Jina kuu la YESU KRISTO litukuzwe ndugu yangu. Karibu tujinze maneno ya uzima.
Cha kushangaza, Bwana Yesu alipokuwa duniani hakulenga kundi Fulani maalumu la watu ili wawe wanafunzi wake, jaribu kufikiria siku ile alipokesha usiku mzima kumwomba Mungu ampe watu wa kufuatana naye, tulitazamia angekwenda kuchukua watu watakatifu katikati ya waandishi na mafarisayo, lakini cha kustaajabisha alienda kuchukua watu ambao wangeweza kuwa ni hatari sana kwake na katika jamii inayomzunguka.
Embu mtafakari huyu mtu anayeitwa Simoni Zelote. Hilo neno Zelote sio jina la Baba yake, hapana bali jina la CHAMA CHA WAPIGANIA DINI ya kiyahudi kilichokuwa Israeli wakati huo ndio walioitwa WAZELOTE. Ni watu ambao wakati wote walikuwa wanaupinga utawala wa Rumi, na walitumia silaha, na kila mbinu ili kuidondosha dola ya Rumi iliyokuwa inatawala Israeli, na Uyahudi unyanyuke. Hivyo watu hawa walikuwa ni hatari na Simoni huyu alikuwa ni mmojawapo, kwasasa tunaweza kuwaita al-quida wa Wayahudi. Lakini Yesu alikwenda kumchagua na kumfanya kuwa mwanafunzi wake.(Luka 6:12)
Embu mtafakari Mathayo mtoza ushuru. Kumbuka zamani zile watoza ushuru wote walikuwa wanajulikana kama ni watu wenye dhambi, watu wa rushwa na dhuluma sikuzote. Mathayo alikuwa ni tajiri na pia msomi, mtu wa ofisini, aliyekuwa analitumikia taifa la Rumi kule Israeli kwa kulikusanyia Kodi, cha ajabu anakwenda kukutana na maadui wa Warumi, Simoni Zelote. Lakini Yesu anawakutanisha wote pamoja.
Mtafakari tena Yuda: Ni mtu ambaye alikutwa katika tabia zake za wizi na tamaa za viwango vya juu vya fedha, ni mtu ambaye alikuwa yupo tayari kutoa kitu chochote kile ili tu apate fedha, kama alifikia hatua ya kumuuza Bwana, akifahamu kabisa ni mtu asiyekuwa na hatia unategemea vipi, asiwe amefanya mambo mengine maovu huko nyuma kabla ya kukutana na Kristo. Lakini Yesu alimwona pia na kumwita.
Watafakari wale wavuvi: Ni watu ambao hawakwenda shule hata mmoja, Ni kazi za watu waliodharaulika wasio na elimu, vile vile sio kwamba nao walikuwa wanauhafadhali kwa matendo mema, hapana mfikirie mtu kama Petro anafikia hatua ya kutoa panga lake na kumkata mtu sikio, jambo ambalo hata wewe sasa hivi ni ngumu kulifanya,lakini Petro alilifanya japo alishatembea na Kristo muda wote ule na kuona huruma yake na upendo wake..kama aliweza kumkata mtu sikio mbele ya jeshi kubwa kama lile unadhani alikuwa katika hali gani kabla ya kukutana na Bwana, ni wazi kuwa pengine alishaondoa viungo vya watu wengi sana waliomkorofisha… Kuna Wale wanafunzi wawili wavuvi (Yohana na Yakobo) nao pia walimshauri Yesu ashushe moto autekeze mji wote, unaona ni watu ambao hawakuwa na huruma, mpaka Yesu akawaambia hamjui ni roho ya namna gani mliyonayo. (Luka 9:54).
Hiyo yote ni kuonyesha ni jinsi gani Bwana asivyokuwa mbaguzi, aliwachagua watu mbalimbali aliwachagua matajiri, aliwachagua maskini, aliwachagua wenye elimu aliwachagua wasio na elimu, aliwachagua wanafki, aliwachagua kapigania dini.. wote hao, aliwaita sawa sawa wawe mitume wake..Hata na leo hii anaita watu wote, wewe ni fisadi anakuita,wewe ni mpenda fedha ambaye ilifikia hatua ukamtoa mama yako kafara au mtoto wako kwa waganga kwa ajili ya kupata mali, bado KRISTO anakuita leo, wewe ni muuza karanga anakuita, wewe ni mwanasiasa anakuita, wewe ni bilionea bado anakuita uwe mwanafunzi wake, wewe ni tapeli anakuita, wewe ni mlemavu anakuita. Vyovyote vile ulivyo anakuita. Kinachojalisha ni jinsi utakavyomaliza na sio jinsi ulivyosasa.
Tunaona mitume wote wa Kristo mwisho wa siku walikuja kubadilishwa tabia na kuwa mitume waaminifu wenye upendo, mashujaa walioishindania Imani hata kufa, isipokuwa mmoja tu, ambaye ni YUDA huyo peke yake ndiye alikufa na tabia zake zile zile, kwasababu hakuthamini nafasi ya kipekee aliyopewa. Halikadhalika na wewe usipoithamini nafasi hii ya upendeleo unayopewa na Yesu mwenyewe, utakufa katika dhambi zako, na utaishia motoni.
Mathayo 22:14 “Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache”.
Hivyo hapo ulipo anza maisha yako upya na Bwana, anakupokea wewe jinsi ulivyo, haijalishi ni mtenda dhambi kiasi gani, haijalishi una madhaifu kiasi gani, anakuita uambatane naye, uwe mwanafunzi wake kuanzia sasa, anataka akubadilisha uwe MTEULE WAKE kama alivyofanya kwa mitume wake.
Bwana akubariki.
No comments:
Post a Comment