"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, May 16, 2018

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 2


Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha Yuda, leo tukiendelea na sehemu ya pili. Kama tulivyokwisha kuona ile sehemu ya kwanza, Yuda mtumwa wa BWANA, alitoa angalizo na maonyo kwa watu wa Mungu kwamba waishindanie imani waliokabidhiwa watakatifu mara moja tu, na kwamba maonyo hayo hawakupewa watu wote (yaani watu waovu na wema), hapana bali waraka ule uliandikwa kwa watu wa Mungu tu walioitwa peke yao (yaani wakristo). Hivyo ni vizuri ukafahamu hilo unapokisoma hichi kitabu,tukiendelea na mistari inayofuata tunasoma..;

7 Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele.
8 Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, HUUTIA MWILI UCHAFU, HUKATAA KUTAWALIWA, NA KUYATUKANA MATUKUFU.
9 Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee.
10 Lakini watu hawa huyatukana mambo wasiyoyajua, na mambo wayatambuayo kwa asili wajiharibu kwayo kama wanyama wasio na akili.
11 Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika NJIA YA KAINI, na KULIFUATA KOSA LA BALAAMU pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika MAASI YA KORA.
12 Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung'olewa kabisa;
13 ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao WEUSI WA GIZA ndio akiba yao waliowekewa milele”.
Kama ukichunguza watu hawa ambao Yuda anawazungumzia, ambao wanakataa kutawaliwa, wanaoenenda kwa kufuata mambo ya mwili, na wanaotukana matukufu, watu wanaofananishwa na nyota zinazotea ambao weusi wa giza ni sehemu yao waliowekewa milele, wanaonena maneno makuu magumu wasiyoyajua, Utaona kuwa Yuda amewapata kutoka katikati ya hawa watu watatu (yaani KAINI, BALAAMU na KORA). Kuna kitu kikubwa cha ajabu katikakati ya hawa watu.

Sasa tuwatazame ni kwa namna gani wamefananishwa na mawingu yasiyokuwa na maji, yachukuliwayo na upepo, na miamba ya hatari, na miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung'olewa kabisa; Kumbuka hawa watu wanaozungumziwa ni watu waliopo katikati ya kundi la Mungu waliojiingiza kwa siri.

NJIA YA KAINI;

Kumbuka Kaini hakuwa wa uzao wa Adamu kwa asili tangu mwanzo bali wa nyoka. Na nyoka kabla hajalaaniwa alikuwa hatembei kwa matumbo,bali alisimama wima kama mtu na alikuwa anazungumza kama mtu, ni kiumbe kilichokuwa karibu sana kufanana na mwanadamu, alikuja kuwa reptilia (nyoka tunayemwona sasa) baada ya kulaaniwa. Lakini Habili ndiye aliyekuwa mwana halisi wa Adamu, na uzao wake baada yake ndio ulioitwa "WANA WA MUNGU", na uzao wa Kaini baada yake uliitwa "WANA WA BINADAMU ",

Na kama tunavyosoma tabia zote zilizokuwa kwa Kaini na uzao wake hazikutoka kwa Mungu, mfano tabia ya uuaji, alimuua ndugu yake kwasababu ya wivu, na ukichunguza uzao wake baada yake ulikuwa na tabia hiyo hiyo, mtoto wake Lameki alisema kama Bwana akimlipa Kaini kisasi mara 7 hakika Lameki atalipwa mara 77, sasa unaweza ukaona jinsi huyu mtu alivyokuwa muuaji kushinda hata baba yake.(Mwanzo 4:23), Ikiwa na maana kuwa kama baba yake aliweza kumuua mwenye haki mmoja (Habili), basi yeye ataua wenye haki 77.

Kadhalika tabia ya kuoa wake wengi ilianzia katika uzao wa Kaini, Ukisoma utaona huyu Lameki alikuwa na wake wawili jambo ambalo Mungu hakuliagiza. Lakini uzao wa Adamu (ambao ndio wana wa Mungu), walikuwa ni watu wanaomcha Mungu na kuutafuta uso wa Mungu siku zote soma(Mwanzo 4:25). Lakini agenda ya shetani siku zote ni kuwatafuta watu wa Mungu, na sio watu wa ulimwengu kwasababu hao tayari alishawapata. Na njia pekee anayoweza kutumia ni kuwakosesha wao na Mungu wao. Ili Mungu mwenyewe aamue kuwaangamiza, na ndio maana tunasoma katika mwanzo 6 utaona wana wa Mungu(yaani uzao wa Adamu) waliwatamani binti za binadamu (yaani uzao wa kaini) ambao ulikuwa ni mwovu, na kwenda kuwaoa na kusababisha kitendo cha kuchanganyika kwa mbegu. Hilo ndio likawa jambo pekee lililosababisha Mungu kuleta gharika kwa kuona mbegu takatifu imeharibika. Tunaona hapo japokuwa ulimwengu ulikuwa ni mwovu lakini hasira hasaa ya Mungu iliwaka juu ya wana wa Mungu kutoilinda enzi yao. Kumbuka "wana wa Mungu" kama wanavyozungumziwa pale sio malaika, kwasababu malaika hawazai wala hawazaliani. Na Mungu angewaadhibu malaika ingekuwa ndio wao waliozini, lakini badala yake waliadhibiwa wanadamu. Hivyo wana wa Mungu wanaozungumziwa pale ni wana wa uzao wa Adamu.

Ndio jambo linaloendelea leo katikati ya watu wanaojiita wakristo, shetani akishagundua upo katika mstari wa Imani, hali akijua wewe ni mzao mteule wa Mungu, atakuja kwa NJIA YA KAINI. Atakuletea jamii ya Viongozi wa Dini/Imani mfano wa Kaini, atakuletea wahubiri watakaokuhubiria kuoa wake wengi ni sawa watatumia Biblia kukuhakikishia jambo hilo, watakufundisha kuoa/kuolewa na mwanamke yeyote ni sawa tu! kumbuka hiyo ni njia mwovu siku zote wale binti wa Kaini ndio waliowakosesha wana wa Mungu, na ndio waliomkosesha pia na Sulemani,.Watakuhubiria kunywa pombe ni sawa biblia inaruhusu, watakufundisha Mungu haangalii mavazi, anaangalia moyo, hivyo hata ukivaa kimini na suruali na kupaka rangi usoni ni sawa....Na wewe hujui kwamba shetani ameshakumaliza..kukukosesha wewe na Mungu umeishindwa kuilinda enzi na IMANI yako uliyokabidhiwa mara moja tu! kwa kutokudumu katika maagizo yake, jambo litakalokutokea ni kuwekwa katika vifungo vya giza, kama watu wa Nuhu walivyofanywa na wale malaika walioasi..Na Bwana Yesu alisema kama zilivyokuwa katika siku za Nuhu.......

KOSA LA BALAAMU:

Kama wewe ni mwanafunzi wa biblia utajua kabisa Balaamu alikuwa ni nabii lakini sio mwisraeli, Alikuwa ni nabii na bado alikuwa ni mchawi vile vile biblia inasema hivyo! sasa unaweza ukauliza je! Mtu anaweza akawa ni mchawi na bado akawa ni nabii?? JIBU NI NDIO!! (soma Kumbukumbu 13),ni nabii kabisa na anapokea mafunuo kutoka kwa Mungu lakini alikuwa ni mchawi. Sasa wakati wana wa Israeli walipokuwa jangwani wanakaribia kupita katika nchi ya Moabu, yule Balaki mfalme wa Moabu aliwazuia wasikatize katika nchi yao. Hivyo Wamoabu wakaongezea kwa kumuajiri Balaamu aje kuwalaania(kuwaloga) wana wa Israeli. Lakini Mungu alimwoonya asifanye hivyo, kama alivyomwonya Kaini tu, lakini kwasababu ni mtu aliyependa fedha, akatafuta njia mbadala ya kuwakosesha watu wa Mungu.

Ndipo akaja na wazo jipya la kishetani zaidi, kama lile linalofanana na uzao wa Kaini, Akamwambia Balaki mfalme wa Moabu watu hawa (Waisraeli) hawalaaniki kwa namna yoyote isipokuwa kwa njia ya kuwakosesha wao na Mungu wao. Na njia pekee ni kuwaalika na kuwapa binti zenu wale walio wazuri wakaolewe na wana wao, ili watoe sadaka kwa miungu yao, na kufanya karamu za anasa, kitu ambacho Mungu wao amewakataza wasifanye. Na baada ya hapo Mungu wao atakasirishwa nao na kuwaangamiza. Na kweli njama zao zilifanikiwa baada ya kitendo kile walidondoka waisraeli elfu 24, (Hesabu 22-25).

Unaona hapo balaamu ni aina ya wahubiri wa uongo waliopo duniani sasa, ni kweli wanaweza wakawa na karama za kinabii,wanaona maono saa nyingine wanakutabiria jambo na linatimia, lakini kumbe ni wachawi walioajiriwa na shetani kuwaharibu watu waliosimama katika imani. Agenda yao kubwa ni kwa wakristo wa kweli waliosimama. Mafundisho yao yanakupeleka moja kwa moja kufanya uzinzi wa kiroho,(Kumchanganya Mungu na ibada za sanamu), watakuhubiria ibada za miungu mingi, kuwaomba watakatifu waliokufa zamani na walio hai, watakufundisha kuna nafasi ya pili baada ya kifo, watakufundisha hakuna kuzimu, n.k na wengine wanakutabiria na inatokea..

Na ndio maana Bwana alisema katika ufunuo 2: 13 Napajua ukaapo, NDIPO PENYE KITI CHA ENZI CHA SHETANI; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.
14 Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu WASHIKAO MAFUNDISHO YA BALAAMU, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa SADAKA KWA SANAMU, NA KUZINI.
15 Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile.
16 Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.
17 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.

Umeona hapo Bwana anazungumza na watu ambao wameishikilia IMANI, na akawaonya watubu watu wote wanaoshikilia mafundisho ya balaamu. Hivyo ndugu umeona kiti cha enzi cha shetani kilipo?? Hakipo freemason, kipo kwenye dini na mafundisho yote ya uongo katikati ya kanisa la Mungu. Hivyo kama unayashikilia toka huko, vinginevyo Bwana anasema atakuja kufanya vita na wewe kwa huo upanga wake.


MAASI YA KORA:

Kora naye alikuwa ni nabii kama Balaamu isipokuwa huyu sasa anatoka katikati ya wana wa Israeli tena katika uzao wa kikuhani (wana wa Lawi),alikuwa ni kuhani naye pia aliaminiwa na kupewa heshima kubwa katikati ya umati wa wana wa Israeli, Lakini aliinuka moyo na kuona kuwa MAMLAKA iliyowekwa na Mungu haistahili kuwaongoza, akaidharau TORATI ya Mungu na mtumishi wake, na kupeleka mashtaka juu ya mtu wa Mungu Musa,na kutoa maneno makuu ya kufuru, sasa kilichotokea alikusanya watu na kutaka kuwaundia MAMLAKA yake mwenyewe na kuwaongoza katika nchi yake ya ahadi anayoijua yeye. Lakini tunasoma mwisho wa siku ardhi ilipasuka na kummeza yeye pamoja na wafuasi wake wote waliomfuata (Hesabu 16).
 

Hii inafunua nini? Kora ni mfano wa viongozi wa dini wanaokataa MAMLAKA KUU, wanaokataa kutawaliwa na katiba maalumu ambayo Mungu kaiweka ambayo ni BIBLIA TAKATIFU. Wanayapinga yaliyoandikwa huko kwa faida zao wenyewe, Kama vile Kora, alivyoikinai njia Mungu aliyoiweka ya kupita nyikani, vivyo hivyo wahubiri hawa wataipinga njia ya msalaba kwa mafundisho yao,..hawawafundishi watu watubu, wajitwike misalaba yao wamfuate YESU, badala yake watawafundisha watu wajitwike mabunda ya pesa wamfuate Yesu ndio uthibitisho kwamba wanaelekea kaanani. Kumbuka Kora alikuwa anaona kama vile Musa anawatesa jangwani, wanapitia shida, na taabu, hiyo siyo njia ya Mungu..Vivyo hivyo na hawa wanapoona Watoto wa Mungu wanapitia magumu katika Imani zao wanakuja kuwavunja moyo na kuwafundisha,waache uongozi wa njia ya Mungu aliyoiweka, na wafuate uongozi wa kibinadamu.

Kora mahubiri yake yalikuwa ni kuwafariji kuwa wote ni watakatifu(Hesabu 16:3). Vivyo hivyo na hawa mafundisho yao ni kuwafariji watu na kuwaambia yote ni sawa, nyie ni watakatifu hata ukiishi maisha ya kawaida tu, utaenda mbinguni wewe bado ni mtakatifu kwanini kujiumiza kuishi maisha ya kilokole?.

Hivyo tukishafahamu tabia za hawa watu katikati ya kundi la Mungu, tunaonywa tujiepushe nao kwasababu ni nyota zipoteazo.

Biblia imerudia kuelezea habari hii ya kitabu cha Yuda katika kitabu cha 2Petro 2 soma kwa utaratibu itakusaidia sana kulinganisha yote mawili.

Inasema..

Mlango 2

1 Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.
2 Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa.
3 Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.
4 Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu;
5 wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu;
6 tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya;
7 akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu;
8 maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria;
9 basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu;
10 na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu. na kudharau mamlaka.
11 Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana.
12 Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao;
13 Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi;
14 wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana;
15 wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu;
16 lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule.17 Hawa ni visimavisivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliyowekewa.
18 Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu;
19 wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.
20 Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.
21 Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.
22 Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.

Hivyo ndugu, Kanisa tunaloishi ni la hatari sana, je! umeufanya imara wito wako na uteule wako?. Unaishindania imani?. Kama hujatubu dhambi zako fanya hivyo sasa.

Mungu akubariki.

Usikose mwendelezo wa kitabu hichi..na pia share kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki

No comments:

Post a Comment