"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, July 16, 2018

KWANINI USIICHAGUE TUZO ISIYOHARIBIKA?

Mara nyingi sana Mungu huwa anazungumza na sisi kupitia maisha yetu ya kawaida tunayoishi kila siku, tunapokosa shabaha ni pale tunapotarajia Mungu aseme nasi kwa njia zile tunazozifahamu, kwamfano, kuona maono au ndoto, unabii au kutokewa na malaika, mambo ambayo sio muda wote Mungu anayatumia kuzungumza na watu wake. Sehemu kubwa Mungu anayotumia kuzungumza na watu wake ni kupitia maisha, na ndio maana inatugharimu kuyasoma maisha ya BWANA wetu Yesu Kristo na maisha ya watakatifu waliotangulia nyuma ili kuichuja na kuitambua sauti ya Mungu nyuma ya maisha yao.Kwamfano tunasoma tunaposoma kitabu cha mwanzo, au wafalme au Esta au Ruthu, au Nehemia au Ezra au hata safari ya wana wa Israeli hivyo ni vitabu vinavyoelezea maisha ya watu, na huko huko tunajua kusudi la Mungu kwetu sisi ni lipi.

Siku zote Mungu anajifunua katika mambo madogo, ambayo inahitaji utulivu vinginevyo tutaishia kusema Mungu hajawahi kuzungumza na sisi kabisa kama watu wengine wanavyosema..na kumbe alishazungumza na sisi mara nyingi, lakini hutukutia mioyo yetu ufahamu na kuelewa.

Kuna wakati Fulani mahali tulipokuwa tumepanga tulipata nafasi ya kuwa pamoja na wachezaji wawili wanaochezea timu moja maarufu hapa Tanzania, kwetu sisi hatukuona ni kitu cha ajabu sana kukutana nao kwa mwanzoni (kwasababu sisi sio washabiki wa michezo,hata hivyo ni kinyume kwa mkristo kuwa mshabiki wa mambo kama hayo) lakini maisha yao kwa jinsi tulivyoendelea kukaa nao yalitustaajabisha kidogo, kwa jinsi yalivyokuwa ya kipekee sana. Kwasababu kama wachezaji wa kidunia tulitazamia watakuwa ni watu wasiokuwa na nidhamu katika jamii (yaani kuishi maisha kama tu ya wasanii wengine wa kidunia), lakini kwa hawa tuliona utofauti wa mbali wa ya tulivyodhania.

Ratiba yao ilikuwa ni hii ; Kila siku wanaamka asubuhi sana saa 12 kamili, na kwenda uwanjani kufanya mazoezi mpaka saa 3, wakisharudi kutoka huko wana pumzika kidogo mpaka saa 7 mchana wakati wa jua kali, wanarudi tena uwanjani (saa 7 na saa 8) peke yao kufanya mazoezi ya nguvu kuliko waliyoyafanya asubuhi kwenye jua kali, kisha wanarudi kupumzika tena mpaka saa 11 jioni ndio warudi tena uwanjani kujumuika na wengine katika mazoezi ya kawaida, na hayo ndiyo yalikuwa maisha yao asubuhi, jioni, kila siku.

Lakini hicho nacho hakikutushangaza sana, kilichotushawishi zaidi mpaka kufikia hatua ya kutaka kuwauliza ni baada ya kuwatazama kwa muda mrefu, na kuwaona wakijiweka mbali na wanawake,na ulevi, uzururaji, na kuwa na idadi ndogo ya marafiki wanaokuwa nao..wao kazi yao ilikuwa ni mazoezi tu na kupumzika basi!!..hawakuwa wanafanya kitu kingine cha ziada.

Na ndio Siku hiyo moja tukawauliza ni kwanini nyie mnaishi maisha kama hayo tofauti na wengine, wakatujibu; Mambo yanayowakosesha wengi katika michezo na kuwafanya washuke viwango vyao kwa haraka, ni kuchanganya mambo mawili kwa wakati mmoja,wakasema; unapokuwa mchezaji na unataka kiwango chako kisishuke ni lazima uzingatie mambo yafuatayo; 1) Kukaa mbali na uasherati. 2) kukaa mbali na pombe na sigara 3) kukaa mbali na uzuraraji (ANASA). 4) Na kuzingatia mazoezi kwa bidii hususani katika wakati mgumu..hivyo mtu akizingatia yeyote akizingatia mambo hayo michezo haitakuwa na ugumu wowot kwake .

Sasa baada ya watu hao wa kidunia(ambao sio wakristo) kutuambia maneno kama hayo, tulifahamu hiyo ni sauti ya Mungu inayosema na sisi moja kwa moja, na andiko la kwanza lililotujia kichwani ni hili..;
1Wakorintho 9: 24 “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.
25 NA KILA ASHINDANAYE KATIKA MICHEZO HUJIZUIA KATIKA YOTE; BASI HAO HUFANYA HIVYO KUSUDI WAPOKEE TAJI IHARIBIKAYO; bali sisi tupokee TAJI isiyoharibika .26 Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;
27 bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”.

Ikiwa hao hawajapewa neema ya kuishinda dhambi kama tuliopewa sisi katika Bwana wetu Yesu Kristo pale tunapomwamini lakini wanao uwezo wa kuyakataa mambo ya kidunia ili tu wasipoteze mataji yao, Inatupasaje sisi tunaojiita wakristo?. Wao wanajua kabisa huko wanapokwenda watakutana na watu wenye ujuzi mkubwa kama wa kwao, hivyo wanagharimika sasa hivi kujitaabisha katika mazingira yote magumu ili watakapoenda kule kushindana na wale wengine iwe ni rahisi kwao kushinda na kupokea tuzo iliyobora ambayo inagombaniwa na wengi.

Mtume Paulo aliandika ..
2Timotheo 2: 4 “Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari.
5 HATA MTU AKISHINDANA KATIKA MACHEZO HAPEWI TAJI, ASIPOSHINDANA KWA HALALI”.
Katika Maneno hayo tunaona Mungu anatufundisha Neno lake katika maisha yanayotuzunguka, kumbuka ukiwa mkristo, haimaanishi kuwa ndio umefika, hivyo kuanzia huo wakati ustarehe tu hapana! ni lazima ujue kuwa huko unapokwenda pia kuna TUZO zimeandaliwa, tena tuzo zenyewe ni tuzo zisizoharibika..na ni watakatifu wengi wanaozigombania, na yeye aliyestahili ndiye atayeipokea Tuzo ya juu zaidi kuliko wengine.. Bwana Yesu alisema “12 Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo”. (Ufunuo 22:12)

Lakini Tuzo hiyo hatuipati kama hatutaziingia gharama kama Paulo alizozisema ..”Ninautesa mwili wangu na kuutumikisha”… Ikiwa wachezaji wa ulimwengu huu wanaitesa miili yao na kuitaabisha (sio kana kwamba wenyewe wana madhaifu hapana! Bali Wanafahamu wanachokitafuta,) watawashinda wakristo kwa kujizuia na mambo mengi ili tu kupokea taji ambayo kesho inakwisha thamani yake..Unadhani inatupasa tuingie gharama kubwa kiasi gani sisi tunaojiita wakristo ili kupokea ile TUZO isiyoharibika (yaani inayodumu milele?)…Bila shaka ni kubwa zaidi ya wale, ni kujizuia zaidi ya wale, ni kujinga na mizigo ya dhambi mara nyingi zaidi ya wale.

Biblia inasema lipo WINGU kubwa la MASHAHIDI linalotuzunguka katika mashindano yaliyopo mbele yetu ukipata nafasi lisome hili wingu lote katika Waebrania sura ya 11, utaona ni jinsi gani walishinda mbio kwa saburi, na kama sisi tusipokuwa na juhudi katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu, basi zile tuzo nono kule zitachukuliwa na wengine waliostahili, ukisoma biblia inatuambia watu wale(wingu kubwa la mashahidi) ulimwengu haukustahili kuwa nao, walikuwa ni wasafiri duniani, watu ambao mawazo yao waliyaelekeza katika ulimwengu ujao mpaka kuhesabu maisha ya hapa duniani kuwa si kitu (mfano Ibrahimu), mpaka kufikia hatua Mungu mwenyewe anajivunia kuitwa Mungu wao kwa vile walivyoyaelekeza mawazo yao mbinguni, walikatwa na misumeno, walipigwa, walisulibiwa lakini hawakuikana imani yao,na sisi je! Tutapate kuwa kama hao kama tusipojikana na tusipojitesa na kuitumikisha miili yetu sasa hivi?..(soma waebrani 11 yote utaona jambo hilo)

Ukizidi kuisoma habari ya hilo Wingu la Mashahidi mpaka kufikia sura ya 12, ndio mtume Paulo anahitimisha kwa kusema…

Waebrania 12: 1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, NA TUWEKE KANDO KILA MZIGO MZITO, NA DHAMBI ILE ITUZINGAYO KWA UPESI; NA TUPIGE MBIO KWA SABURI KATIKA YALE “MASHINDANO” YALIYOWEKWA MBELE YETU,
2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
3 Maana mtafakarini sana yeye ALIYESTAHIMILI MAPINGAMIZI MAKUU NAMNA HII ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu”.

Dada/Kaka nawe pia hawa wanamichezo wanaokuzunguka wanakufundisha nini? siku ile utajisikiaje kuona waliokuwa warembo kuliko wewe, ambao wangeweza kuutumainia uzuri wao kupata kila kitu katika dunia hii lakini walijizuia na tamaa za kitambo na zaidi ya yote unawafahamu, utajisikiaje kuwaona siku ile wanang’aa kama nyota na wewe unakuwa sio kitu mbele yao milele?, siku ile wanapewa tuzo wewe utakua uko wapi? Utajisikiaje kuona yupo ndugu unayemfahamu mwenye uwezo kuliko wewe ambaye angeweza kuutumainia uwezo wake kupata kila kitu katika hii dunia lakini alijizuia kwa ajili ya Kristo na kuhesabu dunia ya miaka 70 sio kitu kulinganisha na umilele unaokuja huko mbeleni na siku ile anakuwa mfalme na wewe si kitu..utajisikiaje? ??

Ndugu ufalme wa mbinguni unapatikana kwa nguvu na wenye nguvu ndio wanaouteka biblia inasema hivyo, Weka mbali mambo ya ulimwengu huu, kajiwekee hazina sasa mbinguni, Kama hujamkabidhi Bwana maisha yako huu ndio wakati, fanya hivyo sasa ili uanze kuiunda tuzo iliyo bora tutakapofika kule siku ile….

Swali ni lile lile ninakuuliza tena hawa wanamichezo wanaokuzunguka wanakufundisha nini katika mashindano ya aina yako ya kikristo?.

Mungu akubariki.

Tafadhali share ujumbe huu kwa wengine na Bwana atakubariki.

No comments:

Post a Comment