"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, May 13, 2017

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 14

SWALI 1: Mathayo 6:7 Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.Nisaidie ninaweza kuomba vipi nikaonekana kuwa sijapayuka payuka mbele za Mungu?

JIBU:Mungu akubariki ndugu, mstari huo ukiangalia kwenye tafsiri nyingine hilo neno "kupayuka-payuka" halimaanishi kama "kupaza sauti kwa nguvu," kama watu wengi wanavyodhani, hapana bali linamaanisha "KURUDIA-RUDIA" maneno yale yale, Hilo la kupaza sauti kwa nguvu mstari wake ni ule wa juu yake kabla ya huu unaosema "Mathayo 6: 5 Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.
6 Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.

Na ndipo sasa mstari unaofuata unasema...

7 Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.
8 Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. "

Hivyo watu wanao rudia-rudia maneno, kwa mfano watu  dini nyingine na watu wanaosali rozari na sala za bikira mariamu wanafahamu,huwa wanarudia maneno yale yale kwa muda mrefu hata masaa na masaa wakidhani kuwa kwa kufanya vile Mungu atasikia dua zao. Hizo ni desturi za kipagani ndio maana tumeonywa tusifanane na hao. kwahiyo tunapoenda mbele za Mungu tuwe na malengo, tutoe hoja zetu zote, kisha zikishaisha, basi, tushukuru tuondoke Tukiamini kuwa Mungu kashatusikia na sio kuanza kurudia rudia tena kile tulichokiomba kana kwamba Mungu hasikii,. kwa ufupi usiweke mfumo fulani unaoonyesha mrudio rudio katika kusali, kuwa huru mbele za Mungu ndivyo Sala zako zitakavyokuwa na thamani mbele za Mungu.

SWALI 2: Katika ule mfano wa wanawali kumi Bwana Yesu alioutoa katika mathayo 25, wanawali werevu walikuwa na mafuta katika taa zao pamoja na mafuta ya ziada lakini wale wapumbavu walikuwa na mafuta lakini hawana ya ziada. swali ni je! Haya mafuta ya ziada ni nini?


JIBU: Kama inavyoeleza wote walikuwa ni wanawali ikiwa na maana wote  ni wakristo wanaomngojea Bwana. Na yale mafuta waliokuwa nayo wote ni "Roho Mtakatifu". Lakini wengine walionekana kuwa na mafuta ya ziada, na wengine hawana.Hii inafunua aina mbili za wakristo watakaokuwepo siku za mwisho,
 AINA YA KWANZA: Hawa ni wale wakristo werevu waliopokea Roho Mtakatifu na kuruhusu Roho wa Mungu kufanya kazi ndani yao kwa kutaka kujifunza na kuendelea kupokea mafunuo ya Roho wa Mungu mpaka kufikia utimilifu, mtu wa dizaini hii kila siku anakuwa tayari kujifunza jambo jipya, hivyo anahama kutoka utukufu hadi utukufu kila siku kiu na bidii ya kuendelea kumjua Mungu inaongezeka, hafungwi na mifumo fulani ya dini au dhehebu, bali Neno la Mungu ndio taa yake, Hivyo basi Mungu anamfungulia mlango wa kufahamu mafunuo ya ziada (ile mana iliyofichwa, ufunuo 2:17) kutokana na jitihada yake ya kumtafuta Mungu hivyo basi inamfanya yeye kuwa watofauti na wakristo wengine. Kwahiyo hata Bwana atakapokuja atakuwa na NURU ya kwenda kumlaki hatakuwa gizani. 

AINA YA PILI: Hawa ni wale  wakristo wapumbavu ambao walishapokea Roho Mtakatifu (ambayo ndio yale mafuta kwenye taa zao) lakini sasa baada ya kupokea Roho wa Mungu wanamzimisha ndani kwa kutomruhusu tena aendelee kuwafundisha mambo mapya. kwasababu kazi ya Roho Mtakatifu ni kukuongoza katika kuijua kweli yote, soma Yohana 16:13" Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. ". Kwahiyo aina hii ya wakristo wanakuwa wameridhika na hali walionayo na mafundisho ya dini zao au madhehebu yao tu, hawataki kujifunza jambo jipya na wakiambiwa hata kama linatoka kwa Mungu hawatataka kusikia, kiu na bidii ya kuendelea kumjua Mungu hawana wanaridhika na mafundisho ya madhehebu yao tu. Hivyo basi wakati Bwana atakapokuja hawatakuwa na NURU ya kumtambua na kwenda kumlaki.  

Kwahiyo kama wewe ni mkristo fahamu jambo moja Mungu mpaka leo anatenda kazi anaongea, anatoa mafunuo mapya, anaonya, anawapasha watu habari ya mambo yajayo, na anawapa wale tu wanaompenda na kumtafuta kwa bidii na kutaka kuufahamu ukweli hao ndio atakaowafunulia, Ndugu fahamu tu UNYAKUO hautakuwa SIRI kwa watu wote, wale wapumbavu ndio hawatajua siku ya kuondoka, lakini wenye mafuta ya ziada watajua. Kwahiyo ukiwa kama mkristo kwa ulimwengu tunaoishi leo mtafute Bwana kwa moyo wako wote aendelee kujifunua kwako ili siku ile isikujie kama mwivi. kwahiyo usiwatazame hao wakristo wapumbavu wewe kuwa mwerevu kwa kumruhusu Roho Mtakatifu kuendelea kufanya kazi ndani yako.
SWALI 3:  Naomba kuuliza..ni nani anayetawala dunia kati ya Mungu na shetani? Na kama ni Mungu anayetawala kwa nini kuna matukio ya kutisha kama ajali mbaya za magari,ndege,mafuriko kama ya Japan kama Mungu ndiye anayetawala kwanini hayazuii anaacha yanaua watu??? Na ukisoma mathayo 4:1 na kuendelea unasoma shetani anamwambia Yesu dunia ni Mali yake, nataka kufahamu pia je! Kuna  tofauti gani kati ya dunia na ulimwengu nisaidie?


JIBU:
Dunia yote ni ya Mungu ukisoma; Zaburi 24: 1-2 "1 Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.
2 Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya mito ya maji aliithibitisha. "Na pia Bwana Yesu Kristo baada ya kufufuka kwake aliwaambia wanafunzi wake

 mathayo 28:18"Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. "Kwahiyo kwa maandiko hayo tunaona kabisa kuwa dunia yote inamilikiwa na Mungu na wala sio shetani, lakini "dunia sio ulimwengu". Huu ulimwengu ndio mali ya shetani na ndio yeye anayeumiliki na kitakachokuja kuteketezwa sio dunia bali ni ulimwengu huu mbovu wa shetani ambao ni milki yake aliyojijengea..


Tofauti kati ya dunia na ulimwengu ni hii;

  • Dunia ni vitu vyote vya asili na vya kijeografia unavyoviona  kama vile mabara, bahari, miti, milima, hewa, ardhi, mito,mabonde, visiwa,anga, n.k.

  • Na Ulimwengu ni ustaarabu uliobuniwa na aidha Mungu au shetani ili kuifanya dunia iwe na mantiki paonekane kama ni mahali pa kuishi. mfano. elimu, burudani, miziki, utawala, uchumi, mahakama,Milki, fahari, uchukuzi, mawasiliano,  n.k. Haya yote ni mambo yaliyobuniwa kuipa dunia muonekano unaoleta maana. Na ndio maana kwenye mathayo 4 shetani alimwambia Bwana Yesu nitakupa ULIMWENGU na fahari yake ukianguka kunisujudia.

Kwahiyo dunia itadumu siku zote, lakini ustaarabu uliowekwa na shetani (yaani ulimwengu )utaangamizwa utabaki tu ule uliowekwa na Mungu, na hata hivyo 99% ya ustarabu uliopo duniani leo hii unakaliwa na shetani na ndio maana siku ya Bwana itaharibu ustaarabu wote wa shetani na kuleta ustaarabu mpya wa Kristo hapa duniani huo ndio utakaodumu milele na  utakaokuwa ni ule utawala wa miaka 1000 ufunuo 19 & 20.


Na sababu ya Mungu kuruhusu mambo mabaya kutokea kama ajali, vimbunga, mafuriko ni kwasababu ya mambo maovu ya huu ulimwengu yaliyopo kama umwagaji damu, rushwa, uasherati, ulevi, uaribifu wa mazingira, ushoga, vita, n.k. mambo kama haya ardhi haiwezi ikavumilia, yanaiharibu  dunia na kupelekea gadhabu ya Mungu kumwaga juu ya nchi.
Tujitahidi tujiepushe na mambo ya ulimwengu huu yanayopita..Tuyatazame yaliyo juu.


Mungu akubariki

Ukiwa na swali, lolote unaweza ukatutumia, kwa neema za Bwana tutalijibu na kukutumia. Weka jina lako, na swali lako, tutakutumia kwa njia ile unayoitaka. (inbox, e-mail, whatsapp).

No comments:

Post a Comment