"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, August 6, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 35

SWALI 1:Bwana Yesu aliposema huu mfano alikuwa anamaanisha nini?.. "Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki? Kimefanana na WATOTO wanaokaa SOKONI,WANAOWAITA wenzao,wasisema,Tuliwapigia FILIMBI,wala hamkucheza; TULIOMBOLEZA,wala hamkulia.MAANA YOHANA ALIKUJA,HALI WALA HANYWI,WAKASEMA,YUNA PEPO.MWANA WA ADAMU ALIKUJA,AKILA NA KUNYWA,WAKASEMA,MLAFI HUYU,NA MLEVI,RAFIKI YAO WATOZA USHURU NA WENYE DHAMBI!" NA HEKIMA IMEJULIKANA KUWA INA HAKI KWA KAZI ZAKE".(Mathayo11:16-19).

 JIBU: Mfano huo ni sawa ni kizazi cha sasa hivi tulichopo tuchukulie tu mfano, Mtu akitokea ni mtumishi wa Mungu kweli, maisha yake yote ameyachagua ni kukaa tu kanisani, au milimani kuomba, hafanyi kazi yoyote isipokuwa ni kuomba tu, na kuhudumu kanisani, hana pesa nyingi, nguo zake sio mpya sana, hana mke, wala marafiki, yeye kazi yake ni kumtumikia tu Mungu basi, kajikana maisha yake yote hataki chochote isipokuwa Mungu kajizuia kila kitu kwa ajili ya ufalme wa mbinguni ..Unadhani watu huku nyuma watamchukuliaje mtu kama huyo??..Si ajabu watamwita mlokole masalia, au kalogwa, watasema Mungu hayupo hivyo, Mungu anataka watumishi wake wawe na maisha ya kujifurahisha, kama vile Sulemani, na sio kuwa kama vichaa wa barabarani wasiokuwa na malengo..watamwambia hakika wewe utakuwa umeingiliwa na roho nyingine ambayo si ya Mungu….hivyo hatutaweza kukusikiliza mtu kama wewe maskini wa roho na kimawazo…sisi tunawasikiliza wahubiri wenye malengo, na mafanikio.

 Lakini watu hao hao, mfano wakimuona mtumishi wa Mungu kweli labda Mungu kampaka mafuta anahubiri Neno na Mungu katika kweli yote, kambariki na maisha mazuri ya duniani, labda kampa nyumba nzuri, nguo nzuri, kampa familia nzuri, kampa mali nyingi, analo kanisa kubwa, ..utashangaa watasema, watumishi wa Mungu huwa hawapo hivyo, watumishi wa Mungu hawawezi wakawa matajiri, huwa wanakaa tu milimani wanautafuta uso wa Mungu usiku na mchana, na sio kwenye majumba ya kifahari kama watu wa mataifa…..Kwahiyo kwao pia watasema hatuwezi kuwasikiliza nyie matapeli mnakula Fedha za waumini..
 Na ndivyo ilivyokuwa katika mfano huo, Mungu alipojaribu kuwapeleka Israeli nabii aliyejikana kwa kila jambo, (Yohana mbatizaji) wakasema mtu wa kawaida hawezi kuishi maisha kama hayo ya kutokula wala kujichanganya na wengine, ni lazima atakuwa anao pepo, Lakini Bwana alipokuja anakula na kunywa pengine akidhani kuwa labda watamsikia na yeye wakamwambia ni mlafi na mlevi, manabii wa Mungu hawawi hivyo…….Ndio mithali hiyo inakuja, walipopigiwa filimbi ili wacheze wakakataa, pengine wanahitaji maombolezo, lakini pia walipoombolezewa hawakulia,..sasa waelewekeje! Kwenye raha hawapo kwenye huzuni hawapo..Na ndivyo ilivyo katika kizazi hiki..hata kipewe ishara gani ya nabii hakitaamini isipokuwa wale tu waliokusudiwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu ndio watakaoamini ..


 SWALI 2: Kuna tofauti gani kati ya SALA na DUA?


JIBU: SALA ni neno la ujumla linalojumuisha maombi yote, iwe ya shukrani, mahitaji, ibada, sifa, toba,ulinzi, Baraka n.k…Kwamfano yale maombi ya Baba yetu uliye mbinguni Yesu aliyowafundisha wanafunzi wake….Ni mfano wa SALA. Kwahiyo unaposhukurau ni sala, unapoomba toba ni sala, unapomba hitaji lolote Kwa Mungu kama chakula, mavazi, nyumba n.k. hizo zote ni sala, unapomshukuru Mungu kwa maombi ni sala, na pia unapomwimbia Mungu sifa kama Daudi alivyokuwa anafanya kadhalika ni sala.

Lakini maombi ya Dua ni tofauti kidogo na sala, kwasababu sala ni Neno la ujumla kama tulivyosema lakini DUA imeegemea sana katika maombi ya MAHITAJI.. Kumbuka pia kuna maombi ya kawaida ya mahitaji haya ni yale ambayo unamwomba Mungu akufanyie jambo Fulani, kama tulivyosema hapo juu kuomba rizki, chakula, pesa, n.k. lakini Dua ni maombi ya hitaji isipokuwa haya yanakwenda ndani zaidi, ndiyo yanayohusisha na kuomba rehema, kumsihi Mungu akutendee jambo Fulani ambalo pengine usingestahili kulipata, na dua huwa inaambatana na kujinyenyekeza kwa hali ya juu, na wakati mwingine inahusisha pia na kufunga kwa muda mrefu. Kwamfano unapoomba toba juu ya Kanisa, nchi au familia yako, au ndoa yako kwamba Mungu airehemu kwa makosa Fulani yaliyofanyika, huwezi kwenda kwa maombi ya kawaida tu kama unavyokwenda kumwomba akupe chakula, au pesa, au mavazi, au kazi, hapana hapo utamwendea kwa unyenyekevu, kwa kuomboleza, wakati mwingine kufunga kumsihi Mungu juu ya uovu wa kanisa, au nchi au familia yako ausamehe, sasa hiyo ndio inayoitwa Dua.

Mfano ulio hai tunaweza kuuona kwa Danieli, pale alipoomba DUA juu ya makosa na uovu wa watu wake uliowasababishia mpaka kupelekwa Babeli,
(Danieli 9: 2 katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.
3 Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa MAOMBI NA DUA, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.
4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake;
5 tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako…………; )

Maombi ya namna hii tunaona pia yalifanyika kwa Nehemia, pale alipopata taarifa juu ya uharibifu wa Yerusalemu na maovu ya watu wake yaliyokuwa yametendeka Yerusalemu, aliomba Dua kwa Mungu kwa kuomboleza na kufunga kama Danieli alivyofanya. Soma (Nehemia 1).

Tunaona pia kwa malkia Esta na wayahudi wote walipotangaziwa kuuawa, walijinyenyekeza mbele za Mungu kwa kufunga na kuomboleza kwa ajili ya maangamizi yao, Mungu akasikia dua zako, akawaokoa na maangamizi.

Kadhalika na Daudi mara nyingi alipokuwa akipitia shida, aliingia katika maombi ya Dua kwa ajili yake mwenyewe na Mungu amwepushe na adui zake.(Zaburi 28:2, zaburi 30:8).

Bwana wetu Yesu Kristo pia alikuwa anaomba Dua. Waebrania 5: 7 “Yeye [YESU], siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, MAOMBI NA DUA pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;” Unaona hapo?

Hata sisi pia tunapaswa tuwe watu wa SALA na DUA kwa ajili yetu wenyewe kuomba rehema mbele za Mungu, na kwa ajili ya Kanisa, na kwa ajili ya Nchi ili Mungu aweze kufungua mambo mengine yaliyofungwa mbele yetu. Kwasababu biblia pia imetukumbusha hilo katika:

1Timotheo 2: 1 “Basi, kabla ya mambo yote, nataka DUA, na SALA, na MAOMBEZI, na SHUKRANI, zifanyike kwa ajili ya watu wote;
2 kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.
3 Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu;”

 SWALI 3: Petro aliambiwa na Bwana Yesu UKIONGOKA WAIMARISHE NA NDUGU ZAKO. Sasa kuongoka maana yake nini?.

JIBU: Kuongoka maana yake ni kugeuka au kutubu..Katika habari hiyo tunasoma..

Luka 22: 31 “Akasema [YESU], Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano;
32 lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe UTAKAPOONGOKA waimarishe ndugu zako.
33 Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni.
34 Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui.”

Tunaona hapo Bwana alishafahamu kuwa wakati wa mamlaka ya giza umefika, kwa Bwana pamoja na wanafuzi wake katika muda mchache mbeleni watatiwa chini ya yule mwovu, na ndio maana kwa kulijua hilo kuwa wanafunzi wake watashindwa kustahimili majaribu pasipo msaada wake, alimwambia Petro maneno yale, “Nimekuombea wewe ili imani yako isitindike”, kwasababu shetani atakwenda kuwapepeta kama ngano, hivyo inaweza ikawapelekea kuikana Imani mara moja, na kurudi nyuma kuacha kabisa kuambatana na Bwana…

Tena Bwana akamwambia nimekuombea ili Imani yako isitindike pale utakapojaribiwa, na utaona jaribu lile lilikuwa ni kumkana Yesu mara tatu muda mchache baadaye, hivyo kama Bwana asingemuombea angeweza kujinyonga kabisa kama Yuda au kuacha kabisa kuambatana na njia ya Kristo badala ya Kuongoka(kutubu). Utakuja kuona Wale wanafunzi wengine walikuwa tayari katika mashaka ya kuiacha imani..Hivyo Bwana alimchagua Petro ili baada ya yeye kutubu (kuongoka) kwa machozi pale alipata nguvu ya kwenda kuwaimarisha na wale wanafunzi wengine waliokuwa wametawanyika.

Na ndio maana baada ya Bwana kufa Petro ndiye alikuwa anashughulika kuwakusanya wanafunzi wote, hata wakati wa kwenda kuvua samaki wanafunzi wengine walitaka kwenda nae, utaona pia yeye ndiye aliyetoa pendekezo la kuteuliwa mwanafunzi mwingine mahali pa Yuda kadhalika hata katika siku ile ya Pentekoste Petro ndiye alikuwa wa kwanza kufungua kinywa na kuwaeleza watu upya habari ya maneno ya wokovu kwa nguvu nyingi…Kwahiyo Petro alishughulika sana kuwaimarisha ndugu zake (mitume) waliokuwa naye.

Kadhalika hili neno KUONGOKA, limeonekana katika 1Timotheo 3: 2 “Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha;
3 si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha;
4 mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu;
5 (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)
6 WALA ASIWE MTU ALIYEONGOKA KARIBUNI, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.
7 Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.”

Sasa hapo neno hilo limetumika kwa mtu aliyetubu hivi karibuni (yaani kumpa Bwana maisha yake hivi karibuni)..Mtume Paulo alitoa maagizo kwamba kazi ya uaskofu inahitaji mtu aliyedumu kwa muda fulani mrefu katika Imani, ili isiwe rahisi kwa mtu huyo kunaswa na mitego ya ibilisi kiwepesi.

Tunajifunza nini?..Kama tu vile shetani alivyowataka mitume kuwapepeta kama ngano, na sisi vivyo hivyo anatutaka leo kutupepeta, na nia yake ni tuikane imani, hivyo wewe kama mkristo ni jukumu lako kudumu katika fundisho la mitume(biblia), na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali, kama maandiko yanavyotuagiza katika (Matendo 2:42 ). Ili uwe na nguvu ya kushinda mawimbi ya shetani.

Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment