"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, September 30, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 38


 SWALI 1: Katika Mathayo 15:21-28, Yesu alikuwa na maana gani alipomwambia huyu mama kwamba chakula cha watoto hawapewi mbwa?. Pia kwanini alisema hakutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa Israeli.?

JIBU: Tusome, Mathayo 15: 21 “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni.
22 Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.
23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.
24 Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.
26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.
27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.
28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. “

Kumbuka Bwana Yesu alipokuja duniani, hakutumwa kwanza kwa watu wa mataifa, hapana kwasababu wao hawakuwa wanamtazamia mwokozi yeyote, kadhalika watu wa mataifa walikuwa ni watu wasiokuwa ni dini, wapagani, wasiomjua Mungu, walikuwa wanaabudu miungu,na ndio maana Bwana akawafananisha na mbwa katika mfano huo…

Lakini wayahudi ni watu wa Mungu tangu zamani uzao wa Ibrahimu, pamoja na hayo kwa miaka mingi walikuwa wanalitazamia taraja la wokovu wao ambalo lingeletwa tu na MASIHI mwenyewe atakayeshuka kutoka mbinguni, Hivyo kwa kuwa wale ni uzao wa Mungu, uzao wa Ibrahimu, sasa ulipofika wakati wa Mungu kuwatimizia haja yao waliyokuwa wanaisubiria kwa muda mrefu, ndio akamleta Bwana Yesu duniani aje kuwakomboa..

Na ndio maana sasa tunamwona Bwana Yesu alipokuwa duniani, hakuhubiri katika nchi yoyote ya mataifa, kadhalika hakuwatuma hata wanafunzi wake katika mji au kijiji chochote cha mataifa, kwasababu hakutumwa kwao, bali kwa wale waliomtazamia (yaani wayahudi).

Lakini hapa tunamwona huyu mwanamke ambaye ni mtu wa Tiro, (mwanamke aliyekuwa wa kimataifa), asiyekuwa na dini wala Imani katika Mungu wa kweli, alipomwona Bwana akipita kando kando ya miji yao, akamfuata ili ahudumiwe naye, lakini Bwana hakuonyesha kumjali kwa namna yoyote ile, lakini kwa vile alivyokuwa akimsumbua sumbua, ndipo Bwana akamwambia sikutumwa [kwa watu wa mataifa] ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli (yaani wayahudi)..lakini alipozidi kumsumbua sumbua, aliongezea na kumwambia “si vema kutwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa”..yaani akiwa na maana kuwa si vizuri kuiondoa ile neema ya wokovu kwa wale waliostahili kuipokea(yaani wayahudi) na kuwapatia watu ambao hawakustahili kuipokea au kuitazamia(watu wa mataifa).

Lakini pamoja na hayo tunakuja kuona baadaye, ile neema ililetwa kwetu sisi mataifa, baada ya wale ambao waliostahili kuipokea kuikataa, hivyo sisi sasa sio mbwa tena bali tumefanywa kuwa wana wa Mungu kwa damu ya Yesu Kristo.
Hiyo ndio siri iliyokuwa imefichwa tangu zamani kwamba sisi watu wa mataifa tumehesabiwa kuwa warithi wa wokovu sawa na wayahudi kwa njia ya Yesu Kristo. Haleluya. Hivyo ndio maana Mtume Paulo akasema katika..

Waefeso 3: 4 “Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.
5 Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;
6 ya kwamba MATAIFA NI WARITHI PAMOJA NASI WA URITHI MMOJA, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; “

Hivyo somo la kujifunza, hapo ni lipi?. Tumwendeapo Mungu, kwa haja ihusuyo wokovu wetu, hata kama ni kweli tutakuwa hatustahili mbele za Mungu, pengine njia zetu zimekuwa mbaya sana, na tumeomba mara ya kwanza, na ya pili na ya tatu hatujajibiwa…Hatupaswi kukataa tamaa, tuzidi kuomba tuzidi kuomba kama yule mwanamke..Kwasababu Bwana Yesu alishatupa mfano unaofanana na huo, juu ya yule kadhi dhalimu, aliyekuwa hamchi Mungu, lakini yule mwanamke mjane alivyomwendea mara ya kwanza hakupewa haki yake, lakini kwa jinsi alivyokuwa akimwendea endea mara kwa mara, alimpatia haki yake, japo hamchi Mungu, ili asije akamsumbua daima…(Luka 18:1-8)

Vivyo hivyo na sisi tusiache kumwomba Mungu neema ya wokovu, neema ya uponyaji, mahitaji binafsi, hata kama hatutaona dalili zozote za kujibiwa maombi yetu. Kwasababu Mungu anapendezwa na mtu aombaye kwa bidii.

 SWALI 2: Ndugu zangu Mungu anasababisha AJALI yeyote?.Iwe ya meli,gari,pikipiki,baiskeli,angani ndege,moto n.k?.Mfano wa ajali ya meli ya 'titanic'","mfano wa ajali ya gari lililobeba wale watoto wa shule ya Lucky Vicent(na hizo ajali nyingine)","mfano wa ajali za hosteli/mabweni kuungua moto na watu kufia huko",n.K.K..Ndugu zangu hizi zote zinasababishwa na BWANA wetu YESU KRISTO au ni Shetani.?Karibuni sana ndugu zangu..

JIBU: Mungu hasababishi ajali yoyote ile, japo Mungu anaweza akamwadhibu mtu kwa makosa yake. Shetani ndiye mwenye lengo siku zote la kuangamiza hata wakati ambapo mtu hana makosa, kama alivyofanya kwa Ayubu, kwasababu biblia inasema yeye alikuwa ni muuaji tangu mwanzo.(Yohana 8:44).

Asilimia kubwa ya ajali na majanga yanaletwa na shetani. Na pia biblia inasema yapo majanga mengine yanaletwa na Mungu mwenyewe, na mpaka imefikia hivyo ujue ni adhabu kutokana na makosa ya watu wenyewe, na pia Bwana anasema huwa hafanyi jambo lolote bila kuwafunuliwa hao watumishi wake manabii, kuwaonya kama tunavyoona alivyofanya kwa watu wa Ninawi.

Leo hii mtu anamuudhi Mungu labda ni muuaji, lakini kabla Mungu hajamwadhibu atamwonya pengine kwa kumtumia Mtumishi wa Mungu au kwa kusikia mahubiri, na akajua kabisa Mungu anamwonya atubu utakuta pengine alisikia Neno likisema “Uaye kwa upanga, atauawa kwa upanga”..

Lakini yeye akapuuzia na kuendelea na tabia yake ya kuuiba na kuua watu pasipo hatia.. Sasa mtu kama huyo inatokea mazingira labda siku moja amekutana na kundi la wanyang’anyi usiku, na kwa bahati mbaya wakamvamia na kumchoma kisu, kisha na kufa..Sasa kwa nje unaweza ukasema ni shetani lakini sio shetani bali ni Mungu mwenyewe kamlipizia kisasi juu yake.

Hivyo zipo ajali zinazotoka kwa Mungu mwenyewe. Kadhalika zipo pia zinazotengenezwa na shetani, ambazo hizo ndio nyingi kuliko zile zinazotoka kwa Mungu.

 SWALI 3:Matendo15:37"Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.38"Bali Paulo HAKUONA VEMA kumchukua huyo aliyewaacha huko pamfilia,asiende nao kazini.39"Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana....,swali Kwanini huyu mtume Paulo hakumsamehe huyu Yohana aitwaye Marko hata waende naye wawe watatu yaani Barnaba,Yohana aitwaye Marko,pamoja na yeye Paulo wa tatu.Kwanini walishindana na wao ni Wakristo??

JIBU: Ukisoma kitabu cha matendo 13:13 utaona Yohana, aliwaacha wakina Paulo na Barnaba huko Pamfilia, inaonekana aliogopa dhiki itakayokwenda kuwakuta mbeleni, kwasababu Paulo bado mzigo wa kupeleka injili duniani kote alikuwa nao, hivyo walipomsihi waende pamoja alikataa, lakini sasa baadaye tunakuja kumwona tena akikutana na mtume Paulo na Barnaba na kutaka kujumuika nao katika kwenda kuipeleka injili, na ndio hapo tunaona mtume Paulo hakukubali jambo hilo kwasababu kama alishindwa kuandamana nao wakati wa tabu za awali,

kadhalika hataweza kushikamana nao katika dhiki zinazofuata, hivyo sio kwamba Paulo hakumsamehe, alimsamehe lakini hakutaka kuambatana naye tena ili asiwe kikwazo cha injili kwenda mbele.

Ni mfano tunaopaswa tujifunze na sisi [watumishi wa Mungu], kazi ya Mungu si ya kuifanya kirafiki tu, hapana bali wale watakaoitenda kazi kiuaminifu ndio tuambatane nao na kuwatambua hata kama watakuwa si watu wetu wa karibu sana. Lakini ikiwa ni ndugu halafu anaipuuzia kazi ya Mungu, hapo ni kumweka kando, Biblia ilishasema

Wafilipi 2: 12…utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.
13 Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu,

 SWALI 4: Ni sahihi kwa Mkristo mtakatifu kumwambia BWANA ailaze roho ya mtu aliyekufa mahali pema PEPONI?.Mfano mtu huyu ni Yeze amekufa aidha alikuwa Mwema ama muovu sasa ni sahihi kwa Mkristo mtakatifu kusema "Bwana Yesu Ailaze roho ya marehemu Yeze MAHALA PEMA PEPONI"?..

JIBU: Sio sahihi, kwasababu ameshakufa. Tumepewa amri ya kuombeana sisi kwa sisi, yaani tunapokuwa tunaishi hapa duniani, baada ya kufa hatujapewa amri ya kuombeana. Hakuna maombi yoyote yanayoweza kubadilisha hatima ya mtu aliyekufa, kilichobakia kwa mtu aliyekufa ni hukumu tu! (waebrania 9:27).

Mazishi ya watu wasioamini ni tofauti na mazishi ya watu waliomwamini BWANA wetu Yesu Kristo, wasiomwamini wao hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na mambo yatakayofuata baada ya kifo, ndio maana wanasema maneno hayo, lakini sisi tulioamini ndio tunaoelewa kwamba kama ndugu yetu amekufa katika Bwana, basi tunalo tumaini la kukufuka tena kwasababu ni kama amelala tu!.. Lakini kama mtu amekufa katika dhambi na hakumpokea Kristo basi huyo hana tumaini la uzima wa milele, hivyo hawezi kuokolewa kwa maombi yoyote yale. Kwasababu Bwana Yesu alitupa maagizo ya kuenenda ulimwenguni kote kuihubiri injili, AAMINIYE NA KUBATIZWA ATAOKOKA, hakutupa agizo la kuenenda ulimwenguni kote kuwaombea wafu waokoke au walazwe mahali pema peponi.

Kwahiyo saa ya wokovu ni sasa katika maisha haya, baada ya maisha haya ni hukumu.

Ubarikiwe.

.

No comments:

Post a Comment