,.jambo fulani limetokea chukua iwe ndio fursa ya wewe kumwona Mungu wako usitegemee akili zako, wala mwanadamu wala kitu chochote,mwachie yeye na utauona utukufu wake kila siku.

Hiyo ndio njia pekee itakayokufanya uone UWEZA WA MUNGU maishani mwako na ndio njia Paulo aliyoinena na kuiishi iliyomfanya amwone Mungu siku baada ya siku katika huduma yake. kwa mfano shedraki, Meshaki na Abednego walipohukumiwa kutupwa katika tanuru la moto hawakusita walimwachia Mungu yote na kwa kufanya hivyo waliweza kukutana na Mungu kule na kupelekea Mungu wao kutukuzwa babeli yote, vivyo hivyo na Danieli pia alipotupwa katika tundu la simba aliuona uweza wa Mungu kule, tukiwaangalia pia akina Paulo na Sila walipotupwa gerezani ndipo walipouona uweza wa Mungu pale malaika wa Mungu alipoitetemesha ardhi na kufungua malango ya gereza. Hawa wote ni kwasababu walikubali kuwa wadhaifu kwa ajili ya Bwana hivyo ikawafanya wauone utukufu mkubwa wa Mungu.

Mithali 3:5-6 " Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zake mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye naye atanyosha mapito yako."

Amen!

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 18



SWALI;-Mwanzo 1:26 ""Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi."" Hapa Mungu alikuwa anaongea na nani?

JIBU: Mara nyingi Mungu alikuwa anatumia neno "sisi" kama wingi kuashiria hakufanya mambo yote peke yake, bali alikuwa na wengine aliowashirikisha mawazo yake, Kumbuka kuumba aliumba yeye peke yake lakini mawazo yake ya kufanya baadhi ya mambo aliwashirikisha wengine, hivyo hapo aliposema na tumfanye mtu kwa mfano wetu alikuwa anaongea na malaika zake, na hakuwa anazungumza na nafsi ya tatu katika uungu wake, Mungu ni mmoja tu na hana nafsi tatu, neno "TUMFANYE" halimaanishi ni watatu tu! bali linaweza likamaanisha wawili, watano, mia au milioni n.k. Hivyo mtazamo wa kusema Mungu ana nafsi tatu kwa kuusimamia mstari huu sio kweli, pale Bwana alikuwa anazungumza na malaika zake ambao walikuwa wameshaumbwa kabla yetu sisi,

Tunaona pia jambo hili linajirudia sehemu nyingine nyingi katika biblia Bwana akizungumza na malaika zake, soma mwanzo 3:22"Bwana Mungu akasema basi huyu mtu amekuwa kama MMOJA WETU, kwa kujua mema na mabaya"..., pia mwanzo 11:6-8"Bwana akasema tazama watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja, na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya na TUSHUKE HUKO, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao." .. sehemu zote hizi mbili Bwana alionekana akijadiliana na malaika zake. Mungu huwa anatenda kazi na malaika zake.

Tukisoma pia Isaya 6:8 Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, nimtume nani? naye ni nani atakayekwenda KWA AJILI YETU? Ndipo niliposema mimi hapa nitume mimi. Naye akaniambia enenda ukawaambie watu hawa fulizeni kusikia lakini msifahamu; fulizeni kutazama lakini msione..." Unaona hapo Bwana alimuuliza nabii Isaya ni nani atakayekwenda kwa ajili ya Mungu na jeshi lake la mbinguni?.

Kwahiyo Mungu kujadiliana na malaika zake sio jambo jipya tunaweza tukaliona pia kwenye ile habari ya mfalme Ahabu na nabii Mikaya ukisoma "2 nyakati 18:15-22" .Kwahiyo pale Mungu alikuwa hazungumzi na YESU wala Roho Mtakatifu bali na malaika zake waliokuwepo kabla yetu sisi.

SWALI 2: Nataka kuuliza je! sadaka ya Habili ilikataliwa kwasababu ipi?

JIBU : Ukisoma mwanzo 4:3-4 sababu kuu iliyomfanya Kaini sadaka yake ikataliwe ni kwasababu hakujua malengo na sababu ya kuitoa hiyo sadaka (kukosa ufunuo)..mwenzake Habili alipata ufunuo wa yeye kwanini atoe mnyama na wala si kinginecho kwani alifahamu baada ya wazazi wao kula tunda na kujiona kuwa uchi kwa aibu walienda kutafuta majani kama njia ya kujisitiri, lakini Mungu aliona hawajasitirika bado hivyo aliamua kuwachinjia wanyama na kuwavisha ngozi zao ndipo walau walipata tena kibali cha kuzungumza na Mungu..

Hii ndio sababu Habili hakwenda tena na sadaka ya majani ili amkaribie Mungu bali alienda na sadaka ya wanyama ndipo Mungu akamtakabari, lakini ndugu yake aliona ni vema kutumia njia ile ile ya kwanza ya kutumia mazao ya ardhi ndipo Mungu akaikataa sadaka yake.

pamoja na hayo Mungu alimshauri afanye kama ndugu yake Habili lakini hakukubali. Ni vema tufahamu kuwa Mungu ana njia yake aliyoichagua yeye ya kumkaribia, Leo hii sadaka inayokubalika mbele za Mungu ni yule mwanakondoo aliyechinjwa kabla kuwekwa misingi ya ulimwengu(Yesu Kristo) hakuna sadaka nyingine inayokubalika mbele za Mungu zaidi ya hiyo kwasababu biblia inasema YESU ndiye njia, na kweli na uzima mtu hafiki kwa Baba ila kwa njia ya yeye, Hivyo usijidanganye kwamba unatoa sadaka sana, au unatenda matendo mema, au unasaidia yatima, au sio mlevi, n.k. na huku haujaoshwa dhambi zako kwa damu ya YESU Kristo hautakuwa na tofauti na Kaini unamtolea Mungu dhabihu ya mazao badala ya mwanakondoo, kumbuka hata wasio wakristo dini nyingine kama waislamu, wahindu,n.k. wanafundishwa kutenda matendo mema, wanatoa sadaka, wanasaidia maskini, sio walevi, sio waasherati, lakini Mungu hawatambui hao kwasababu hawapo chini ya damu ya mwanakondoo YESU KRISTO.

Hivyo mpe Kristo maisha yako ili dhambi zako zisafishwe kwa kubatizwa kwa jina la YESU KRISTO uwe na uhakika na wokovu wako.
 Amen!