"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, January 16, 2018

MAELEZO JUU YA UFUNUO 21.



Bwana YESU KRISTO atukuzwe, Karibu katika mafunzo ya kitabu cha Ufunuo, leo tukiwa katika ile sura ya 21,

Tukisoma..

Mlango 21:1-8

1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.
2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.
3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.
4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.
5 Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.
6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.
7 Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.
8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili. 
Sura hii inaelezea juu ya MBINGU MPYA NA NCHI MPYA, ikiwa na maana kuwa hapo mwanzo kulikuwa na mbingu ya zamani na nchi ya zamani, na hizi si nyingine zaidi ya hizi zilizopo sasa, kama mtume Petro alivyosema katika 2Petro 3:5-6"...
 Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;
6 kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.
7 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.
8 Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.
9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.
10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.
11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa,
12 mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka?
13 Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia MBINGU MPYA NA NCHI MPYA, ambayo haki yakaa ndani yake.
14 Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake. "

Kwahiyo kwa maneno hayo tunaona dunia ya wakati ule wa Nuhu iliangamizwa kwa maji, vivyo hivyo na hii dunia tuliyopo sasa itaangamizwa kwa moto, kisha ndio ije mbingu mpya na nchi mpya ambaye HAKI yakaa ndani yake. Kumbuka DUNIA haitakunjwa kunjwa kama karatasi na kutupwa kuzimu kama watu wengine wanavyofikiria, hapana bali itakuwa ni dunia hii hii isipokuwa itarekebishwa na kurejeshwa katika utukufu usioneneka ambao Mungu alishaukusudia kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, Hivyo Dunia hii ndiyo makao ya mwanadamu ya milele, Mbinguni tutakaa kwa kitambo tu, kisha tutarudi kutawala na Kristo hapa duniani milele.

Mbingu mpya na nchi mpya itakuja mara baada ya ule utawala wa miaka 1000 kuisha, vilio, misiba, mauti, uchungu, biblia inasema havitakuwepo tena, kwasababu shetani atakuwa ameshatupwa katika lile ziwa la moto pamoja na waovu wote, huko ng'ambo kutakuwa na mambo mapya kabisa ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia, Vitu kama Bahari havitakuwepo tena, Mambo mazuri yasiyoneneka yatakayokuwepo huko, itapelekea hata zile taabu za kwanza zisiingie akilini. Ndugu sio sehemu ya kukosa, uchungu hautakuwa kwasababu utaangamizwa milele, uchungu utakuja pale utakapogundua unayakosa mambo matamu ya Mungu ya umilele.

Lakini tukisoma mstari wa 2, tunaona jambo jingine..." Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe." .. Mstari huu unafunua kuwa huu mji mtakatifu si mwingine zaidi ya BIBI-ARUSI, na ndio maana ukisoma mstari wa 9-10 tunaona jambo hilo likiendelea kwa urefu,"
"9 Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule BIBI-ARUSI MKE WA MWANA-KONDOO,
10 Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule MJI MTAKATIFU, YERUSALEMU, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; 
"..Unaona hapo Yohana alionyeshwa bibi-arusi mke wa mwana-kondoo mfano wa MJI.

Kwahiyo hii YERUSALEMU MPYA inayozungumziwa hapo ni BIBI-ARUSI wa Kristo na sio mji tu kama mji mfano wa Ninawi au Nazareti. Kumbuka mji huu Mungu amekuwa akiuundaa tangu vizazi na vizazi, na Mungu hakai katika maskani yenye muundo wa mfano wa kibinadamu, bali maskani ya Mungu ni KANISA lake TAKATIFU, kama tunavyosoma katika waefeso 2:19-22" 
19 Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.
20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni JIWE KUU LA PEMBENI.
21 Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe HEKALU TAKATIFU katika Bwana.
22 Katika yeye ninyi nanyi MNAJENGWA PAMOJA KUWA MASKANI YA MUNGU KATIKA ROHO. "
Kwahiyo sisi kwa pamoja, (wakristo) tunajenga mwili mmoja maskani ya Mungu ambayo yeye mwenyewe anakaa ndani yake, na ndio mji ambao Ibrahimu aliuona tokea mbali akasema..Waebrania 11:8 Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia MJI WENYE MISINGI, AMBAO MWENYE KUUBUNI NA KUUJENGA NI MUNGU.". Hivyo upo mji wenye misingi ambao Mungu anaundaa.

Na pia tunaona Mtume Paulo kwenye wagalatia 4, akifananisha wakristo kama watoto wa ile Yerusalemu ya mbinguni iliyofananishwa na Sara, Wagalatia 4:25-31
25 Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa anatumika pamoja na watoto.
26 Bali YERUSALEMU WA JUU NI MWUNGWANA, naye ndiye mama yetu sisi.
27 Kwa maana imeandikwa, Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; Paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu; Maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi Kuliko wa huyo aliye na mume.
28 Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi.
29 Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.
30 Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana.
31 Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, BALI TU WATOTO WA HUYO ALIYE MWUNGWANA. " . Mtume  Paulo pia alionyeshwa hilo kwamba watakatifu ni watoto wa ahadi wa ule mji utokao juu(Yerusalemu mpya.)

Hivyo kwa mistari hiyo mpaka hapo tunaweza kupata picha kuwa MJI MTAKATIFU YERUSALEMU MPYA ambao Mungu alikuwa akiiunda kwa muda mrefu sio makasri ya kifahari na barabara nzuri zenye kupendeza bali hayo yote ni picha inayoelezea uzuri wa wateule wake bibi-arusi safi asiye na mawaa aliyemnunua kwa thamani ya damu yake mwenyewe.

Sasa tukiendelea na mistari inayofuata katika ile sura ya 21 tunasoma..

     
 
  Mlango 21:9-14 
9 Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo.
10 Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu;
11 wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri;
12 ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli.
13 Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu.
14 Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.

Kama tunavyosoma hapo juu mji huu unaonekana wenye misingi 12, na wenye majina 12 ambao ni mitume 12 wa Bwana Yesu Kristo, kumbuka kama tulivyotangulia kusoma kwenye Waefeso 2:20 inasema.."Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni". Hivyo hawa waliojengwa juu ya huu msingi wa mitume na manabii ni sisi watu wa mataifa, lakini pia kuna wayahudi ambao ni wazao wa ahadi ambao pia walikuwa wakiutazamia mji huu, vivyo hivyo nao walijengwa juu ya wale wana 12 wa Yakobo, ambao kwa ujumla wanatengeneza taifa la Israeli, Hivyo wote kwa pamoja (yaani wakristo na wayahudi ) wataunda ile YERUSALEMU MPYA ya mbinguni. Na ndio maana ule mji hapo unaonekana ukiwa na msingi 12, na milango 12 ambao ni mitume 12 na wana 12 wa Yakobo.

Tukiendelea....    


        MLANGO 21:15-17

15 Na yeye aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu, apate kuupima huo mji, na milango yake, na ukuta wake.
16 Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa.
17 Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia na arobaini na nne, kwa kipimo cha kibinadamu, maana yake, cha malaika.

Tunaona picha nyingine hapa huu mji unaonekana ukipimwa, na vipimo vyake vinaonekana kuwa ni sawasawa, havijazidiana,wala kupungukiana kuashiria kwamba uko sawa umejengwa katika utashi wa hali ya juu hivyo ni wa kudumu milele, lakini kama ungepimwa na kuonekana umepunguka, HAKIKA usingedumu milele, ungeanguka tu kama BABELI Mji ule mkuu ulivyopimwa na kuonekana umepunguka, ukaanguka. ukisoma Danieli 5:24-28" Ndivyo Babeli ilivyoanguka kwasababu vipimo vyake vilionekana vimepunguka, lakini mji huu mtakatifu ambao Mungu ameubuni na kuujenga kwa muda mrefu VIPIMO VYAKE VIPO SAWASAWA, HALELUYA.!!!. na ndio tunafahamu kwanini biblia inasema huko hakitaingia KINYONGE.
Kwasababu mji huo(bibi-arusi) ni mkamilifu.

Tukimalizia kusoma..  



     MLANGO 21:18-27

18 Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi.
19 Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi;
20 wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto.
21 Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu.
22 Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake.
23 Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.
24 Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake.
25 Na milango yake haitafungwa kamwe mchana; kwa maana humo hamna usiku.
26 Nao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yake.
27 Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.

Amen.

Na kama inavyoonekana mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuangaza, bali UTUKUFU wa Mungu huutia nuru ikiwa na maana kuwa hili kundi linalounda BIBI-ARUSI wa Kristo litapelekwa katika kiwango kingine kikubwa cha UTUKUFU, Kumbuka duniani wakati huo watakuwepo watu wengine wa kawaida, mbali na bibi-arusi, watu hawa watakuwa wametoka katika kumshinda shetani katika ule utawala wa miaka 1000, na baadhi ya waliohukumiwa katika hukumu ya kiti cheupe ambao majina yao yalionekana katika kile KITABU CHA UZIMA. kundi hili ni mbali na BIBI-ARUSI, hawa ndio watakaotawaliwa na kuleta heshima na utukufu kwa Mungu kupitia BIBI-ARUSI wake(Ambaye ndiye YERUSALEMU MPYA).
 

Kwahiyo bibi-arusi pekee ndiye atakayezichukua siri za Mungu na kuwafundisha mataifa pamoja na hayo utukufu wa miili yao itakuwa ni tofuauti sana na wale wengine, hawa watakuwa na uwezo na ujuzi mwingine wa kipekee kutoka kwa BWANA.

Hivyo ndugu kundi linalounda bibi-arusi wa Kristo ni dogo sana, ni wale tu wanawali werevu waliokwisha kuweka taa zao tayari pamoja na mafuta ya ziada kwenda kumlaki BWANA wao, Huu ni wakati wa kuyaangalia tena maisha yako na kujiweka sawa, Bwana yupo mlangoni kuja na mwanawali mwerevu tu, ndiye atakayemlaki BWANA, na baada ya hapo mlango utafungwa, (Mathayo 25). Biblia inasema Luka 13:23" Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia,
24 Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.
25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; "
    
 
JE! HAPA BWANA ALIMAANISHA NI MLANGO UPI TUJITAHIDI KUUINGIA?
Jibu: ni kuingia katika milango ya MJI WA YERUSALEMU MPYA ambaye ni bibi-arusi safi. kwasababu itafika wakati nafasi ya kuwa bibi-arusi haitakuwepo tena.. Ufunuo 22:14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na KUINGIA MJINI KWA MILANGO YAKE. Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya. "

Kama tulivyosoma hapo juu biblia inatuambia:

7 Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.

Hivyo maombi yangu sisi sote tufanye bidii tuwe mojawapo wa bibi-arusi wa Kristo.

AMEN!
Mungu akubariki.

2 comments: