"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, November 23, 2018

UMEFUNGWA KATIKA GIZA NA UVULI WA MAUTI?

Ni rahisi kudhani kuwa watu wote walio waovu, au wauaji au wanaofanya vitendo vya giza kama vile uchawi ni mambo ambayo walizaliwa kuyapenda, na hiyo wakati mwingine inapelekea hata maombi yetu kwa Mungu tunayoyaelekeza kwao ni ya kifo tu, na si kingine. Lakini hatujui kuwa wengi wao wanaofanya mambo kama hayo mwanzoni hawakuwa na nia ya kuwa wachawi, au wauaji, bali ilitokea kuna wakati waliingiwa na tamaa ya kitu Fulani labda tuseme mali, na ndani ya mawazo yao wanafikiria mali tu na si kingine, huo ndio mtengo mkubwa shetani anaowanasia watu kwasababu biblia ilishasema katika..
1Timotheo 6.10 “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni KUPENDA FEDHA; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”
Unaona sasa katika kuhangaika kwao ndio wanajikuta kidogo kidogo wanaanza kwenda kwa waganga, na kule kwa mganga anapewa labda masharti Fulani ambayo yanamgharimu kuwa mshirikina, na kwa jinsi siku zinavyozidi kuendelea, kwa kuwa lengo la shetani ni kumvuta kwake ili awe mtumishi wake wa UHARIBIFU hivyo anampa vitu anavyovihitaji kwa muda na baadaye analazimishwa kuwa mchawi na huko ndiko anapopewa majukumu makubwa hata ya kutoa roho za watu ili tu aendelee kuishi na kwamba asipofanya hivyo yupo katika hatari ya kuuliwa yeye naye, sasa hatua hiyo aliyofikia hata akijaribu kutoka hawezi, haoni pa kukimbilia, hivyo anajikuta anamalizia kuendelea tu hivyo hivyo huku dhamira yake ikiugua kila siku akifahamu kuwa anayofanya sio sahihi, lakini hawezi kutoka kwasababu ameshaingia katika mtego asioweza kujinasua tena..

Na sisi kwa kuwa hatuna jicho lingine la mbali katika ulimwengu wa roho tunawaombea kifo,.Hatujui kuwa chanzo cha mambo yote ni ibilisi. Kadhalika unakuta na mtu mwingine alijiingiza katika kazi za ujambazi, lengo lake halikuwa kuuwa watu, hapana bali ni kupata mali, sasa hajui kuwa kumbe ni lengo la shetani kumfanya awe muuaji, pasipo kufahamu yeye anaingia huko, na mwisho wa siku katika harakati zake za wizi, siku moja pale anapoona kuwa anakaribia kukamwata analazimika kutoa bunduki na kumpiga mtu na kumuua pasipo yeye mwenyewe kupenda kwa lengo la kujilinda. Lakini sisi huku tunasema Yule jambazi ni katili sana, hana hata huruma.
Kadhalika wapo watu wengine ambao sio wachawi na wala sio wafanyaji wa vitendo viovu, lakini shetani naye anafanikiwa kuwanasa katika mitego yake ya uharibifu.

Kwamfano ngoja nikupe kisa kimoja ambacho kimetokea hapa mtaani kwetu wiki hii.

Kuna kijana mmoja mdogo tu kama miaka 18, ni kijana ambaye ni mtulivu, hakuwa mlevi wala mtumiaji wa sigara, wala hakuwa katika vikundi vya vijana waporaji wa mitaani, lakini ghafla siku ya jumapili tulipata habari kuwa amejinyonga kwa kamba ndani kwao. Na kule kwenye msiba kulikuwa na mtu mwingine aliyehudhuria msibani naye anasema ndugu yake wiki hii hii kajinyonga. Sasa Kama ukichunguza watu wa namna hii vyanzo vinavyowapelekea wao mpaka kufikia hatua hiyo ngumu namna hiyo za kujitoa uhai hazijulikani..

Kwamfano huyu kijana wa kwanza alishawahi kujaribu kujiua mara mbili, haukufanikiwa moja alijaribu kumvamia dereva wa dalala ili aachie usukani gari lipinduke watu wafe pamoja naye kwenye gari, lakini alishikiliwa na watu, na baadaye kupigwa sana nusu kuuawa, na mara ya pili tena alikunywa sumu lakini walimuwahi akapona.

Sasa kwa namna ya kawaida kwa nje, ni rahisi kusema hawa watu ni WAJINGA, WAUAJI, au WANA DHAMBI NYINGI, WAKATILI, MASHETANI n.k. pasipo kujua kuwa wamenaswa katika mitego ambayo hawawezi kutoka kiuwepesi kama wewe unavyodhani na ndio maana wamelazimika kufanya hivyo, sio kwa hiari yao bali ni sababu ya vifungo vya giza kutoka kwa yule adui zimewafanya kuwa hivyo au kufanya vitendo kama hivyo.

Nguvu hiyo hiyo ilimnasa hata mmoja wa mtume wa BWANA wetu YESU KRISTO, naye ni Yuda, ambaye yeye ndio kabisa alikuwa anakula na kutembea na Bwana kila mahali je! Si zaidi kutunasa na sisi watu wa kawaida tusipokuwa makini?. kumbuka lengo la Yuda halikuwa kumsaliti Bwana ili auawe, hapana bali lilikuwa ni fedha tu basi, lakini kwasababu shetani alikuwa anaona mbali akijua kabisa Yuda atajutia kwa tendo lile na kisha baadaye amshawishi ajinyonge hivyo akatumia udanganyifu wa mali kumvuta kwake, na aliponaswa, akiona kuwa maji tayari yameshamwagika hayawezi tena kuzoleka. sasa ile nguvu ya adui ndipo ilipoanza kufanya kazi ndani yake kumpa sababu ya yeye kujiondoa uhai wake..Usidhani ni rahisi kujinasua unapofika katika hatua kama hiyo..Ni ngumu sana hapo inahitaji mkono wa Mungu ulio hodari..Lakini Yuda alizidiwa mpaka kufikia hatua ya KUJINYONGA.

Watu wa namna hii wapo wengi, wamenaswa katika mitego ya adui ya namna mbali mbali na hawawezi kutoka, inawezekana wewe unayesoma habari hii ni mmojawapo. Imefika hatua umezama kwenye uchawi na ushirikina wa viwango vya juu na unaona ni ngumu kutoka tena huko, umezama katika uuaji, umetoa mimba nyingi, umeua watu na shetani anakuambia kuwa wewe dhambi yako haiwezi kusameheka tena, na hivyo unahitaji njia ya kuutoa uhai wako, pengine umekata tamaa ya kuishi baada ya kugundua kuwa umeambukizwa ukimwi au unaugonjwa wa kufisha kama saratani, hivyo kila siku unatamani roho yako itoke usiendelee kuishi tena unatamani hata upate ajali ufe. Ndugu usifanye hivyo yupo tabibu anayeweza kuuganga moyo wako na kukufanya kuwa upya tena kana kwamba hukuwahi kutenda dhambi yoyote, kana kwamba hukuwahi kuumwa, au kumkosea Mungu.

Kama yeye mwenyewe anasema WENYE AFYA HAWAHITAJI TABIBU, BALI WALIO HAWAWEZI.(Mathayo 9:12).Huhitaji kudhani kuwa tatizo lako halina mtetezi..Kumbuka moja ya makusudi maalumu Bwana YESU yaliyomleta duniani ni pamoja na hiyo ya kuwaganga waliovunjika mioyo, na waliofungwa kufunguliwa kwao. Na hakuna yoyote mwingine zaidi yake anayeweza kuwa na hiyo Taaluma.
Isaya 61: 1 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao”.
Yeye pekee ndiye anayeweza kukupa wewe tumaini la uzima, haijalishi umeasi kiasi gani, haijalishi umefungwa katika vifungo vikubwa kiasi gani haijalishi umeshajiunga katika vikundi vya kichawi (occultic groups) vingi kiasi gani, haijalishi umeloga au umehudhuria kwa waganga wengi kiasi gani, haijalishi umeuwa na umetoa mimba nyingi kiasi gani, haijalishi una ugonjwa wa mauti kiasi gani ambao uliupata kwa kutokana na uzembe wako wa kuzini ovyo, hiyo haijalishi embu soma hapa:

Zaburi 107: 10 “Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma,
11 KWA SABABU WALIYAASI MANENO YA MUNGU, WAKALIDHARAU SHAURI LAKE ALIYE JUU.
12 Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi.
13 WAKAMLILIA BWANA KATIKA DHIKI ZAO, AKAWAPONYA NA SHIDA ZAO.
14 ALIWATOA KATIKA GIZA NA UVULI WA MAUTI, AKAYAVUNJA MAFUNGO YAO.
15 Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.
16 Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma.”
17 WAPUMBAVU, KWA SABABU YA UKOSAJI WAO, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa.
18 Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti.
19 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.
20 HULITUMA NENO LAKE, HUWAPONYA, HUWATOA KATIKA MAANGAMIZO YAO”.
 

Bwana leo atalituma Neno lake na kukuponya kama utakuwa tayari kumruhusu yeye ayabadilishe maisha yako. Uwe tu tayari kutubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa, uwe tayari kusema kuanzia leo mimi na ulimwengu basi, mimi na shetani basi, mimi na dhambi basi namgeukia Bwana Yesu, tumaini langu, kisha ukishatubu hatua inayofuata ni kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO ili upate ondoleo la dhambi zako, popote pale upendapo. Na kuanzia hapo na kuendelea Bwana atakupa uwezo wa kipekee wa kumshinda adui, hayo mapepo yaliyokufunga na yaliyokuwa yanakutishia kukuua yataondolewa na YESU mwenyewe,bila hata kutumia nguvu. huo ugonjwa wa mauti wanaosema hauponyeki YESU KRISTO atakuponya, hiyo hofu ya kutokusamehewa iliyo ndani yako na inayokutaka ujiue,jua tu ni ibilisi ndio kaiweka na Yesu pekee ndio ataiondoa.. Hivyo chukua uamuzi sasa maadamu damu ya Yesu ipo kukuganga, usisubiri baadaye au kesho, saa ya wokovu ni sasa.

Mathayo11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; NANYI MTAPATA RAHA NAFSINI MWENU;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
RAHA YA NAFSI YAKO UTAIPATA KWA YESU TU PEKEE.
Ubarikiwe sana.

“Share” Ujumbe huu kwa wengi,Kadhalika ukiihitaji kujifunza mafundisho mengi zaidi usisite kutembelea tovuti yetu .www.wingulamashahidi,org

No comments:

Post a Comment