"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, October 16, 2016

NGURUMO SABA

Katika kufunguliwa kwa mihuri saba, kwenye kile kitabu cha ufunuo, tunaona kuwa muhuri wa saba unatimia kabla ya muhuri wa sita, kwasababu muhuri wa sita unaelezea juu ya ile siku ya kuogofya ya Bwana, ambayo itakuja mwishoni baada ya ile dhiki kuu kuisha, Lakini muhuri wa saba unaelezea, mambo ya mwisho yatakayotokea kabla ya ujio wa pili wa Bwana Yesu Kristo kulichukua kanisa lake. Kwa ufupi muhuri wa kwanza, na wa pili, na wa tatu, na wa  nne, unaelezea jinsi roho ya mpinga kristo ilivyoanza kutembea katika kanisa la mataifa(ufunuo 6) kama inavyoonekana katika historia ya kanisa na tonaona pia zile Roho za wenye uhai wanne ambazo wakwanza alikuwa kama mfano wa simba, wapili mfano wa ndama, watatu mfano wa uso wa mwanadamu, na wanne mfano wa tai arukaye. Hizi ni Roho za Mungu zilizoachiwa kupambana na ile Roho ya mpinga kristo katika vipindi vya makanisa. Na muhuri wa tano unaelezea juu ya wayahudi waliouawa kipindi cha vita vya pili vya dunia(holocaust) chini ya utawala wa kimabavu wa Adolf Hitler wa ujerumani, inakadiriwa zaidi ya wayahudi milion 6 waliuawa. hizi ndizo zile roho zilizoonekana chini ya madhabahu kwenye ule muhuri wa tano ulipofunguliwa.(ufunuo 6:9)

Na leo tunauzungumzia ule muhuri wa saba, unaobeba zile ngurumo saba:

Tukisoma ufunuo 8:1" Hata alipoifungua muhuri ya saba, kukawa kimya mbinguni kama muda wa nusu saa." Muhuri huu ulipofunguliwa biblia inarekodi kulikuwa na ukimya mkubwa mbinguni kuonyesha kuwa tukio fulani kubwa linaenda kutokea. Na hili sio lingine zaidi ya Bwana wetu YESU KRISTO ,akinyanyuka kutoka kwenye kiti chake cha enzi, na kushuka kudai walio wake. zekaria 2:13"Nyamazeni, ninyi nyote wenye mwili, mbele za Bwana; kwa maana ameamka, na kutoka katika maskani yake takatifu."

Jambo hili tunaendelea kuliona katika ile sura ya kumi.
 ufunuo 10 :1-8 "Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto. 2 Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi.
3 Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.
4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike.
5 Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni,
6 akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya; 7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.
8 Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.
9 Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.
10 Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.
11 Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi."


Malaika huyu mkuu mwenye nguvu aliyeshika kitabu kidogo aliyeonekana akishuka kutoka mbinguni sio mwingine bali ni BWANA YESU KRISTO, Na kile kitabu alichokishika  ndio kile kitabu kilichokuwa kimefungwa na ile mihuri saba, lakini sasa hapa kinaonekana kimefunguliwa.

Na aliposhuka akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na wa kushoto juu ya nchi, naye akalia kwa sauti kuu kama simba angurumavyo, na alipolia zile NGURUMO SABA, zikatoa sauti zao. Lakini hapa tunaona alipolia kwa sauti kuu, ile sauti iliambatana na sauti ya zile NGURUMO SABA. Hivyo basi tunaona hizi ngurumo saba zinabeba sauti ya BWANA zenye ujumbe unaohusiana na kile kitabu alichokuwa amekishika.

 Katikati ya waaminio wengi wa ujumbe wa malaki 4, kumekuwa na mgawanyiko mkubwa,na kutengeneza makundi mawili makubwa. Kuna kundi linaloamini kuwa ngurumo saba zimeshafunuliwa, na kuna kundi lingine linaloamini kuwa ngurumo saba bado hazijafunuliwa. katika kundi linaloamini kuwa ngurumo saba zimeshafunuliwa limegawanyika tena katika vikundi vikundi, kuna wanaoamini ngurumo saba ni ufunuo wa ile mihuri saba, kuna wengine wanaoamini kuwa ngurumo saba ni, zile hatua saba za kimo cha mtu mkamilifu 2petro 1:5-7. kuna wengine wanaamini ngurumo saba ni yale maono saba ya William Branham alioonyeshwa kabla ya kurudi kwa pili kwa BWANA YESU KRISTO, na wengine wanaamini ngurumo saba ni zile huduma tano zilizowekwa kulijenga kanisa waefeso 4.. n.k. Na kundi linaloamini kuwa ngurumo saba bado hazijafunuliwa wapo wanaoamini kuwa ngurumo saba ni watu 7 kabla ya unyakuo, na wapo wanaoamini kuwa ngurumo saba zitafunuliwa mara baada ya unyakuo kupita.

Ni wazi kabisa ndugu Branham alisema kuwa ufunuo sura ya kumi inazungumzia kuja kwa Bwana YESU KRISTO, 
kwenye kitabu cha ufunuo wa mihuri saba-William Branham { muhuri wa kwanza, pg 12, march 1963 William Branham alisema "Na ndipo kunakuja Ngurumo saba za siri ambazo hata hazijaandikwa kamwe. Hiyo ni kweli. Nami naamini ya kwamba, kupitia Ngurumo hizo Saba, zitafunuliwa katika siku za mwisho ili kumkusanya Bibi-arusi pamoja kwa ajili ya kupata imani ya kunyakuliwa. Kwa sababu, ile tuliyo nayo sasa hivi, ha_hatungeweza kufanya jambo hilo. Kuna jambo fulani. Hatuna budi kupiga hatua mbele zaidi. Sisi, hatuwezi kupata imani ya kutosha kwa ajili ya uponyaji wa Kiungu, ni vigumu. Lazima tuwe na imani ya kutosha kubadilishwa, katika dakika moja, na kunyakuliwa tutoke katika dunia hii."

mahali pengine alisema,
{kwenye Muhuri wa tatu, pg 25, march 1963 "Bi-Bibi arusi hajawa na uamsho bado. Mnaona? Hakujakuwako na uamsho humo, hakujakuwako na madhihirisho ya Mungu kumwamsha Bibi-arusi bado. Mnaona? Tunautarajia huo sasa. Itahitaji hizo Ngurumo Saba zisizojulikana kule nyuma, kumwamsha Yeye tena, unaona. Naam. Yeye atazituma. Aliliahidi."

Ikiwa kama ngurumo saba zilishafunuliwa ni dhahiri kuwa tungekuwa tumeshapata imani ya kwenda kwenye unyakuo, Nabii alihubiri kuwa hizo ngurumo saba zitakapolia zitampa bibi-arusi imani ya kwenda kwenye unyakuo. Hivyo tunaona kuwa mawazo ya kusema kuwa ngurumo saba zimeshafunuliwa hayana uhalisia wowote wa kimaandiko.

Ngurumo saba ni hatua ya mwisho ya UAMSHO ya kumpa bibi arusi imani ya kwenda kwenye unyakuo, kwahiyo ninakubaliana na wanaosema kuwa hizi NGURUMO SABA NI WATU SABA, ambao Mungu ataenda kuwanyanyua katika kipindi hichi cha mwisho, watakaohubiri siri zile ambazo Yohana aliambiwa asiziandike, watahubiri mambo ambayo hayajarekodiwa kwenye biblia mahali popote, na kama vile zile nyota saba za makanisa saba ni watu saba, vivyo hivyo ngurumo saba zitakuwa watu saba, ambao watatoa jumbe zao tofauti tofauti kwa wakati mmoja, Na hawa watu saba watakapotoa sauti zao zitasikika duniani kote na itakuwa ni kwa muda mfupi, watakaopata ulewa wa jumbe hizo ni bibi arusi tu, aliyekwisha kujiweka tayari kwa kuuamini ujumbe wa malaki 4(yaani kupokea Roho Mtakatifu huko ndiko kuuamini ujumbe wa malaki4) lakini kwa waliobakia hizo jumbe zitasikika  kwao kuwa kama ushuhuda tu, kwahiyo injili itakayohubiriwa haitakuwa ya kuwavuta watu kwa Kristo tena, Bali ya kumpa bibi arusi imani ya kwenda kwenye unyakuo.

baada ya ngurumo 7 kutoa sauti zao ambao ni watu 7, Mungu atakaowanyanyua wakati wa mwisho kuzungumza siri zilizopo katika kile kitabu kidogo kilichobeba siri za ukombozi wa mwanadamu. Lakini tunaona pia hapo kwenye mstari wa 8 Yohana alipewa kile kitabu akile, hapa Yohana anawakilisha bibi arusi wa kristo, na alipokila kile kitabu ambacho kilikuwa kitamu mdomoni mwake bali kichungu tumboni mwake, maana yake ni  kwamba ule ufunuo atakaoupata kutoka katika kile kitabu ambacho kitahubiriwa na zile ngurumo 7 utakuwa ni mzuri kuusikia lakini utakuwa ni mgumu kuupokea na kuuhubiri. kwahiyo kama tunavyoona kwenye mstari wa 10 yohana (alinawakilisha bibi arusi) alivyoambiwa imempasa atoe tena unabii juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi, hii inamaana bibi arusi baada ya kuupokea ujumbe wa zile ngurumo 7, Roho kuu ya Mungu ya uvivuo itawajilia na ndio watakaopeleka injili duniani kote kwa mara nyingine tena, kwa udhihirisho mkuu wa nguvu za Mungu kwa namna ambayo haijawahi kutokea kabla ili kuwa ushuhuda kwa mataifa yote, hapo ndipo ule mwisho utakapokuja(mathayo 24:14). Kwahiyo kuna uamsho mkuu unakuja mbeleni utakaopita dunia yote.

Ndugu umeona hatua tuliyopo sasa, ni wakati wa jioni, Kristo alisema ufunuo 22:11 "Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa. " Hizo ngurumo saba zitakapotoa sauti zao Ndugu yangu kutakuwa hakuna muda tena, kitakuwa ni kipindi cha check-in process, pale wale wanawali wapumbavu watakapoona bwana arusi anakuja, na kuanza kwenda kutafuta mafuta, na waliporudi walikuta wenzao wameshaingia karamuni na ndivyo itakavyokuwa wakati huo zile ngurumo saba zitakapotoa sauti zao, kumbuka ni wale tu wenye Roho Mtakatifu ndio watakaoweza kupokea na kuzielewa jumbe hizo zitakapotelewa, lakini wewe unayejiita mwamini hauna Roho Mtakatifu na unalifahamu hilo unaishi maisha yasiyofanana na ukristo, siku hiyo itakukuta itakujia kama mwivi, wakati wewe umeshtuka na kuanza kwenda kutafuta mafuta wakati huo wenzako watakuwa wameshaondoka wapo mbinguni.
mimi sitaki kubaki sijui wewe ndugu yangu??.

Tafuta ROHO MTAKATIFU sasa, kabla hayo mambo hayajatokea maana yapo mlangoni, Nabii (William Branham) ameshakuja, katoa ujumbe wake kaondoka, ni jukumu lako wewe sasa kutafuta Roho Mtakatifu, ambao ndio muhuri wa Mungu, PASIPO HUYO HAKUNA UNYAKUO.

MUNGU AKUBARIKI....

No comments:

Post a Comment