"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, May 29, 2019

UTAWALA WA MIAKA 1000.

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze maandiko matakatifu, kama Biblia inavyosema katika Zaburi 119:105 “ Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”..Ikiwa na maana Neno la Mungu ni mwongozo wetu, tukilijua Neno la Mungu hata tukikosa vitu vingine vyote bado tutaishi.Amen.

Leo tutajifunza juu ya utawala wa miaka 1000. Swali utawala wa miaka 1000 ni nini?...Utawala wa miaka 1000 ni utawala ambao utakuja kuanza hapa duniani, ambapo Bwana wetu Yesu Kristo atatawala na wateule wake katika hii dunia..Maandiko yanasema mbinguni hatutakaa milele, tutakaa kule kwa kipindi cha Miaka 7 tu na baada ya hapo tutarudi hapa duniani kutawala kwa muda wa miaka 1000, na baada ya hiyo miaka 1000 kuisha, ndipo kitu kinachoitwa MUDA kitasimama, na umilele utaaanza.

Hatua kanisa inayosubiria sasa, ni unyakuo, ambao upo karibuni sana kutokea, watakatifu waliokufa katika Bwana watafufuliwa, wataungana na watakatifu walio hai na kwa pamoja tutakwenda kumlaki Bwana wetu mawinguni. Huko mbinguni mambo yatakayokuwa yanaendelea huko ndio kile (jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia), ni mambo mazuri na mapya..Biblia inapafananisha na mahali pa karamu. Ni kama mahali pa mwaliko, kama ulishawahi kualikwa kwenye sherehe labda harusi unaweza ukaelewa kwa sehemu furaha iliyopo kwenye harusi.

Sasa Wakati karamu ya mwanakondoo inaendelea mbinguni, huku chini duniani Mpinga-Kristo atanyanyuka kuanza kufanya kazi zake, atafanya kazi kwa muda wa miaka 7, ambapo miaka mitatu na nusu ya kwanza ataudanganya ulimwengu mzima kupokea chapa ya mnyama kwa injili yake ya uongo ya amani.

Kwa kivuli cha kuleta amani atafanikiwa kuwadanganya wengi wapokee chapa ya mnyama..na baada ya hiyo miaka mitatu na nusu ya kwanza kuisha itaanza miaka mingine mitatu na nusu, ambayo hiyo itakuwa ni dhiki kwa wale waliokataa kuipokea hiyo chapa yake…Na mwishoni kabisa mwa hiyo miaka mitatu na nusu kuna siku kadhaa zitaongezeka pale, kama siku 75 hivi (Daniel 12:12) ambazo hizo zitahusiana na kumwagwa kwa ghadhabu ya Mungu juu ya nchi kwa wale wote walioipokea ile chapa ya mnyama.(kumbuka hii ghadhabu ya Mungu inahusiana na vile vitasa saba, ufunuo 16, kama utakuwa hujajua vitasa 7 ni nini unaweza ukanitext inbox nikutumie somo juu ya hilo). Na ndani ya hizo hizo siku ndio vita ya Harmagedoni itakapopiganwa.

Hivyo Baada ya hukumu ya Mungu kupita juu ya nchi, na vita vya Harmagedon kupita, duniani watu wengi watakufa sana..biblia inasema watu wataadimika kuliko dhahabu (Isaya 13:12)…kama ilivyoshida kuziona au kuzipata dhahabu ndio siku hiyo itakavyokuwa shida kumwona mwanadamu mmoja chini ya jua…labda siku hiyo mji wa Dar es salaam itabakiwa na watu watano tu! Pamoja na idadi yake ya watu kuwa mamilioni..watu wengi sana watakufa walioipokea ile chapa ya mnyama, na baada ya kufa biblia inasema sehemu yao itakuwa ni katika lile ziwa liwakalo moto (Ufunuo 14:9-10).Hivyo watakaa huko kuzimu pamoja na watu wengine waovu wakisubiria ufufuo wa wafu ambao utakuja mara baada ya ule utawala wa miaka 1000 kuisha, wote wahukumiwe kisha watupwe kwenye lile ziwa la moto.

Sasa utendaji kazi wa Mungu upo hivi, huwa haaribu na kuleta kitu kipya, hapana! Bali huwa anakiponya kile kitu na kisha kukifanya kuwa kipya zaidi…hiyo ndio njia ya Mungu ya kufanya mambo yote kuwa mapya….kwamfano Mtu anapoumwa ili Mungu amrudishe katika hali yake hamwui Yule mtu na kumtengeneza upya..hapana, anachofanya ni kukirejesha kile kitu kama kilivyokuwa hapo kwanza, ndio hapo utaona mtu alikuwa anauvimbe ghafla unapotea, alikuwa ana ugonjwa ghafla anapona n.k..Hata sisi tutakaponyakuliwa hatutauliwa roho zetu na miili yetu na kuumbwa upya hapana! Tutakuwa ni sisi sisi, isipokuwa tutavikwa miili mingine ya utukufu, ile ya kwanza haitauliwa hapana, bali tutavikwa juu mipya juu yake hii, Ndio maana siku ile ya unyakuo wafu watafufuliwa kwanza warudi katika hali zao walizokuwa nazo wakiwa hai.Kisha miili yao ikutane na ile miili ya mbinguni wafanywe kuwa bora zaidi..siku hiyo ndiyo utajua lile neno Bwana alilolisema kuwa hautapotea unywele hata mmoja wa vichwa vyenu, litatumika wapi..(Luka 21:18)

Kadhalika na dunia tunayoishi sasa imeharibiwa sana na shetani na wanadamu…Lakini Mungu hana desturi ya kufuta na kuumba upya, bali anadesturi ya kuponya…yaani kile kile kitu anakirudisha katika hali yake ya kwanza,
sasa kutokana na anguko la mwanadamu, ardhi ililaaniwa, Hivyo aliweka njia ya kuiponya hii dunia na kuirudisha katika hali yake kama ilivyokuwa pale Edeni, ulikuwa ni mpango wa Mungu tangu zamani, kama ilivyokuwa mpango wa Mungu kumrudisha mwanadamu awe karibu na yeye tena.

Kwahiyo kitendo cha kuisafisha dunia, ni kuirudisha dunia katika hali yake ya kwanza,

Ni baada ya vile vitasa vitano vya kwanza vya ghadhabu ya Mungu kumiminwa juu ya wale wanadamu waliobaki duniani walioipokea ile chapa ya mnyama,..na kile kitasa cha sita ndio kinahusu vita vya Harmagedoni (ufunuo 16:12-16) ambayo itapiganwa katika Taifa la Israeli mahali panapojulikana kama Megido..Wakati huo Mataifa yote ulimwenguni yakiongozwa na mataifa kutoka maawio ya jua yaani China, korea, Japani na mengineyo yatakusanyika kwenda kufanya vita na taifa la Israeli, akilini mwao wakidhani wanapambana na Israeli kumbe wanapambana na Bwana Yesu Kristo mwenyewe pamoja na watakatifu wake ambao watakuwepo kwa mfumo wa kimalaika wakati huo…lakini Baada ya muda mfupi sana vita vitakwisha kwasababu Yesu Kristo sio mwanadamu…atawaua wote mara moja kwa Neno lake, na damu nyingi sana zitachurizika kama mto maeneo yale…watashangaa tu kuona maiti zilizochinjika chinjika zimelala chini, na aliyewaua haonekani…

kama ilivyokuwa katika kipindi cha mfalme wa Ashuru katika (2Wafalme 19:35), ambapo alimtukana Mungu wa Israeli, na malaika wa Bwana akashuka kwenye kambi ya jeshi lake, akaua wanajeshi wote ambao idadi yao ilikuwa ni watu laki moja na elfu themanini, walipoamka asubuhi walikuta maiti tu! Na aliyewaua hajulikani..Ndivyo itakavyokuwa katika vita vya Harmagedon, biblia inataja majeshi ya wapanda farasi watakaoanguka siku hiyo watakuwa ni elfu ishirini mara elfu kumi hiyo ni sawa na watu milioni 200, watakutwa wamechinjika vibaya sana na damu yao nyingi…Ndipo ndege wote wanaokula mizoga watakusanyika kuja kula nyama zao.
Ufunuo 19: 11 “Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.
12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.
13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.
15 Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.
16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA Bwana WA MABwana.
17 Kisha nikaona malaika mmoja amesimama katika jua; akalia kwa sauti kuu, akiwaambia ndege wote warukao katikati ya mbingu, Njoni mkutane kwa karamu ya Mungu iliyo kuu;
18 mpate kula nyama ya wafalme, na nyama ya majemadari, na nyama ya watu hodari, na nyama ya farasi na ya watu wawapandao, na nyama ya watu wote, waungwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa.
19 Kisha nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake”…………….. 
19.21 na wale waliosalia waliuawa kwa upanga wake yeye aliyeketi juu ya yule farasi, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.
Sasa baada ya maangamizi hayo ya mwisho ya duniani kuisha, yatakayofanywa na Bwana mwenyewe , hapo ndipo ishara yake itaonekana mbinguni, jua litazima ghafla, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, nyota zitajificha, kutakuwa na tetemeko kubwa la ardhi, ambalo halijawahi kutokea tangu dunia kuumbwa..siku zote Huwa Bwana Anapojidhihirisha hahitaji mwanga, kwasababu yeye mwenyewe ni NURU kila kitu kitatii chini yake… dunia itakuwa giza tororo na kutoka mawinguni Bwana ataonekana pamoja na kundi kubwa la watu walionyakuliwa waking’aa kama jua…Hapo ndio kila jicho litamwona.(yaani hao watu wachache waliobahatika kusalimika duniani watamwona LIVE akishuka mawinguni), …Litakuwa ni jeshi kubwa, ambalo litatoka mbinguni wakiwa na mavazi meupe na wamepanda farasi..
Bwana atashuka hapa duniani na kuanza kuitengeneza tena upya…Majangwa yatabadilika na kuwa bustani nzuri zenye misitu yenye kuvutia, ardhi haitazaa michongoma tena, jua halitakuwa kali tena, nchi itazaa yenyewe kama hapo mwanzo, maji ya bahari yatapungua na sehemu ya nchi kavu itaongezeka, na maji hayatakuwa na chumvi tena, hakutakuwa na matetemeko wala vimbunga, wala tatizo la maji, nchi itatoa chemchemi nyingi sana...chakula kitakuwa tele…

Kwasababu kwa vile vitasa saba, ghadhabu ya Mungu imetimilika (Ufu.15:1)..hakutakuwa tena na ghadhabu au hasira ya Mungu juu ya dunia baada ya kitasa cha saba…hivyo wale wachache waliosalimika wasiokufa katika yale mapigo, watapata nafasi ya kuingia katika huo utawala wa miaka 1000, wakiwa na miili yao ya asili, yenye kusikia njaa, yenye tamaa ya mwili nk. Wakati huo Shetani atafungwa asiwadanganye tena kwa muda wa miaka 1000, watu hawa watakuwa watu wazuri kwa kitambo kwasababu shetani amefungiwa (Ufu.20:1-3)…Na kwasababu utawala wa amani unaanza wataishi kwa amani, na watazaliana na kuwa na watoto katika Edeni ya Bwana. Na wataongezeka na kuwa wengi mpaka kuijaza dunia.

Na laana Bwana aliyoipiga nayo dunia itafutika…
 
1) Laana ya kuzaa kwa uchungu.(wanawake hawatazaa kwa uchungu tena).wala wanyama

2) Laana ya kula kwa jasho…(Nchi itazaa yenyewe), hawa watoto waliozaliwa ndani ya huo utawala hawatalima kwa uchungu wala kwa ugumu kama sasa…

3) Uadui kati ya watu na wanyama utaondolewa na Bwana..Biblia inasema katika utawala wa miaka 1000, simba hatakula nyama tena, atakula majani, wala wanyama hawatakulana, na mtoto atacheza na nyoka na wala hawatadhuriana n.k kama ilivyokuwa Edeni.
Isaya 11: 6 “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.
7 Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe.
8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.
9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari”.
Isaya 65:25 “Pia inatabiri jambo hilo hilo “ 25 Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng'ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema Bwana.”

Sasa hawa watoto watakaozaliwa katika utawala huo wa miaka 1000, biblia ndio inasema tutakaowatawala….hao ndio watakaoitwa mataifa wakati huo… Sisi tuliorudi na Bwana kutoka mawinguni tutakuwa wafalme juu yao, na Yesu Kristo atakuwa Mfalme wa Wafalme. Sisi hatutakuwa na miili kama ya kwao ya asili, kwasababu sisi tumeshavuka huko, na kupewa miili ya utukufu..miili ambayo ipo kama ya malaika, isiyozeeka, isiyo na tamaa,isiyosikia njaa, isiyochoka, kwetu sisi kutakuwa hakuna kuoa wala kuolewa wala kuzaliana, tutakuwa kama malaika katika hii dunia...utukufu wetu utakuwa mbali sana na hawa watu watakaozaliwa katika utawala huo..

Hapo ndipo litatimia lile neno katika Luka 19:16 “Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.
17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya MIJI KUMI.
18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.
19 Akamwambia huyu naye, WEWE UWE JUU YA MIJI MITANO”.
Wale waliokuwa waaminifu kwa Bwana watapewa miji mingi zaidi ya kutawala zaidi ya wale wengine waliokuwa wavivu katika masuala ya Kimungu n.k

Mathayo 19: 27Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli”.

Ulimwengu mpya unaozungumziwa hapo ndio huo utawala wa miaka 1000.

Katika utawala huo, Dunia itakuwa na lugha moja na usemi mmoja…Bwana ataiondoa ile laana aliyowalaani wanadamu pale Babeli, ya kuchafuliwa lugha na usemi ambayo mpaka sasa inaendelea kufanya kazi….ndio maana utaona kama kuna nguvu Fulani inayotusogeza mbali sisi kwa sisi tusifanane kiusemi na kitabia inayotokana na lugha…kwamfano utaona hii hii lugha ya Kiswahili tunayozungumza ukienda Kenya ina lafudhi tofauti na Tanzania, vivyo hivyo watu wanaotoka kanda za kaskazini, wanaongea kwa lafudhi tofauti na watu wa kanda ya ziwa na pwani ni tofauti…sasa hii nguvu inayobadilisha lafudhi unaposogea umbali kidogo na jamii ya watu wako ndio hiyo hiyo iliyotokea pale babeli…isipokuwa pale babeli haikuishia kubadilisha lafudhi tu, bali hata maneno kabisa…na kadhalika siku zinavyozidi kwenda lugha moja inavunjika na kuzaa nyingine hivyo hivyo, na itaendelea hivyo mpaka mwisho wa dunia...ndio maana utaona lugha zote za kibantu zinafanana..kuonesha kuwa kwa namna moja au nyingine zilitoka kwenye lugha moja isipokuwa kuna nguvu Fulani iliivunja na inaendelea kuivunja vunja kwa jinsi muda unavyozidi kwenda.

Sasa Mungu aliiachilia hiyo nguvu ya machafuko makusudi kabisa..ili watu wasikae pamoja wakakusudia kutengeneza miungu ya kuiabudu..kama pale babeli. Mungu anatujua sisi wanadamu nia zetu na anaona mbali..Kwa usalama wetu haina budi iwe hivyo tu.

Lakini katika utawala wa miaka 1000 hiyo itaondolewa…ndio maana unaitwa utawala wa Amani wa Miaka 1000…dunia yote itajawa na kumjua Mungu..Kristo atakapotawala kila kitu kitatii..kutakuwa hakuna wakalmani…ni kusikia na kutenda. Kutakuwa hakuna vita wala mafarakano, wala mapishano ya usemi na watu watamtii BWANA YESU na wafalme wake pasipo shuruti..na wakati huo huo itakuwa ni sehemu ya amani na furaha kama ilivyokuwa pale Edeni, wote watakuwa na nia ya kumjua Mungu.
Ufunuo 20:1 "Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake.
2 Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;
3 akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.
4 Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.
5 Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.
6 Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu”.
Sasa mwishoni mwa hiyo miaka 1000 kuisha, Bwana Yesu atamruhusu shetani afunguliwe kwa kitambo kidogo..kwanini aruhusiwe? Ni ili awajaribu mataifa, awajaribu hao watoto waliozaliwa ndani ya huo utawala…Maana ni sheria ya Mungu kila kiumbe chake kijaribiwe…hata sasa tunajaribiwa sasa na huyo huyo shetani…sharti na wao wajaribiwe..shetani atakapofunguliwa wapo baadhi watakaodanganyika naye na wachache watakaomkataa na kudumu katika kuutii utawala wa amani wa Bwana Yesu Kristo..

Wengi watadanganyika kama tu shetani anavyowadanganya wengi leo wasimwamini Bwana Yesu Kristo na uweza wake..kwahiyo wataungana pamoja na kutaka kuleta mapinduzi juu ya utawala wa Kristo..magugu na ngano vitajitenga, kabla hawajajaribu kufanya lolota…litatokea kama lililotokea HARMAGEDON. Moto utawateketeza pale pale walipo na uwingi wao, hatapona hata mmoja..wachache waliokataa kujiunga na hilo jeshi kushindana na Bwana, watahifadhiwa na watakuwa wameshinda.
Ufunuo 20:7 “Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;
8 naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.
9 Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala.
10 Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.”
Baada ya hilo jaribio kuisha..kutakuwa hakuna tena kizazi kingine cha wanadamu kilichosalia kwa ajili ya kujaribiwa, hivyo wakati uliobakia ni wa hukumu. Kila mtu kulipwa kama kazi yake ilivyo.

Kuanzia mwanzo wa wanadamu wote mpaka mwisho, watafufuliwa..walioko kuzimu watafufuliwa…Vitabu vitafunguliwa (ambacho kila mtu ana cha kwake). Na kitabu kimoja cha uzima kitafunguliwa..na endapo mtu hakuonekana jina lake kwenye kitabu cha uzima atatupwa katika lile ziwa la moto,[ kama hujajua nini maana ya jina lako kuonekana kwenye kitabu cha uzima unaweza ukanitext inbox nikutumie somo lake kwa urefu]...

Ufunuo 20:11 “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.
12 Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.
13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.
15 Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto”.
Siku hiyo watu wengi wataona sababu ya wao kupelekwa katika ziwa la moto. Itakuwa ni uchungu usioelezeka.Kwasababu kila kitu kitawekwa wazi mbele ya mashahidi wengi.

Na baada ya hukumu kuisha, itakuja mbingu mpya na nchi mpya..Katika mbingu mpya na nchi mpya..Ni hii hii dunia isipokuwa itavikwa na utukufu usioelezeka..itakuwa ni sehemu nzuri zaidi ya mbinguni…Huko kutakuwa hakuna tena muda..ni mambo mapya..wala hakuna bahari tena.

Ufunuo 21:1 “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.
2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.
3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.
4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.
5 Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.
6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.
7 Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.
8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Umempa Bwana maisha yako? Mwisho wa mambo yote umekaribia, hutasema siku hiyo hujasikia, biblia inasema walevi, waasherati, waabudu sanamu, sehemu yao ni katika lile ziwa la moto..

Neema ya Kristo iwe pamoja nawe.

No comments:

Post a Comment