"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, June 1, 2018

KITABU CHA UFUNUO: Mlango wa 2

Sehemu ya pili.
Libarikiwe jina la mwokozi wetu YESU KRISTO milele na milele AMINA!. Karibu katika kujifunza kitabu cha Ufunuo. Leo tukiendelea katika ile sehemu ya pili ya mlango huu. Kama tulivyotangulia kuona katika sehemu ya kwanza juu ya kanisa la Kwanza (EFESO) na ujumbe wake kutoka kwa Bwana..Kwamba watu wa kanisa lile waliuacha ule upendo waliokuwa nao hapo mwanzo, na jinsi Bwana alivyowaonya watubu na kwamba wasipotubu Bwana atakuja kukiondoa kile kinara chao cha taa. Lakini tukiendelea na Kanisa la Pili linaloitwa SMIRNA tunasoma;

KANISA LA SMIRNA.
Ufunuo 2:8 " Na kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika; Haya ndiyo aneneyo yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai".

Hapa tunaona Bwana anaanza kwa utambulisho kwamba "yeye ni wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai". Kumbuka Kama tulivyotangulia kujifunza utambulisho wa awali wa Bwana unakuwa na uhusiano mkubwa sana na kanisa husika kabla hata ya ujumbe wenyewe kutolewa. Mfano hapa Bwana anaposema aliyekuwa amekufa kisha akawa hai, kama alivyotangulia kujitambulisha hivyo hivyo katika ile sura ya kwanza (Ufunuo 1:18), Hii ikifunua kuwa kuna mapito ya mateso na dhiki nyingi mpaka kupelekea KIFO lakini pia kuna matumaini ya kufufuka baada ya kifo kama Bwana alivyopitia. Na ndio maana hapa hakujitambulisha kama yeye mwenye ule upanga mkali utokao kinywani mwake(maana upanga unawakilisha vita na hapa hajaja kufanya vita), au mwenye uso kama unaong'aa kama jua n.k bali ni "yeye aliyekuwa amekufa kisha akawa hai"

Tukiendelea kusoma;
Ufunuo 2: 9 "Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.
10 Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima".

Kumbuka neno "SMIRNA" tafsiri yake ni "(MANE MANE ILIYOSAGWA au CHUNGU)". Hivyo kama jina lilivyo ndivyo kanisa lilivyokuwa, Hili kanisa lilipitia uchungu mwingi na mateso kutokana na IMANI yao. Kanisa hili lilianza mwaka 170WK na kuisha mwaka 312WK. Katikati ya hichi kipindi maelfu ya wakristo waliuliwa kwa kuingizwa magerezani, wengine walitupwa kwenye matundu ya simba, wengine waliburutwa,wanawake walikatwa matiti na kuachwa damu zichuruzike mpaka kufa, wengine walichomwa moto, wengine walisulibiwa n.k. Hivyo historia inarekodi walipitia dhiki nyingi sana kama vile tu Bwana alivyopitia akiwa hapa duniani. Na Bwana aliwaambia pia kuwa anajua UMASKINI wao, na dhiki yao lakini ni matajiri. Ni kweli watakatifu wa wakati huo walikuwa ni maskini, lakini mbele za Mungu walikuwa ni matajiri..Kama vile Bwana alivyokuwa duniani maskini lakini mbele za BABA alikuwa ni tajiri kuliko watu wote duniani. 2Wakorintho 8: 9 "Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake". Vivyo hivyo na hawa watu wa hili kanisa hawakupenda maisha yao hata kufa kwa ajili ya BWANA. Walichekwa na kudharauliwa na kuonekana kama watu wasiostahili kuishi katikati ya jamii za watu wengine (Waebrania 11:38).



Tunaona pia Bwana aliwaambia " huyo Ibilisi atawatupa baadhi yao gerezani ili wajaribiwe nao watakuwa na dhiki siku kumi ". Tunaona jambo hilo lilikuja kutimia katika utawala wa Rumi chini ya kiongozi mkatili aitwaye Diocletian ndani ya miaka 10 aliwaua maelfu ya wakristo katika magereza kuanzia mwaka 300WK hadi 310WK. (Hizo ndio zile siku 10 zilizozungumziwa na Bwana). Pamoja na hayo BWANA aliwaambia " wawe waaminifu hata kufa, naye atawapa taji ya uzima. "..Haya ni maneno ya faraja kutoka kwa BWANA mwenyewe kwa watu wa kipindi kile ambapo Bwana alitumia kinywa cha IRENIO kama mjumbe wa kanisa hilo kuwafariji watakatifu na kuwarudisha kwenye Neno akiyapinga yale mafundisho ya Wanikolai ambayo tuliyoyaona katika lile kanisa la kwanza, na hapa Bwana anawaita sinagogi la shetani, wanajifanya kuwa watu wa Imani kumbe sio.

Kadhalika walikuwepo pia watu wengine waliokuwa waaminifu kama wakina Polycarp ambao Mungu aliwatumia pia kunyanyua imani za watu na kuwafariji kwa kufa vifo vya kishujaa kama Bwana.Waliishindania imani kwa nguvu zote.

Bwana alimalizia na kusema "11 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. ". Hivyo Japo Bwana aliruhusu WAFE (wapate mauti ya kwanza ya mwili). Lakini aliwaahidia wale watakaoshinda kuwa hawatapatikana na mauti ya pili (Kifo cha Roho). Kumbuka mauti ya kwanza ni hii roho ya mtu kutenganishwa na mwili hivyo mwili unakuwa umekufa lakini roho ya yule mtu bado inaendelea kuishi. Sasa mauti ya pili ni roho inakufa kabisa kama vile mwili unavyokufa. Na hii inauliwa katika lile ziwa la moto tu. Na kama vile mauti ya kwanza inavyokuwa na uchungu, si zaidi sana mauti ya roho? itakuwa na uchungu mara nyingi zaidi.

Watu wa kanisa hilo walizingatia lile Neno Bwana alilosema katika Mathayo 10: 28 " Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum".

Unaona hapo, watu hawa japokuwa walikuwa ni maskini sana, watu wenye dhiki nyingi sana, mpaka kufikia wakati Bwana anawaambia "kifo kinakuja mbele" lakini hawakuikana IMANI, Walizidi kuishikilia imani mpaka kufa. Je! na sisi tunaweza tukawa kama hawa?. Jiulize leo hii unapopitia tabu kidogo, aidha magonjwa, au dhiki fulani unajitenga na Imani..Ujawezaje kupokea taji ya uzima . Na kuepuka madhara ya mauti ya pili? siku ile Bwana atakapokuja? .

Huu ni wakati wa kujihakiki na kujiweka sawa, ili wakati wa kujaribiwa utakapofika tuweze kuwa imara, kama Bwana wetu YESU KRISTO aliyapitia hayo, na watakatifu wake wa kanisa la mwanzo, kadhalika sisi nasi siku yatakapotujia hayo yatupasa tuyashinde kama Bwana.

Ubarikiwe.

Tafadhali share ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki

No comments:

Post a Comment