Kuna namna nyingi watu wanavyompokea YESU katika maisha yao, lakini sio namna zote zina manufaa kwa ajili ya uzima wa mtu. Ni muhimu sana kufahamu kusudi la msingi la Bwana Yesu lililomfanya aje duniani vinginevyo utadhani kwamba unatembea na Mungu kumbe Hayupo na wewe.
Tunaweza tukajifunza baadhi ya mifano katika biblia: Mahali fulani Petro alipokuwa anavua samaki, katika kuhangaika kwake usiku kucha bila kuwa na matumaini ya kupata chochote alimuona mtu anakuja asiyemfahamu na kuanza kufundisha watu kando kando ya Habari pembezoni mwa chombo chake, kisha alipomaliza akamwambia Petro tweka ukavue samaki vilindini, pengine Petro alimuona kuwa ni mtu wa Mungu hivyo akaona ayatii yale maagizo, lakini walipofika hata sio mbali, walipata samaki wengi sana kimiujiza kiasi cha nyavu kuweza kukatika, mpaka iliwabidi waombe msaada kwa wavuvi wenzao waliokuwa kando kando yao, nao pia wakajaza vyombo vyao kwa wingi wa samaki wale.
Lakini je! jambo gani lilitokea baada ya hapo?
Tunasoma;
Luka 5:4-11" Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;7 wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.8 Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, ONDOKA KWANGU, KWA KUWA MIMI NI MTU MWENYE DHAMBI, BWANA.9 Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata;10 na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.11 Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, WAKAACHA VYOTE WAKAMFUATA.
Hapo ni jambo gani tunajifunza? Petro baada ya kuona ule muujiza wa samaki saa hiyo hiyo alijisalimisha kwa Bwana na kumwambia, ondoka kwangu mimi ni mwenye dhambi!!..muujiza ule ulimfanya ajihukumu maisha yake akijua kuwa ni Mungu amesimama mbele yake na kusema naye, na zaidi ya yote aliacha hata ile kazi aliyokuwa anaifanya pamoja na wale samaki aliowapata na kumfuata YESU , Lakini kwa mtu mwingine asiyekuwa na ufahamu angechukulia lile tendo kuwa ndio FURSA ya kumtumia YESU kama chombo cha baraka katika kazi zake za uvuvi, kama wanavyofanya watu wengi leo.
Mtu angesema Mungu kaona mateso yangu ya kuteseka kwangu usiku kucha na leo hii kanikumbuka na kunibariki..Angesema leo hii Mungu kajifunua kwangu nimemuona biashara yangu inafanikiwa, Bwana kanipa utajiri jana tu nilikuwa maskini leo nimekuwa tajiri, Bwana kawaaibisha maadui zangu, Nimeuona mkono wa Mungu katika maisha yangu mtaji wangu umeongezeka... Lakini kumbuka kwa PETRO haikuwa hivyo, hakuona hayo mambo kwa BWANA, alijua kuwa ile ishara sio kwa ajili ya tumbo lake bali ilikuwa kwake kama chachu ya yeye KUMTAZAMA KRISTO. Na ndio maana tunaona baada ya hapo alifikia mpaka hatua ya kuacha vyote na kumfuata YESU.
Lakini tunaweza tukajifunza pia katika kundi lingine la watu, na hili tunasoma habari zake katika kitabu cha Yohana 6:1-32. Watu hawa walitendewa muujiza unaofanana na ule wa Petro isipokuwa hawa Bwana aliwagawanyishia mikate 5 na samaki 2 kwa maelfu yao, Lakini walipoona ile ishara walitaka kwenda kumshika wamfanye mfalme, sio kwasababu awe mfalme kwao ili waokolewe bali kwasababu waliona kama akiwa mfalme wao atawasaidia katika vipindi vya njaa na vigumu kwa kuwashushia chakula kimujiza kama vile Musa jangwani. Ni sawa tu na sasa hivi watu wanamtafuta Bwana Yesu ili awavushe tu katika vipindi vyao vigumu na si zaidi ..Tunasoma
Yohana 6:24-27"24 Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu.25 Hata walipomwona ng'ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?26 Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ISHARA, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.27 Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu. "
Hiyo ndio sababu YESU aliwakimbia, hakuambatana nao, kwasababu walikuwa wanaangalia TUMBO na sio BWANA. Walimchukulia kama yeye ni fursa ya kuwafanikisha katika mambo yao lakini mambo mengine zaidi ya hapo hawakutaka,
Lakini tunaona wakati mwingine Bwana alimponya kipofu mmoja aliyekuwa vile tangu kuzaliwa kwake, na baada ya kuponywa alijua tu ni YESU amemponya ila hakumwona, lakini kwa kuzidi kutaka kumjua na kuushikilia ushuhuda wake mpaka walipomfukuza nje ya sinagogi kwasababu ya kiu yake kwa YESU, ndipo YESU akamjia na kujifunua kwake na kumjua, lakini hapo kabla alikuwa hamjui japo aliponywa na yeye(Yohana 9).
Vivyo hivyo katika maisha ya sasa, Bwana anawatendea miujiza watu wengi lakini hawatambui kwanini Mungu anawatendea hiyo miujiza, wanadhani kwa kuwatendea hivyo ni Mungu kajifunua kwao! Hapana, miujiza ni kitu(chambo) cha kuwafanya watu wamgeukie yeye, hivyo kusudi kubwa la yeye kufanya hivyo ni kuwafanya watu watubu, au wazidi kumsogelea karibu na sio kuwarahisishia mambo tu.
Mungu anapokuponya ugonjwa wako, hapo Bado haujamwona Mungu, Mungu kukufanikisha katika kazi za mikono yako, hapo bado haujamwona Mungu, ni sawa na wale waliovunjiwa mikate nyikani, wakala wakashiba na kuishia hapo hapo, Bwana kukufaulisha katika mambo yako hapo bado haujampata yeye, mpaka pale utapotambua maana ya yeye kukunyooshea mkono wake ni ipi?. Siku utakapotambua UTATUBU na KUJINYENYEKEZA MBELE ZA BWANA..utafikia mahali na kusema kama Petro alivyosema..ONDOKA KWANGU MIMI NI MWENYE DHAMBI, kuonyesha kuwa haustahili mbele zake..Ukilijua hilo hautatamani hata vile vitu alivyokubariki navyo bali yeye tu wala hautamchukulia Bwana kwa jinsi unavyomchukulia leo.
Bwana aliyesema fedha na dhahabu ni mali yangu, ndiye huyo huyo alisema "ITAKUFAIDIA NINI UUPATE ULIMWENGU MZIMA NA KUPATA HASARA YA NAFSI YAKO?". Kumbuka kusudi la msingi kabisa la Bwana Yesu kuja hapa duniani sio kutufanya sisi kuwa mabilionea, au kutuponya magonjwa yetu, au kutufanikisha katika mambo yetu, hapana bali ni KUTUOKOA sisi kutoka katika dhambi, kama tafsiri ya jina lake lilivyo {YESU= YEHOVA MWOKOZI}, ndipo mambo mengine yafuate.
Hivyo ndugu ishara na miujiza yote Mungu anayokutendea leo, ni kukufanya wewe utubu, akuponye roho yako, kumbuka Bwana ataanza tu KUJIFUNUA KWAKO pale utakapoamua kumruhusu afanye kazi katika maisha yako, lakini ukiangalia KIGANJA CHAKE tu atakupa nini! atakukimbia kama alivyowakimbia wale wasamaria hivyo ule wokovu hautafunuliwa kwako ambacho ndio kiini cha maisha ya kila mwanadamu...Siku ile atakuambia ulinifuata mimi si kwasababu ulitaka kuokolewa bali kwasababu ulitaka gari, ulitaka pesa, ulitaka mtoto, ulitaka kuolewa. Na kundi la namna hii ndilo kubwa kabisa katika kanisa hili tulilopo la siku za mwisho.
Maombi yangu ni utafakari mambo yote makuu Mungu aliyokutendea ujue kuwa hayo ni kukutaka utubu kabla wakati haujaisha, utubie uasherati wako, ulevi wako, wizi wako, ufisadi wako, usengenyaji wako, utukanaji wako, ibada zako za sanamu n.k.
hii ndio sababu ya Mungu "kuruhusu" miujiza na ishara nyingi kupita kiasi zitendeke KILA MAHALI katika kizazi chetu hichi tunachoishi, kila kitu unachomwomba Mungu hata kama ni mwenye dhambi anakupa, unaumwa anakuponya, sio kwasababu anafurahishwa na wewe, bali anataka utubu, lakini usipotubu alisema maneno haya:
Mathayo 11:20-24 "Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu HAIKUTUBU.21 Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe. "
Mungu akubariki.
No comments:
Post a Comment