SWALI 1: Bwana YESU alimaanisha nini pale aliposema "mkono wako ukikukosesha ukate ni heri uingie mbinguni kigutu kuliko kutupwa jeganamu ukiwa na mikono yako kamili. mguu wako ukikukosesha ukate,macho yako yakikukosesha yangoe?
JIBU: Hapo ni kama inavyojieleza, kiungo kinaweza kikawa kiungo kama kiungo cha mwilini, hususani viungo vya uzazi hivyo ndivyo vinavyowakosesha wengi,…lakini pia kinaweza kikawa kiungo cha nafsi yako, mfano ndugu, marafiki, jamii, kazi, fani, n.k….Yaani kwa ujula chochote kile kinachoweza kukufanya usiwe na uhusiano mzuri na Mungu, unapaswa ukiweke kando, mana ni heri kufanya hivyo uokoke kuliko kuwa nacho kisha ukaishia kuzimu.Kwasababu Bwana Yesu alishasema katika Mathayo 16: 25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?.swali:Sasa ukikata kiungo kimoja chamwili halafu ukafa moja kwa moja sutaonekana kama umejinyonga utasamehewa kweli ?
Ndugu uaposema kinaweza kuwa kiungo sasa viungo vya uzazi,je kama ni kiungo cha uzazi inabidi kikatwe ?kama ni ndiyo je kwa mwanamke inabidi nini kifanyike? Nakumbuka zambia kuna mtu mmoja aliweza kukataa sehemu zake za siri baada ya kufundishwa hivyo ,je siyo kosa tena kuondoa kiungo chenye kutimiza agizo la 'nendeni mkazaliane?Jibu:
Leo hii mwanamke akiambiwa na daktari kwamba ana saratani ya kizazi, na daktari akamwambia achague moja afe au kizazi kiondolewe? Wewe unadhani atachagua kipi?..Sasa kama mtu anaweza akatoa kiungo chake kimoja ili mwili wake wote usife, Si Zaidi mtu kutoa kiungo chake kimoja cha mwili ili roho yake yote isipotee katika ziwa la moto?. Sasa mwili na Roho kipi chenye thamani Zaidi?
Na pia kuhusu utoaji wa viungo zipo njia za kitaalamu na salama za kufanya hivyo mahospitalini, na hilo sio jambo jipya mambo kama hayo kufanyika, yapo mataifa kama China na India wanafanya hivyo, na wanaofanya hivyo wanalipwa.
Kwahiyo Bwana Yesu alivyosema vile alimaanisha kwanza kama ilivyo,kiungo kama kiungo, kisha tafsiri nyingine ndizo hizo tulizozizungumzia zifuate.
Mbarikiwe.
SWALI 2: Shalom nini maana ya huu mstari? “30 Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu. ”
JIBU: Mfano huu Bwana alioutoa unahusu siku za mwisho, na kumbuka siku za mwisho ndio hizi tunazoishi sasa mimi na wewe, kwamba Bwana atatuma wavunaji watakaovuna watu, sasa ili kuelewa hawa wavunaji ni wakina nani hebu tusome mstari ufuatao..Mathayo 9:37 “ Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.38 Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”Unaona hapo, siku hizi za mwisho, wahubiri ndio wavunaji, na siku hizi za mwisho Bwana amesema atawatuma wengi,wa ukweli na wauongo, ambao watawavuna watu wote walioko ulimwenguni (waovu na wema), wale walio waovu (wanaofananishwa na magugu) watafungwa matita matita (yaani watafungwa katika madhehebu mbali mbali) na watasubiria kutupwa katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti, kwasababu ni magugu.Kama Mtu anapenda uasherati, atapata muhubiri atakayemfariji katika uasherati wake, vivyo hivyo na mambo mengine maovu, atapata wahubiri na waalimu na makanisa yanayochukuliana na hayo mambo.Lakini wale walio wema(yaani zile ngano njema) zitakusanywa pamoja na kuhifadhiwa ghalani (na ghalani ni mbinguni), wale walio tayari kufumbua macho yao waone, kufumbua masikio yao wasikie, Bwana anawakusanya katika siku hizi za mwisho kupitia wahubiri wake waaminifu na wa kweli na kuwaweka tayari kwa ajili ya unyakuo.Je! Na wewe umejiandaaje? Huu ni wakati wa kukusanywa,Unakusanywa wapi leo? Kwenye dhehebu lako? au katika Neno la Mungu?.Kanisa/muhubiri asiyekuhubiria kwamba Ibada za sanamu,ulevi,ulavi,ulawiti,uongo,rushwa,wizi,masturbation, chuki,usengenyaji,uvaaji vibaya, ni tiketi ya kwenda motoni, basi huyo ni mvunaji ametumwa kukufunga katika tita lake, na kukupeleka motoni, Biblia inasema mtu asipozaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho hawezi kuuona ufalme wa mbinguni na pasipo huo UTAKATIFU hakuna mtu atakayemwona Mungu.
SWALI 3: Watumishi naomba kufahamu huu mstari una maana gani mithali 14:4 'zizi ni safi ambapo hapana ngombe;bali nguvu za ngombe zaleta faida nyingi, ?.
JIBU: Hiyo ni hekima ya kidunia Sulemani aliiona ambayo pia inafananishwa na mambo ya rohoni. Ni wazi kuwa zizi lisilokuwa na ng’ombe au mfugo wowote, huwa ni safi ikiwa na maana kuwa hakuna mnyama atakayeweza kulichafua kwa kinyesi, au mikojo, au majani, hivyo kama ni mtu analimiliki hatateseka kwa namna yoyote ile kuligharamia, hatapoteza muda wake mwingi kulitunza, yeye atalifunga tu kwasababu litaendelea kuwa safi daima na kukaa pasipo na taabu yoyote, lakini mtu kama huyo kipo kitu atakikosa..Lakini zizi ambalo lina mifugo, kama ng’ombe n.k. tunafahamu zizi kama hilo haliwezi kuwa safi kwasababu ng’ombe watakuwa wanajisaidia huko kila saa, mikojo itakuwa inafagiliwa mara kwa mara, kadhalika zizi nalo litapaswa liwe linapigwa dawa za kuuwa wadudu kila wakati vinginevyo mifugo haitaweza kukaa, zizi pia ni lazima liwe na majani ya kutosha, kama tunavyofahamu Ng’ombe ni mnyama anayekula sana hivyo mmiliki itampasa awe maporini muda mwingi kutafuta majani ya mifugo…Hivyo mmliki wa zizi hilo atapata dhiki na taabu nyingi zaidi ya yule ambaye zizi lake halina mfugo wowote isipokuwa huyu taabu yake haitakuwa ya bure, kuna wakati ataona taabu ya kuhangaika kwake.Na ndio hapo tukirudi kwenye mithali anatumbia “bali nguvu za ng’ombe zaleta faida nyingi”…Hii Inamaana gani?.Inamaana kuwa yule ng’ombe atakwenda KUMLIMISHA katika shamba lake, na kumletea faida nyingi kwa nguvu zake, tofuati na yule aliyeona ni taabu kumlea ng’ombe, siku ya ukulima wake itampasa sasa yeye mwenyewe akalime au aajiri kibarua.Kadhalika katika roho, wengi wanapenda kuwa na mavuno mengi kwa Bwana, lakini hawapendi kuingia gharama za kuyafikia. Bwana Yesu aliwaambia makutano waliokuwa wanamfuata, wale waliopendezwa na njia ya Bwana lakini hawakuwa tayari kuingia gharama..somaLuka 14: 25 Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.27 Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.33 Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.Hivyo na sisi pia tunapashwa ili tuwe na mavuno mengi Bwana anatuagiza tuwe tayari kuingia gharama za kuyapata mavuno hayo..Na gharama zenyewe ndio hizo Bwana alizozitoa hapo juu.Amen.
SWALI 4: Naomba kujua utofauti wa ZAKA/FUNGU LA KUMI na SADAKA Utofauti wao niupi?
JIBU: ZAKA/FUNGU LA KUMI Ni moja ya kumi au sehemu ya kumi ya mapato yako yote, hicho huwa kinakwenda kwa Bwana na ni wajibu kwa kila mkristo mwenye shughuli ya kujipatia kipato kumtolea MUNGU sehemu hiyo ya mapato yake..Walawi 27: 30 Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana. Malaki 3: 8 Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. 9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. 11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.Sasa fungu la kumi au zaka ni tofauti na ‘sadaka/matoleo’. SADAKA yenyewe ni kile ulichonacho juu ya fungu la kumi, kile ulichokirimiwa pasipo sharti lolote la utoaji unampelekea Mungu, sasa zipo sadaka za aina tofauti tofauti kulingana na mahali au mtu mwenyewe, kwa mfano zipo.1) sadaka za shukrani, hizi huwa mtu anatoa baada ya Mungu kumtendea au kumfanikisha katika jambo Fulani, aidha, afya, ulinzi, masomo, biashara, kazi, familia, n.k. Huwa anaambatanisha sadaka yake ya shukrani mahali Bwana anapolia kiroho ni tofauti na fungu la kumi.2) Zipo sadaka nyingine za michango: Hizo zipo nyingi kulingana na uhitaji wa kanisa, mfano jengo, uenezaji injili, vyombo vya nyumba ya MUNGU, mahitaji n.k. Hivyo sadaka/matoleo yapo ya aina nyingi, na pia Mungu hajaweka sharti lolote la utoaji ni jinsi mtu atakavyoguswa moyo na Mungu wake, ndicho atakachotoa.Kutoka 35: 5 Katwaeni kati yenu matoleo kwa Bwana; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba;Kwahiyo jambo la kukumbuka pia katika agano jipya, ni kwamba Mungu hajamwekea mtu sheria au tanzi yoyote katika kutoa ZAKA hata kama hajisikii tu atoe , hapana hiyo haipo katika Ukristo kwasababu Mungu hapendezwi na mtu atoaye kwa moyo wa huzuni au wa kulazimishwa. Lakini ni vizuri pia ikumbukwe kuwa ni wajibu wa kila mkristo yoyote kumtolea MUNGU wake aliyemuokoa. Ni ngumu kwa mtu yeyote kusema amejazwa Roho halafu suala la utoaji kwake ni mzigo.2Wakorintho 9: 7 Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. 8 Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; 9 kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele.Ubarikiwe.Ukiwa na swali, lolote unaweza ukatutumia, kwa neema za Bwana tutalijibu na kukutumia. Weka jina lako, na swali lako, tutakutumia kwa njia ya inbox, e-mail, au whatsapp.
No comments:
Post a Comment