"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, October 1, 2016

MIHURI SABA

Katika kitabu cha ufunuo sura ya tano, tunaona Mungu akiwa ameketi katika kiti chake cha enzi akiwa na kitabu katika mkono wake wa kuume, kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa mihuri saba. Na hapakuonekana mtu yeyote mbinguni wala duniani aliyestahili kukifungua hicho kitabu wala kukitazama, Ni kitabu kilichobeba siri zote za ukombozi wa mwanadamu,kuanzia mwanzo wa mambo yote hadi mwisho wake, jambo lililomfanya Yohana alie machozi kwa kuwa hapakuona mtu yeyote aliyestahili kukifungua wala kukitazama. Lakini alionekana mmoja aliyestahili kukifungua hicho kitabu, naye ni BWANA YESU KRISTO haleluya!. (soma ufunuo sura ya tano yote.).
MUHURI WA KWANZA:
Ufunuo 6:1-2, "Kisha nikaona napo Mwana kondoo alipofungua moja ya zile muhuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo! nikaona na tazama, farasi mweupe na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda."

Tunaona kuna wenye uhai wanne na farasi wanne.Wale wenye uhai wanne walioonyeshwa katika sura hii, wanaashiria nguvu ya Mungu iliyoachiwa kwa watu wake, kupambana na uovu na njama za yule adui.Mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba, na wa pili alikuwa mfano wa ndama na wa tatu kama mwanadamu, na wanne kama tai arukaye.
Kwahiyo muhuri wa kwanza ulipofunguliwa, yule mwenye uhai wa kwanza aliposema njoo! akatoka farasi mweupe, na aliyempanda juu yake ana uta (upinde wa mshale). Na hiyo ni roho ya mpinga Kristo ikianza kutembea katika kanisa la Mungu kwenye kanisa la kwanza, 2thesalonike 2:3 " Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yeyote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu: akafunuliwa yule mwana wa kuasi, mwana wa uharibifu." kwahiyo hapo tunaona kuwa mwisho wa yote usingefika kabla ya ule uharibifu( ukengeufu) kuja kwanza na kuingia katika kanisa.

hii roho ya shetani ilianza kuingia katika kanisa la kwanza baada ya mitume kuondoka hapa Paulo anasema matendo 20:29 " najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao." 1Yohana 2:18 aliongezea kusema " watoto ni wakati wa mwisho na kama vile mlivyosikia ya kwamba mpinga kristo yuaja, hata sasa wapinga kristo wengi wamekwisha kuwapo. kwasababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wakwetu wangalikaa pamoja nasi.Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu."

Kwa hiyo hapa mitume walilionya kanisa juu ya mafundisho ya uwongo ambayo hayakuhubiriwa na mitume. Hivyo yule farasi mweupe ni roho ya mpinga kristo ikitembea katika kanisa la kwanza, na alionekana mweupe na aliyempanda ameshika uta (upinde) lakini hana mshale, kuashiria kutokuwa na madhara yoyote (yaani kuhusisha mauaji ya watakatifu) . roho hii ilanza kuingia kama mafundisho ya uwongo lakini Mungu aliachia Roho ya kuishinda iliyofananishwa na yule mwenye uhai wa kwanza ambaye ni Simba. Tabia ya simba ni mnyama asiyeogopa, mwenye ujasiri hivyo wadristo wa kipindi kile waliweza kuishinda ile roho ya mpinga kristo kwa ujasiri wa neno la Mungu.

Nyakati hii ilidumu kati ya kipindi cha 53AD-170AD. katika kanisa la kwanza ambalo ni Efeso.

Kristo alitoa pia angalizo kwa kanisa hili tunasoma katika kitabu cha ufunuo 2:2" nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio ukawaona kuwa ni waongo......lakini unalo neno hili, ya kwamba wayachukia matendo ya wanikolai ambayo na mimi nayachukia.".


MUHURI WA PILI:
ufunuo 6:3-4 " Na alipoifungua muhuri ya pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema Njoo!. akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyeimpanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa."

Hapa tunaona shetani (mpinga kristo), baada ya kuona ameshindwa kuwazuia wakristo wa kweli kumwabudu Mungu katika Roho na kweli wakisimamia neno wakiongozwa na ile nguvu ya Mungu kwa mfano wa simba ambayo ndiyo ile Roho ya Mungu aliyoiachia kwa watu wake kumshinda shetani, Hivyo shetani akabadilisha mbinu zake za kuwashambulia wakristo, kwa kubadilika kutoka farasi mweupe kwenda kuwa farasi mwekundu, na runaona aliyempanda ni yule yule aliyekuwa anamwendesha yule farasi wa kwanza. Tunasoma kuwa alipewa mamlaka ya kuiondoa amani na upanga mkubwa, kuashiria kuleta dhiki za mauaji kwa wale watu wanaomwamini Mungu na kuzishika amri zake.

Katika utawala wa Roma, Historia inaonyesha kuanzia mwaka 354AD hadi kufikia kipindi cha matengenezo ya kanisa utawala wa Rumi chini ya kanisa katoliki ulifanikiwa kuwauwa wakristo zaidi ya milioni 68, kwa dhumuni la kuimarisha itikadi za dini yao. kwa mtu yeyote kuwa na imani nyingine nje ya dini ya kikatoliki adhabu ilikuwa ni kifo. Wakristo na wayahudi wengi waliuawa kwa kusimamia imani yao. damu nyingi za watakatifu zilimwagika.

lakini Mungu aliachia Roho ya kuweza kuikabili hiyo nguvu ya mpinga kristo nayo ni nguvu iliyofananishwa na ndama, Ndama ni mnyenyekevu sana yupo tayari kwenda kuchinjwa na anaandaliwa kwa ajili ya kutolewa sadaka, hivyo wakristo wengi kwa kutaka wenyewe walijitoa maisha yao kwenda kuuawa kwa ajili ya imani yao bila kuogopa kwani Mungu ndiye aliyeachia hiyo Roho juu yao, walichinjwa, walisulibiwa, waliliwa na simba, waliburutwa lakini jinsi walivyozidi kuwauwa ndivyo walivyozidi kujitoa. warumi 8:36 " .....kwa ajili yako tunauwa mchana kutwa, tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa" kipindi cha huyu farasi mwekundu kilidumu mpaka mwishoni mwa kanisa la pili.


Na hii roho ya mauaji dhidi ya wakristo bado inatenda kazi hata leo, katika baadhi ya nchi.


MUHURI WA TATU:

Ufunuo 6:5 "na alipoifungua muhuri ya tatu,nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wa nne, ikisema, kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai."

Baada ya shetani kuona anawaua wakristo na bado wanaendelea kukubali kwenda kuuawa kwa kuishikilia imani yao akaamua kubadili mbinu ya kulivamia kanisa la Mungu kwa namna nyingine kwa kubadilisha rangi kutoka kuwa farasi mwekundu kwenda kuwa farasi mweusi

Hichi ni kipindi kinachojulikana na wanahistoria wengi kama kipindi cha giza (dark age) kilidumu kwa zaidi ya miaka 1000 kuanzia karne ya 5 mpaka karne ya 16. Ni kipindi ambacho utawala wa kipapa ulianza kuuza kile wanachokiita neno la Mungu kwamfano mtu akitaka kuoa au kuolewa ni lazima atoe fedha, ibada za kuwaombea wafu (ambazo ni kinyume na neno la Mungu) ni lazima utozwe pesa, kushiriki meza ya Bwana ni lazima utoe pesa, ukitaka kusamehewa dhambi unapaswa kutoa pesa, ukitaka kuombewa kama unaumwa ni lazima utoe pesa n.k ndio maana tunasoma yule mpanda farasi alikuwa amebeba mizani mkononi mwake hii inamaanisha kuwa ukitaka kitu lazima utoe kitu. Kwa njia hii kanisa katoliki likiongozwa na utawala wa papa lilijikusanyia utajiri mkubwa sio ajabu hata leo hii tunaona jinsi taifa la Vatican lilivyo na utajiri mkubwa na halifanyi biashara yoyote ya kuliingizia kipato.

Lakini pamoja na hayo Mungu aliachilia nguvu ya kulishinda hilo giza kwa watu wake,na ile sauti iliyosikika ikisema usiyadhuru mafuta wala divai. Mafuta yanaashiria Roho Mtakatifu na divai inaashiria ufunuo wa neno la Mungu, hivyo basi lile kundi dogo la Mungu lililopitia kwenye hichi kipindi kirefu cha giza Bwana aliachia Roho ya ufunuo juu yao kwa mfano wa uso wa mwanadamu ikiashiria hekima ya kibinadamu

Katika hichi kipindi cha giza hadi kwenye matengenezo ya kanisa Mungu alinyanyua watu waliotumia hekima kama Martin Luther alihubiri (mwenye haki wangu ataishi kwa imani) ambapo hapo mwanzo ilikuwa hairuhusiwi mtu yeyote kufundisha au kusoma biblia isipokuwa kwa viongozi tu wa kanisa katoliki tu!.hivyo Mungu aliendelea kunyanyua wengine wengi kama, Zwingli, Calvin, Knox,Bucer n.k kwa ajili ya matengenezo ya kanisa.


MUHURI WA NNE:
Ufunuo 6:7-8 "Na alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu na yeye aliyempanda jina lake ni mauti, na kuzimu ikafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, na kwa hayawani wa nchi."

Tunaona hapa shetani ambaye ndiye mpinga Kristo alipoanza kubadilika kutoka kwenye farasi mweupe akaenda kwenye farasi mwekundu, akaenda tena kuwa farasi mweusi na sasa amekuwa farasi wa kijivu jivu. Rangi ya kijivujivu inaashiria mchanganyiko wa rangi zote tatu yaani nyeupe, nyekundu na nyeusi. ambayo pia inaashiria udanganyifu na mauti.

Hii ni roho ya mpinga kristo inayotembea sasa katika kanisa hili la mwisho (laodikia), farasi huyu amechanganyikana na anazo tabia zote tatu. Ameitwa kuzimu na mauti inamfuata kwasababu katika hichi kipindi cha mwisho anaonyesha rangi zake zote na kujifunua yeye ni nani kwa kuwaua watu na kuwapeleka kuzimu kwa mafundisho yake ya uongo, akiyaleta makanisa yote pamoja(world council of churches) na kuunda ile chapa ya mnyama. Na bado hazina yote ya dunia ipo Roma hii inaonyesha yule farasi mweusi pia bado anatembea katika utawala wa kanisa katoliki, na ni mwekundu kwasababu anawaua watu katika roho walewe kwa mvinyo wa uasherati wake na kuwafanya watu wengi wawe vuguvugu na bado pia atakuja kuwaua wakristo wengi na wayahudi katika kipindi cha dhiki kuu ambacho kiko mbioni kutokea pale mpinga kristo atakaponyanyuka kwa kupitia utawala wa kiPapa chini ya kanisa katoliki.

Pamoja na hayo Mungu ameachia nguvu ya kupambana na roho hii ya mpinga kristo nayo imefananishwa na Tai. Tai ana uwezo wa kuona vitu vya mbali na Bwana aliwafananisha manabii wake na Tai, hivyo basi katika kanisa hili la Laodikia ambalo ndio la mwisho Bwana ameachia Roho ya kinabii kuweza kuzitambua hila za yule adui, na kuturudishwa katika imani ya mababa na nguvu Mungu aliyoiachia ni ufunuo wa kumtambua Mpinga Kristo na chapa yake na ujumbe wa kutoka kwake na kutokushiriki mafundisho yake ya uongo..ufunuo 18:4 "...tokeni kwake, enyi watu wangu msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake." Ikiwa wewe ni mkristo na hauna ndani yako Roho ya ufunuo ya kuona mbali kama Tai huwezi kamwe kumshinda shetani, utaangukia kumezwa na yule mnyama kwa mafundisho yake ya uwongo na unajua ni jambo gani linaambatana naye, biblia inasema ni MAUTI NA KUZIMU, hakuna namna yoyote utakayoweza kumshinda shetani kama upo kwenye mifumo ya madhehebu, umekwisha pokea chapa ya mnyama pasipo wewe kujijua, Kama hauna Roho Mtakatifu mwombe Mungu akupe na Roho ya ufunuo ya kulielewa neno lake.Amen!

MUHURI WA TANO:
Ufunuo 6:9-11 "Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vilevile kama wao."

Hapa tunaona hakuna mwenye uhai yeyote akitangaza kufunguliwa kwa muhuri huu, hivyo hatuoni kanisa la mataifa likihusishwa. lakini ulipofunguliwa muhuri wa tano zilionekana roho nyingi chini ya madhabahu zikimlilia Mungu. Hizi roho ni wayahudi waliouawa kipindi cha utawala wa kimabavu wa Hitler (Holocaust), waliuliwa kwa sababu moja tu kuwa wao ni wayahudi, historia inasema Hitler aliwaua wayahudi zaidi ya milioni 6 katika kipindi cha vita ya pili ya dunia.

wana theolojia wengi wanasema kuwa hizi roho xilizo chini ya madhabahu ni wakristo waliouawa katika kipindi cha kanisa la kwanza chini ya utawala wa Roma, lakini hiyo sio kweli, hapa tunaona kuwa hawa walikufa kwa ushuhuda wao, na sio ushuhuda wa Yesu Kristo, na pia hawa wanamwomba Mungu alipize kisasi juu ya maadui zao, kwani kulingana na torati kulipiza kisasi ni desturi ya wayahudi. kwamfano tunaona kuna maandiko yanayosema jino kwa jino, jicho kwa jicho,n.k kwahiyo hatuwezi tukashangaa kwanini hapa walikuwa wanamwomba Mungu alipize kisasi juu ya maadui zao, lakini hiyo siyo desturi ya wakristo. Wakristo hawalaani wala hawaombi kisasi, bali wao husema baba uwasemehe, tunaona mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo na Stefano walivyofanya.Hivyo hizi roho zinazozungumziwa hapa ni wayahudi na sio wakristo.

Pia tunaona walipewa nguo ndefu nyeupe, hizi zinaashiria kupewa neema ya wokovu kwa ushuhuda wao wenyewe walioushikilia, kwa lile agano Mungu alilomuahidia Ibrahimu na uzao wake,hawa ni wale wayahudi waliokuwa waaminifu na dini yao ya kiyahudi wakiishikilia torati kikamilifu hata kufa na sio wayahudi wote walio waliouliwa na Hitler walikuwa waaminifu na imani yao warumi 9:6 "Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli. "

wakaambiwa tena wangojee kwa kipindi kifupi mpaka idadi ya wajoli wao itimie ambao watakufa kama wao.hii inamaanisha katika kipindi cha ile dhiki kuu. Ambayo mpinga kristo atawaua wayahudi wengi na kulivunja lile agano atakalofanya na wayahudi ambalo limezungumziwa katika kitabu cha Danieli sura ile ya tisa.(Wayahudi wakiwa katika kambi za mateso chini ya utawala wa Hitler,Nazi)

MUHURI WA SITA:
Ufunuo 6:12-17 " Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu, na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi. Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake. Na wafalme wa dunia, na wakuu na majemedari na matajiri, na wenye nguvu na kila mtumwa, na mungwana wakajificha katika pango la chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye akitie juu ya kiti cha enzi, na hasira ya mwanakondoo kwa maana siku iliyokuu ya hasira yao imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?."

Hapa tunaona muhuri huu ulipofunguliwa dunia nzima iliathirika na ndiyo ile siku kuu ya kuogofya ya Bwana kama Yesu Kristo alivyoizungumzia katika katika mathayo 24:29-30 " Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi". Hii siku ya Bwana itakuja mwishoni mwa miaka mitatu na nusu baada ya kumalizika ile dhiki kuu

Siku hii ya Bwana itadumu kwa kipindi cha siku 75 ikianzia kwa kumimina ghadhabu ya Mungu katika dunia, ambayo itahusisha vita vya harmagedoni (ufunuo 19-21, zekaria 14:1-4, 12).ndani ya siku hizi 75 kutakuwa pia na kufufuliwa kwa watakatifu waliouawa katika kipindi cha dhiki kuu (ufunuo 11:18, 20:4), itamalizia na hukumu ya mataifa (mathayo 25:31-46) kabla ya kuingia katika matengenezo ya utawala wa miaka 1000 wa Bwana Yesu Kristo (mathayo 19:28).

hizi siku 75 zinapatikana kutoka katika zile siku 1335 zilizozungumziwa katika kitabu cha daniel 12:12. siku hizi 1335 ukitoa siku 1260 (au miezi 42) ambayo mpinga kristo atatawala baada ya kuikomesha sadaka ya kuteketezwa ya daima daniel 9:24-27"......Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu."

MUHURI WA SABA:
Ufunuo 8:1 "Hata alipoifungua muhuri ya saba, kukawa kimya mbinguni kama muda wa nusu saa. "
Mstari wa pili unaelezea juu ya wale malaika waliojiweka tayari kupiga baragumu ambayo ni habari nyingine isiyohusiana na muhuri wa saba, Huu ukimya mbinguni unaashiria kuna jambo linakwenda kutokea ambalo ndilo tunaloliona katika ufunuo sura ya kumi.

katika sura ya kumi.ufunuo 10:1-4 "Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto. Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi. Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao. Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike."

Malaika huyu anayeonekana hapa si mwingine bali ni Bwana Yesu Kristo akiwa ameshika kile kitabu kidogo. Na ndani ya muhuri huu wa saba ambao bado haujafunuliwa kwetu kwa sasa lakini utakapokuja kufunuliwa utampa bibi arusi wa Kristo imani ya kwenda katika unyakuo(ambayo siri hii imejificha katika zile ngurumo saba Yohana alizoambiwa asiziandike).Na muhuri huu wa saba utatimia kabla ya muhuri wa sita kutimia, kwasababu muhuri wa sita unaelezea siku kuu ya Bwana ambayo ni mwisho wa mambo yote.

kulingana na 1thesalonike 4:16-17 "Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele".

Kuja kwa Bwana kutafuata hatua tatu, ya kwanza ni Bwana atakuja na mwaliko(shout) na ya pili ni sauti ya Malaika Mkuu na ya tatu ni parapanda ya Mungu. Hatua ya kwanza ya mwaliko ndiyo tuliyopo sasa hivi iliyoletwa na Mjumbe wa kanisa la saba(William Branham) yenye ujumbe wa kutuandaa sisi kumpokea Kristo na kuturudisha katika ukristo wa biblia.mathayo 25:6 "Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki" Mjumbe wa kanisa la saba alikuja kututangazia ujio wa Bwana Yesu Kristo ni wakati wa sisi kuzitengeneza taa zetu na kuwa tayari kumlaki Bwana Yesu mawinguni.

Hatua ya pili ni sauti ya Malaika mkuu. na ndiye tunayemwona katika ufunuo 10 na si mwingine zaidi ya Yesu Kristo, na ujumbe wake utakuwa kwa yule bibi arusi aliyekwisha kujiweka tayari kumlaki, bikira safi ambaye taa yake inawakaa, huyu ni mkristo aliyebatizwa na Roho Mtakatifu aliyejitenga na uasherati wa yule kahaba(katoliki na madhehebu yote) yasiyofanya neno la Mungu kuwa mwongozo wao na kushikilia mafundisho ya wanadamu na ibada za kipagani. Huyu bibi arusi pekee ndiye atakayeisikia sauti ya malaika mkuu ambayo itahubiriwa na zile ngurumo saba tunazoziona katika kitabu cha ufunuo 10:3-4 Yohana alizoambiwa asiziandike lakini mwingine yoyote asiye bikira mwenye busara hatoweza kuisikia sauti ya hizo ngurumo saba.

Ngurumo saba ni Sauti za watu saba ambao Mungu atawanyanyua katika kipindi hichi cha mwisho na kuleta uamsho duniani kote, ambazo kupitia hizi sauti saba tutapata imani itakayotuwezesha sisi kwenda katika unyakuo. Na hizi ngurumo saba zipo karibuni kutoa sauti zake..je? umejiweka tayari? unaye Roho Mtakatifu? watakaoweza kuupokea ujumbe wa ngurumo saba ni bibi arusi tu mwenye Roho wa kristo. Na wakati huo ukifika kutakuwa hakuna muda tena, ni wakati wa wewe kutengeneza mambo yako sasa vizuri kwa Bwana.

Hatua ya tatu na ya mwisho ni parapanda ya Mungu. katika kipindi hichi kila mmoja wetu aliye mkristo ataisikia sauti ya Mungu ikimwita na gafla tutaona mabadiliko ya miili yetu na kuchukuliwa juu mbinguni kwa Bwana milele na milele haleluya!.

Shalom!

No comments:

Post a Comment