"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, March 20, 2018

JE! NI KWELI UMEMFUATA YESU?


Tomaso akawaambia..

Yohana 20:25”…, Mimi nisipoziona mikononi mwake KOVU ZA MISUMARI, na kutia kidole changu katika mahali pa MISUMARI, na KUTIA MKONO WANGU KATIKA UBAVU WAKE, mimi sisadiki hata kidogo.”

Wengi tunadhani Tomaso alikuwa hatambui anachosema pale alipotoa matamshi kama hayo, lakini ukweli ni kwambaTomaso alitaka kupata uhakika ya kuwa je! Huyu ndiye Yule YESU aliyesulibiwa msalabani au la?. Na tunaona alipomthibitisha kuwa ndie mwenyewe kwa zile alama zilizokuwa mwilini mwake alimkiri na kusema.. “BWANA WANGU na MUNGU WANGU”.
Bwana Yesu alisema na sisi katika Luka 9:23” Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.”

Maneno haya yanatufundisha kwamba USHAHIDI wa kwanza kama kweli tumeamua kumfuata YESU,ni lazima tutakuwa na misalaba migongoni mwetu, hii ikiwa na maana kuwa kama hatujaibeba misalaba yetu ni dhahiri kuwa bado hatujaanza safari ya kumfuata hata kama tutadai kiasi gani kuwa tunampenda YESU, au tunamwamini YESU, au vyovyote vile hapo bado hatujamfuata YESU mpaka siku ile tutakapochukua uamuzi wa kujitwika misalaba yetu na kuambatana naye.

Msalaba ni nini?

Ni Kiashiria cha dhiki au mateso utakayopitia kwa ajili ya Imani yako. Hivyo mtoto wa Mungu yeyote anapomwani Kristo, na kuchukua hatua ya kumfuata YESU kweli kweli ni lazima apitie mahali hapo kujaribiwa kwa imani yake kama kweli alimaanisha kuchukua uamuzi huo au alijaribu tu?.

Hichi ni kipindi cha dhiki za kitambo, ambacho hakikwepeki kama kweli utakuwa ni mtoto wa Mungu, ndio hapo utaona mtu akiamua kuchukua uamuzi wa kumfuata Kristo, ghafla vikwazo vinaanza kuibuka, pengine ndugu wanaanza kukupiga vita, au kujitenga na wewe, pengine hali yako ya kiuchumi inaanza kuyumba, wengine inafikia hatua hata ya kukosa chakula, wengine pindi tu wanapoamini wanakumbana na misiba kufiwa na wazazi au watoto, wengine magonjwa ya ajabu yanazuka, wengine wanafukuzwa kazi kutokana na imani yao, wengine wanaingizwa magerezani, wengine wanaishia kupigwa, wengine jamii inayowazunguka inakuwa kama mwiba katika maisha yao. wengine wanadharauliwa, heshima yao inashuka hata watoto wadogo wanawadharau kisa tu kaamua kuuweka msimamo wake kwa YESU. kiasi cha kwamba mtu anaweza akafikiria yeye ni mtu wa bahati mbaya au ana mikosi, Lakini si kweli, hapo ujue unajaribiwa kama utaiacha ile imani au la.

Kumbuka hapa namzungumzia mtoto wa Mungu aliyeamua kumfuata BWANA YESU kwa moyo wake wote, na sio mtu yeyote tu ambaye hana habari na Kristo anapitia matatizo akidhani kuwa anajaribiwa, hapo ni shetani anafanya kazi juu ya maisha ya huyo mtu.

Hivyo dhumuni la kukuambia haya yote sio kukuogopesha au kukukatisha tamaa, hapana bali ni kukutia moyo pale utakapokutana na mambo kama hayo katika safari yako ya kumfuata Kristo, usikate tamaa wewe upo katika njia sahihi, haujalaaniwa wala huna mikosi, japo wengi watakukatisha tamaa lakini wewe songa mbele, usirudi nyuma wala usimuacha Kristo. Habari njema ni kwamba dhiki hizo ni za muda tu utafika wakati hutaziona tena, zitaondolewa mbele yako biblia inasema…

1Petro 5:
9 Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.
10 Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, MKIISHA KUTESWA KWA MUDA KIDOGO, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na KUWATIA NGUVU.”

Unaona hapo dhiki hizo ni kwa muda tu, tena ni kwa ajili ya kututengeneza na kututhibitha, kwasababu yeye siku zote anatuwazia mawazo yaliyo mema kutupa sisi tumaini katika siku zetu za mwisho.(Yeremia 29:11).

Pia alisema katika 1Petro 4: 12 -16
 
 ”12 Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama MOTO ili KUWAJARIBU, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.
13 Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo,FURAHINI; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
14 Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; KWA KUWA ROHO WA UTUKUFU NA WA MUNGU ANAWAKALIA.
15 Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.
16 Lakini ikiwa kwa sababu ni “MKRISTO” asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.”

Kama tu vile wana wa Israeli walipotoka Misri, hawakuingia moja kwa moja katika nchi ya AHADI iliwapasa wapitie kwanza jangwani katika nchi kame isiyokuwa na maji, walikula chakula cha shida, na kukumbana na hatari nyingi huko nyikani,(Kumb.8) lakini Mungu hakuwaacha aliwapitisha kule makusudi sio kwa kuwatesa hapana bali kwa kuwafundisha, na kuwapa hukumu zake, ili watakapoingia nchi yenye asali na maziwa waweze kuenenda nayo pasipo kumsahau Mungu wao.

Kwahiyo ndugu yangu MKRISTO wewe uliyeamua leo hii kuchukua msalaba wako na kumfuata yeye ambaye alikufa kwa ajili ya Roho yako, umeingia gharama ya kuacha anasa na marafiki wamekutenga, umeamua kuacha ibada za sanamu na ndugu zako wamekutenga au kukuchukia na kanisa limekutenga, binti umeamua kuacha suruali & vimini,lipsticks,bangili & hereni kwa ajili ya Kristo na umeonekana mshamba, pengine kwa kufanya hivyo imehatarisha kazi yako, umeamua kuacha pombe na sigara na uasherati unaonekana mwanaume ambaye hujakamilika, n.k. hayo mateso yote na hizo dhiki ambazo hukuziona hapo kabla ni uthibitisho kamili kwamba upo katika njia iliyosahihi…Umekidhi vile vigezo kuwa UMEBEBA MSALABA WAKO na kumfuata YESU na hakika utaiingia kaanani yako kwa muda Mungu aliouamuru.

Lakini wewe ambaye anajiita mkristo, halafu hauna ALAMA zozote kuonyesha kuwa umemfuata KRISTO, swali kwako litakuwa kama lile la Tomaso alilouliza, NIONYESHA MAKOVU YA MISUMARI katika mikono yako, onyesha ubavu wako ndipo tusaidiki kuwa uliuchua msalaba wako na kumfuata Kristo.

Onyesha ni wapi ulipitia changamoto kwasababu ya imani yako? Ni wapi ulidharauliwa, au ulichekwa,au ulitengwa,au uliabishwa, au ulipigwa,au ulitukanwa,au uliteseka, au ulishushwa chini, n.k. kwa ajili ya kuchukua uamuzi wa kumfuata Kristo??,. Kama bado basi ujue bado hujaanza safari ya kumfuata yeye. Bado upo Misri haijalishi unaenda kanisani namna gani, unaimba kwaya kiasi gani, unapaswa uchukue uamuzi wa moja kwa moja kumfuata Kristo. Kuweka mawazo yako mbinguni, na kusema mimi duniani ni mpitaji bali makao yangu ni mbinguni. Mimi na dhambi basi!!!

Hivyo ndugu huu ni wakati wako wa kujitathimini kwa kina je! Ni kweli umemfuata Kristo au umeifuata dini au umefuata dhehebu?. Kama ni kweli umemfuata Kristo ni lazima utabeba msalaba wako na kama unao msalaba lazima alama za makovu ya mijeledi na misumari, pamoja na taji la miiba, vionekane katika safari yako ya kumfuata Kristo. Yahakiki maisha yako na uchukue uamuzi. Na Bwana atakusaidia.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment