"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, March 21, 2018

SAUTI AU NGURUMO?


Yohana 12:28-30

28 Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja SAUTI kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.
29 Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba KUMEKUWA NGURUMO; wengine walisema, Malaika amesema naye.
30 Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, BALI KWA AJILI YENU.”


Katika habari hii tunasoma kuwa kuna SAUTI ilitoka mbinguni ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya umati uliokuwa unamsikiliza BWANA, lakini cha kuogopesha haikuwafikia walengwa kama SAUTI bali ilikuja kama NGURUMO. Ndugu Kumbuka biblia ni sauti ya Mungu katika maandishi, kabla haijaandikwa ilizungumzwa na Roho wa Mungu mwenyewe ndipo baadaye yale maneno yakaja kuandikwa kwa ajili yetu katika karatasi.

Hivyo biblia kwetu sisi inakaa kama ngurumo na inahitaji Roho wa Mungu kuisikia sauti nyuma ya hiyo ngurumo vinginevyo hatutaelewa chochote kilichomo humo.

Na hichi kitabu kinajishuhudia chenyewe kuwa ni kitabu kilichofungwa soma (Danieli 12:4 & Ufunuo 10:4 utaona jambo hilo). Hivyo inahitajika Roho wa Mungu mwenyewe kukifungua, sisemi kuwa hutaelewa hadithi zilizoandikwa humo hapana, unaweza ukaelewa habari zote, lakini hautapata ufahamu wa kuelewa ufunuo wa yaliyoandikwa kule hata uwe ni msomi wa theolojia kiasi gani. Kama hakuna msaada wa Roho wa Mungu kitakachosomwa huko ni ngurumo tu! Na sio sauti ya Mungu.

Mahali Fulani Bwana Yesu alitoa mfano wa mpanzi kwa makutano, na alipomaliza akaondoka bila kuwafafanulia chochote. Wale makutano kwa kuwa hawakuwa na kiu ya kutaka kujua zaidi walikisia pengine ni hadithi tu inayohusu habari Fulani ya mkulima isiyokuwa na ulinganifu wowote na mahitaji yaliyowapeleka pale, na kwasababu wao kilichowapeleka pale ni miujiza tu, wakapuuzia zile habari za ule mfano wakidhani wameelewa na kuondoka zao wakiwa wameponywa kwa furaha. Na Bwana naye akawaacha hivyo hivyo mpaka wanafunzi wake kwa unyenyekevu mwingi walipoamua kumfuata na kuomba wafafanuliwe maana ya ule mfano..Ndipo Bwana Yesu akawaambia;

Mathayo 13:10-16

10 Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano?
11 Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.
12 Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.
13 Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa.
14 Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, KUSIKIA MTASIKIA, WALA HAMTAELEWA, KUTAZAMA MTATAZAMA, WALA HAMTAONA.
15 Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.
16 Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.”

Na tukiendelea kusoma ndipo tunaona Bwana Yesu akiwafumbua macho wanafunzi wake tu na kuuelewa ule mfano wa mpanzi.

Na vivyo hivyo kila mahali alipokuwa akifundisha makutano alimalizia na kusema “MWENYE MASIKIO NA ASIKIE”. Ikiwa na maana kuwa linahitajika sikio lingine la ziada kusikia kile ambacho Mungu anazungumza, vinginevyo itakuwa kwako kama ngurumo badala ya sauti.

Ukiona unasoma biblia wewe unayejiita mkristo halafu maisha yako ni yale yale, hapo umesikia ngurumo bado hujaisikia sauti ya Mungu. Tafuta kuisikia sauti ya Mungu.

Ukiona unahubiriwa injili halafu haubadiliki, Sikio lako limefumbwa ili unaposikia usielewe. Tafuta mapema kusikia sauti ya Mungu kabla nyakati za hatari hazijakufikia.

Jenga tabia ya kuchunguza maandiko kama mitume, wao hawakuridhika na ufahamu waliokuwa nao kuhusu Maneno ya Mungu, na ndio maana unaona walikuwa wanamfuata Yesu faraghani na kumuuliza, na ndipo wanafafanuliwa, sasa kama mitume waliochaguliwa na Mungu walifanya hivyo. Inatupasaje sisi??.

Unaweza ukawa umepitia biblia yote mwanzo hadi mwisho, lakini bado hujamsikia Mungu, bali ngurumo tu kwasababu maisha yako yanaonyesha. Unaweza ukawa umesoma biblia yote lakini bado msengenyaji, bado mwasherati. Hapo kusoma umesoma lakini hujaelewa. Laiti ungesikia SAUTI YA MUNGU usingebakia hivyo hivyo.

Kwahiyo ndugu unaposoma Neno la Mungu usilichukulie tu juu juu, fahamu kuna sauti nyuma yake inayosema na wewe. Muombe Mungu akupe ufahamu wa kuisikia, Na hiyo ndiyo itakayokupa sababu ya wewe kuishi maisha yanayompendeza Mungu.

Fungua moyo wako sasa, utafute kujifunza habari za Mungu, na sio kusoma tu kama kitabu cha hadithi, Na Mungu atakusaidia kuisikia sauti ya NENO lake inayosema nawe katika maisha yako na sio NGURUMO.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment