"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, December 16, 2017

BARAGUMU 7


Katika kile kipindi cha juma la mwisho la Danieli ambalo ni kipindi cha miaka 7 ya mwisho, kutakuwa na mambo mengi  sana  ya kutisha, ndani ya huu muda kutajumuisha Kipindi cha DHIKI KUU, na mapigo ya zile BARAGUMU SABA, na baada ya hii miaka 7 kuisha kitabu cha Danieli kinarekodi kutakuwa na siku nyingine 75 zitakazoongezeka, sasa ndani ya hizi siku 75 mbali na ile miaka 7  kitakuwa ni kipindi cha KIKOMBE CHA GHADHABU YA MUNGU kukumiminwa juu ya dunia yote kwa  vile VITASA SABA, kipindi hichi ndicho kinachoitwa SIKU YA BWANA.

Kumbuka biblia inaposema "siku ya Bwana" haimaanishi kuwa ni siku moja bali ni kipindi fulani cha wakati, ambacho Mungu amekitenga maalumu kwa ajili ya kujilipiza kisasi juu ya waovu wote wakaao juu ya nchi, sio kipindi cha kutamani kuwepo kabisa.

Je! zile BARAGUMU 7 zinazungumzia nini na zinamuhusu nani?


Siku zote baragumu ikipigwa ni ishara ya kujiweka tayari au kujiandaa kwa kitu kinachoenda kutokea kwa mfano baragumu inapopigwa vitani, askari wanajiweka tayari kwa vita wanavyokwenda kukumbana navyo, ni kama tu mbiu au kengele tunafahamu inapopigwa wanafunzi wanajiandaa kwa tukio fulani kusikia aidha dharura, au mwanzo wa vipindi au hatari au matangazo n.k. Vivyo hivyo Tunaona katika Ufunuo 8:2 wale  malaika 7 wakipewa BARAGUMU 7 kuzipiga juu ya nchi. Kwahiyo zile Baragumu wanazokwenda kuzipiga zinaashiria ONYO au TAHADHARI kwa mambo yanayokuja huko mbeleni na si nyingine zaidi ya HUKUMU YA MUNGU YA VILE VITASA 7 vitakavyomiminwa juu ya ulimwengu mzima.

Kwa maelezo mafupi zile Baragumu 4 za kwanza, zitaambatana na mapigo yatakayoletwa na wale MASHAHIDI WAWILI wa kwenye ufunuo 11, na zile Baragumu 3 za mwisho zitakuja baada ya wale manabii 2 kuawa yaani ndani ya kile kipindi cha miaka mitatu na nusu ya mwisho. Na pia mapigo haya ya Baragumu yanayoitangulia SIKU ILE YA BWANA yataathiri THELUTHI tu ya dunia lakini mapigo ya vile VITASA SABA yataathiri dunia nzima.
BARAGUMU LA KWANZA:

Ufunuo 8:6 Na wale malaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari ili wazipige. Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea. "

Jambo hili litatokea wakati wa wale mashahidi 2 wanapotoa unabii kwa wayahudi  Israeli, tunaweza tukasoma walipewa uwezo wa kufunga mbingu mvua isinyeshe katika siku za unabii wao, na kupiga nchi kwa kila pigo kila  watakapo, mfano wa jambo kama hili pia tunaona lilitokea kipindi cha Musa kwa yale mapigo aliyompiga Farao mojawapo ilikuwa ni ile mvua ya mawe iliyokausha mimea yote na mashamba yote katika nchi ya Misri,

Vivyo hivyo hawa nao wataipiga nchi kwa mapigo kama hayo hususani eneo la mashariki ya kati, lakini Mungu anafanya hivyo kwa lengo la watu watubu wamgeukie Mungu ili kuepuka hukumu inayokuja huko mbeleni. Hivyo theluthi ya dunia itakuwa na shida nyingi isiyokuwa ya kawaida, ukame, njaa, joto kali vitawatesa wengi taabu itakuwa kila mahali

Si ajabu hata wale manabii wawili baada ya kufa watu walifurahia kwasababu biblia inasema waliwatesa hao wakaao juu ya nchi.


BARAGUMU LA PILI:


Ufunuo 8:8 "Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto, kikatupwa katika bahari; theluthi ya bahari ikawa damu. 9 Wakafa theluthi ya viumbe vilivyomo baharini, vyenye uhai; theluthi ya merikebu zikaharibiwa. 

Mungu ataendelea kuipiga dunia kwa kupitia huduma za wale mashahidi wawili, tunaona biblia pia inasema walipewa amri ya kuigeuza bahari kuwa damu. Kama vile Mungu alivyoipiga nchi ya Misri kwa pigo la maji kuwa damu kwa mkono wa Musa, ndivyo itakavyokuwa katika hicho kipindi, theluthi ya maji ya dunia nzima itageuzwa kuwa damu. Hivyo viumbe vya majini kama samaki, nk vitaangamia vingi, na safari za majini nyingi zitasimama, kutokana na kwamba sehemu kubwa ya bahari itabadilika kuwa damu isiyoruhusu shughuli zozote za ubaharia, itachafuka sana. Hofu kuu itawaingia wanadamu wakiona mambo yanayotokea duniani.BARAGUMU LA TATU:


Ufunuo 8:10-11"
10 Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya theluthi ya mito, na juu ya chemchemi za maji.
11 Na jina lake ile nyota yaitwa Pakanga; theluthi ya maji ikawa pakanga, na wanadamu wengi wakafa kwa maji hayo, kwa kuwa yalitiwa uchungu. "


Tunaona hapa visima na chemchemi za maji nazo zinapigwa, kumbuka haya mapigo hayajamgusa bado mwanadamu ni vitu vya asili tu, Hivyo shida ya maji eneo kubwa la dunia itakuwepo kama maji yatatiwa uchungu mfano wa yale maji WANA WA ISRAELI waliyoyakuta kule jangwani jinsi yalivyokuwa hayanyweki mpaka mahali pale wakapaita "MARA" na ndivyo itakavyokuwa kipindi hicho, unaweza ukafikiria mahali hakuna mimea, bahari imekuwa damu na sasa hata maji ya mito yaliyobaki wametiwa uchungu, fikiria ni dhiki kiasi gani, na hapo bado ile hukumu KUU ya Mungu yenyewe haijaanza, hizi ni BARAGUMU tu kwa ajili ya kuonya hukumu ya Mungu inayokuja huko mbeleni ili watu watubu hususani wayahudi maana wakati huo kanisa litakuwa limeshanyakuliwa. Mambo haya watakuwa wazi dunia nzima ikiyatazama hata wale wanaosema Mungu hayupo, kipindi hicho watakuwa wanaomboleza.

BARAGUMU LA NNE:


Ufunuo 8:12" Malaika wa nne akapiga baragumu, theluthi ya jua ikapigwa, na theluthi ya mwezi, na theluthi ya nyota, ili kwamba ile theluthi itiwe giza, mchana usiangaze theluthi yake, wala usiku vivyo hivyo.. "

Hapa tunaona Mungu ataipiga tena theluthi ya jua na mwezi, na nyota visiangaze, kumbuka hapa jua halitazima lote kama itakavyokuja kuwa katika ile siku kuu ya ghadhabu ya BWANA ambapo jua litazimwa lote, na mwezi na nyota kuondolewa kuwa giza, Unaweza ukajenga picha theluthi ya jua ikipigwa, ni dhahiri kuwa nuru itafifia duniani, jua la saa 7 mchana litakuwa kama la saa 12 jioni, jiulize la saa 10 jioni litakuwaje? ni wazi kutakuwa na giza na baridi kali, na ile mimea inayohitaji mwanga wa kutosha itakufa, chakula kitakuwa cha shida nishati ya umeme duniani itapungua maisha yatakuwa ya taabu sana, sio kipindi cha kutamani kuwepo ndugu kama hujamkabidhi BWANA maisha yako leo ni vyema ukafanya hivyo kabla hizo siku za kutaabika hazijafika.

OLE! OLE! OLE!


Baada ya zile baragumu nne kupiga, sasa  biblia inasema..Ufunuo 8:13 Kisha nikaona, nikasikia tai mmoja akiruka katikati ya mbingu, akisema kwa sauti kuu, Ole, ole, ole wao wakaao juu ya nchi! Kwa sababu ya sauti zisaliazo za baragumu za malaika watatu, walio tayari kupiga. " Kumbuka mapigo manne ya kwanza hayakumgusa mwanadamu lakini haya yaliyosalia yanamhusu mwanadamu na mifumo yake. Na hizi ole tatu (ambazo ndio zile baragumu tatu za mwisho ) zitakuwa kati ya kile kipindi cha miaka mitatu na nusu ya mwisho yaani kipindi cha DHIKI KUU.OLE WA KWANZA:

BARAGUMU LA TANO:


Ufunuo 9:1-11"1 Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu.
2 Akalifungua shimo la kuzimu; moshi ukapanda kutoka mle shimoni kama moshi wa tanuru kubwa; jua na anga vikatiwa giza kwa sababu ya ule moshi wa shimoni.
3 Nzige wakatoka katika ule moshi, wakaenda juu ya nchi, wakapewa nguvu kama nguvu waliyo nayo nge wa nchi.
4 Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu cho chote kilicho kibichi, wala mti wo wote, ila wale watu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao.
5 Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe miezi mitano. Na maumivu yao yalikuwa kama kuumwa na nge, aumapo mwanadamu.
6 Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia.
7 Na maumbo ya hao nzige yalikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita, na juu ya vichwa vyao kama taji, mfano wa dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama nyuso za wanadamu.
8 Nao walikuwa na nywele kama nywele za wanawake. Na meno yao yalikuwa kama meno ya simba.
9 Nao walikuwa na dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani.
10 Nao wana mikia kama ya nge, na miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia yao.
11 Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni. "

Sasa tunaona pigo hili limeachiliwa kwa ajili ya wanadamu, wale nzige wanaozungumziwa pale sio nzige kama nzige bali ni MAPEPO yatakayoachiliwa kutoka kuzimu na mfalme wao ni malaika wa kuzimu (Abadoni yaani shetani), kwasasa haya mapepo hayajaanza kufanya kazi duniani kwasababu biblia inasema YUPO AZUIAYE, ambaye ni Roho Mtakatifu kumbuka maasi tunayoyaona leo duniani ni matokeo ya kazi ya mapepo machache sana, utakuja wakati jopo jipya la mapepo maovu kushinda haya yatafunguliwa, duniani kutatokea tabia ambazo hazijawahi kuonekana, watu watapagawa kwa namna ambazo hazipo, tabia chafu za wanadamu zitazidi, magonjwa mapya yasiyojulikana, mkandamizo mkubwa wa mawazo yatakayoletwa na hayo mapepo utawaingia watu, hofu, na mashaka yasiyo ya kawaida biblia inasema

Luka 21:25  "Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake;
26 watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika. "


Watu wataona ni heri kufa kuliko kuishi lakini biblia inasema kifo kitawakimbia...Ni mambo ya kutisha na ya ajabu yanakuja huko mbeleni. Haya mapepo yaliyofananishwa na hao nzige yataleta vurugu na mikanganyiko katika ngazi zote kuanzia mtu binafsi, familia, na taifa, kwa wale wasiokuwa na muhuri wa Mungu katika vipaji vya nyuso zao.


OLE! WA PILI:

BARAGUMU LA SITA:


Ufunuo 9:12 Ole wa kwanza umekwisha pita. Tazama, bado ziko ole mbili, zinakuja baadaye.
13 Malaika wa sita akapiga baragumu, nikasikia sauti moja iliyotoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu,
14 ikimwambia yule malaika wa sita aliyekuwa na baragumu, Wafungue nao malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Frati.
15 Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu.
16 Na hesabu ya majeshi ya wapanda farasi ilikuwa elfu ishirini mara elfu kumi; nilisikia hesabu yao.
17 Hiyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao waliokaa juu yao, wana dirii kifuani, kama za moto, na za samawi, na za kiberiti; na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoka moto na moshi na kiberiti.
18 Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kiberiti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao.
19 Kwa maana nguvu za hao farasi ni katika vinywa vyao, na katika mikia yao; maana mikia yao ni mfano wa nyoka, ina vichwa, nao wanadhuru kwa hivyo.
20 Na wanadamu waliosalia, wasiouawa kwa mapigo hayo, hawakuzitubia zile kazi za mikono yao, hata wasiwasujudie mashetani, na sanamu za dhahabu na za fedha na za shaba na za mawe na za miti, zisizoweza kuona wala kusikia wala kuenenda.
21 Wala hawakuutubia uuaji wao, wala uchawi wao, wala uasherati wao, wala wivi wao. "


Baragumu hili linafungua njia kwa ajili ya ile vita ya HARMAGEDONI itakayopiganwa kati ya mataita yote ulimwenguni yakiongozwa na yale mataifa kutoka mawio ya jua, dhidi ya Mungu mwenyezi, yale mapepo yaliyofunguliwa katika lile baragumu la tano, sasa yanawaeleka wakuu wa mataifa na yule mnyama kwa ajili kuleta vita dhidi ya Mungu mwenyezi.

Wale farasi wanaashiria nguvu za kijeshi, na katika vivywa vya wale farasi hutoka moshi, na moto na kiberiti, ni dhahiri kabisa hizo ni dhana za kivita kama vile vifaru, makombora ya masafa marefu na mabomu ya nyuklia. Na wale wapanda farasi idadi yao ni milioni 200, ni wanajeshi wengi sana, lakini mwanakondoo atawashinda hawa wote katika ile vita ya harmagedoni kwa kuwa yeye ni BWANA WA MABWANA, na MFALME WA WAFALME.
Lakini pamoja na mapigo hayo yote biblia inasema hawatatubia maovu yao na ibada zao za sanamu, na ndio maana ile SIKU YA BWANA ni lazima ije.


OLE WA TATU:
BARAGUMU LA SABA:


Ufunuo 11:14-19"
14 Ole wa pili umekwisha pita, tazama ole wa tatu unakuja upesi.
15 Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele.
16 Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vya enzi vyao wakaanguka kifulifuli, wakamsujudia Mungu
17 wakisema, Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umeutwaa uweza wako ulio mkuu, na kumiliki.
18 Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na wa kuwapa thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu, na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi.
19 Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua ya mawe nyingi sana. "


Barugumu la mwisho ambalo litapigwa karibia na mwishoni mwa ile miaka 7, lenyewe litatangaza utawala unaokuja wa YESU KRISTO na hukumu ya ghadhabu ya Mungu aliyokuwa ameiandaa kwa hao waiharibuo nchi, baada ya malaika huyu wa mwisho kupiga Baragumu, kitakachofuata ni hawa hawa malaika 7 kujiandaa kuchuka vile VITASA 7 vilivyojaa ghadhabu ya Mungu ili kuvimwaga juu ya nchi, Hivyo baragumu hii ya saba inatangaza kuwa mwisho wa mpango wa wokovu wa Mungu kwa wanadamu umekwisha kilichobaki ni  kuwaangamiza waovu wote na kuwapa thawabu wenye haki.

 Kwa mwendelezo wa vitasa saba ambavyo katika hivyo ghadhabu ya Mungu imetimia unaweza ukasoma kupitia link hii..>>>https://wingulamashahidiwakristo.blogspot.com/2017/05/siku-ya-bwana-inayotisha-yaja.html#links

Hivyo ndugu usidanganyike kwamba unyakuo bado sana, UNYAKUO upo karibuni kutokea, mpinga-kristo anaiandaa chapa yake, biblia inasema .."pale wanaposema kuna amani ndipo uharibifu unapokuja kwa ghafla"..Unaweza kuona leo kama kuna amani( japo ni amani feki), lakini mambo hayo yote biblia iliyoyatabiri yakuja ghafla.

Hivyo umejiandaaje? umebatizwa  kwa ubatizo sahihi na kupokea Roho Mtakatifu? ..Kama Bwana akija kulichukua kanisa lake utakuwa miongoni mwa hao watakaoenda?. Maombi yangu ni ugeuke mapema umtazame Kristo kabla siku za hatari na za kutisha hazijafika.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment