"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, December 8, 2018

ANGUKO LA UFALME WA SHETANI:

Bwana Yesu alitufundisha SALA iliyo ya kipekee sana, ambayo tunaweza kusema ni sala mama iliyobeba vipengele vyote muhimu vitakavyotuongoza sisi katika kumwomba Mungu daima. Na katika sala hiyo kuna mahali tukifika tunasema UFALME WAKO UJE.

Ulishawahi kujiuliza au kutafakari kwa karibu kidogo ni kwanini ufalme wake uje?. Hiyo inatupa picha kuwa Upo ufalme ambao bado hujafika, nao si mwingine zaidi ya ule wa mbinguni. Mambo yanayoonekana mwilini siku zote yanafunua mambo ya rohoni, katika mwili tunaona falme nyingi tofauti tofauti na kila falme inatafuta kuwa kubwa na yenye nguvu zaidi ya nyingine ili imiliki.. Lakini pia unapaswa kujiuliza ikiwa wanadamu wote ni sawa, ikiwa wanadamu wote walitoka kwa mtu mmoja Adamu, ni kwanini basi wasingekuwa na ufalme mmoja imara, unaomiliki dunia yote?. Ni kwanini basi tunaona falme nyingi tofauti tofauti duniani na kila moja inataka kuwa zaidi ya nyingine?. Ipo sababu inayoifanya dunia kuwa hivyo,

Tunafahamu siku zote ili familia isimame haiwezi kuwa na mababa wawili, ni lazima awepo mmoja tu atakayetawala na kuongoza kila kitu kwenye nyumba vinginevyo kama ingekuwa hivyo basi migongano lazima ingejitokeza na hivyo familia isingeweza kusimama, kadhalika na hii dunia ili isimame haiwezi ikawa na FALME zaidi ya moja inayotawala kote. Vinginevyo siku zote kutaendelea kutokea uharibifu kama tunaouna leo hii duniani.

Sasa ili tufahamu hatma ya falme hizi zote za dunia zilizopo sasa ni vizuri kujifunza kwanza hatma ya falme zilizotutangulia huko nyuma hata kabla ulimwengu kuumbwa, zilitokeaje tokeaje na kusimamaje mpaka leo hii Tunaona kuna ufalme mmoja tu usioasika wa MUNGU ambao ndio huo tunautazamia uje hivi karibuni Kwasababu biblia inasema,

Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani(1Wakorintho 10:11)”.

Embu sasa tujifunze jinsi ule ufalme wa mbinguni ulivyoweza kusimama, Kama tunavyosoma biblia inatuambia hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi..Ikiwa na maana ya MBINGU makao ya malaika na NCHI makao ya wanadamu. Lakini haituambii kuwa mbingu ilikuwa ukiwa, bali nchi ndio iliyokuwa ukiwa na ukiwa huo uliendelea kwa kipindi Fulani biblia isichokitaja mpaka hapo Mungu aliposhuka tena kuiunda dunia na kumuumba mwanadamu ndani yake na baadaye kuja kumpa ufalme.

Sasa tukirudi kule mbinguni baada ya malaika kuumbwa aliunda mfumo wa ufalme, utakaoweza kutawala mambo yote ya kule. Na kama tunavyofahamu ni kawaida ya Mungu kuvitawaza viumbe vyake ili visimamie kazi zake zote za umiliki. Na ndio hapo tunakuja kuwaona malaika wa juu kabisa wakina Michaeli, Gabrieli, na Lusifa,(ambaye ndio shetani) wanatokea ili waongoze vyote katika upana wa mbingu ile, waongoze jamii kubwa sana ya malaika watakatifu waliokuwa mbinguni, wasimamie kazi zote za Mungu zilizokuwa zinaendelea mbinguni. Wauendeshe ule ufalme Mungu aliouweka chini yao katika kanuni zote na utaratibu wote ambao Mungu alikusudia ufanyike. Waende sawasawa na mapenzi ya Mungu.

Ni ufalme uliokuwa wa amani kwa muda mrefu,Mungu aliufurahia akiona jinsi malaika zake wanavyokwenda kwa hekima zake lakini ilifika wakati mambo yakabadilika, Shetani kwa kuona ujuzi uliokuwa ndani yake kuwa ni mwingi, kwa kuona uzuri na hekima aliyokuwa nayo katika bustani ya Mungu ya mbinguni akatamani kuwa kama Mungu, akatamani ule ufalme ungekuwa wake ajitawale mwenyewe, sasa ameshajua kila kitu hana haja tena ya kutembea chini ya kanuni za Mungu, anataka na yeye akawe na ufalme wake ajitegemee, na mawazo yake yalikuwa siku moja amwangushe muumba wake chini ili amiliki vyote(Isaya 14). Hivyo alianza kidogo kidogo kubudi njia zake mwenyewe za udanganyifu huku akisapotiwa na baadhi ya malaika wengine waliokuwepo mbinguni ambao nao pia hawakutaka kutawaliwa. Ikaendelea hivyo hivyo mpaka mapambano yalipozuka mbinguni.

Lakini shetani kwa akili zake chache alifahamu kuwa utaleta upinzani mkubwa sana kwenye ufalme ule kiasi cha kutetemesha mbingu. Alijua hata kama vita itatokea na akashinda basi ufalme ule utagawanyika na kuwa falme mbili. Yeye ataondoka na vyake, na wale kubakiwa na vyao, Hakujua kuwa kama kuna yeyote mbinguni anaouwezo wa kumshusha chini kiasi ambacho tunamwona sasahivi..

Embu jaribu kufikiria mpaka shetani anafikia hatua hiyo ya kuonyesha kiburi kikubwa namna hiyo, Mungu alikuwepo wapi asimpoteze kabisa?. Hii inatuonyesha kuwa Mungu ni Mungu wa uhuru, ikiwa mtu utauchagua uovu uwe sehemu ya maisha yako, Mungu hatakuja kukuondolea kama apendavyo japo anao uwezo huo, bali atamshauri lakini akikataa atamwacha uende kumwangamiza, kwasababu sisi hakutuumba kama maroboti tusiokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi.

Hivyo kiburi cha shetani kilivyozidi kunyanyuka, alivyojiona kuwa ndio anazidi kupata nguvu mbinguni, anaamua sasa atakalo.. Biblia inatuambia ALIANGUKA GHAFLA KAMA UMEME KUTOKA MBINGUNI.
  
Siku yalipomtokea hayo hakuamini kama ingekuwa ni kiwepesi namna hiyo jinsi alivyoanguka kwa ghafla dizaini ile...Yaani kitendo cha kufumba na kufumbua yeye na malaika zake walijikuta wametupwa chini kwenye dunia ambayo hapo mwanzo ilikuwa haijakawaliwa na wanadamu.

Na ndio maana Bwana Yesu anasema Luka 10:8 “..NILIMWONA SHETANI, AKIANGUKA KUTOKA MBINGUNI KAMA UMEME.”
  
Unaona hapo?. Hakuna kitu kinachosafiri haraka hapa duniani kama Umeme, Hivyo Bwana Yesu kusema hivyo alitaka kuonyesha ni jinsi gani kuanguka kwa shetani kulivyokuwa kwepesi kushinda alivyoweza kufikiria na kwa haraka, yaani wakati alipoanza kujiundia ufalme wake bandia ambao ulionekana kama ni mkubwa kule mbinguni, ulivunjwa mara moja, na kujikuta yeye pamoja na malaika zake hawapo tena mbinguni. Ni tendo la haraka sana kama vile UMEME.

Embu tusome kidogo baadhi ya unabii uliomuhusu Shetani na ufalme wake aliokuwa amejiundia.:

Ezekieli 28: 12 “Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri.
13 Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.
14 Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto.
15 ULIKUWA MKAMILIFU KATIKA NJIA ZAKO TANGU SIKU ILE ULIPOUMBWA, HATA UOVU ULIPOONEKANA NDANI YAKO.
16 Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto.
17 Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.
18 Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao.
19 Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele”.

Isaya 14: 11 “Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, Na sauti ya vinanda vyako; Funza wametandazwa chini yako, Na vidudu vinakufunika.
12 Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa!
13 Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.
14 Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.
15 Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.
16 Wao wakuonao watakukazia macho, Watakuangalia sana, wakisema, Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, Huyu ndiye aliyetikisa falme;
17 Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?
18 Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima, Kila mmoja ndani ya nyumba yake mwenyewe;
19 Bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako, Kama chipukizi lililochukiza kabisa; Kama vazi la wale waliouawa, Wale waliochomwa kwa upanga, Wale washukao mpaka misingi ya shimo; Kama mzoga uliokanyagwa chini ya miguu.
20 Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi, Kwa maana umeiharibu nchi yako, Umewaua watu wako; Kizazi chao watendao uovu hakitatajwa milele”.

Hivyo ndivyo Shetani na ufalme wake ulivyo sasa. 
SASA MAMBO HAYO YANATUFUNDISHA NINI?.
Kama Mungu aliziumba Mbingu na nchi, na kule mbinguni aliweka ufalme, kadhalika na katika nchi aliweka ufalme wake. Na ufalme huo Ulianzia Edeni katika bustani ya Mungu. Akamweka mwanadamu wa kwanza katika bustani hiyo, naye ndiye Adamu kama tu vile Mungu Mungu alivyomweka shetani katika Edeni ya mbinguni bustani ya Mungu (kama tulivyosoma hapo juu kwenye Ezekieli 28:13). Lakini mwanadamu hakutaka kutawaliwa na Mungu ndipo naye akausikiliza ule uongo wa shetani akaasi, na kuanzia hapo ndipo ukawa mwanzo wa ufalme mbovu huko huko zikatokea na nyingine nyingi duniani na kila moja ya hizo falme zipo chini ya malaika wa shetani sasa. Na shetani akiwa kama mfalme wa wafalme wa ulimwengu huu sasa.

Kumbuka shetani alishashindwa mbinguni akijua kuwa lile anguko lake lilikuwa kuu sana. Hivyo alipotupwa huku duniani anawavaa wanadamu wawe na tabia kama za kwake ili nao siku ya uharibifu wao ufike kwa ghafla na haraka sana kama UMEME. Ili wote kwa pamoja wajikute katika lile ziwa la Moto.

Na ndio maana biblia ilishasema katika 1Wathesalonike 5: 2 “Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, NDIPO UHARIBIFU UWAJIAPO KWA GHAFULA, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.”

Ndugu, anguko la ufalme huu mbovu wa shetani unaoendelea sasa duniani utakuja kwa ghafla sana na haraka, mahali ambapo wanadamu wanasema sasa sayansi yetu imetufikisha mbali, ustaarabu wetu wa umoja wa mataifa na haki za kibinadamu sasa zinazuia uvunjifu wa amani duniani, hivyo dunia inaweza kuendelea kuwepo kwa muda wa mabilioni ya miaka, Kumbuka hapo hapo ndipo shetani alipofikia kabla hajaanguka aliwaza kule mbinguni. lakini siku yalipompata ndipo alipojua kuwa aliye juu ndiye anayetawala. Kadhalika ndivyo itakavyokuwa kwa dunia hii ambayo ipo karibuni kutoweshwa, Ni lazima iwe hivyo ili kuupisha ufalme wa Mungu kuchukua nafasi yake kwa kupitia YESU KRISTO BWANA WETU.

Mji wa Babeli, uliotukuka sana duniani zamani hizo na uliohusika kuwachukua wana wa Israeli mateka, ulikuwa ni ufalme ambao hakuna mtu angeweza kutegemea kama ungeanguka, kwa jinsi ulivyokuwa na ulinzi mkubwa, na kuta imara, na ustaarabu mkubwa..lakini ulipofika siku yake ya maangamizi, Viganja vilitokea ukutani mwa mfalme wa ufalme huo na kuandika MENE MENE, TEKELI na PERESI..Usiku huo huo ndio ulikuwa mwisho wa mji unaoitwa Babeli. Ndivyo itakavyokuwa kwa falme zote za duniani zilizopo leo, uharibifu utakuja gafla na UFALME WA YESU KRISTO, UTAKUJA.

Ufunuo 11:15  "Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, UFALME WA DUNIA umekwisha kuwa UFALME WA BWANA WETU NA WA KRISTO WAKE, naye atamiliki hata milele na milele".

Hivyo ndugu, usifuate upepo wa huu ulimwengu unavyoelekea, ukapumbazika kwa jinsi unavyozidi kunawiri ukadhani kuwa bado muda mrefu Kristo kurudi mara ya pili na kuangusha huu ufalme wa giza uliopo sasa. Jua tu uharibifu wake utakuja saa watu wasioweza kuutazama. Utaanguka kama umeme. Ni maombi yangu kuanzia sasa utajiweka tayari na kuanza kutazama mambo ya ufalme wa mbinguni unaokuja usiohasika zaidi ya mambo ya ulimwengu huu ambayo ni kitambo tu.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.

2 comments: