Shalom, mwana wa Mungu karibu tujifunze maneno ya Uzima, yaliyo taa ya miguu yetu (Zaburi 119:105). Leo tutaona mwonekano wa Edeni ulivyokuwa hapo mwanzo na sasa ulivyo. Ukisoma kitabu cha Mwanzo, utaona baada ya Mungu kumaliza kuumba mbingu na nchi na vitu vyote tunaona alifanya tena kazi nyingine ndogo ya ziada, nayo ni kutengeneza BUSTANI. Bustani hii Mungu aliifanya mashariki mwa Eneo linaloitwa Edeni, aliitengeneza kuwa makao ya kiumbe chake maalumu kinachoitwa Mwanadamu. Mungu alikipa heshima ya kipekee mpaka kumtengenezea makao ndani ya makao, Bustani hii ilikuwa ni tofauti kabisa na maeneo mengine ya Dunia yaliyosalia.
Hivyo pale bustanini Mungu aliweka kila kitu ndani yake kinachomfaa na kumtosheleza mwanadamu.. Edeni tunaweza kusema ulikuwa ni kama mji mkuu wa Adamu, na ile Bustani ni Kasri lake. Wanyama wote na viumbe vyote viliweza kuishi nje ya Edeni lakini Adamu hakuishi nje na Bustani ile Mungu aliyompa.
Mwanzo 2:8 “Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.9 Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.10 Ukatoka mto katika Edeni wa kuitilia bustani maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne.11Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu;12 na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham.13 Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi.14 Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli; ndio unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati.15 Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.
Zipo sababu kwanini Mungu hakumwambia Adamu akaishi mahali popote tu anapopapenda duniani. Sababu mojawapo ni kwamba huko kwingine Mungu hakuweka utukufu wake wa kiungu kama ilivyokuwa pale Bustanini Edeni, na ndio maana Mungu alipotaka kuzunguza na Adamu alizungumza naye pale bustanini tu. Na pia kumbuka mahali popote utukufu wa Mungu upo, mahali hapo kunakuwa na (UTAJI) WIGO fulani au ULINZI Fulani. Adui au chochote kisichohusika hakiwezi kupenyeza.
Ili kulielewa hili vizuri tunaweza kujifunza katika mambo yanayotuzunguka ya kila siku. Siku hizi kuna kilimo kijulikanacho kama “ kilimo cha Banda-kitalu” kwa lugha ya kigheni iliyozoeleka na wengi kinaitwa GREEN HOUSE farming. Kilimo hichi hakina tofuati na kile kingine isipokuwa tu, hichi mmea au mboga, au matunda, au maua huwa yanawekwa katika banda maalamu lililozibwa pande zote katika uzalishaji wake. Na wanafanya hivyo sio kwasababu wamependa tu iwe hivyo hapana, lakini kama wewe ni mkulima mzuri utajua kuwa kulima mazao yako katika green-house,kuna faida kubwa kuliko kulima huria, sababu kubwa kwanza ni kinazuia wadudu waharibifu wa mazao kuvamia shamba, pili kinazia mionzi mikali ya jua kuharibu mimea, hivyo inasaidia kuhifadhi unyevunyevu na kutokutumia gharama nyingi za kupiga madawa, kwa ajili ya wadudu. Na matokeo yake ile mimea huwa inakuwa vizuri, yenye afya, na mwisho wa siku kuleta mazao mengi kuliko hata Yule ambaye yalilimwa mabondeni tu. Huyu anaweza akajiona analoshamba kubwa, lakini mimea ikiaanza kumea tu wadudu waharibifu wanakuja, na hivyo atajikuta anahangaika kupiga madawa, mimea inaliwa na kukosa mvuto na hata akifanikiwa kupeleka sokoni bidhaa yake hainunuliwi kwasababu inakuwa haina ubora unaostahili. Maua mengi ya thamani kama Maua Rose, yanalimwa ndani ya Green house, nje na hapo matokeo yatakuwa hafifu, na ndio maana unaona ubora wake na thamani yake ni kubwa.
