"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, September 1, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 36


 SWALI 1:  Ndugu zangu Bwana wetu Yesu Kristo kwanini amesema"Waandishi na MAFARISAYO wameketi katika KITI CHA MUSA;"basi YEYOTE watakayo watakayowaambia,MYASHIKE na KUYATENDA;LAKINI KWA MFANO WA MATENDO YAO MSITENDE;""maana wao hunena lakini hawatendi"".""Wao hufunga MIZIGO MIZITO na kuwatwika watu mabegani mwao;WASITAKE WENYEWE KUGUSA KWA KIDOLE CHAO.""Kwakuwa hupanua HIRIZI ZAO,huongeza MATAMVUA yao"".(Mathayo23:1-5).

JIBU: Kwanini alisema hivyo sababu ameshaitoa hapo…”hunena lakini hawatendi” hiyo ndiyo sababu akawaambia wanafunzi wake wasitende matendo kama yao.
Na aliposema mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa anamaana mafarisayo na masadukayo, wameisoma sana torati ya Musa na ni wepesi kuhukumu kwa kupitia hiyo torati, hivyo wanakuwa kama wawakilishi wa Musa, jambo lolote likitokea mfano mwanamke kafumaniwa kwenye uzinzi ni rahisi kutumia torati ya Musa kuhukumu,.na hali wao wenyewe ndani ya mioyo yao wanafanya hayo hayo.

Na aliposema wao WANAPANUA HIRIZI ZAO hakumaanisha wao wana hirizi, kama hizi wanazotumia wachawi, hapana! Neno hirizi zamani lilitumika kuwakilisha
“kiboksi” kidogo kilichobeba maandishi Fulani madogo ambacho watu walikuwa wanatembea navyo, kama kumbukumbu kila waendapo wasisahau yale waliyoyakusudia kuyafanya au kuyatunza katika maisha yao. Mfano katika dunia ya sasa wanandoa wanavaa pete na kutembea nazo kila mahali,..zile ni hirizi za wakati huu wa sasa, kwamba mtu akiitazama inamkumbusha agano aliloingia yeye na mke wake mbele za Mungu siku ile walipofunga ndoa.

kwahiyo, wana wa Israeli waliamuriwa na Mungu waandike baadhi ya vifungu vya maneno ya torati katika viboksi Fulani vidogo kisha wawe wanatembea navyo popote waendapo, wavivae kama utepe katikati ya macho yao, au mkononi. sasa huo utepe waliokuwa wanauvaa katikati ya kipaji cha uso ndio unaoitwa hirizi.

Tukisoma (kumbu 6:4-9) 4 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.
5 Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.
6 Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako;
7 nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.
8 Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako.

Kwasasa jambo hili limezoeleka kuonekana likifanywa na wachawi, lakini asili ya neno hirizi sio uchawi. Kama vile neno kafara lisivyokuwa la wachawi, shetani anatabia ya kugeuza mambo na kuyafanya yawe yake. Isipokuwa sisi wakristo hatufungi hirizi mwilini bali hirizi zetu [sheria za Mungu] tunazifunga rohoni.(Yeremia 31:31-34)

Sasa hawa mafarisayo, wenyewe badala ya kuweka utepe mdogo tu(mfano wa kiboksi kidogo cha nchi 2) katikati ya macho yao, wao waliongeza ukubwa wa utepe likawa ni li-boksi likubwa ili waonekane na watu kuwa ni watakatifu sana,

kadhalika na MATAMVUA yao waliyaongeza, matamvua ni sehemu ya mwisho wa kanzu za wayahudi katika sehemu za mikono, hizo waliamuriwa wazishone wakichanganya na michirizi ya rangi ya samawi(yaani blue), lakini wao wakawa wanashona makubwa kupita kiasi ili waonekane na watu kuwa ni watakatifu zaidi.
(matamvua)

Hivyo badala ya hizo hirizi zao kuwa ni za kiasi tu, wao wakaziongeza na kuwa kubwa ili waonekane na watu ni watakatifu zaidi na wanashika sheria zaidi, kadhalika na matamvua yao badala yawe ya madogo kiasi wao wakayafuma na kuwa mafundo makubwa kupita kiasi ili kila mtu atakapowaona waonekane kuwa wanaijua sheria zaidi, ili kuelewa vizuri tazama picha chini…

Huu ni mfano dhahiri, wa viongozi wa kidini na madhehebu na baadhi ya wakristo wa sasa, wanavaa majoho marefu, na misalaba mikubwa, na kubeba biblia kubwa na kujionyesha mbele za watu, nia yao hasaa sio kumtangaza Kristo, hapana bali waonekana na watu kuwa ni watu wa kuheshimiwa zaidi na kuogopwa katika kanisa, nia yao ni kuonyesha vyeo vyao, lakini ndani yao hawayashiki yale wanayoyaonyesha kwa nje.

Hivyo tunafundishwa na sisi pia tusiwe wanafki, kuigiza mambo ambayo sisi wenyewe hatuyatendi ni unafki mbele za Mungu..na itageuka kuwa OLE!! Katika siku ile.


SWALI 2:  Je? Ni hatua zipi muhimu za kufuata baada ya kubatizwa?

JIBU: Ubarikiwe ndugu...Kwanza, ni vizuri kufahamu kubatizwa, ni tendo la rohoni, na linapaswa litoke rohoni, kitendo cha mtu kwenda kubatizwa kwanza anapaswa awe tayari kugeuka [kutubu], kwa kumaanisha kabisa kutoka moyoni mwake, kuacha maisha ya dhambi, na kuanza maisha mapya katika Kristo...

Sasa mtu wa namna hiyo BWANA YESU KRISTO akishaona moyo wake kweli umedhamiria kugeuka, na hajafanya hivyo kama ni desturi za kidini tu ili kutimiza wajibu, sasa moja kwa moja mtu wa namna hiyo anapewa UWEZO WA KUSHINDA dhambi, kwasababu yeye mwenyewe hawezi. soma Yohana 1:12 "Bali wote waliompokea ALIWAPA UWEZO wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake"

Sasa Uwezo huo hauji juu ya mtu kama hajadhamiria kabisa kuacha dhambi zake, ikiwa na maana kudhamiria kuacha ulevi, anasa, uasherati, utukanaji, uongo, wizi na mambo yote yanayofanana na hayo..

Hivyo kitendo cha Kubatizwa kama mtu akizingatia vigezo hivyo, ubatizo ule unakuwa na maana kubwa sana katika maisha yake kuanzia huo wakati na kuendelea, yeye anakuwa ni milki halali ya Kristo YESU. Ile hatia ya dhambi Bwana anaifuta juu yake, na UWEZO wa kushinda dhambi unaachiliwa juu yake..Kwahiyo, kitu anachopaswa kufanya sasa kuanzia huo wakati wa kubatizwa na kuendelea, ni KUTOKUMZIMISHA ROHO WA MUNGU NDANI YAKE....Na hii inakuja kwa kudumu katika usafi wa roho, na kujifunza Neno la Mungu, na kukaa karibu na ndugu wa kikristo wenye Imani moja na wewe.

Ubarikiwe.

Ukiwa na swali, lolote unaweza ukatutumia, kwa neema za Bwana tutalijibu na kukutumia na kulipost kwa faida ya wengine. Weka jina lako kamili, na swali lako,na ututumie kwa namba za simu, zilizopo upande wa kulia wa ukurasa huu, au kwa kupitia email >> bibliayetu@wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment