"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, April 6, 2018

UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KIRAHISI.

Bwana Yesu aliposema “UTAFUTENI kwanza ufalme wake na haki yake..”. Alikuwa na maana kubwa zaidi kuliko inavyodhaniwa,.kitu kama ni cha kutafuta inamaana kuwa kimesitirika na kinahitaji nguvu ya ziada kukipata. Kumbuka tunapompa Bwana maisha yetu leo haimaanishi kuwa tumeupata ufalme wa Mungu, hapana bali tumepiga hatua ya kwanza katika kuutafuta ufalme wake. Ni sawa na mtu anapokwenda kuandikishwa shuleni darasa la kwanza, haimaanishi kuwa tayari ameshakuwa msomi, hapana bali hiyo ni hatua ya kwanza tu ya yeye kupata elimu na ndivyo ilivyo katika ukristo. Unapompa Bwana maisha yako leo haimaanishi kwamba umeshaupata ufalme tayari.

Ndipo Bwana Yesu akawajibu alipoulizwa katika Luka 17:20-21

“20 Na alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza;
21 wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu. “.

Wakati huo watu walidhani kuwa ipo siku ufalme wa Mungu utawajilia juu yao na kuutambua, lakini yeye alisema tazama ufalme wa Mungu tayari umo ndani yenu. Ikiwa na maana kuwa ni kitu kinachopatikana kwa mtu yoyote na mahali popote alipo atakapo. Sasa ni jukumu lake yeye kujua namna ya kuufanya uwe wake, kwasababu ni kweli unaweza ukawa upo ndani yako lakini usiwe wa kwako.

Mfano huo unalingana na utafutaji wa mali, kwamfano ukihitaji pesa huwezi ukasema unaenda kuzichukua benki kuu kwasababu tu benki kuna mkusanyiko mkubwa wa Fedha. Hutapata chochote, lakini badala yake ulitambua kuwa fedha hazipatikani kule bali zinapatikana hata hapo ulipo, zipo katikati ya jamii ya watu unaoishi nao. Ni wewe tu kufanya bidii kuzitoa kwao kwa njia halali na kuzifanya ziwe zako, sasa ili kwamba zoezi hilo lifanikiwe inakupasa ukafanye kazi kwa nguvu zako uzipate pengine ukafanye biashara, au ukauze duka, au ukalime shamba, n.k. ili uzipate, na ndipo kwa bidii zako utazipata baada ya kuzisumbukia.

Na ndio maana Bwana Yesu alisema ufalme wa Mungu hautashuka kwa kuusubiria bali upo katikati yetu, mioyoni mwetu, lakini haimaanishi kuwa kwasababu upo ndani yetu tumeshakwisha kuupata hapana bali inahitajika bidii ya ziada ili kuufanya uwe wa kwetu.Kama vile fedha ipo katikati yetu lakini si ya kwetu mpaka tuifanyie kazi. Zipo pia gharama za kuupata ufalme wa Mungu na kazi pia ipo.

Mahali pengine Bwana alisema Mathayo 11: 12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.” Kama mkristo inahitajika bidii kumjua Mungu ili kuelewa kwa kina mapenzi yake ndani yako.

Tunaupataje ufalme wa Mungu?

Hii inakuja kwa kutaka kujifunza jambo jipya kila siku lihusulo Imani yako. Kwa kuyachunguza maandiko siku baada ya siku, kama vile fedha isivyotafutwa kwa chanzo kimoja, vivyo hivyo hata kwa ufalme wa mbinguni, unapaswa kutokugota katika ngazi moja ya kiroho siku zote, (Mathayo 13: 52 Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale).

Bwana alisema heri walio na njaa na kiu ya haki maana watashibishwa, biblia inasema pia..Tuutafute ufalme wa Mungu kama tunavyotafuta fedha (Mithali 2:4). Haupaswi kuridhika katika hali moja hiyo hiyo ya kiroho bali kila siku unapaswa utafute chanzo bora zaidi cha kuongeza maarifa yako juu ya Mungu. Paulo alimwambia Timotheo JITAHIDI KUJIONYESHA KUWA UMEKUBALIWA NA MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.”

Hakuna mwanafunzi kila siku yupo kwenye ngazi moja tu, kila siku anavuka daraja. Tatizo kubwa lililopo katikati ya wakristo ni kuridhika na mapokeo ya madhehebu yao, na kupelekea kutokupiga hatua mbele, hawa biblia inawafananisha na wale wanawali wapumbavu, waliobeba taa zao bila kuwa na mafuta ya ziada pindi walipokuwa wanakwenda kumlaki Bwana wao (Mathayo 25). Lazima uwe na mafuta ya ziada ndugu, kwa kuutafuta ufalme wa Mungu maishani mwako kila siku.

FAIDA ZA KUUPATA UFALME WA MUNGU.

Unapoupata ufalme wa Mungu ndani yako, unakuwa sio mtu wa kutikiswa na kila upepo wa elimu, na mafundisho potofu ya uongo. Unakuwa na uwezo mkubwa wa kupambanua ukweli na uongo, na pia unaongeza uhusiano wa kipekee na Mungu wako, na mwisho unapokea ahadi za kipekee katika ule ufalme wa milele unaokuja kwenye mbingu mpya na nchi mpya.

Mitume wa Bwana Yesu pindi walipoingia gharama ya kuutafuta wakaahidiwa ahadi kubwa na za kipekee, Bwana aliwaambia katika ufalme ujao wataketi pamoja naye wakiyahukumu makabila 12 ya Israeli,

Vivyo hivyo na wote katika makanisa 7 walioshinda walipewa ahadi za kipekee vile vile, katika huo ulimwengu unaokuja, Kanisa letu la mwisho linalofananishwa na kanisa la LAODIKIA, Bwana aliahidi wale watakaoshinda atawapa nafasi ya kuketi pamoja naye katika kiti chake cha enzi kama yeye alivyoshinda.(Ufunuo 3:21). Kumbuka sio kila mkristo atakayeenda mbinguni atapokea hizo ahadi za kipekee, bali ni wale tu walioupata ufalme wa Mungu hapa duniani, na kushinda kama Bwana wao. Mambo yote yanakamilika hapa duniani mbinguni ni kuvikwa mataji tu. Hivyo kwa bidii shika sana ulichonacho asiye mwovu akalitwaa taji lako. asema BWANA.

Ufunuo 22: 12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.” Jitahidi ndugu kuutafuta ufalme wa Mungu sasa angali muda tumepewa, kwa maana unapatikana kwa nguvu kama vile fedha inavyopatikana kwa nguvu kwasababu ni kitu cha thamani. 
Uufanye imara wito wako na uteule wako kila siku na Bwana mwenyewe atakusaidia.
 
Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment