"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, March 23, 2018

TABIA YAKO NI YA MNYAMA GANI?


Kila mnyama tunayemwona, kwa namna moja au nyingine yupo mwanadamu au jamii au taifa linalobeba tabia zinazofanana na huyo mnyama, Kwamfano Bwana Yesu kumwita Herode “Mbweha” hakuwa anamtukana, bali alikuwa anaelezea jinsi tabia yake inavyofanana na ya mbweha. Mbweha ni mnyama anayekaribia kufanana na mbwa, isipokuwa huyu anararau wanyama wadogo wadogo na pia tabia yake nyingine inayofanana na mbwa ni kuzaliana na mbweha mwingine yeyote bila mpangilio maalumu, hivyo tabia hizi zilionekana kwa Herode, Kwanza alikuwa muuaji: alimuua Yohana Mbatizaji nabii wa Mungu, na bado akaongeza kuoa mke wa ndugu yake, tabia zisizo na tofauti na mbweha.

Kadhalika kitabu cha Danieli kinaeleza juu ya zile Falme 4 zitakakuja kutawala mpaka mwisho wa Dunia, nazo pia zilifananishwa na tabia za wanyama, kwa mfano Babeli ilifananishwa na Simba, Umedi & Uajemi ilifananishwa na dubu, vivyo hivyo na Uyunani ulifananishwa na Chui.(Danieli 7)n.k.

Shetani naye alifananishwa na joka, kwasababu ya tabia aliyokuwa nayo nyoka ya kumdanganya mwanadamu kumuasi Mungu kwa kula tunda. Kama tu anavyoendelea kufanya sasa hivi kuudanganya ulimwengu watu wamwasi Mungu, waishie kwenda katika ziwa la moto.

Vivyo hivyo na BWANA wetu YESU KRISTO alifananishwa na mnyama fulani na huyu si mwingine zaidi ya MWANA-KONDOO.
KWANINI MWANA-KONDOO?

Tabia ya kwanza ya kondoo ni mnyenyekevu na mpole, na ni mnyama ambaye hawezi kujiongoza mwenyewe siku zote anategemea mchungaji wake kumuongoza tofauti na mbuzi, Mbuzi yeye anao uwezo wa kujichunga mwenyewe.

Na ndio maana tunaona sehemu zote Bwana Yesu aliitwa “mwanakondoo”, Yohana alimwona kama mwanakondoo achukuaye dhambi za ulimwengu, si ajabu hata kuzaliwa kwake kulikuwa ni kwenye hori la ng’ombe. YESU Alipoishi duniani alikuwa ni mpole na mnyenyekevu sana, kiasi kwamba japo alikuwa ni Mtakatifu lakini alikaa katikati ya watoza ushuru na makahaba, japo alikuwa ni mfalme lakini aliwaosha miguu wanafunzi wake. Biblia inamshuhudia alikuwa anawakemea waovu lakini moyoni mwake alijaa huruma. Yeye mwenyewe alishuhudia na kusema..

Mathayo 11: 28 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa MIMI NI MPOLE NA MNYENYEKEVU WA MOYO; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”.
 Ni mtu ambaye aliwaponya maadui zake waliokuja kumuua kwa mapanga na marungu, Alilia kwa dua nyingi na machozi kwa ajili ya ndugu zake(mimi na wewe).

Na kama vile kondoo wanaponyolewa manyoya yao kwa ajili ya sufu au wanapopelekwa machinjoni wanakaa kimya tofauti na mbuzi, ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana wetu Yesu, alitukanwa hakurudisha, alipigwa makofi hakurudisha, alitemewa mate, hakurudisha, japo alisikia maumivu kama mwanadamu mwingine yeyote lakini aliishia na kusema BABA WASAMEHE. Hii ilitoka ndani ya moyo wake kabisa na sio kinafiki.

Nabii Isaya alimwona miaka mingi sana kabla ya kuja kwake akaeleza habari zake..

Isaya 53:3-8

“Alidharauliwa na kukataliwa na watu; MTU WA HUZUNI NYINGI, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
4 HAKIKA AMEYACHUKUA MASIKITIKO YETU, AMEJITWIKA HUZUNI ZETU; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
6 Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.
7 Alionewa, lakini ALINYENYEKEA, Wala hakufunua kinywa chake; Kama MWANA-KONDOO APELEKWAYE MACHINJONI, Na kama vile kondoo ANYAMAZAVYO Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, HAKUFUNUA KINYWA CHAKE.
8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.”

Haikuishia hapo Zekaria naye alimuona miaka mingi iliyopita naye akamzungumzia na kusema…

Zekaria 9: 9 “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; NI MNYENYEKEVU, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.” Haleluya, Bwana Yesu alikuwa ni wa kipekee sana.

Vivyo hivyo Roho Mtakatifu alifananishwa na HUWA (yaani NJIWA)..Kutokana na tabia za njiwa huwa ni MPOLE. Na njiwa siku zote anatua sehemu zenye utulivu na amani..hawezi kutua sehemu nyingine yoyote kama Kunguru. Wanaofuga njiwa wanaelewa itakuchukua muda mrefu sana mpaka akuzoee kiasi cha kufikia hatua ya kutua kwenye mikono yako au mabegani mwako, Njiwa anayo desturi ya kuhakiki jambo Fulani kwa muda mrefu mpaka alizoee, inahitaji upole wa hali ya juu. Na inajulikana mahali palipo na makelele njiwa huwa hakai atahama hata kama anahudumiwa vizuri kiasi gani.

Na hapa tunaona ROHO mfano wa HUWA akitua juu ya Bwana Yesu Kristo kiashirio kuwa ni mahali sahihi penye utulivu wa kutua. Roho aliridhishwa na upole na unyenyekevu wa Bwana YESU kama mwanakondoo.

Marko 1: 9 “Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani.
10 Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake;
11 na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”

Vivyo hivyo na watoto wa Mungu wote wanafananishwa na wana-kondoo, na hao ndio ROHO WA MUNGU anaowashukia juu yao. Wanapaswa wawe wapole, wanyenyekevu, wanapotukanwa hawarudishi, wanapoudhiwa hawawaudhi wengine, hawasengenyi, wanawaombea wanaowaudhi, wanawapenda maadui zao na kuwasamehe kama Bwana alivyokuwa. Na zaidi ya yote hawajiongozi wenyewe kama mbuzi, wanamtegemea Mungu(Mchungaji mkuu YESU) kwa kila kitu, hawachukui maamuzi yoyote pasipo yeye, wanadumu katika NENO tu, hawaabudu miungu mingine, wanachofikiria ni utakatifu tu, wapo tayari hata kutoa uhai wao kwa ajili ya ndugu zao wengine kama yeye alivyoutoa uhai wake kwa ajili yetu. Watu kama hawa Roho wa Mungu anashuka juu yao na kuwafanya waendelea kuzaa matunda yote ya Roho.(wagalatia 5:22).

Lakini wasio wa Mungu wanafananishwa na mbuzi, wao huwa wanajiongoza wenyewe na kujiamulia mambo yao, hawana haja na mchungaji (yaani Bwana YESU), hawa hawawezi kuwa wanyenyekevu au wapole kwasababu wanajiona kuwa wanafahamu kila kitu.

Je! Wewe ni kondoo au mbuzi?. Kumbuka Roho wa Mungu hawezi kukaa juu ya mbuzi. Japo leo hii wanajificha katika kanisa la Mungu lakini utafika wakati wa kutengwa..KONDOO upande wa kuume, na MBUZI upande wa kushoto. Je! Utakuwa upande upi siku ile??

Mathayo 25: 32-46 “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;
32 na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;
33 ATAWAWEKA KONDOO MKONO WAKE WA KUUME, NA MBUZI MKONO WAKE WA KUSHOTO.
34 Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;
35 kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;
36 nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.
37 Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?
38 Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?
39 Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?
40 Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.
41 Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;
42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;
43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.
44 Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?
45 Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.
46 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.

Shalom.

No comments:

Post a Comment