JIBU: Kwanza kumbuka katika lugha ya kiswahili hilo neno ELOHIM, halionekani likitajwa katika biblia yetu kwasababu halipo katika lugha ya kiswahili. Hili ni neno la Kiebrania linalomaanisha Mungu, Kama tukisoma katika sura ya kwanza kabisa ya kitabu cha mwanzo biblia inasema " 1Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. "..Hii ni katika lugha yetu ya kiswahili lakini kwa kiebrania inatafsiriwa hivi; Hapo mwanzo ELOHIM aliziumba mbingu na nchi"..Unaona tofauti hapo? na neno hili limetokea kwenye agano la kale mara 2500 katika biblia yao ya kiyahudi, lakini kwetu limetafsiriwa kama Mungu.
Wakati mwingine hili neno ELOHIM limefupishwa kama "EL" ..Na ndio maana sehemu nyingine anajulikana kama EL'Shadai ikiwa na maana kuwa yeye ni "Mungu mwenyezi" kwa lugha yetu ya kiswahili (Mwanzo 17:1, kutoka 6:3 )..Sehemu nyingine anatajwa kama EL ROI, ikimaanisha "Mungu anayeona"(Mwanzo 16:13)..Kadhalika sehemu nyingine anatajwa kama El Elyoni ikimaanisha “Mungu aliye juu”…Haya majina yote utayakuta katika nakala za biblia ya kiebrania.
mahali pengine tuliomwona Bwana Yesu akilitamka hili jina kama lilivyo, pale alipokuwa msalabani tunaona alisema..EL'OI ELOI lama Sabakthani...tafsiri yake ni Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha?..
Kwahiyo jina Elohimu ni Mungu ikimaanisha kwamba ni Mungu asiyekuwa na mwanzo, wala mwisho, Mungu mwenyezi, muweza yote, muhukumu, muumba, n.k. kwa ufupi hilo jina Elohimu linabeba tabia zote za Mungu.
SWALI 2: Naomba unifafanulie maana ya hichi kipengele Bwana Yesu alichokuwa anakizungumzia katika Luka 13:1 "Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya DAMU YAO NA DHABIHU ZAO. 2 Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? 3 Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. 4 Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? 5 Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.
JIBU:Kama ukiitazama kwa ukaribu habari hiyo picha utakayokujia hapo ni kwamba kwa wakati huo ambao Bwana aliokuwepo na hao watu, kulikuwa na habari iliyozagaa sana mjini kote, maeneo kadha wa kadha uko uyahudi,ni habari ya tukio ambalo sio la kawaida kutokea katikati ya jamii ya watu wa Israeli,nalo si lingine zaidi ya kuuawa kwa wayahudi kikatili tena kibaya zaidi na cha kushtusha ni kuchangwa damu zao na za wanyama .
Tuchukulie kwamfano hapa Tanzania wakati ule tulivyosikia ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent kule Arusha, jambo lile liliwashutusha watu wengi sana, mpaka kupelekea tukio kama lile kuzungumziwa mara kwa mara katika vyombo vya habari Tanzania nzima, na tunajua habari za matukio kama hayo huwa kwa namna ya kawaida zinachua muda mrefu kidogo kuacha kuzungumziwa, Na ndio maana unaona hapo wale watu walimwendea Bwana Yesu kumuuliza ili waone kama na yeye anazo hizo taarifa au la! na kama anazo je! yeye naye analizungumziaje suala hilo? Ni kwanini Pilato aamue kufanya kitendo cha kikatili kama kile cha kuchanganya damu za wale wagalilaya na dhabihu zao wenyewe?.
Hilo ni swali lililokuwa ndani ya vichwa vya watu wengi sana kwa wakati ule.
Lakini kama tunavyofahamu kwenye biblia Pilato alikuwa ni Liwali (Governor) wa Uyahudi,(Luka 3:1) chini ya utawala wa kikatili wa Rumi (Kumbuka kwa wakati ule Bwana akiwa duniani Dola ya Rumi ndio ilikuwa inatawala Dunia) Hivyo yeye kama Liwali aliyeteuliwa na Kaisari mkuu wake huko kutoka makao yao makuu Rumi, aiongoze Yudea, alikuwa na jukumu la kuhakikisha Maeneo aliyowekwa ayaongoze yanatulia kikamilifu chini ya utawala . kwahiyo jambo lolote ambalo lingeonekana kujitokeza aidha usaliti, au vurugu, au mapinduzi, au uvunjaji wa amani katika uyahudi lisingevumilika kwa namna yoyote chini ya utawala wa Pilato kwasababu naye pia alikuwa ni mkatili...tunamwona baadaye alikuja kuhusika hata na kifo cha Bwana Yesu.
Kwahiyo biblia haijaeleza sababu hasaa ya Herode kutaka kuwaua wale Wagalilaya waliokwenda kuabudu Yerusalemu wakati wa sikukuu. Inaeleza tu waliposhuka kutoka Galilaya kwenda kuabudu ghafla kikosi cha Pilato kiliwadondokea na kuwachinja na si mahali pengine zaidi ya Hekaluni kwasababu huko ndiko dhabihu zilikuwa zinatolewa , kisha kuchukua damu zao na kuzichanganya na damu za wanyama waliokuja nao kutolea dhabihu kwa Mungu wao..Pengine Pilato alihisi kuna tukio la usaliti au uvunjaji amani lilipangwa na hao watu au vinginevyo hatujui lakini inaelekea itakuwa ni sababu ya kiusalama zaidi.
Na tunaona pia na wale{makutano} nao hakuwajua sababu hasaa ya Pilato kufanya vile, Wao WALIKISIA TU! mioyoni mwao, labda wale watu watakuwa na laana kutoka kwa Mungu na ndio maana wamekutwa na mambo kama yale, au walimkufuru Mungu katika mioyo yao,na ndio maana Mungu akaruhusu Pilato aje kuwaua, au walikuwa na dhambi sana zisizovumilika na ndio maana yakawapatwa mambo kama yale n.k.,
Lakini Bwana akifahamu mawazo yao, akawaongezea kuwakumbusha kisa kingine cha kushtusha kinachofanana na hicho kilichowatokea pengine miezi michache tu! nyuma huko huko Israeli kabla ya tukio hilo, nacho ni kuhusu wale watu walioangukiwa na mnara kule Siloamu..,kwamba wasidhani na wale yaliwapatwa na yale mambo eti kwasababu walimuudhi Mungu kupita kiasi? jibu lake lilikuwa ni hapana..
... Na ndio maana ukiendelea kusoma utaona Bwana anawaambia sivyo kama wanavyofikiri..
Soma tena hapo hiyo habari utaona mawazo ya wale watu yalikuwa ni nini?...Luka13:1 Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. 2 Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? 3 Nawaambia, SIVYO; lakini MSIPOTUBU, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.
Unaona hapo Bwana Yesu alijua mawazo yao kwamba wanadhani kuwa yale mambo yaliyowakuta wale watu ni kutokana na dhambi zao kuwa nyingi sana. Lakini yeye aliwambia sivyo kama wanavyofikiri.
Bwana aliwaambia hata wao pia wasipotubu yatawapatwa na mambo kama hayo hayo. Kadhalika, tetemeko la ardhi lililotokea Kagera, tunadhani wale watu walikuwa na laana sana kuliko sisi??..Ile mvua ya mawe iliyouwa makumi ya watu kule Geita tunadhani wale watu walimkosea sana Mungu kuliko sisi?? ajali ya MV BUKOBA wale watu walikuwa waovu zaidi yetu sisi?..hapana Hakika na sisi pia tusipotubu yatatukuta kama hayo hayo.. Tsunami iliyotokea 2004 huko Indonesia na kuua maelfu ya watu duniani, na sisi kunusurika, tunadhani zile nchi zilimkosea Mungu sana zaidi yetu sisi ...Sivyo, tusipotubu na sisi yatatukuta kama hayo..
Huyo jirani yako aliyekufa na ajali wiki chache zilizopita unadhani alikuwa anayo bahati mbaya sana kuliko wewe?..Sivyo lakini usipotubu siku moja yatakukuta na wewe kwa ghafla na kujikuta umeenda kuzimu.
Hivyo tujichunguze kwanza sisi mioyo yetu, kisha tujue kuwa uvumilivu wa Mungu ni kutuvuta sisi tufikie toba. Mungu amekupa uhai na pumzi, sio kwasababu wewe ni mwema sana zaidi ya yule aliyekufa jana hapana..lakini fahamu kama usipomzalia matunda ya uhai wako sasa, yatakukuta hata pengine makubwa zaidi ya hayo yaliyowakuta hao wengine. Je! Umeokolewa? Je! Una uhakika wa kwenda mbinguni ukifa leo kifo cha ghafla?... yahakiki maisha yako tena, na umgeukie Mungu maadamu muda upo.
SWALI 3: Yohana hapa anasema Bwana ametufanya kuwa Ufalme na Makuhani ufunuo1:6 ...(Sasa hapa anamaanisha hivi sisi ni wafalme na makuhani au ni katika ule umilele ujao?) na je! ni sahihi kumuita mwanamke kuhani??
JIBU: Ndio sasahivi sisi ni ufalme na makuhani wa Bwana katika roho,..kama vile Bwana Yesu alivyokuwa duniani tangu siku za kuzaliwa kwake mpaka siku za kuondoka kwake,,...tayari yeye alishakuwa mfalme,..Kama unakumbuka wale Mamajusi walimuuliza Herode yuko wapi mfalme wa wayahudi tunataka kumsujudia..
(Mathayo 2:3)? unaona hapo tangu alipokuwa mdogo tayari ni mfalme, pia Pilato tunaona baadaye siku chache kabla ya kuondoka kwake duniani alikuja kumuuliza Bwana ...
Yohana 18: 33 "Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia, Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi? 34 Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu? 35 Pilato akajibu, Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini? 36 Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa. 37 Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu".
Kwahiyo hata sisi tuliookolewa, na kuoshwa kwa damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, ni makuhani na ufalme. Lakini mambo hayo yatakuja kudhihirika katika ulimwengu unaokuja kama Bwana alivyosema ufalme wake ni wa ulimwengu unaokuja!...Na ukuhani wenyewe hautakuwa wa kuvukiza uvumba tena, ule ulikuwa ni taswira ya mambo yatakayokuja yanayofunua kumkaribia Mungu.. Vivyo hivyo na katika huo ulimwengu unaokuja hatutakuwa tu wafalme bali tutakuwa na uwezo kumkaribia Mungu kwa namna ya kipekee mfano wa makuhani, ambao sio watu wote watapewa uwezo huo bali ni wale watakaoshinda tu!.. Na thawabu hiyo itakuwa ni kwa wote...wanawake na wanaume.
Hivyo ukuhani wako mbele za Mungu unautengeneza ukiwa hapa hapa duniani, kwahiyo tunapaswa tukaze mwendo ili tusikose thawabu hizo.
SWALI 4: Ni nini maana ya uwe mwenye kukesha na uvipige vita vilivyo vizuri?
JIBU:Ubarikiwe. Maana ya kukesha sio kukesha katika mwili, bali katika roho, kwahiyo katika roho sasa hivi duniani ni giza, uthibitisho ni matendo ya giza yanayoendelea, watu kuwa vuguvugu,ulevi, anasa, uongo na matendo yote ya giza yanayofanana na hayo, na kama unavyojua, giza likishaingia usingizi unaambatana nao, kwahiyo sasahivi wote watendao matendo ya giza ni sawa na wamelala usingizini, hivyo basi maana ya kukesha maana yake, utoke katika matendo ya giza uwe macho, wakati ulimwengu umelala, wewe uwe macho, uiwashe taa yako maana Bwana anakuja kipindi cha usiku wa manane..
Luka 12: 35 Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; 36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. 37 Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. 38 Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao. 39 Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. 40 Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.
Zamu ya pili ni saa sita usiku, na zamu ya tatu ni saa tisa usiku, kwahiyo unaona hapo Bwana anakuja kipindi cha usiku, hivyo ukijitenga na matendo yote ya giza ambayo ni uasherati, uzinzi, ulafi, usengenyaji,uongo na mambo yote yanayofanana na hayo na zaidi ya yote kuiwasha taa yako kwa kuruhusu Roho Mtakatifu kila siku kukuongoza na kukutia katika njia ya kweli huko ndiko kukesha Bwana alikokuzungumzia.
Na maana ya kuvipiga vita vizuri, ni kuvaa silaha zote za haki na kuishindania imani hata mwisho kwa uvumilivu wote pasipo kuchoka, na kwa saburi na subira, hata kufikia ushindi,na silaha zenyewe ndio zile tunazozipata katika..
Waefeso 6: 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. 12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. 14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; 16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; 18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote
Ubarikiwe.
No comments:
Post a Comment