"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, December 27, 2017

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 20

SWALI 1:  kumekuwa na mjadala mkubwa kati ya wakristo kuhusu suala la sabato,Wapo,wanaosema j2 na pia wapo wa jmosi..je! ni wapi walio sahihi?


JIBU:Neno la Mungu linasema Mungu ni Roho nao wamwabuduo imewapasa wamwabudu katika roho na kweli. Wakristo hawahesabiwi haki mbele za Mungu katika siku, miezi au miaka ya kuabudia, aidha uabudu j2, j3, jmosi au j5 huo ni utaratibu wako tu! haimuongezei mtu chochote katika uhusiano wake na Mungu. Biblia inasema..

wagalatia 4:9 "Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. "

Na Pia inasema tena.....

Wakolosai 2:16 "Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO;  mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.

Hivyo Maana ya NENO sabato ni "pumziko", na pumziko kwa wakristo lipo rohoni, na Yesu ndiye BWANA wa sabato hivyo ukimpata YESU umepata SABATO au "pumziko la rohoni" na ndio maana anasema.. mathayo 11:28

"28 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami NITAWAPUMZISHA.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi. "

Kwahiyo wanaoabudu jmosi, au j2 au j3 hawafanyi makosa, ni utaratibu wao tu, kwa mfano tunasoma katika biblia wakristo wakwanza waliiteua siku ya kwanza ya juma ( yaani JUMAPILI) kwa ajili ya kukusanyika na kufanya changizo pamoja na kumega mkate,soma  matendo 20:7 pia 1wakoritho 16:1-2, kwahiyo sio shida kwa mantiki hiyo  lakini ibada halisi ipo rohoni na Mungu anaabudiwa katika roho na kweli, na sio katika siku maalumu au miezi au miaka bali ni kila saa na kila wakati.


 SWALI 2:Mpendwa habari katika mambo yanayo niumiza sana kichwa ni suala KUZIMU ,hivi kuzimu wanaishi watu au kukaa na je Watu hupata mateso? zipo shuhuda nyingi zinazo nigusa moyo wangu kuhusu kuzimu.
JIBU: Kuzimu ipo, na ni sehemu iliyo halisi kabisa...
Mtu anapokufa katika dhambi (yaani haujaoshwa dhambi zake kwa damu ya YESU KRISTO)..mtu anaenda  moja kwa moja kuzimu/jehanum, huko kuna mateso mengi sana, mtu huyo atakaa huko akingojea ufufuo wa wafu, ambao utakuja baada ya ule utawala wa YESU KRISTO wa miaka 1000 kuisha ambapo wafu wote watafufuliwa na kuhukumiwa mbele ya kile kiti cheupe cha Hukumu..
Ufunuo 20: 12 "Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.
13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.
15 Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto".

Ukisoma pia Yohana 5:28 BWANA YESU aliyasema maneno hayo.." Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.
29 Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. "

Unaona wale wanaotenda mabaya wote watafufuliwa kwa ufufuo wa hukumu, hivyo baada ya kuhukumiwa kulingana na matendo yao ndipo watakapotupwa kwenye lile ZIWA LA MOTO atakapokuwepo shetani na malaika zake, lenye mateso mengi kuliko jehanum. ni kama tu vile mtu anapokamatwa na hatia anawekwa kwanza mahabusu kwa muda fulani akisubiria kupandishwa mahakamani, sasa akishahukumiwa mahakamani kulingana na makosa yake ndipo anapopelekwa magereza kutumikia makosa yake. na ndivyo itakavyokuwa kwa waovu wote walioikataa neema ya msalaba wa Bwana YESU KRISTO watakapokufa sasa hivi wataenda kuzimu kwenye vifungo na mateso, wakingojea hukumu ya mwanakondoo kisha baadaye watatupwa kwenye lile ziwa la moto.

Lakini wanaokufa sasa katika haki, wanapelekwa mahali panapoitwa  "Paradiso" . Paradiso ni mahali panapofanana na mbinguni,lakini sio mbinguni, ni mahali pa raha, wanawekwa humo kwa muda fulani wakingojea ufufuo wa wenye haki, atakapokuja Bwana mawinguni, watafufuliwa na kuvaa miili ya utukufu na kuungana na watakatifu walio hai na kwa pamoja kwenda na Bwana mbinguni kwenye karamu ya mwana kondoo.

1 Wathesalonike 4: 15 "Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.
16 Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.
17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele."


SWALI 3:Mtumishi nakuomba unipe majibu ya haya maswali, 1).Inaruhusiwa Kula nyama ya Nguruwe kwa Mkristo wa Kweli?  2).Mkristo wa Kweli Anaruhusiwa Kunywa Pombe/kuvuta sigara? 3).Ubatizo Wa Mkristo Wa Kweli Ni Wa Namna Gani?


JIBU:1) Hakuna tatizo lolote kula nyama ya nguruwe au chakula chochote ambacho mtu anaweza kukipokea kwa shukrani mbele za Mungu...biblia inasema viumbe vyote vimetakaswa na Mungu, Tukisoma  1Timotheo 4:1-5 inasema.. "Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;
2 kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;
3 wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru WAJIEPUSHE NA VYAKULA, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.
4 Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani;
5 kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba. "

Hivyo vyakula vyote ni halali lakini biblia inasema tule kwa IMANI, ila tukila kwa mashaka ni dhambi, na pia biblia inasema anayekula asimuhukumu asiyekula, wala asiyekula asimuhukumu anayekula, haupaswi kumkwaza mwenzako kwa ujuzi wako, ukimkosea mwenzako kisa hali nguruwe ni sawa na kumkosea Kristo mwenyewe 1wakorintho 8:13 inasema "Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu."....."8 Lakini chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu; maana, tusipokula hatupunguziwi kitu, wala tukila, hatuongezewi kitu.
Na pia tukisoma warumi 14:14 -17 "Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi.
15 Na ndugu yako akiingia huzuni kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.
16 Basi, huo wema wenu usitajwe kwa ubaya.
17 Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.

2) Mkristo wa kweli haruhusiwi kunywa pombe wala kuvuta sigara wala kuuharibu mwili wake kwa namna yoyote ikiwemo kuchora alama kwenye miili, kwasababu biblia inasema miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu, hivyo hekalu la Mungu lazima liwe ni safi,

3) Kuhusu ubatizo, ubatizo sahihi kulingana na maandiko ni wa kuzamishwa katika maji mengi, na inapaswa iwe ni kwa JINA LA YESU KRISTO, na sio kwa jina la BABA na Mwana na Roho Mtakatifu, kama inafanyika kimakosa na makanisa mengi, kwa ufafanuzi mrefu kuhusu UBATIZO SAHIHI fuata link hii.>>>https://wingulamashahidiwakristo.blogspot.com/2016/09/ubatizo-sahihi_28.html#links




SWALI 4: Kuna aina ngapi za ubatizo?

JIBU: Kuna aina 3 za ubatizo kulingana na maandiko ,wa kwanza ni-ubatizo wa maji, wapili ni ubatizo wa Roho mtakatifu, na watatu ni ubatizo wa moto (Mathayo 3:11)....huu ubatizo wa moto unafuata baada ya kupokea Roho mtakatifu ambapo Mungu anampitisha mtu katika majaribu mbalimbali  ili kuiweka imara imani yake huyo mtu, ndio usishangae mtu akishakuwa mkristo kuanza kukutana na changamoto mbalimbali mfano kutengwa na marafiki,au ndugu, kudhihakiwa imani yako, wakati mwingine mipango yako ya mwanzo yote inavurugika, wakati mwingine misiba, dhahabu ili ing'ae lazima ipitishwe kwenye moto, na sisi tunafananishwa na dhahabu safi mbele za Mungu, na pia Bwana Yesu alisema Marko 9:49" Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto". ...sasa huo ndio ubatizo wa moto Mungu anaompitisha mtu ili kuuondoa uovu na kumnyenyekeza mbele zake na kumweka katika njia ya kusudi lake..lakini ni kwa muda tu, Mungu akishakwisha kukutengeneza anakufanya uwe chombo bora kwa kazi yake.


SWALI 5:  BWANA YESU asifiwe! Naomba kuuuliza swali.
Hivi ni kweli kwamba, ukimuombea mtu aliye uawa na wachawi anaweza kurudi tena??? Na Je, utakitambuaje kifo halisi au cha kiini macho????

 
JIBU: Mchawi anapokuua ni sawasawa na mtu yeyote anavyoweza kukuua wewe, au jambazi kumuua mtu asiyekuwa na hatia..wote wanao uwezo wa kusababisha kifo halisi  kwa mtu

Lakini kuna vifo vingine vinaonekana kama ni vifo halisi lakini kumbe sio, unakuta huyo mtu bado anaishi sehemu nyingine hajafa, watu wanawaita misukule n.k sasa hawa hawajafa bali wamehamishwa tu, na wanaweza kurudishwa kwa njia ya maombi kwa jina la Yesu.
Na pia kuhusu namna ya kutambua kama ni kifo halisi au kiini macho hayo ni mambo ya rohoni ambayo Bwana anaweza akakufunulia au asikufunulie, na kama hujafunuliwa na BWANA lakini wewe ukahisi tu, jambo ni moja tu, kuomba kwa imani maana biblia inasema yote yanawezekana kwa yeye aaminiye ..hapo haijalishi amechukuliwa kwa kiini macho au amekufa kifo halisi, atarudi tu!..lakini hayo yote yanafanyika kwa imani, vinginevyo hakuna lolote litakalotokea.

Ubarikiwe na BWANA YESU.

1 comment:

  1. Asante sana kwa majibu mazuri ila rudia kujibu swali kuhusu ubatizo. Soma Mathayo 28:19.
    Hakuna ubatizo batili iwapo mtu akitubu na kumkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake. Kuhusu Maji mengi kwa ulimwengu wa sasa sio salama maana kuna magonjwa mengi mfano magonjwa ya ngozi na fungus kichwani. Na kama ni lazimakubatizwa maji mengi vipi kwa wale wanaookoka jangwani au wagonjwa wasiojiweza ?? Na kama ni lazima maji mengi basis ni lazima Yordani na sio kila maji mengi.

    Warumi 10:4 " kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria ili kila amwaminiye ahesabiwe haki"

    ReplyDelete